Monday, June 3, 2019

SERIKALI HAINA MPANGO WA KUVIBADILI VYUO VYA MAENDELEO YA WANANCHI KUWA VETA- OLE NASHA.

Image may contain: 1 person, smiling
Serikali imesema haina mpango wa kuvibadili Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kuwa VETA na badala yake imejikita katika kuviboresha Vyuo hivyo kwa kuvikarabati na kuviongezea vifaa vya kujifunzia na kufundishia ili viweze kutoa mafunzo bora zaidi.


Kauli hiyo imetolewa Bungeni leo Juni 03, 2019 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha, wakati akijibu swali la Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Rufiji), aliyetaka kujua kama serikali haioni umuhimu wa kukibadili chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ikwiriri FDC kuwa VETA ili kubadili fikra za wananchi wa Rufiji, Kibiti na Ikwiriri na hatimaye kuleta mwamko wa elimu.


Ole Nasha amesema serikali inaendelea kuvikarabati vyuo hivyo ambapo awamu ya kwanza ya ukarabati unaohusisha vyuo 20 upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji na kwamba awamu ya pili inatarajiwa kuanza mapema mwezi Juni, 2019.


Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ikwiriri kilikuwa katika Awamu ya kwanza na ukarabati umekamilika.


Aidha katika mwaka wa fedha 2019/20 Rufiji ni miongoni mwa wilaya zilizotengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha Wilaya.


"Kwa sasa, Serikali haina mpango wa kuvibadili Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kuwa VETA na badala yake, imejikita katika kuviboresha Vyuo hivyo kwa kuvikarabati na kuviongezea vifaa vya kujifunzia na kufundishia viweze kutoa mafunzo bora" alisema Ole Nasha


Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilianzishwa kwa lengo la kumsaidia mwananchi kukabiliana na changamoto za kimaendeleo katika mazingira yake kwa kumpatia Maarifa na Stadi anuwai ambapo vyuo hivi hutoa Elimu ya Ufundi Stadi katika hatua ya Kwanza hadi ya Tatu.


Mafunzo yanayotolewa katika vyuo hivyo ni pamoja Ujasiriamali, Kilimo, Uvuvi, ufugaji na mengine kulingana na mahitaji ya eneo husika na kwamba hivi sasa nchini kuna vyuo vya maendeleo ya wananchi 55.

BODI YA NISHATI VIJIJINI YATAKA MKANDARASI KUONGEZA KASI YA KUSAMBAZA UMEME.

NA HADIJA HASSAN, LINDI


Bodi ya Wataalamu wa Nishati Vijijini (REA) imemtaka mkandarasi wa State Grid anaetekeleza Mradi wa Kusambaza umeme Vijijini kupitia Mpango wa Rea Mkoani Lindi kuongeza Magenge ya vijana ili kuharakisha Ukamilishaji wa Usambazaji wa Umeme Katika Mkoa huo.


Wito huo umetolewa na kaimu mwenyekiti wa Bodi hiyo Dk, Andrew Komba walipokuwa katika zihara ya siku mbili Mkoani humo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa mpango wa usambazaji wa umeme vijijini.


Komba alisema pamoja na Bodi kuonyesha kuridhishwa na kazi zilizofanywa na mkandarasi huyo Mzawa lakini bado inamshauri kuongeza magenge ya vijana ili kazi iliyosalia iweze kumalizika kwa wakati.


Hata hivyo bodi ilimtaka mkandarasi huyo kuwa pamoja na kupeleka miundombinu hiyo ya umeme pia ahakikishe anaendelea kuunganisha huduma hiyo kwa wananchi.


Alisema ili azima ya Serikali ya kusambaza umeme vijijini iweze kukamilika inaenda sambamba na wananchi kuunganishiwa pamoja na kutumia huduma hiyo.


"hili lisiishie hapa tuu katika kupeleka miundombinu lengo kuu la Serikali kuleta huduma ya umeme Vijijini ilikuwa ni pamoja na kuhakikisha Wananchi wanaunganishiwa ili waweze kupata huduma hivyo malengo yenu mnayopanga kutekeleza yaendane na kusambaza umeme kwa wananchi" Alisema Dk, Komba.


Nae Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Rea mhandisi Amosi Maganga alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi wa Mkoa huo ambao wamepitiwa na mradi wa umeme vijijini kuchangamkia fursa ya umeme waliyoipata kuunganisha umeme katika maeneo yao pamoja na kuanzisha shuguli ndogo ndogo za kiuchumi ili kuweza kujiongezea kipato.


Alisema Serikali tayari imeshatoa fedha za kutosha ili kutekeleza miradi hiyo ikiwa pamoja na kushusha gharama za uunganishwaji lengo likiwa kuwafikia wananchi wote katika maeneo yao tena kwa bei nafuu.


Nae mkurugenzi wa State Grid Charles Mlawa anaetekeleza Mradi huo wa usambazaji Umeme Vijijini Katika Mkoa wa Lindi aliihaidi Bodi hiyo kukamilisha kazi kabla ya mwezi desemba mwaka huu.


Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo wa Rea Meneja wa Shirika la umeme Tanesco Mkoa wa Lindi Felisian Makota alisema kuwa Mradi huo wa Rea hadi kukamilika kwake unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 20 za kitanzania sawa na Bilioni 4.7 kwa fedha za kimarekani na unatarajiwa kuunganishwa katika vijiji 133 vya Mkoa huo.


Aidha Makota pia alibainisha Wigo wa mradi huo ni kuunganisha 33kv Msongo wa kati wa umeme kwa km 392.350, 04/023kv Msongo mdogo wa Umeme 380,60km, 50kvA Mashine umba 185 Pamoja na 100KVA Mashine Umba 2, wateja wa laini moja 4708 na Wateja wa laini tatu 524 ambapo alieleza kuwa kazi hizo kwa sasa zimeshakamilia kwa Zaidi ya asilimia 40

Sunday, June 2, 2019

DC BAGAMOYO ATOA NASAHA KWA WANANCHI.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa  amefuturisha ofisini kwake na kuwataka wananchi kudumisha amani iliyopo wilayani humo ili kila mmoja afanye shughuli zake za maendeleo kwa uhuru.


Alisema katika kipindi hiki cha Mwezi wa Ramadhani kila mmoja amejifunza subira, huruma na kusamehe na kusema kuwa hali hizo zinapaswa ziendlezwe katika miezi mingine iliyobaki.


Katika hutuba yake mara baada kufuturu aliwataka wananchi wa wilaya ya Bagamoyo kujitokeza kwenye uchaguzi wa serikali za mita unaotarajiwa kufanyika mwaka huu ili kila mmoja ashiriki kwa nafasi yake kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo ndani ya wilaya hiyo.


Alisema wale wote wenye sifa wajitokeze kugombea nafasi hizo huku wananchi wote wanapaswa kushiriki kwenye uchaguzi huo kwa kujitokeza kupiga kura.


Aidha, alisema takwimu inaonyesha Mkoa wa pwani unaongoza kwa ujenzi wa viwanda hapa nchini na kwamba wilaya ya Bagamoyo ni miongoni mwa wilaya zenye viwanda vingi mkoani Pwani.


Alitumia nafasi hiyo kuwataka wazazi na walezi kuendelea kuwasimamia watoto waende shule ili hatimae wapate elimu itakayowasidia kupata ajira kwenye viwanda hivyo.


Mkuu huyo wa wilaya amemalizia kwa kuwataka wanachi wa Bagamoyo kujiandaa kuupokea mwenge wa uhuru ambao unatarajiwa kuingia katika wilaya hiyo Tarehe 24 Julai.


Alisema Bagamoyo imekuwa ikifanya vizuri kila mwaka katika mapokezi ya Mwenge na kwamba kufanya vizuri huko kunatokana na umoja, mshikamano miongoni mwa wananchi na wataalamu kutoka idra mbalimbali za serikali na watu binafsi.


Aliwataka wananchi kuendelea na mshikamano huo ili kwa mara nyingine wilaya ya Bagamoyo ifanye vizuri katika miradi yake ambayo inatarajiwa kuzinduliwa na Mbio za Mwenge za mwaka 2019.


 Katibu wa ccm wilaya ya Bagamoyo, Salim Mtelela wa kwanza kushoto, akiwa na mzee maarufu mjini Bagamoyo Aliy bin Nasiri (katikati na Sheikh Ramiya Muhammad Ramiay, kulia.

 Waislamu an wanachi mbalimbali wakiwa katika mstari wa kupata futari ofisini kwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo alipokuwa anafuturisha katika viwanja vya ofisi yake.

 
Waislamu an wanachi mbalimbali wakiwa katika mstari wa kupata futari ofisini kwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo alipokuwa anafuturisha katika viwanja vya ofisi yake.