Sunday, December 22, 2019

VULU AMSHUKURU RAIS MAGUFULI.

 Na Omary Mngindo, Kibiti

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynabu Vulu, amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa namna anavyoitekeleza kwa vitendo ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Vulu ametoa kauli hiyo akiwa ziarani katika wilaya za Kibiti, Kisarawe na Kibaha Mji, akihudhuria Mabaraza ya Jumuia ya Wanawake (UWT- CCM) yaliyofanyika kwenye wilaya hizo.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, imedhamiria kuwakomboa wananchi kwa kujenga hospitali mpya kila wilaya, ujenzi wa vituo vya afya, zahanati ikiwemo ununuzi wa ndege na miundombinu ya umeme, barabara sanjali na usafiri wa reli na bahari.

Akiwa Kibiti kwenye siku yake ya kwanza ya ziara hiyo, Vulu akizungumza na wana-UWT hao alisema kuwa Rais Magufuli amezifanyia kazi sekta zote, huku akishukuru zaidi sekta ya afya inayolenga kuhakikisha wanaanchi wananufaika na huduma hiyo.

"Rais wetu amefanya mambo mengi makubwa na anaendelea na juhudi hizo, niwaombe wana-UWT wa Kibiti na wilaya zote tumuunge mkono katika harakati hizo za kimaendeleo anazozitekeleza, kwa fedha zetu za ndani" alisema Vulu.

Aidha amekabidhi kipimo cha sukari na presha kwenye Kituo cha afya Kibiti, huku akimshukuru Mbunge wa Jimbo hilo Ally Ungando, Madiwani, Mkuu wa wilaya na viongozi wote sanjali na wananchi katika kujiletea maendeleo.

Akiwa Kisarawe alizungumza na wana-UWT hao kisha kuwakabidhi boksi za karatasi (rimu) kwa ajili ya matumizi ya Jumuiya zote pamoja na chama ikiwa na lengo la kuboresha utendajikazi kwa wana-CCM hao, huku akimshukuru mbunge Alhaj Suleiman Jafo kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya.


Juzi alikuwa Kibaha Mji, ambapo Vulu aliwapongeza wana-Jumuiya kwa kufanikisha ushindi serikali za mitaa, huku akimpongeza mbunge wa Jimbo Silvestry Koka kwa kazi anayoifanya akishirikiana na Mkuu wa wilaya, Madiwani na ofisi ya Mkurugenzi kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mji Judith Mluge alimpongeza Vulu na wabunge wote wa Viti Maalumu kwa namna wanavyoshirikiana katika kuiendeleza Jumuiya hiyo.

Baadhi ya wenyeviti wa UWT kata zinazounda wilaya ya Kibaha mji
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynabu Vulu, (mwenye kilemba cha kijani) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa jumuiya ya wanawake Kibaha mji muda mfupi baada ya kuzungumza na kukabidhi boksi za karatasi

PICHA ZOTE NA OMARY MNGINDO.  

TANESCO YATOA TAHADHARI KWA WANANCHI

Meneja Mahusiano wa Shirika la Umeme nchini, (TANESCO), Leila Muhaji akizungumza na waandishi wa habari.
.....................................

Na. Farida Saidy, Morogoro.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewataka wananchi wanaofanya shughuli mbalimbali za kibinadamu jirani na miundombinu ya umeme kuacha mara moja ili kujiepusha na madhara yatakayotokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali nchini.


Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Kaimu Meneja Mahusiano TANESCO, Leila Muhaji amesema wale wote wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo kuegesha magari, kulima, kujenga makazi ya kuishi, na kufanya biashara katika miundombinu ya umeme wanatakiwa kuacha.


Amewatahadharisha wananchi kutoshika au kukanyaga nyaya za umeme zilizoanguka hususan katika kipindi hiki cha mvua.


“Ni vyema kutoa taarifa Tanesco kitengo cha dharura kwa msaada zaidi,”alisema.


Katika hatua nyingine amesema kuwa iwapo mvua itaambatana na radi au upepo mkali, umeme utapungua nguvu na kuongezeka ndani ya nyumba hivyo wananchi wanashauriwa kuzima umeme kwenye ‘Main switch’, ili kuepukana na majanga yatokanayo na shoti ya umeme.

 

ALIYEKUTWA UCHI YEYE NA MTOTO WAKE ASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MOROGORO

Kamanda wa Polisi mkoa wa morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbroad Mutafungwa, akiwaonyesha wanahabari (hawapo pichani ) panga na msumeno alivyokutwa navyo, bwana Benson Benard (31) aliekutwa Uchi wa Mnyama yeye na Mtoto wake katikati ya Maporomoko ya Maji eneo la Mlimani, Nguzo Camp.
............................................


Na farida saidy morogoro

Jeshi La Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia Benson Benard (31) aliyekutwa Uchi wa Mnyama yeye na Mtoto wake katikati ya Maporomoko ya Maji eneo la Mlimani Nguzo Camp ndani ya manispaa hiyo. 


Mtu huyo alipoamuliwa kuondoka eneo hilo hatarishi akajirusha na kujizamisha kwenye Maji yaliyokuwa yakitiririka kwa kasi kabla ya kushikiliwa na Polisi.


Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbroad Mutafungwa Askari wake walipokea taarifa toka kwa raia mwema juu ya uwepo wa tukio hilo na baada ya kufika eneo la tukio ambapo  ni eneo la chanzo cha maji wakamkuta mtuhumiwa akiwa na Mtoto wake, na katika hali ya kushangaza wote walikua uchi wa mnyama.

 
  

 Aidha katika Eneo hilo la Tukio Askari Polisi walikuta Panga na Msumeno ambapo pia kunadaiwa kumefanyika uharibifu wa mabomba ya maji, na sasa mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano.

 

Hata hivyo Mtoto amekabidhiwa kwa mama yake mzazi Mary Shao mkazi wa Kihonda, ambae nae anasema mumewe alianza kubadilika kwa kuongea mambo yasiyo eleweka na siku hiyo ya tukio aliaga anaenda kuogelea.