Wednesday, October 4, 2023

NG'OMBE WA BBT WAKO SALAMA - ULEGA

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema ng'ombe walio katika programu ya Jenga kesho iliyo bora (BBT) Mifugo, katika Kituo cha Shamba la Serikali Mabuki Mkoani Mwanza wako salama na vijana wanaendelea na shughuli zao za unenepeshaji wa ng'ombe hao.


Waziri Ulega amesema hayo alipotembelea katika kituo hicho kwa lengo la kuona maendeleo ya shughuli za unenepeshaji wa mifugo zinazoendelea kituoni hapo leo Oktoba 4, 2023.


Mhe. Ulega amesema pamoja na kutokea jaribio la wizi katika kituo cha Mabuki kilichopo Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza ambalo lilizua taharuki, ng'ombe wote wako salama, huku akitumia nafasi hiyo kuushukuru uongozi wa Mkoa wa Mwanza, Wananchi na Vijana kwa ushirikiano na kazi kubwa wanayoifanya kituoni hapo.


Amesema kuwa Serikali ya Rais, Dkt. Samia mwaka huu itaendelea kuongeza vituo vingine vya BBT ili vijana wengi zaidi wapate fursa ya kupata elimu hiyo na waweze kujikwamua kimaisha.


Ameongeza kuwa mwaka huu wanakwenda kuongeza vituo vingine kama hivyo katika mikoa ya Tabora, Morogoro, Pwani na Arusha.


Awali, Waziri Ulega ameielekeza Idara ya masoko iliyopo katika Wizara yake kuhakikisha inaendelea kutafuta masoko ya ng'ombe hao wa BBT ili vijana hao waweze kuendelea kufanya biashara na kutimiza lengo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutengeneza fursa nyingi za ajira kwa vijana nchini. 




MAHAKAMA YATOA MAAMUZI KUHUSU PORI LA AKIBA NGORONGORO

 





RAIS DKT. SAMIA ANA UTASHI WA KUKUZA MICHEZO -MAJALIWA

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana utashi mkubwa wa kisiasa katika kukuza sekta ya michezo kwa kufanya uwekezaji na mabadiliko kwenye sekta hiyo.


 


Amesema hayo leo (Jumatano, Oktoba 4, 2023) wakati wa hafla ya kukabidhi shilingi milioni 500 kwa timu ya Taifa ya mpira wa miguu (Taifa Stars) ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Dkt. Samia kwa timu hiyo baada ya kufuzu michuano ya AFCON 2024.


 


“Uamuzi wa Rais Dkt. Samia wa kuridhia asilimia tano ya kodi itokanayo na michezo ya kubashiri (sports betting) ipelekwe katika Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ili kusaidia shughuli za maendeleo ya michezo hapa nchini umelenga kuikuza zaidi sekta hiyo.”


 


Ameongeza kuwa hatua ya Rais Samia kuiundia sekta ya michezo wizara yake ni uthibitisho tosha kwamba anataka kuhakikisha kwamba Tanzania inafikia hatua ambazo mataifa mengine yameshafikia kwenye sekta ya michezo.


 


“Hayo ni baadhi tu ya mambo ya kujivunia katika kipindi hiki cha utawala wa Jemedari na nguli wa michezo, kiongozi shupavu, mama yetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.”


 


Kabla ya kukabidhi hundi hiyo, Waziri Mkuu alikagua ukarabati unaoendelea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwemo vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo, chumba cha matibabu, hali ya uwanja, chumba cha VAR na chumba cha kufuatilia kamera za ulinzi wa uwanjani. Alisema ameridhishwa na kazi ya ukarabati inayoendelea kwenye awamu hiyo ya kwanza.


 


Akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro alisema kutokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, vijana wa timu ya Taifa walipambana hadi wakafuzu kwenda AFCON kwa mara ya tatu.


 


Alisema Tanzania, Kenya na Uganda ziliungana na kuomba kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON kwa mwaka 2027. “Nchi hizi tatu, kwa mara ya kwanza zitakutana huko Mombasa mwezi huu wa kumi ili kuratibu shughuli hii kwa pamoja,” alisema.


 


Mapema, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), Wallace Karia alisema mbali na kujenga viwanja vipya huko Arusha na Dodoma, Benjamin Mkapa na Amri Abeid ni miongoni mwa viwanja vinavyofanyiwa ukarabati ili vitumike kufanya mazoezi wakati wa mashindano ya AFCON.


 


Aliiomba Serikali iwasaidie kupata usafiri wa moja kwa moja kwenda Morocco ili wawahi kurudi nyumbani kwa ajili ya mechi ya marudiano. 





SEKTA YA MADINI KUFUNGAMANISHWA NA MIPANGO YA TAIFA UWEKEZAJI

 


Imeelezwa kuwa, Wizara ya Madini imeweka Mipango ya kuhakikisha Sekta Madini inafungamanishwa na mipango ya taifa ili kuwa na Matumizi yenye tija katika rasilimali za nchi hususan katika Sekta ya Madini.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 4, 2023 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde alipokutana na Waziri Ofisi ya Rais Uwekezaji na Mipango Prof. Kitila Mkumbo wakati wa kikao kifupi kilicholenga kujenga mahusiano mazuri ya uwekezaji nchini Ofisi za Wizara ya Madini Jijini Dodoma.

Amesema ushirikiano wa Wizara hizo mbili utaimarishwa ili Sekta ya Madini iweze kuingizwa katika mipango yenye tija kwa taifa na hatimaye kukuza uchumi wa madini.

Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa madini ni sayansi hivyo Sekta ya Madini itahakikisha inafanya utafiti wa madini nchini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kuvutia wawekezaji nchini.

"Lazima tupate taarifa sahihi za madini yaliyopo nchini hususan kwenye mahitaji makubwa ya madini muhimu na madini mkakati ili madini hayo tuyachimbe kwa kiasi kikubwa nchini," amesema Waziri Mavunde.

Kwa upande wake Prof. Kitila Mkumbo ,amesema Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji inaratibu na kuweka mazingira mazuri yanayoratibika kwa uwekezaji katika Taasisi za Umma

Ameongeza kuwa, kuhusu Madini Muhimu na Madini Mkakati Prof. Kitila amesisitiza mahitaji ya madini hayo duniani iwe chachu kwa Tanzania kutumia fursa hiyo katika kujenga mazingira bora ya kiuchumi ikiwa pamoja na kuibua maeneo mapya ya uwekezaji.

Pia, Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini Angelo Haule amesema mapendekezo ya Vipaumbele kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 ni kuendelea kufanya utafiti wa jiofizikia kwa kutumia ndege (High Resolution Airborne Geophysical Survey) na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji maduhuli na utoaji wa leseni.

"Tutaimarisha uwekezaji na Teknolojia katika Sekta ya Madini ili kuendeleza madini muhimu na madini mkakati katika kuhamasisha uwekezaji, biashara na uongezaji thamani Madini," amesisitiza Haule.

Vile vile, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba amesisitiza kuwa, kama Dira 2030 ya wizara Madini ni Maisha na Utajiri Sekta ya Madini itafanya utafiti ili kufikia maeneo mengi nchini na kuwawezesha wachimbaji wadogo kuchimba kwa tija badala ya kubahatisha.

Kikao kimehudhuriwa na Watendaji mbalimbali kutoka wizara hizo mbili na kwa pamoja wameahidi kushirikiana ili kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini.





PROF. MHANDO ANG’ATUKA ZIFF, SHIVJI AKABIDHIWA MIKOBA YAKE

 



Na Andrew Chale, Dar Es Salaam.

TAMASHA la Kimataifa la Filamu la Zanzibar [ZIFF] mapema jana Oktoba 3, 2023 limemtambulisha rasmi mwongoza filamu Amil Shivji kuwa Mkurugenzi mpya wa tamasha hilo, ambalo ni miongoni mwa matamasha kongwe Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likiwa na umri wa miaka zaidi ya 26.

Awali akizungumza wakati wa kukabidhi nafasi hiyo, Prof. Martin Mhando , Mkurugenzi wa tamasha anayemaliza muda wake, amesema, ‘’Mtengenezaji filamu huyo mchanga na mwenye utashi ndiyo chachu inayohitajika ili kulihuisha tamasha ambalo limeonesha dalili za kuchakaa katika miaka ya hivi karibuni.

Hivyo namtambulisha kwenu Amil Shivji, mtayarishaji mashuhuri na kazi zinazosifika kama vile ‘Vuta N’kuvute’ [2022] na ‘T-Junction’ [2017].

Ni mwana maono ambaye anaamini katika kutumia nguvu ya filamu kukosoa kanuni zilizopo na kuangazia mapambano ya jamii, hasa zisizo na uwezo.’’ Amesema Prof. Mhando.

Aidha, amemuelezea Shivji kuwa ni msomi aliyefuzu katika Chuo Kikuu cha York na mwenye Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Utayarishaji wa Filamu kutoka Toronto, Canada, lakini pia, Amil ndiye mwanzilishi wa Kijiweni Productions, taasisi ya utayarishaji filamu iliyojipambanua katika kusimulia hadithi kwa viwango vya kimataifa.’’ Amesema Prof Mhando.

Na kuongeza kuwa, Chande Omar, Mwenyekiti wa ZIFF na msanii mkongwe wa filamu, alionyesha imani yake kwa Shivji, akisema, "Analeta maono mapya yanayoendana kikamilifu na kaulimbiu ya ZIFF ya 2024 ya 'Kuhuisha.' 

Haiba yake na dhamira yake itahamasisha kila mtu kuungana na kuiweka ZIFF katika viwango vipya." Amesema Prof Mhando na kumalizia kuwa ameamua kung’atuka katika nafasi hiyo aliyodumu kwa muda wa miaka zaidi ya 15.

‘’Tamasha hadi sasa linatimiza miaka 26, Nimedumu kwa muda wa miaka 15. Mimi nimeoa nina miaka 26 hivyo kwa umri huu sasa ni mkubwa naamua nikae pembeni kupisha damu changa.

ZIFF tulianzisha kurejesha kasi ya kuangalia filamu, lakini pia tulijikita katika kukuza na kuinua uandaaji wa filamu hivyo kazi hii ni kubwa na inatakiwa kuendelezwa na vijana’’ amesema Prof. Mhando.

Kung’atuka kwangu sio kama nimechoka, bali kuendeleza mawazo mapya, naamini uwezo wa Amil Shivji na ni mtu ambaye naamini anaweza na ataongoza taasisi muhimu hii ya ZIFF.’’ Amemalizia Prof Mhando.

Kwa upande wake, Amil Shivji amepokea nafasi hiyo kwa mikono miwili huku akiomba ushirikiano kwa wadau na watu wote katika tasnia ya filamu.

‘’Nashukuru kwa nafasi hii tokea nimekuja kama mshiriki wa tamasha na kuingiza filamu yangu kwa mara ya kwanza na kushinda, lakini pia ZIFF ndio iliyonipokea na kunilea.

Kwa zaidi ya miaka 10, ZIFF imenijenga na kukuza taaluma yangu hii kwani mara ya kwanza hakuna aliyenielewa tokea kuleta filamu yangu ya kwanza iliyokuwa ya dakika 14, mwaka 2013, Nimekuzwa na nimeendelea kujikuza, naamini ZIFF sio tu tamasha bali ni chuo na nawashukuru wote akiwemo Prof Mhando na watendaji wengine wote tunamomba aendelee kutushika mkono’’ Amesema Amil Shivji.

Aidha, Shivji amesema kuwa, ZIFF sio tu tamasha bali ni taasisi inayofanya kazi kwa muda wa mwaka zima kila mwaka, hivyo Vijana wanaotaka kujifunza wanakaribishwa ZIFF watajifunza vingi, iwe kuandaa filamu ama kupiga picha ama kuandika mswada. 

Sote kwa pamoja, tuhakikishe ZIFF inaendelea vizuri, tutahakikisha tutakuwa na mabadiliko mengi ilikuwa na mtazamo wa vijana, na kuwa na mtazamo tofauti zaidi, lengo kuvuta watu wote kuja ZIFF kutoka Mataifa yote kuleta filamu na hata kuja kuangalia filamu.’’ Amesema Amil Shivji.

Aidha, Shivji amesema tamasha sio kuandaa kwa ajili ya wasanii kushinda tuzo, tamasha ni njia ya kutazama filamu, hivyo watayarishaji na wasanii wa Bara na Zanzibar na Nchi zote za Afrika na Ulaya ni nafasi yenu ya kuleta filamu zaidi.’’ Amesema Shivji.

Aidha, Shivji amesema dhamira yake kwa sasa ni kuona linaendelea kuwa tamasha bora zaidi duniani.

"Tunahitaji kuliweka tamasha hili sawa na matamasha bora zaidi barani Afrika na duniani. Zanzibar ina mambo yote ya kuifanya ZIFF kuwa tukio kuu barani Afrika, na hilo litakuwa lengo langu katika miaka ijayo.

Natoa wito kwa wapenda filamu wote wa Tanzania, mashirika ya serikali, na viongozi wa mashirika kuunga mkono ZIFF na kuhakikisha inabakia na nafasi yake kama kinara wa utamaduni katika Afrika Mashariki." Amesema Shivji.

Shivji amesema kuwa, ushawishi mkubwa ni kuibua midahalo muhimu katika tasnia ya filamu Tanzania, na kusogeza tasnia mbele.

ZIFF, inajivunia tamaduni tajiri za Bara la Afrika, India, Pakistan, Mataifa ya Ghuba, Iran, na visiwa vya Bahari ya Hindi, na huhusisha pia mashindano ya kimataifa ya filamu, muziki, sanaa za maonyesho, warsha, semina, makongamano, na programu za kitamaduni.

Tuesday, October 3, 2023

NDEGE MPYA YA ABIRIA YAWASILI UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA JULIUS NYERERE.

 



Ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737- MAX9 yenye uwezo wa kubeba abiria 181 ikiwasili nchini kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Oktoba 2023.

ATCL KUWA NA NDEGE ZAKE MPYA 16"-PROF. MBARAWA 

 



Na Andrew Chale, Dar Es Salaaam.

WAZIRI wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amebainisha kuwa, Tanzania kupitia shirika lake la ndege (ATCL) linaenda kuwa na ndege zake mpya 16.


Prof. Mbarawa ameyasema hayo mapema jana Oktoba 2,2023, wakati wa kutangaza hafla ya mapokezi ya ndege mpya ya abiria aina ya Boeing B737-9MAX pamoja na uzinduzi wa ndege mbili aina ya CESSNA 172S itakayofanyika leo Oktoba 3,2023 majira ya kuanzia Saa nne asubuhi katika kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dar Es Salaam.


"Nitumie fursa hii kuutarifu umma wa Tanzania kuhusu ujio wa ndege  mpya ya abiria aina ya Boeing B737-9MAX pamoja na uzinduzi wa ndege  mbili za mafunzo aina ya Cessna 172S JNIA ambapo shamrashamra zinatarajiwa kuanza majira ya saa Nne asubuhi na watu wote wanakaribishwa." Amesema Prof. Mbarawa.


Ambapo amesema: "Mwaka 2016, Serikali ilichukua hatua za kuifufua ATCL kuanza kuinunulia ndege na kufanya mabadiliko ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi.


Hadi Septemba, 2023 ATCL imeshapokea ndege 12 mpya ambazo zimenunuliwa 
na Serikali. Ndege mbili kubwa aina ya B787-8 Dreamliner ambazo zinauwezo wa kubeba abiria 262 kila moja, ndege nne za masafa ya kati aina ya Airbus A220-300 ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 132
kila moja, ndege tano za masafa mafupi aina ya D8 Q400 ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na ndege kubwa ya mizigo aina ya B767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54.2." Amesema Prof. Mbalawa.


Prof Mbarawa amebainisha kuwa,  Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Dkt, Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuhahakikisha kuwa ATCL, inatoa huduma zenye kuhimili ushindani kwa kuanzisha safari za moja kwa moja kwenda kwenye masoko ya kikanda na kimataifa na Julai, 2021 Serikali iliingia mikataba na Kampuni ya Boeing ya Marekani ya ununuzi wa ndege nne mpya zenye teknolojia ya kisasa.


"Ndege hizo ni ndege mbili za abiria za masafa ya kati aina ya B737-9MAX zenye uwezo wa kubeba abiria 181 kila moja, ndege moja ya abiria ya masafa marefu aina ya B787-8 Dreamliner yenye uwezo  wa kubeba abiria 262 na ndege moja kubwa ya mizigo aina ya Boeing B767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54. Ndege ya mizigo aina ya B767-300F tayari ilishawasili na inaendelea kutoa huduma zake na ndege moja ya masafa ya kati aina ya B737-9Max uundaji wake umekamilika na inatarajia 
kuwasili nchini leo tarehe 03 Oktoba, 2023.


Aidha, Ndege mbili zinaendelea kuundwa ambapo zinatarajia kuwasili nchini mwezi Disemba, 2023 na mwezi Machi, 2024." Amesema Prof. Mbarawa.


Ambapo ameeleza kuwa,ndege ya abiria ya masafa ya kati aina ya B737-9MAX inauwezo wa kubeba abiria 181 katika madaraja mawili ambapo daraja la kawaida “economy class” ni abiria 165 na daraja la biashara (business class) abiria 16, pia uwezo wa kubeba mzigo wa tani 6 na kuruka wastani wa masaa 8 bila kutua." amesema Prof Mbalawa.


Prof Mbarawa amebainisha kuwa,kuwasili kwa ndege hiyo kutaifanya ATCL kuwa na ndege 13 mpya zilizonunuliwa kutoka na utekelezaji wa mpango mkakati wa Serikali 
ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2016 na hivyo kuwa na ndege 14 zinazosimamiwa na ATCL katika uimarishaji wa wigo wa mtandao wa safari zake ndege kwa soko la ndani, kikanda na kimataifa.


Kwa sasa ATCL inahudumia vituo vya ndani vipatavyo 14 ambavyo ni Mwanza, Bukoba, Songea, Zanzibar, Katavi, Dar es Salaam, Iringa, Geita, Kigoma, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, na Tabora.


Pia, ATCL inahudumia vituo vya Kikanda na kimataifa ambavyo ni Entebbe-Uganda,
Nairobi-Kenya, Bujumbura-Burundi, Hahaya-Comoro, LubumbashiDRC, Ndola,Lusaka-Zambia,Harare-Zimbabwe.


Pia Johannesburg- Afrika Kusini, Mumbai-India, na Guangzhoa – China na Dubai.


Ujio B737-9MAX kutaiwezesha ATCL kuongeza vituo vya Pemba, Tanga, Mafia, Nachingwea, na Musoma kwa mtandao wa safari za ndani. Pia itaongeza miruko ya safari za usiku kwa viwanja vya ndege ambavyo vina taa pamoja na kuanzisha 
safari za usiku katika viwanja vya ndege vya Dodoma na Songea ambavyo miradi ya ufungaji wa taa za kuongozea taa imekamilika."


Kwa upande wa mtandao wa safari nje,ATCL itaendelea kuongeza miruko ya kwenda Mumbai, India na Guangzhou, China huku ikianzisha safari mpya za Kinshasa, Goma,Dubai, Muscat, na Lagos.


Prof Mbarawa amesena sambamba na uimarishaji wa ATCL tangu mwaka 2016 Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa ndege zinazonunuliwa zinakuwa na wataalamu wa ndani wa kuzihudumia ili kupunguza gharama za kutumia wataalam wa nje hususani Marubani na Wahandisi ndege.


Ambapo hatua hizo ni pamoja na kukijengea uwezo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kukijengea majengo, ununuzi wa mitambo na vifaa vya kufundishia, ununuzi wa ndege za mafunzo, na kuweka 
miundombinu wezeshi kwa ajili kutoa Kozi za muda mrefu za Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege (Degree and Diploma); Kozi za kutoa mafunzo ya Wahudumu wa Ndani ya Ndege (Cabin Crew) na Uendeshaji wa Safari za Ndeg pamoja na Ndaki ya Chuo cha Urubani (Flight Crew).


"Hadi sasa Chuo kinatoa mafunzo ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege, Uendeshaji wa Safari za Ndege pamoja na Uhudumu wa Ndani ya Ndege kwa Ithibati 
za TCAA.


Vilevile, Chuo kinatoa mafunzo ya Air Fares and Ticketing, Airport Operations Fundamentals, Airline Marketing pamoja na Airline Customer  Service kwa Ithibati ya IATA.


Prof Mbarawa amesema,Mwaka 2021 Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliiwezesha NIT kuingia mkataba wa ununuzi wa ndege mbili za mafunzo ya Urubani aina ya Cessna 172 Skyhawk
zinazotumia injini moja kila ndege toka Kampuni ya Textron Aviation Inc ya 
Marekani.


Ndege hizo ziliwasili nchini mwezi Januari, 2023 zikiwa zimevunjwa ambapo kwa sasa zimekamilika kuundwa na zipo tayari 
kuzinduliwa kwa ajili ya kuanza kutoa rasmi mafunzo ya Urubani. Ndege hizo kila moja inauwezo wa kubeba watu wanne (4) ikijumuisha rubani, na zinatumia mfumo wa kisasa wa uendeshaji (glass cockpit) ambao 
unamuwezesha rubani kuratibu taarifa kiurahisi na hivyo kuongeza umakini 
na usalama wakati wa urushaji ndege.

 
Ndege hizo zitatumiwa na NIT kutoa mafunzo ya Urubani kwa daraja la awali 
(PPL) ambayo yatachukua miezi 6 kwa ada ya TZS 21,000,000/= na daraja la biashara (CPL) ambayo yatachukua miezi 12 kwa ada ya TZS 53,800,000/=) na kufanya jumla ya ada kwa mafunzo yote kuwa TZS 74,800,000/= ambayo ni ndogo ukilinganishwa na gharama za kusoma 
mafunzo haya nje ya nchi ambayo kwa wastani hugharimu TZS 300,000,000/=." Amesema Prof Mbarawa,


Na kuongeza: Kwa kuwa ndege moja inaweza kutumika kufundishia 
wastani wa wanafunzi watano (5), Chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili 
wanafunzi 10 kwa mkupuo mmoja.


Katika kuongeza ufanisi wa mafunzo ya urubani mwezi Juni, 2023 Serikali 
ya Awamu ya Sita imewezesha NIT kuingia mkataba na ununuzi wa ndege 
moja ya mafunzo ya injini mbili aina ya Beechcraft Baron G58 toka Kampuni 
ya Textron Aviation Inc. ya Marekani. Ndege hiyo inatarajia kuwasili katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025. Kuwasili kwa ndege hii kutawezesha wahitimu wa kozi ya CPL kufanya mafunzo ya Multi-Engine Class Rating na Multi-Engine Instrument Rating hivyo kukidhi vigezo vya kuingia kwenye ajira.

MNKONDYA AFURAHISHWA NA KASI YA UKUAJI WA VANILLA UNUNIO DAR

 


Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam.


MKURUGENZI Mkuu wa Makampuni ya Kimataifa ya kilimo cha Vanilla Duniani, Simon Mnkondya amefurahishwa na kasi ya ukuaji wa Vanilla katika shamba lililopo Ununio beach, Dar Es Salaam ambalo limeanza kutoa maua na ustawi mzuri. 


Mnkondya amefanya ziara katika shamba hilo akiwa ameambatana na Mke wake Mama Simon Mnkondya Bi. Upendo Ayo, imekuwa ziara yenye matumaini makubwa hasa baada ya kuona kasi ya ukuaji huo wa vanilla.


"Kwetu Vanilla ni zao lisilo na pingamizi kwenye ukuaji.

Soko na bila shaka linabakia kuwa zao la kwanza kwa bei Tanzania na kuwa Vanilla ni zao la pili kwa bei duniani" Amesema Mnkondya.


Aidha,ameongeza kuwa hatua hiyo inapelekea kupigia debe kubwa zao hilo la Vanilla ili ikiwezekana kiwe kilimo cha Taifa.


"Hichi kwetu ni kitu kinachotufanya tulipigie debe kubwa zao la vanilla na ikiwezekana kiwe ni kilimo cha Taifa kwa vile zaidi ya asilimia 80 ya nchi yetu Tanzania Vanilla inamea na kufanya vizuri ikiwa njia za kisasa za 'Greenhouses' na umwagiliaji wa matone zitatumika." Amesema Mnkondya.


Aidha, Mnkondya amesema kuwa, Shamba la Ununio ni shamba lililobezwa kwa sababu ya uwepo wa karibu na mchanga wa bahari mahali hapo lakini umakini wa kampuni ya Vanilla International Limited limekuwa shamba darasa kwa Dar Es salaam."Amesema Mnkondya


Hata hivyo, Mkurugenzi amewaasa wana Ununio na Dar Es salaam kuweza kutembelea kurasa za kampuni hiyo kwenye mitandai yao ilikuwezeshwa namna sahihi za ulimaji wa zao hilo.


MAGAZETI YA LEO TAREHE 03 OKTOBA 2023.

 
















RAIS DKT. SAMIA AFANYA UTEUZI WAKUU WA WILAYA NA WAKURUGENZI.