Tuesday, March 5, 2019

DC PANGANI AWAFUNDA VIJANA

MKUU wa wilaya ya Pangani Mkoani Tanga Zainabu Abdallah akizungumza wakati akifungua warsha ya vijana juu ya kutambua malengo 17 ya maendeleo endelevu  ya Dunia yaliyoendeshwa na serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) yakishirikisha vijana 100 wa kike na kiume kulia ni  Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Alvaro Rodrigues kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya ya Pangani (DAS) Mwalimu Hassani Nyange.
...........................


MKUU wa wilaya ya Pangani Mkoani Tanga Zainabu Abdallah amesema umaskini hauwezi kuondoka ikiwa vijana bado watakuwa mawazo ya potofu kuhusiana na umaskini huku wakitakiwa kuuchukia.

Zainabu aliyasema hayo mjini Pangani wakati akifungua warsha ya vijana juu ya kutambua malengo 17 ya maendeleo endelevu  ya Dunia yaliyoendeshwa na serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) yakishirikisha vijana 100 wa kike na kiume.


Alisema lazima vijana watambua upo umuhimu wa kutumia fursa zilizopo kwenye maeneo yao badala ya kukaa na kuacha kufikiria kukaa vijiweni na kujiingia kwenye makundi yasiyokuwa na tija kwa maendeleo.


“Matatizo ya vijana wanayafahamu vijana hivyo serikali ipo tayari
kuwaunga mkono kwa juhudi zozote mnatakazo anzisha …lakini pia mwaka huu kuna chaguzi za serikali za mita hivyo tunataka viongozi vijana tutakaoweza kuzungumza nao lugha moja na kusimamia maendeleo endelevu ya dunia”Alisema.


Aidha alisema kupitia mafunzo hayo yatasaidia kuongeza wigo mpana wa fursa kwa vijana wilayani humo ambao watakwenda kuibadilisha wilaya hiyo na kuwataka wazazi kuhakikisha wanawapatia elimu bora watoto waop badala ya kujiingiza kwenye shughuli za uvuvi.


Mkuu huyo wa wilaya aliwataka vijana wa Pangani kuchangmkia fursa hiyo ili iweze kuwasaidia ikiwemo kujitambua kwamba wana nafasi gani kwa Taifa na wilaya kwa kujiletea maendeleo kwani wao ndio chachu ya mafanikio kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kiuchumi, kisiasa na kujamii.


Awali akizungumza wakati wa warsha hiyo Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Alvaro Rodrigues alisema uwepo wao ni kwa ajili ya kutekeleza malengo endelevu ambayo ndio malengo ya dunia 2016 hadi 2030 kwa kuwapatia elimu vijana ili wawezi kujitambua na kuona namna ya kutumia fursa zilizopo kwenye maeneo yao.


Alisema pia kwenye mafunzo hayo wanajikita kuwasaidia wanawake kutokana na kwamba asilimia 50 ya watu duniani ni wanawake hivyo wakiachwa nyuma dunia inaweza kudhoofisha maendeleo.


“Nusu ya idadi ya watu dunia ni wanawake hivyo ikiwa wataachwa nyuma kwenye Nyanja zote za kimaendeleo maanake tutakuwa tumerudisha nyuma ukuaji wa uchumi kwa wananchi”Alisema


Hata hivyo alisema ifikapo 2030 wawe na ulimwengu bora kwa kuzingatia malengo ya milenia katika kuhakikisha vijana wanazingatia malengo ya maendeleo endelevu ambayo ni watu, sayari, ustawi, amani na ushirikiano.


Kwa upande wake Mwenzeshaji kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa Didi Nafisa aliwataka vijana walioshiriki kwenye warsha hiyo kuzingatia mafunzo hayo ili yaweze kuwa na tija ikiwemo kubadilisha maisha yao.


Nafisa ambaye pia ni Afisa Habari wa Shirika hilo alisema mafunzo hayo yatasaidia kuwakwamua vijana na tatizo la ukosefu wa ajira ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa nchi nyingi dunia.


“Tatizo la ukosefu wa kazi dunia linaongezeka kutoka watu milioni 170 kwa mwaka 2007 hadi kufikia milioni 202 mwaka 2012  hapo utaona sasa watu milioni 75 kati ya hao ni vijana wa kike na kiume”Alisema.
 Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Alvaro Rodrigues akizungumza kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Pangani Zainabu Abdallah kulia ni  Mwenzeshaji kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa Didi Nafisa ambaye pia ni Afisa Habari wa Shirika hilo
 
 Katibu Tawala wa wilaya ya Pangani (DAS) Mwalimu Hassani Nyange akizungumza
 Mwenzeshaji kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa Didi Nafisa ambaye pia ni Afisa Habari wa Shirika hilo akizungumza
Sehemu ya Vijana kutoka maeneo mbalimbali wilayani Pangani wakifuatilia warsha hiyo kwa umakini 

Monday, March 4, 2019

UMEME UTUMIKE KUONGEZA UFAULU SHULENI- MGALU.

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Bi. Subira Mgalu, Akizungumza wanafunzi wa Shule ya Msingi Chalinze Mzee iliyopo Chalinze Mkoani Pwani kabla ya kuzindua na kuwasha Umeme rasmi katika kijiji cha Chalinze Mzee Mkoani Pwani.
..................

Na Yasini Silayo, Pwani

Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati Mhe. Bi. Subira Mgalu akizindua na kuwasha rasmi miradi ya Umeme Vijijini katika Vijiji vya Chalinze Mzee A-C na Nero Vilivyoko Chalinze, Mkoani Pwani Leo ametoa Rai kwa vijiji vyote ambavyo tayari vimefikiwa ama kuunganishwa na huduma ya Nishati ya Umeme kuitumia fursa hiyo kuboresha ufaulu pamoja na kuinua kiwango cha elimu kwa ujumla.


“Ni mategemeo yetu kuwa ujio na matumizi ya Nishati ya umeme utaboresha na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule mbalimbali kutokana mazingira wezeshi ya kujisomea na kujifunza muda wote kwa kutumia mwanga wa umeme lakini pia kuendana na mahitaji ya elimu ya kisasa inayojikita zaidi katika sayansi na teknolojia hususan matumizi ya kompyupa na maabara za kisasa za mafunzo kwa vitendo” Alisema Mhe. Subira, Akiwa katika shule ya Msingi Chalinze Mzee kijiji Cha Chalinze mzee A, Mkoani Pwani.


Naibu Waziri Mgalu, Aliongeza kuwa, Ndoto ya Serikali ya Awamu ya Tano ni, kusambaza Nishati ya umeme Nchi Nzima na kwa wananchi wote, umeme utakaokuwa chachu ya maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo za Maendeleo ya Huduma za kijamii sambamba na zile za Kiuchumi, sekta ya elimu kwa vijana na watanzania kwa ujumla ikiwemo kama miongoni mwa sekta za vipaumbele.


Naye mwalimu mkuu wa shule hyo aliyejitambulisha kwa jina la Marianus Nyalale, mbali na kuelezea shukurani zake kwa kufikishiwa umeme mpaka shuleni hapo, alisema kuwa Shule ina matarajio makubwa ya kufanya mabadiliko makubwa ya kiufundishaji na ufaulu mara baada ya kuunganishwa na huduma ya umeme wa TANESCO.


“Tunategemea kuanza mpango wa kutafuta fedha kwaajili ya kununua compyuta na vifaa mbali mbali vya kufundishia vinavyotumia umeme lakini pia hivi sasa wanafunzi wataweza kujisomea madarasani hata vipindi vya jioni” alisema Mwl. Nyalale


Aidha, Mhe. Mgali akizindua na kuwasha rasmi umeme katika kijiji cha Nero, alisisitiza na wananchi pia kuchangamkia fursa ya umeme kwa kufanya shughuli mbalimbali za kimaemdeleo na kiuchumi. 


Shughuli zitakazopelekea wao kujiongezea kipato lakini pia kukuza uchumi wa Nchi kwa ujumla.

Sunday, March 3, 2019

Watanzania acheni matumizi ya "headphones" kupita kiasi...Waziri asema ni chanzo cha usikivu hafifu

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kulia) akifanyiwa uchunguzi wa sikio na Daktari bingwa wa masikio Dkt. Godlove Mfuko katika Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Bw. Makwaiya Makani akizungumza jambo katika siku ya Usikivu Duniani ambayo kitaifa imefanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (aliyeketi) akiwekewa vifaa vya uchunguzi wa usikivu na mtaalam wa usikivu Bi. Tedi Uiso kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu(kulia) akisalimiana na watoto waliofika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya usikivu. 




Dar Es Salaam
Spika za masikioni maarufu kwa jina la “Headphones” zimetajwa kuwa chanzo kinachopeleka tatizo la usikivu hafifu kwa watu.
Hayo yamesemwa leo na Waziri mwenye dhamana ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumza na wananchi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Jijini Dar Es Salaam katika kuadhimisha siku ya usikivu duniani.

Waziri Ummy amesema kuwa matumizi ya simu za kisasa yameongeza kasi ya watu kutumia spika za masikioni jambo ambalo linahatarisha kuwa na watu wengi wenye matatizo ya usikivu. 

“Unakuta kijana kuanzia asubuhi mpaka jioni ameweka spika za masikioni anasikiliza muziki hawajui wanajiweka katika hatari ya kupata tatizo la usikivu” amesema Waziri Ummy na kuendelea kusema kuwa kundi la vijana liko hatariki kupata matatizo ya usikivu.
Waziri Ummy ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi kupunguza matumizi ya spika za masikioni ili kuweza kujikinga na matatizo ya usikivu.
“Nitoe rai kwa vijana wapunguze matumizi ya spika za masikioni kwa muda mrefu, tusipo kuwa makini tunaweza kujikuta tuna taifa lenye watu wengi wenye matatizo ya kutosikia vizuri” amesema Waziri Ummy. 
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa tatizo la usikivu hutokea pia kwa njia mbalimbali ikiwemo kwa kuzaliwa na tatizo hilo au kulipata ukubwani kutokana na sababu nyinginezo ambazo zinaambata kwa kukaa kwa muda mrefu kwenye sehemu zenye kelele nyingi pamoja matatizo yanayoambata na afya ya sikio.
Waziri Ummy amesema kuwa ni jambo jema kuona sasa matibabu ya matatizo ya usikivu hafifu yanapatikana hapa hapa nchini huku akiwataka wananchi kukata bima za afya ili kuweza kupata matibabu kwa uhakika.
“Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha tatizo hili linazuiliwa kabla ya kutokea lakini pia kuhakikisha matibabu yanapatikana yakiwemo kutumia mashine ya mawimbi ya sauti, upasuaji wa kuziba tundu la ngoma ya sikio pamoja na kupandikizwa vifaa vya kusaidia kusikia” amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo alisema takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2018 Hospitali ya Muhimbili imefanikwa kuwapatia wagonjwa 116 vifaa vya mawimbi ya sauti, wagonwja 43 walifanyiwa upasuaji wa kuziba tundu la ngoma ya sikio.
Waziri Ummy amesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa na kuhakikisha matibabu yanapatikana hapa hapa nchini.
Awali akitoa taarifa yake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Bw. Makwaiya Makani amesema kuwa wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali katika eneo la usikivu ikiwemo kutoa huduma ya upandikizaji vifaa vya usikivu kwa Watoto wenye matatizo ya hayo.

“Tangu mwezi Juni mwaka 2017 tayari watoto 21 wamepandikizwa vifaa vya usikivu kitaalam kwa jina la 'cochlear implants” amesema Bw. Makani 
Bw. Makani amesema kuwa wameendesha kliniki ya siku mbili katika Hospitali ya Mloganzila kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya matatizo ya usikuvu ambapo watu 264 wamejitokeza kati yao watu 172 walihitaji uchunguzi zaidi wa usikivu, watu 64 wamekutwa na matatizo ya usikivu na tayari wamepatiwa rufaa kwa ajili ya matibabu zaidi na watu 31 wamekutwa na nta za masikioni,pia watu 26 wamekutwa na maambukizi kwenye masikio ambao wamepatiwa rufaa ya matibabu zaidi.
Tatizo la usikivu linazidi kuongezeka siku hadi siku. Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 5 ya watu duniani wana tatizo la usikivu. Tatizo hili litaongezeka maradufu kila mwaka. Inatakiwa kila mmoja achukue hatua kujikinga na tatizo hili ikiwemo kuepuka sehemu zenye kelele na pia kusikiliza mziki kwa sauti kubwa na kwa muda mrefu na kwa kutumia spika za masikioni.

Friday, March 1, 2019

HALMASHAURI YALAZIMISHWA KUHAMISHA DAMPO

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima (wa pili kutoka kushoto) akimsikiliza Mratibu wa Kanda kutoka Baraza la Taifa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Bw. Godlove Mwamsojo mara baada ya kutembelea dampo lililopo katika Kata ya Saja, Kijiji cha Itengelo Wilaya ya Wanging’ombe. Naibu Waziri Sima ameagiza kufungwa kwa dampo hilo na kuteketeza taka zote zilizopo.
…………………..
Na Lulu Mussa,Njombe
Halmashauri ya Mji wa Makambako Wilayani Njombe imeagizwa kusitisha mara moja utupaji wa taka ngumu katika dampo lililopo katika Kata ya Saja, Kijiji cha Itengelo Wilaya ya Wanging’ombe kutokana na kutokidhi matakwa ya Sheria ya Mazingira na malalamiko yaliyotolewa na wananchi katika vijiji vya jirani.
Agizo hilo limetolewa hii leo Mkoani Njombe na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima mara baada ya kufanya ziara ya kikazi na kumuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Makambako Bw. Rashid Hozi kutafuta eneo maalumu litakalokidhi mahitaji husika ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya athari kwa mazingira
Akiwa katika eneo hilo la dampo la Makambako ambalo kwa hivi sasa liko katika Wilaya ya Wanging’ombe, Mhe Sima ameshuhudia wananchi wakiingia kiholela katika dampo hilo kwa ajili ya kuokota bidhaa mfano chupa za plastiki kwa ajili ya kuziuza.
“Serikali inatumia pesa nyingi katika huduma za afya ni wakati sasa tupunguze mzigo huu kwa magonjwa yanayoweza kuepukika kwa kuwa na mazingira safi na salama. Kuanzia sasa ni marufuku wananchi kuingia dampo kuokota chupa za plastiki, hii inahatarisha afya zao wenyewe, hivyo utaratibu wa kutenganisha taka uanzie katika vyanzo vya uzalishaji” Sima alisisitiza.
Awali Mratibu wa Kanda wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira  (NEMC) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Bw. Godlove Mwamsojo amesema kuwa Baraza limetoa notisi ya siku sitini (60) kuanzia tarehe 01/02/2019 kwa Halmashauri hiyo ya kusitisha utupaji wa taka katika eneo hilo na kuwaagiza kuteketeza taka zote zilizopo katika kipindi kilichotajwa.
Bw. Mwamsojo amesema kuwa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 119 kinazitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kutafuta namna bora ya kuteketeza taka ngumu katika maeneo yao na kuainisha kuwa dampo hilo kwa sasa liko katika eneo la mwinuko hivyo kipindi cha mvua hutiririsha maji ambayo si salama kwa wakazi wa maeneo ya chini.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Sima pia amemuagiza Mratibu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha anafuatilia utekelezaji wa agizo hilo na endapo Halmashauri haitatekeleza agizo hilo hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao .
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Makambako Bw. Rashid Hozi amekiri kupokea barua ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira na kuahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa kwa muda muafaka.
Naibu Waziri Mussa Sima, yuko katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Nyanda za juu Kusini kuainisha changamoto za kimazingira katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na  kukagua mitambo ya kuteketeza taka hatarishi katika Hospitali, kujionea hali ya madampo katika mikoa husika endapo utaratibu wa kutenganisha taka unazingatiwa ili kuzuia wananchi kuzifuata baadhi ya bidhaa zinazo rejerezeka katika maeneo ya dampo kwa lengo la kudhibiti milipuko ya magonjwa.
Katika Mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa Mheshimiwa Sima pia atapata fursa ya kuembelea kwenye ikolojia ya vyanzo vya maji vinavyo changia maji katika bonde la Rufiji.