Sunday, May 5, 2019

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YAOMBWA KUHARAKISHWA MCHAKATO WA KUREKEBISHA SHERIA YA USALAMA BARABARANI

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma , Fatma Toufiq, akieleza ushuhuda wake kwa waandishi wa habari juu ya ajali ilivyoweza kumletea cahangamoto ya utendaji katika kazi.

 Kaimu Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania(TAWLA),Mary Richard akizungumza na Waandishi juu wiki ya usalama barabarani 

.....................................


Wito umetolewa kwa Serikali na watunga sera kuhakikisha wanapitia upya na kufanya mabadiliko katika sheria ya usalama barabarani ili kuweza kudhibiti ajali zinazotokana na uzembe wa watu kwa makusudi.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam leo Mei 05, 2019 na Kaimu Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania(TAWLA),Mary Richard alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari juu ya maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani kwa umoja wa mataifa.

 “sheria hiyo kwa sasa ina mapungufu mengi kiasi mtu akikutwa na kosa adhabu zake ni za kawaida na makosa mengi yamebainishwa katika kanuni badala ya sheria yenyewe ametaja sheria hii inamtaja mtu aliyekaa siti ya mbele na Dereva ndio wanapaswa kufunga mkanda wakati kanuni inataja abiria wote wafunge mkanda jambo ambalo lina ukakasi kidogo”amesema Mary.

Mary ametaja kuwa sheria hii ya Sasa inaseama Dereva wa pikipiki ndio anapswa kuvaa kofia ngumu peke yake wakati sasa jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani wameweka kanuni Dereva na abairia ndio wanapaswa kuvaa kofia ngumu hivyo ni bora vitu vyote hivi vingewekwa kwenye sheria ili utekelezaji wake ufanyike kwa mujibu wa sheria. 

Aliongeza kwa kuomba mamlaka zinazohusika pamoja na Wizara ya Mambo ya ndani waangalie utaratibu wa kubadilisha sheria hii ili kuendana na wakati na uhalisia wa matukio.

kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma , Fatma Toufiq amesema kuwa ajali za barabarani zinaepukika kama watanzania wote wataweza kufuata sheria na kuwa makini pindi wanapoendesha vyombo vya moto.

amesema kuwa yeye kama mbunge anayeshiriki katika kutunga sheria atasimama kidete kuhakikisha sheria hii mpya ya usalama barabarani inapatikana ili tuweze kupunguza takwimu za ajali na walemavu wakudumu wanaotokana na ajali za barabarani



JUMAA AISHUKURU TAMISEMI, AISHAURI.

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, (kulia) akiwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Butamo Ndalahwa, wakikagua majengo hayo, Picha na Omary Mngindo.
...................................... 

Na Omary Mngindo, Mlandizi 


MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, ameishukuru Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa fedha kiasi cha sh. Bil. 1.5 zinazojenga hospitali ya wilaya. 


Jumaa ametoa shukrani hizo mwishoni mwa wiki alipotembelea ujenzi wa hospitali hiyo, inayojengwa katika Kitongoji cha Disunyala, Kata ya Kilangalanga, akiambatana na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Butamo Ndalahwa ambapo amejionea maendeleo mazuri ya ujenzi huo. 


Aidha Jumaa ameishauri Wizara hiyo kwamba inapozipatia fedha halmashauri, basi iziache zijipangie wenyewe namna watavyojenga majengo, kulingana na eneo walilonalo, ikiwa wataweza kujenga ghorofa au majengo yatakayoendana na ardhi ya sehemu husika. 


"Mfano wa ushauri wangu nautolea hapa, hili eneo ni kubwa lakini kutokana na kujengwa majengo mbalimbali, hapa katikati imeachwa sehemu ambayo kimsingi haina faida, kwani haiwezi kutumika kwa ujenzi wowote, tungeachiwa tungejenga ghorofa ardhi kubwa ingebaki," alisema Jumaa. 


Aidha mbunge huyo ameridhishwa na kasi ya ujenzi, japokuwa kunajitokeza changamoto za hapa na pale, zinazochangia kusuasua kwa ujenzi huo unaoelekea ukingoni, huku akiwataka wanaosimamia kazi hiyo kuendelea na kazi ili ikamilike kwa wakati muafaka.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Butamo Ndalahwa aliwambia waandishi wa habari kwamba, wameitumia siku ya upandaji miti, ambapo katika eneo hilo amepanda miti 1,200 lengo ni kuweka mipaka ya eneo lenya eka 42. 


Akizungumzia ujenzi huo, Ndalahwa alisema kuwa baada ya serikali kuwapatia kiasi cha sh. Bil. 1.5 za ujenzi wa majengo matano ya awali, tayari wameshapaua maabara, chumba cha mionzi wakati duka la dawa wanasubiri vifaa maalumu vinavyotunzia ubaridi. 


"Majengo ya Utawala, wagonjwa wa nje, kufulia na wodi kwa ajili ya wazazi hayo tunataraji kuyapauwa wiki ijayo, juu ya changamoto za upatikanaji wa vifaa, tumeshaifanyiakazi kwa kuvileta eneo la tukio wiki moja kabla ya kuhitajika," alisema Ndalahwa. 


Mkurugenzi huyo alimalizia kwa kusemaa kwamba, kazi hiyo ya upauaji inataraji kumalizika kwa wakati ambapo mwezi huu wa tano itakuwa imekamilika, huku akiwashukuru mafundi na wasimamizi wa kazi hiyo kwa juhudi zao.
 
 MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, akitumia futi kamba kupima urefu wa ukuta wa moja ya majengo ya Hospitali ya wilaya ya Kibaha wakati alipotembelea kukagua ujenzi unavyoendelea.
    
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, akipima urefu wa dari ili umbali utakaofungwa feni katika moja ya majengo ya Hospitali ya wilaya ya Kibaha wakati alipotembelea kukagua ujenzi unavyoendelea.

Saturday, May 4, 2019

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUACHA KUSHABIKIA NDOA ZA JINSIA MOJA

 Na Ahmed Mahmoud Arusha

JESHI la polisi mkoa wa Arusha, limewataka wanahabari nchini kutokushabikia au kuunga mkono  ndoa za Jinsia moja ambazo ni vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu havikubaliki na ni kinyume cha maadili .


Rai hiyo imetolewa May 3 na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha Jonathan Shana, alipokuwa akifungua kongamano la maadhimisho ya siku ya vyombo vya habari Duniani lililoandaliwa na Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Arusha APC kwenye ukumbi wa hotel ya Golden rose ya jijini Arusha.


Amesema kuna harakati zinazoendelea Ulimwenguni za kutaka kuungwa mkono ndoa za jinsia moja ,wanahabari wasiunge mkono vitendo hivyo na badala yake waungane pamoja kupiga vita  hata kama tutatengwa na Jumuia za kimataifa  vitendo hivyo ni kinyume cha maadili.


Amewataka wanahabari kutambua kuwa hakuna uhuru usio kuwa na mipaka hivyo akawataka wazingatia uzalendo katika kazi zao ili kuhakikisha habari zinazoandikwa zisiwe zinachafua nchi  au mkoa na Uhuru uliopo utumike  kuwalinda wanahabari wenyewe na watu wengine.


Amesema lipo tatizo  la watoto  kubakwa na kulawitiwa mkoani Arusha na wazazi huwa wanayamaliza kienyeji kwa kupitia vikao amesema anaomba wanahabari na wananchi kuwafichua watu wa aina hiyo na jeshi la polisi limewasha moto wa  kupambana na vitendo vyote vya ukatili huo.


Amewahakikishia  ulinzi wa wanahabari wanaokumbana na madhira wakati wa kutekeleza majukumu yao na kuwalinda dhidi ya vitendo vyote vya uvunjifu wa amani na ukiukwaji wa haki za binadamu  ikiwemo wakati wa chaguzi za serikali za mitaa zitakazofanyika nchini kote mwaka huu.


Amewataka wanahabari kutokukubaliwa kutumiwa na watu wenye nia mbaya kuvuruga amani ya nchi na kusisitiza kuwa Arusha ni Geneva ya Afrika na anataka ibakie kuwa Geneva ya kweli kwa kutanguliza maslahi ya taifa mbele katika kutimiza majukumu yao ya kila siku .


Awali mwenyekiti wa APC,Claud Gwandu, amesema kwa siku za karibuni kumekuwepo na migogoro kati ya wanahabari na serikali na vyombo vyake hali ambayo inaondoa uhusiano uliokuwepo na badala yake kujenga chuki .


Amesema haoni sababu ya kugombana kati ya wanahabari na serikali na vyombo vyake,na matokeo yake ni wanahabari kukamatwa na vyombo vya dola na hivyo kuibua migogoro ambayo haina ulazima.


Kauli mbiu ya mwaka huu inasema Jukumu la UTPC na Klabu za waandishi  wa habari  kuchangia uchaguzi huru na haki .