Wednesday, October 4, 2023
RAIS DKT. SAMIA ANA UTASHI WA KUKUZA MICHEZO -MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana utashi mkubwa wa kisiasa katika kukuza sekta ya michezo kwa kufanya uwekezaji na mabadiliko kwenye sekta hiyo.
Amesema hayo leo (Jumatano, Oktoba 4, 2023) wakati wa hafla ya kukabidhi shilingi milioni 500 kwa timu ya Taifa ya mpira wa miguu (Taifa Stars) ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Dkt. Samia kwa timu hiyo baada ya kufuzu michuano ya AFCON 2024.
“Uamuzi wa Rais Dkt. Samia wa kuridhia asilimia tano ya kodi itokanayo na michezo ya kubashiri (sports betting) ipelekwe katika Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ili kusaidia shughuli za maendeleo ya michezo hapa nchini umelenga kuikuza zaidi sekta hiyo.”
Ameongeza kuwa hatua ya Rais Samia kuiundia sekta ya michezo wizara yake ni uthibitisho tosha kwamba anataka kuhakikisha kwamba Tanzania inafikia hatua ambazo mataifa mengine yameshafikia kwenye sekta ya michezo.
“Hayo ni baadhi tu ya mambo ya kujivunia katika kipindi hiki cha utawala wa Jemedari na nguli wa michezo, kiongozi shupavu, mama yetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.”
Kabla ya kukabidhi hundi hiyo, Waziri Mkuu alikagua ukarabati unaoendelea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwemo vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo, chumba cha matibabu, hali ya uwanja, chumba cha VAR na chumba cha kufuatilia kamera za ulinzi wa uwanjani. Alisema ameridhishwa na kazi ya ukarabati inayoendelea kwenye awamu hiyo ya kwanza.
Akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro alisema kutokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, vijana wa timu ya Taifa walipambana hadi wakafuzu kwenda AFCON kwa mara ya tatu.
Alisema Tanzania, Kenya na Uganda ziliungana na kuomba kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON kwa mwaka 2027. “Nchi hizi tatu, kwa mara ya kwanza zitakutana huko Mombasa mwezi huu wa kumi ili kuratibu shughuli hii kwa pamoja,” alisema.
Mapema, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), Wallace Karia alisema mbali na kujenga viwanja vipya huko Arusha na Dodoma, Benjamin Mkapa na Amri Abeid ni miongoni mwa viwanja vinavyofanyiwa ukarabati ili vitumike kufanya mazoezi wakati wa mashindano ya AFCON.
Aliiomba Serikali iwasaidie kupata usafiri wa moja kwa moja kwenda Morocco ili wawahi kurudi nyumbani kwa ajili ya mechi ya marudiano.
SEKTA YA MADINI KUFUNGAMANISHWA NA MIPANGO YA TAIFA UWEKEZAJI
PROF. MHANDO ANG’ATUKA ZIFF, SHIVJI AKABIDHIWA MIKOBA YAKE
Tuesday, October 3, 2023
NDEGE MPYA YA ABIRIA YAWASILI UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA JULIUS NYERERE.
ATCL KUWA NA NDEGE ZAKE MPYA 16"-PROF. MBARAWA
MNKONDYA AFURAHISHWA NA KASI YA UKUAJI WA VANILLA UNUNIO DAR
Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam.
MKURUGENZI Mkuu wa Makampuni ya Kimataifa ya kilimo cha Vanilla Duniani, Simon Mnkondya amefurahishwa na kasi ya ukuaji wa Vanilla katika shamba lililopo Ununio beach, Dar Es Salaam ambalo limeanza kutoa maua na ustawi mzuri.
Mnkondya amefanya ziara katika shamba hilo akiwa ameambatana na Mke wake Mama Simon Mnkondya Bi. Upendo Ayo, imekuwa ziara yenye matumaini makubwa hasa baada ya kuona kasi ya ukuaji huo wa vanilla.
"Kwetu Vanilla ni zao lisilo na pingamizi kwenye ukuaji.
Soko na bila shaka linabakia kuwa zao la kwanza kwa bei Tanzania na kuwa Vanilla ni zao la pili kwa bei duniani" Amesema Mnkondya.
Aidha,ameongeza kuwa hatua hiyo inapelekea kupigia debe kubwa zao hilo la Vanilla ili ikiwezekana kiwe kilimo cha Taifa.
"Hichi kwetu ni kitu kinachotufanya tulipigie debe kubwa zao la vanilla na ikiwezekana kiwe ni kilimo cha Taifa kwa vile zaidi ya asilimia 80 ya nchi yetu Tanzania Vanilla inamea na kufanya vizuri ikiwa njia za kisasa za 'Greenhouses' na umwagiliaji wa matone zitatumika." Amesema Mnkondya.
Aidha, Mnkondya amesema kuwa, Shamba la Ununio ni shamba lililobezwa kwa sababu ya uwepo wa karibu na mchanga wa bahari mahali hapo lakini umakini wa kampuni ya Vanilla International Limited limekuwa shamba darasa kwa Dar Es salaam."Amesema Mnkondya
Hata hivyo, Mkurugenzi amewaasa wana Ununio na Dar Es salaam kuweza kutembelea kurasa za kampuni hiyo kwenye mitandai yao ilikuwezeshwa namna sahihi za ulimaji wa zao hilo.
Monday, October 2, 2023
JAJI MKUU: MAJAJI WAPYA MTAPIMWA KWA KUSHUGHULIKIA MAJALADA YA MASHAURI
NA MWANDISHI WETU, LUSHOTO.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaambia Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa ufanisi wao na utendaji wao wa kazi utapimwa kwa jinsi watakavyokuwa wanashughulikia majalada ya mashauri Mahakamani mara baada ya kuanza kazi hiyo mpya ya Ujaji.
Mhe. Prof. Juma amesema hayo leo tarehe 02/10/2023 wakati akifungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya wanne wa Mahakama ya Rufani na 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania yanayofayika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Mafunzo hayo ambayo kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yatachukua wiki moja na kwa Majaji wa Mahakama Kuu wiki tatu, yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha IJA.
“Uwezo wako katika utoaji wa huduma utapimwa kila siku utakapoingia Mahakamani, na kwa kila jalada utakalolisimamia na kila utakalofanya na kusema litapimwa…viongozi wako watakupima, wananchi na wadau watakaofika mbele yako watakupima na kutoa tathmini juu ya utendaji wako,” amesema Jaji Mkuu.
Aidha Mhe. Prof. Juma amewataka Majaji hao kuishi maisha ya kawaida na kutotumia nafasi zao kwa ajili ya manufaa binafsi na amewakumbusha kujitayarisha kutoa huduma kwa njia ya kidigitali akisema kuwa kwa sasa mhimili wa Mahakama hautarudi nyuma kwenye matumizi ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Washiriki wa mafunzo hayo watapitishwa katika mada mbalimbali ambazo zitawasilishwa na wawezeshaji kutoka Mahakama ya Tanzania, Taasisi mbalimbali za Umma na binafsi.
Nae Jaji Kiongozi Mhe. Mustapher Siyani akitoa neno la shukrani amewaambia Majaji hao kuwa Mahakama na wananchi wana matarajio makubwa kwao, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa ufanisi na kasi kubwa mara baada ya kumaliza mafunzo yao.
“Tuna matarajio makubwa kuwa mara baada ya kupatiwa mafunzo haya, mtashuka kwenye vituo mlivyopangiwa mkiwa mnakimbia kama askari mpya, mfahamu sisi sote na watanzania kwa ujumla tunawasubiri kwa hamu kubwa utendaji kazi wenu,” amesema Mhe. Jaji Siyani.
Awali akitoa neno la ukaribisho, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Paul F. Kihwelo amesema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa ili kuwajenga Majaji hao katika kazi yao mpya ya Ujaji na kwamba mada zimeandaliwa ili kukidhi kiu ya washiriki.
“Mada za mafunzo hayo zimeandaliwa ili kukidhi kiu ya washiriki na kutimiza malengo ya Mahakama na taifa kwa ujumla ,” na kuongeza,
“Mafunzo haya yatawajenga Majaji kwa ajili ya leo na kwa ajili ya Mahakama ya kesho kwenye kazi yao hiyo mpya ya Ujaji.”
Majaji hao wapya waliteuliwa na Rais wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mnamo tarehe 03/09/2023 na kuapishwa tarehe 14/09/2023 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kuteuliwa na kuapishwa kwa Majaji hao wapya kunaongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani kufikia 30 na wa Mahakama Kuu kuwa jumla ya 105.
Ufunguzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, wasajili wa ngazi mbalimbali za Mahakama ya Tanzania, na viongozi kutoka Taasisi mbalimbali za Umma.
Aidha, mafunzo hayo elekezi ya awali ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya mafunzo ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2013, Mpango mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021/22-2024/25, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja na Mpango Mkakati wa Chuo cha IJA wa mwaka 2023/24-2027/28.
















































