Friday, March 8, 2019

WAZIRI MKUU ATOA POLE KIFO CHA KIBONDE.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha Mtangazaji wa Clouds FM, Efraim Kibonde wakati alipokwenda nyumbani kwao marehemu, Mbezi Beach jijini Dar es salaam kutoa pole kwa familia, Machi 8, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
.......................................


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kifo cha aliyekuwa Mtangazaji Muandamizi wa kituo cha redio cha Clouds, Ephraim Kibonde ni pengo kubwa kwa Taifa, Clouds Media Group na tasnia ya habari kwa ujumla.


 Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Machi 8, 2019) alipokwenda kuhani msiba wa Mtangazaji Muandamizi kituo cha redio Clouds, Kibonde kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli, nyumbani kwa wazazi wa marehemu Mbezi Beach Dar es Salaam.Kibonde alifariki dunia jana alfajiri Machi 7, 2019 jijini Mwanza.


 “Msiba huu umetushtua sana na ni tukio ambalo hatukulitarajia ila ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Hivi karibuni sote tulimshuhudia akiongoza ratiba ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba na alienda hadi Kagera kumzika.”


 Waziri Mkuu amesema marehemuKibonde enzi za uhai wake ameshirikiana vizuri na Serikali katika shughuli mbalimbali, hivyo amewaomba wananchi waendelee kushikamana na kuifariji familia. “Tumuombee marehemu apumzike kwa amani.


 Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wazazi, watoto wa marehemu pamoja na wananchi kwa ujumla waendelee kuwa na subira na watulivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Samson Job Kibonde ambaye ni baba mzazi wa Mtangazaji wa Cloud FM, Ephrim Kibonde wakati alipokwenda nyumbani kwao marehemu, Mbezi Beach jijini Dar es salaam kutoa pole kwa familia, Machi 8, 2019. Wapili kulia ni Mkurugenzi wa Clouds Media, Joseph Kusaga.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimfariji Hilda Samson Kibonde ambaye ni mama mzazi wa Mtangazaji wa Clouds FM, Ephraim Kibonde wakati alipokwenda nyumbani kwao  marehemu, Mbezi Beach jijini Dar es salaam, kutoa pole kwa familia, Machi 8, 2019. Katikati ni baba mzazi wa marehemu, Samson  Job Kibonde. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimfariji Hilda Samson Kibonde ambaye ni mama mzazi wa Mtangazaji wa Clouds FM, Ephraim Kibonde wakati alipokwenda nyumbani kwao  marehemu, Mbezi Beach jijini Dar es salaam, kutoa pole kwa familia, Machi 8, 2019. Katikati ni baba mzazi wa marehemu, Samson  Job Kibonde. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

WAHAMIAJI HARAMU 12 WAKAMATWA PWANI.

 NA MWAMVUA MWINYI, PWANI

WAHAMIAJI haramu 12 raia  kutoka Ethiopia ,wamekamatwa mkoani Pwani, eneo la Mwidu porini, Chalinze kwa kosa la kutokuwa na kibali kinyume na sheria.


Aidha watu 14 wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo kwa makosa mbalimbali ya kiuhalifu ikiwemo wizi wa pikipiki na kukutwa na madawa ya kulevya aina ya bangi.


Akielezea juu ya matukio hayo, kamanda wa polisi mkoa wa Pwani,ACP Wankyo Nyigesa, alisema usiku wa kuamkia march 8 ,askari polisi walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu uwepo wa wahamiaji hao waliojificha kichakani eneo la Mwidu barabara ya Dar es salaam -Morogoro.


Alieleza baada ya polisi kufika eneo hilo waliwakamata wakiwa safarini kutoka Ethiopia kuelekea Afrika ya Kusini.


:”Baada ya mahojiano ilionekana watu hao walifichwa hapo na mtu ama watu ambao bado hawajafahamika kwa lengo la kuwatafutia usafiri wa kuelekea nchini Afrika Kusini kutafuta ajira. “


Hata hivyo Wankyo alibainisha, afya ya wahamiaji haramu hao walikuwa wamedhoofika.


Wakati huo huo jeshi hilo linawashikilia watu nane kwa kufanya uhalifu mbalimbali ikiwemo wizi wa pikipiki.
Pia watu sita wamekamatwa kwa kupatikana na dawa za kulevya ikiwemo bangi kete 172.


Wankyo alielezea kwamba, baada ya mahojiano na upelelezi kukamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

WAZIRI NDALICHAKO MGENI RASMI MKUTANO WA KIMATAIFA WA WARATIBU WA KITAIFA WA MIRADI

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojiaa Profesa Joyce Ndalichako anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kimataifa wa waratibu wa kitaifa wa miradi inayotekelezwa na Shirika la nguvu za Atomiki duniani kwa nchi 46 kanda ya Afrika utakaofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 15 mwezi Machi 2019 jijini Arusha wenye lengo la kujadiliana na masuala mbali mbali.

Mkutano huo utashirikisha washiriki 60 kutoka nchini 46 duniani kutoka baara la AFRIKA ambao ni wanachama wa Shirika la nguvu za Atomiki duniani kwa pamoja wataweza kujadiliana masuala mbalimbali.

Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania ,Profesa Lazaro Busagala amaesema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika na kwamba wana imani mkutano huo utaweza kusaidia nchi washiriki kuweza kusonga mbele katika namna ya uboreshaji wa sekta mbali mbali kutokana na miradi inayofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani(IAEA).

Pia Profesa Busagala ameongeza kuwa mkutano huo pia utahudhuriwa na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki kanda ya AFrika Bwana Shaukat Abdurazak ambaye baada ya mkutano huo ataweza kufanya mazungumzo na viongozi mbali mbali na uongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Wizara nne ambazo zimekuwa zikihusika katika miradi mbali mbali ya kitaifa inayotekelezwa na Shirika la Nguvu za Atomiki duninia(IAEA) .
 
Alisemsa kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Mkurugenzi Shaukat atakutana na Waziri wa
Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi .

Kwa upande wa Tanzania Bara Shaukat atafanya mazungumzo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, na Waziri wa Maji.

Pia ataweza kufanya ziara katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Seliani,Taasisi ya Chakula na Lishe na Taasisi ya Saratani Ocean Road. 

Profesa Busagala alisema kuwa mazungumzo hayo yataweza kusaidia nchi kwenye uboreshaji wa miradi mbali mbali inayofanyika hapa nchini hasa katika sekta ya Afya, Kilimo, na maji.

Alieleza kuwa Tanzania ni moja ya nchi iiliyoweza kufaidika kwa kiasi kikubwa kwa miradi katika udhibiti na kuhamasisha matumizi salama ya tekenolojia ya nyuklia inayotekelezwa na Shirika la Nguvu za Atomiki duniani .

AWESO AWAASA WATAALAMU WA MAJI


Na EZEKIEL NASHON, DODOMA 

Naibu Waziri wa Maji Juma Aweso amewataka wataalamu wa maji kutumia taaluma zao vizuri, na kuacha tabia ya kuwadanganya viongozi pindi wanatofuatilia miradi katika maeneo yao  ya kazi kuwa miradi hiyo iko vizuri hali kwamba kuna kasoro katika miradi hiyo.


Aweso ameyasema hayo jana jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi  cha  wadau wa maji, Wakurugenzi, wakuu wa mamlaka za maji na wenyeviti wa bodi za maji waliokaa kwa siku mbili Dodoma kupewa uelewa namna ya utekelezaji wa sheria mpya maji na usafi wa mazingira, pamoja na uanzishwaji wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini.


Amesema wataalamu hao wamekuwa wakitumia taaluma zao vibaya katika nafasi zao na kufikia kipindi kuwadanganya viongozi kuwa hakuna shida kwenye miradi ya maji mbalimbali, lakini ukifuatilia kwa undani unakuta kuna matatizo mengi na wananchi hawapati maji.


“Hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa wataalamu wetu kwa sababu tukifika kukagua miradi ya maji tunaambiwa miradi iko vizuri lakini ikiikagua kwa umakini unakuta kuna matatizo makubwa, tabia hii muache natumaini kupitia kikao hiki mutakuwa mmejifunza mengi,” amesema.


Amesema hata sita kumfukuza kiongozi yeyote ndani ya mamlaka hiyo ambaye atakwenda kinyume na maelekezo yao, hata kama hata kama atakuwa vipi tutamtoa tu, japo hakuna mtu anayependa kumfukuza mtu katika kazi yake viongozi tunapenda kuwaona mkiwa kazini.


Pia amewataka kulinda taaluma zao vipaji, ujuzi na maalifa yao kuhakikisha wananchi wanapata huduma za maji kama makusudio ya serikali yalivyo, amewataka kujidhatiti kuhakikisha wanatatua kero zilizopo katika sekta hiyo.


Kwa upande wake Barnabas Ndunguru ambaye ni mkurugenzi wa Idara ya utawala wizara ya maji,aliyekuwa akimuwakilisha katibu mkuu, amesema watatumia taaluma zao kuhakikisha wanashirikiana na wizara kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kwa ufasaha na hasa katika kutekeleza majukumu ya mamlaka  mpya ya  maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA.


Nae afisa maji bonde la ziwa nyasa Alice Mnali, amesema watahakikisha wanalinda taaluma zao kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na kuleta anufaa katika jamii, na yale yote waliopata katika mawasilisho mbalimbali watahakikisha wanayatendea kazi, na hawatakuwa kikwazo katika sekta ya maji.