Thursday, September 26, 2019

DC BAGAMOYO AWATAKA WANANCHI KUHESHIMU MIPAKA YA VIJIJI KUEPUKA MIGOGORO

Image may contain: 22 people, people sitting
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa amewataka wananchi wa vijiji vya Chamakweza na Pingo katika halmashauri ya Chalinze kuheshimu mipaka ya vijiji vyao na kuacha tabia ya kuuza ardhi kiholela pasipo kuzingatia sheria taratibu na kanuni za ardhi.


Kawawa ameyasema hayo katika mikutano ya kusikiliza kero na migogoro ya ardhi kwa wananchi wa vijiji vya Chamakweza na Pingo ambapo katika mikutano yake hiyo wananchi walitoa malalamiko yao kwa kueleza kuwa mipaka ya vijiji hivyo ina utata unaosababisha baadhi ya wananchi kuuza ardhi ya upande wa kijiji jirani bila kujiridhisha kama eneo linalouzwa liko katika kijiji cha mtu anayeuza hivyo kusababisha mtafaruku baina ya pande mbili za vijiji jirani.


Mkuu wa wilaya katika kutafuta ukweli wa malalamiko ya pande zote mbili alifanya mkutano katika kijiji cha Chamakweza na kusikiliza malalamiko ya wananchi hao ndipo alienda hadi eneo linalosemekana kuuzwa kiholela, na baada ya hapo alienda moja kwa moja katika kijiji cha Pingo na kufanya mkutano na wananchi, pia alisikiliza malalamiko yao dhidi ya upande wa pili.


Kawawa baada ya kupata malalamiko ya wananchi wa vijiji hivyo alitaka maelezo kutoka ofisi ya ardhi wilaya kuhusu malalamiko ya wananchi hao kuhusu mpaka wa vijiji hivyo.

Mtaalamu wa upimaji ardhi Jackson Mchomvu alibainisha mipaka ya vijiji hivyo ambavyo vilipimwa na wataalam wa wizara ya ardhi tangu mwaka 2010, na musema kuwa, mpaka halisi unaotenganisha hivi vijiji kutoka kusini hadi kaskazini ni kutoka mto Msua hadi mto Mbiki, ndio mpaka unaotambulika kwa sasa ambapo awali mto Mbiki ndio uliotenganisha vijiji vya Talawanda na Chamakweza kwa upande wa Mashariki na Pingo kwa upande wa Magharibi.


Kwa mujibu wa mtaalam huyo eneo kutoka Mto Mbiki hadi Mto Mpapaya ni eneo ambalo lilikuwa halijapata muafaka kuwa ni la upande wa Chamakweza au Pingo.


Mwaka 2014 wataalam kutoka wizara ya ardhi walifika ili kukaa na wananchi kuhusu eneo ambalo halikupata muafaka wananchi wa pande zote mbili hawakuweza kukubaliana hivyo muafaka haukupatikana.


”Kimsingi eneo hili ndiyo chanzo cha migogoro na mwingiliano wa wananchi katika matumizi ya ardhi hii”. Mchomvu alisema.


Baada ya ufafanuzi uliotolewa na Mpima Ardhi wa halmashauri na kupata uhalisia wa mipaka ya kila kijiji, Mkuu wa wilaya alitoa maagizo kwa wananchi wa vijiji vyote viwili kuheshimu mipaka hiyo na kuheshimu matumizi ya ardhi kutokana na mpango wa matumizi sahihi ya ardhi, viongozi kuheshimu sheria ya ardhi kwa kuacha uuzaji wa ardhi ya kijiji kiholela ili kuepuka migogoro ya ardhi inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.


Aidha, Kawawa aliendelea kusema, kwa kipande cha ardhi ambacho bado hakijafikiwa muafaka na vijiji vyote viwili yaani kutoka mto Mbiki hadi Mpapaya kitapatiwa muafaka na wananchi wa pande zote mbili.”


Hivyo wananchi wa Chamakweza na Pingo wataalam wa wizara ya ardhi watafika kuiweka sawa mipaka yenu toeni ushirikiano kwa wataalam hao ili mufikie makubaliano yenye tija na yenye kutatua migogoro kwa pande zote mbili.” Mkuu wa wilaya alisisitiza.


MKURANGA KUWEKA MIKAKATI KUDHIBITI MIFUGO.

Image may contain: 5 people, people standing and indoor
Baraza la madiwani wanaounda Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa pwani, wamefanya maamuzi magumu likiwemo kufuatilia kwa karibu mifugo ya Ng’ombe iliyovamia mashamba na kuharibu mazao ya wakulima.


Akijibu maswali ya papo kwa papo katika kikao cha robo ya nne ya mwaka kilichofanyika katika ukumbi wa flex Garden Kiguza Mkuranga, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Juma Abeid alisema wametenga shilingi milioni 17 ili kuendesha operesheni endelevu kubaini Ng’ombe walioingia kinyemela ndani ya Wilaya ya Mkuranga.


Akiendelea kufafanua malengo ya opereshi hiyo amesema lengo kuu la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa Wilaya ya Mkuranga inakuwa salama kwa kuwaondoa Ng’ombe wote na kuwarejesha walikotoka ili kuepusha mapigano kati ya wakulima na wafugaji.


Juma ambaye pia ni Diwani wa kata ya Magawa alifika mbali zaidi kwa kuweka bayana changamoto sugu ya kuvamiwa maeneo ya ardhi na Wilaya jirani za Kisarawe, Temeke, Kibiti, Ilala na Kigamboni huku wakimuomba Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi William Lukuvi kufika na wataalam wake ili kutatua migogoro hiyo.


Aidha ameiomba Timu ya uhakiki wakulima wa Korosho Wilayani humo kwenda mashambani ili kujiridhisha uwepo wa Kangomba huku akitoa mfano wapo ambao wa kilo 300 bado hawajalipwa kwa kisingizio hicho cha kangomba.


Kwa upande wake Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde aliwahakikishia Madiwani suluhisho la migogoro ya Wafugaji na Wakulima itafikia tamati karibuni kufuatia maboresho ya sheria ndogo ya mifugo inayosubiri kupitishwa na Wizara ambayo itatoa adhabu ya kutaifisha na kupigwa mnada mifugo inayozagaa.


Munde ambaye ni katibu wa kikao hicho alitangaza uwepo wa kikao cha wadau wa muhogo wiki hii ambacho kitawashirikisha wanunuzi na Mashirika mbali mbali katika sekta ya kilimo cha muhogo.

RC NDIKILO AWAONYA WATEKAJI WATOTO PWANI.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akimkabidhi cheti mmoja wa wanafunzi waliohitimu darasa la saba katika  mahafali ya 14 ya shule ya Kibaha  Indepent Lisa Vicent  kushoto kwake ni  Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa shule hiyo Alhaji Yusuph Mfinanga akifuatiwa na Mkuu wa shule hiyo Charles Majani.(PICHA NA VICTOR MASANGU)

..................................
VICTOR  MASANGU, PWANI.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amechukizwa na  vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi ya makundi ya watu wahalifu ambao wanawateka watoto wa shule.


Ametoa onyo kwa watekaji na kusema kuwa, Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoani humo ipo macho na itamshughulikia kila anaehusika na vitendo hivyo.


Aidha, amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kuwabaini wale wote wanaofanya vitendo vya kihalifu.


Ndikilo  ametoa kauli hiyo wakati wa sherehe ya  mahafali ya 14 ya darasa la saba  katika shule ya msingi Kibaha Independent  ambapo pia amewaasa wanafunzi wote waliohitimu kutojiingiza  kabisa katika makundi ya uvutaji wa madawa ya kulevya, mahusino ya kimapenzi, uhalifu wa aina zote na badala yake wahakikishe wanakuwa wazalendo na nchi yao na kuzingatia elimu waliyopata kwa lengo la kutimiza malengo waliyojiwekea.


“Kwa kweli ndugu wazazi na walezi kwa sasa kumeanza kuingia kwa baadhi ya watu kuwateka watoto wetu wa shule na hivi karibuni kumetokea mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari Tumbi kutekwa na watu wasijulikana katika mazingira ya kutatanisha na kumpakia kwenye gari ndogo kisha kwenda kumtelekeza maeneo ya ubungo jijini Dar es Salaam, kwa hiyo  kwa sasa bado tunaendelea na msako kwa ajili ya kuwatafuta wahusika,”alisema Ndikilo.


Wakati huohuo, Ndikilo aliupongeza uongozi wa shule ya Kibaha Independent kwa juhudi wanazozifanya katika uboreshaji wa elimu kwa wanafunzi wao ambao wamekuwa wakifanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya darasa la saba katika ngazi ya taifa na kuwataka walimu waendelee na bidii zaidi ili waweze kushika nafasi ya kwanza katika mitihani yao waliyoimaliza hivi karibuni.


“Walimu wa Kibaha Independent kwa  kushirikiana na bodi yote ya wakurugenzi kwa kweli mnafanya kazi nzuri na serikali ya awamu ya tano itaendelea kushirikiana bega kwa began na shule binafsi lengo ikiwa ni kuhakikisha watoto wetu wote wanapata elimu ambayo itawasaidia katika siku za baadae ,”alisema Ndikilo.


Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Kibaha Independent  Charles Majani amempongeza Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli kwa kuboresh sekta ya elimu na kuiomba serikali kuwasaidia upatikanaji wa vibali kwa wakati  kwa ajili ya kuanzisha shule mpya nyingine ambayo itaweza kutoa fursa zaidi ya kutoa taaluma kwa wanafunzi bila ya kuwa na vikwazo vyovyote.

 
Naye Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa shule hiyo Alhaji Yusuph Mfinanga amewataka wazazi  na walezi kuwalinda  kikamilifu watoto wao na kuepukana na matapeli katika suala zima la ulipaji ada.
Aliwataka wazazi na walezi pia, watumie mfumo ambao umewekwa wa kufanya malipo kwa kutumia njia ya taasisi za kibenki ili kuondokana na usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza.


Hama mmoja wa wanafunzi akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake alisema kuwa  elimu waliyoipata imewatoa ujinga na kwamba lengo lao kubwa ni kufika mbali zaidi hadi ngazi ya vyuo vikuu na kuwashukuru walimu wao ambao wameweza kushirikiana nao bega kwa bega katika kipindi chote cha miaka saba kwa kuwapatia elimu na mahalifa katika maisha yao.


Hivi karibuni  Wilayani Kibaha mkoani Pwani kulitokea tukio la kutekwa kwa mwanafunzi mmoja wa kidato cha pili katika  shule ya sekondari tumbi na watu wasiojulikana na kumtelekeza katika maeneo ya Ubungo  Jijijni Dar es Salaam.

Wanafunzi waliomaliza darasa la saba katika shule ya msingi Kibaha  Kibaha Independent wakicheza kwa furaha katika sherehe ya mahafali yao ya 14 ambayo ilihudhuliwa na viongozi mbali mabli wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo.