Thursday, August 1, 2019

RAIS DKT. MAGUFULI ATENGUA UTEUZI WA MKURUGENZI WA MOROGORO VIJIJINI

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli leo Agosti  1/2019 amemtengua Bw. Kayombe Masoud Lyoba aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kwa usimamizi usioridhisha wa miradi ya Maendeleo hususani ujenzi wa hospitali ya Wilaya .

Akizungumza na Waandishi wa habari mapema leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI , Suleimani Jafo(MB) amesema Mkurugenzi huyo alifanya ununuzi wa dawa ya mchwa kwa gharama kubwa ya milioni 66 kinyume cha gharama halisi.

“kutozingatia taratibu za manunuzi na miongozo ya matumizi ya fedha za ujenzi wa hospitali za halmashauri ,kufanya ununuzi wa kokoto kwa gharama ya shilingi Milioni 45 na kuzisafirisha kwa gharama ya milioni 42” Amesema Jafo

Kufuatia utenguzi huo nafasi hiyo ya ukurugenzi kwa sasa itakaimiwa na Mhandisi Godfrey George Mlowe amabye ni Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro hivyo namuelekeza Mhandisi Godfrey Mlowe kusimamia Halmashauri hiyo pamoja na miradi yote ya maendeleo katika wilaya hiyo ikiwemo, ukamilishaji wa majengo ya Hospitali ya Wilaya, Ujenzi wa Vituo vya afya vya Mikese na Kinonko vilivyopokea fedha hivi karibuni .

Waziri jafo amesema kuwa ansisitiza ujenzi wa vituo vya afaya vijengwe kwa utaratibu wa force Account kwa usimamizi wa kamati zilizoundwa katika ujenzi wa vituo hivyo

Waziri Jafo ameiagiza TAKUKURU iendelee na uchunguzi wa kina wa michakato yote ya ujenzi wa Hospitali hiyo ya Wilya.

WENYE ULEMAVU MSANGA WAOMBA MSAADA

Na Omary Mngindo, Kisarawe.

Wananchi wenye Ulemavu wa viungo katika Kijiji cha Msanga Kata ya Msanga wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani, wanawaomba wahisani watakaoweza kuwasaidia kupata mahitaji mbalimbali.


Wakizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG kijijini hapo, wakazi hao wakijitambulisha kwa majina ya Mohamed Kom, Mwajuma Omary na Nuru Simba walisema kuwa wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, kutokana na kutokuwa na uwezo wa kujimudu kiuchumi.


Kom alisema kuwa wanahitaji msaada wa vyakula pamoja na makazi, na kuongeza kuwa wanakabiliwa na hali ngumu ya kimaisha kutokana na kutokuwa na msaada hali inayowaweka katika mazingira magumu kiuchumi.


"Tunaishi maisha ya shida sana, huyu unayemuona kushoto kwangu ni mtoto wangu wa kike, na wale kulia ni wajukuu zangu kama unavyotuona wote tuna ulemavu wa viungo, hatuna uwezo wa kufanya jambo lolote," alisema Kom.


Kwa upande wake Mwajuma ambaye ana ulemavu wa miguu huku akiwa na watoto wawili, alisema kuwa hana msaada wowote zaidi ya mama yake mzazi ambaye nae hana mume, hali inayozidisha kuwa na maisha magumu.


"Hao watoto unaowaona ni wangu, nimezaa na mwanamme lakini amenikimbia kwa sasa msaada mkubwa unatoka kwa mama yangu ambaye nae anategemea kilimo tu," alisema Mwajuma.


Akizungumzia kuhusiana na malezi ya mtoto wake na wajukuu zake, Nuru alisema kwamba kwa sasa anaishi na baba yake mzazi ambaye ni mlemavu, sanjali na mtoto wake ambaye ni Mwajuma na wajukuu zake wawili wote wa kiume.


"Kama unavyoniona ninaishi na familia yangu ambayo wote ni walemavu wa viungo, yule ni baba yangu, Mwajuma ni mtoto wangu, na hawa ni wajukuu zangu wa kiume ambao nalazimika kulala nao chumba komoja," alisema Nuru.


Aliongeza kwamba anaishi peke yake huku akijihusisha na kilimo ambacho hata hivyo hakina tija, hali inayomuweka katika maisha magumu yeye na familia yake.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) kata ya Msanga, Pilli Mavaga alisema kuwa shirikisho lake lipo katika hatua mbalimbali za kuwasaidia ikiwemo mkopo wa asilimia 2 kutoka halmashauri.


"Kuna maombi ya mkopo wa asilimia mbili kutoka halmashauri ambayo kwa sasa tupo katika hatua ya kufungua akaunti ya shirikisho letu," alisema Mavaga.

MAGAZETI YA LEO AGOST 01, 2019.

UHAMIAJI YATOA TAMKO KUSHIKILIWA ERICK KABENDERA

Kamishina wa Uraia na Pasipoti kutoka Idara ya Uhamiaji Gerald Kihinga.
.....................................


Na Said Mwishehe, Michuzi TV
 


IDARA ya Uhamiaji imesema inamshikilia Mwandishi Erick Kabendera na kwa sasa wanaendelea kuchukua taarifa zake kuhusu uhalali wa uraia wake.

Kamishina wa Uraia na Pasipoti kutoka Idara ya Uhamiaji Gerald Kihinga amesema wanamshikilia Kabendera ili kujiridhisha na uraia wake na huo ni wajibu wao pale wanapokuwa na mashaka na uraia wa mtu.

"Idara ya Uhamiaji ilipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuhusiana na utata wa uraia wa Erick Kabendera mwenyewe alikua hajawahi kuhojiwa kuhusiana na uraia wake, kwa kuwa hakufika ofisini pamoja na kumtumia wito mara kadhaa wa kumtaka afike ofisini kwa mahojiano.

"Na ndio maana sasa idara ya uhamiaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imeweza kumtafuta na kumkamata mhusika ili aweze kuhojiwa kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi kuhusiana na uraia wake.Uchunguzi utakapokamilika, matokeo ya uchunguzi huo yatatolewa,"amesema Kamishna Kihinga.

Amefafanua ieleweke kuwa uchunguzi wa utata wa uraia umekuwa ukifanyika kwa watu mbalimbali wakiwemo watu mashuhuri katika jamii.

Hivyo suala hilo limeibua hisia huenda kwa kuwa mhusika ni mwanahabari.

Amesisitiza Idara ya uhamiaji imekuwa ikishirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama katika utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali , kwa hiyo hilo sio suala geni.

Hata hivyo idara hiyo imetoa mwito kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano na taarifa mbalimbali ya kiuhamiaji ili kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama.

Baada ya taarifa hiyo waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya Tanzania vilitaka kufahamu atashikiliwa kwa muda gani na kwa taarifa za awali Kabendera anahusishwa na uraia wa taifa gani.

Kamishina Kihinga amejibu wataendelea kumshikilia hadi pale watakapokamilisha taarifa wanayoihitaji na kuhusu taifa gani anahusishwa nalo hilo kwa sasa bado kwani ndio wanaendelea kukusanya taarifa.

Alipoulizwa Kabendera amekamatwa na nani? Amejibu amekamatwa na Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Alipoulizwa kwanini waliokwenda kumkamata hawakutaka kutoa vitambulisho na walikuwa wamevaa kiraia, amejibu wana mbinu nyingi za kumkamata mtu ambaye ameitwa na kisha akakaidi.

Hivyo waliamua kutumia mbinu ya kutovaa sare za uhamiaji.