Tuesday, February 26, 2019

WATUMISHI SEKTA YA AFYA WAASWA KUTOFANYA KAZI KWA MAZOEA

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akipokea daftari la mama aliyemleta mwanae kupata huduma katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Ligula, wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali hiyo. Wakatikati ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Lobikieki Kissambu.
...................................


Na WAMJW – MTWARA

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewaasa watumishi wa wekta ya afya nchini kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea, na wajikite katika kutoa huduma kulingana na sheria na taratibu za taaluma zao.


Ameyasema hayo leo wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya kwa wananchi katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara – Ligula.


Katika ziara hiyo Dkt. Ndugulile amesema kuwa licha ya jitihada za kuboresha huduma za afya kwa wananchi, ni wajibu wa kila mtoa huduma za afya nchini kuhakikisha anatimiza wajibu wake bila shurti na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.


“Nyinyi mnafanya kazi kwa mazoea, kwa nini hamjajaza taarifa wala kusaini katika fomu ya wagonjwa, na hili linaendana na maelekezo ambayo Serikali tunawapa, kwamba kila mtu aandike tarehe na muda ambao amefanya kazi, nyinyi maabara hamfanyi” alisema Dkt. Ndugulile


Pia, Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali imeboresha vituo vya afya zaidi ya 300, ambavyo vitatoa huduma za dharura za upasuaji wakumtoa mtoto tumboni, na hospitali za wilaya 67, katika Mkoa wa Mtwara hospitali za wilaya 3 zinaenda kujengwa, ili kupunguza mzigo katika hospitali za mikoa,


Aidha, DKt. Ndugulile amesema kuwa amesema kuwa kutokana na Hospitali hiyo kuwa na Changamoto za x-ray na gari la kubebea Wagonjwa, Serikali imeahidi kuzitatua changamoto hizo kwa muda mfupi ili wananchi wa Mtwara waanze kupata huduma hizo mara moja.


“Mmeongelea huduma za mionzi (x-ray), niwaahidi tutawaletea mashine mpya ya x-ray za kidigitali, lakini vile vile kama kuna changamoto ya gari la kubebea wagonjwa, zikija tutazigawa, tunataka hospitali za mikoa zianze kuonekana kwamba ni hospitali za mikoa kweli” alisema Dkt. Ndugulile


Mbali na hayo Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali inatambua pengo la watumishi katika sekta ya afya,  hivyo mwaka uliopita iliweza kuajiri watumishi takribani 11,000, huku watumishi 3000 kuziba pengo la watumishi ambao hawakuwa na vigezo, na 8000 walikuwa ni ajira mpya.


“Tumeweza kuajiri Watumishi takribani 11,000, 3000 kuziba pengo la watumishi ambao hawakuwa na vigezo na vyeti, na ajira mpya ni 8000, kuwahiyo jumla watumishi 11, kadri tunavoendelea kupata uwezo tutaendelea kuongeza rasilimali watu kuhakikisha kwamba tunaziba mapengo yaliyopo” alisema DKt. Ndugulile.
 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua mkoba wa Vifaa vya kujifungulia, wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Ligula.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua Kadi inayoonesha Idadi ya Dawa katika Chumba cha dawa, wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Ligula.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua  Idadi ya Wagonjwa waliosajiliwa kwenye mfumo, wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Ligula.

TASAF KUWAFIKIA WALENGWA WOTE- MKUCHIKA.

Kutoka Kushoto alievalia suti ya Blue  ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga katika ni Mzee Athumani  Nadonde  mnufaika wa kaya masikini kijiji cha Maumbika  Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani Lindi akitoa maelezo mafupi kwa Waziri wa Ofisi ya Rais menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Mkuchika ya namna alivyofanikiwa kuweka Bati katika Nyumba yake
......................................


NA HADIJA HASSAN, LINDI.
 

Serikali imesema kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF awamu ya iii B imedhamiria kuwafikia walengwa wote wanaostahili kuingizwa kwenye Mpango wa kunusuru kaya masikini 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawara bora kapteni msaafu George Mkuchika jana  alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata ya Mahumbika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani Humo.

Mkuchika alisema awamu hiyo ya tatu B inatarajiwa kuanza mapema katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 na kwamba Serikali imekwishafanya maandalizi ya jambo hilo.

Alisongeza kuwa changamoto kubwa iliyokuwepo kwa TASAF  ni Kutowafikia walengwa wote katika Vijiji ambapo mpaka sasa ni asilimia 70 tu ndiyo waliofikiwa huku  30% wakiwa bado kufikiwa.

Ameongeza kuwa katika mpango huo wa kunusuru kaya masikini licha ya Baadhi ya Wananchi kutonufaika na mradi katika maeneo yao pia vipo vijiji vingine ambavyo havijafikiwa kabisa na Mpango huo huku akiwataka wananchi ambao wako kwenye mpango lakini bado hwajafikiwa kuwa wavumilivu.

Awali akisoma Taarifa ya Utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF 3) Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga alisema  Halmashauri ya wilaya ya Lindi ni miongoni mwa Halmashauri zinazotekeleza Mpango wa Kaya Masikini ambapo jumla ya kaya 9732 ziliandikishwa katika vijiji 88 viliivyoingizwa  kwenye mpango kati ya vijiji 140  vilivyopo katika Wilaya hiyo.

Hata hivyo Ndemanga alisema kuwa idadi hiyo imeendelea kupungua  kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo , vifo, kuhama pamoja na uhakiki endelevu ambao umekuwa ukiwaondoa walengwa waio na sifa za kuendelea kuwemo kwenye Mpango

Aidha amesema hadi kufikia Novemba-Disemba 2018 idadi za kaya zinazoendelea kunufaika na mpango huo wa kunusuru kaya masikini ni 8,842 katika vijiji 88 vya Wilaya hiyo.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Lindi amebainisha pia  kuwa katika mpango huo baadhi ya Walengwa wameweza kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha shughuli ndogo ndogo za uzalishaji mali na kuboresha makazi yao lakini pia wamejiunga katika vikundi vya kuweka na kukopa.

Akitoa ushuhuda mbele ya Waziri Mkuchika  Athumani Nandonde mnufaika wa Mpango huo wa kumusuru kaya masikini aliishukuru Serikali kwa kuanzisha mpango huo kwani kupitia fedha anazozipata kutoka TASAF ameweza kuweka bati katika nyumba yake huku akiwahasa walengwa wezie kutumia fedha wanazozipato kupitia mpango huo kuzitumia katika mambo ya maendeleo

Muonekano wa Nyumba ya Mzee Athumani Nandonde Mnufaika wa Mpango wa kunusuru kaya masikinj  Mkazi wa kata ya Maumbika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani Lindi