Tuesday, February 26, 2019

MGALU AZINDUA UMEME KIJIJI CHA NAMATULA, NACHINGWEA.

Image may contain: 4 people, including Subira Mgalu, people smiling
NA HADIJA HASSA, LINDI

Naibu Waziri wa Nishati Subira  Mgalu amezindua  Umeme katika kijiji cha Namatula kilichopo wilaya ya Nachingwea  mkoani  Lindi  kinachopelekewa umeme na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kwa kuwasha katika shule ya sekondari Namatula

Kuwashwa kwa umeme katika shule hiyo uwenda utakuwa mwarobaini wa shule hiyo kufanya vizuri katika mitihani yao ya kitaifa kwa mwaka 2019

Ikumbukwe kuwa shule ya sekondari ya Namatula ilishika nafasi ya mwisho kitaifa katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018 .

Awali akizungumza na walimu pamoja na wanafunzi Mgalu Alisema uwepo wa umeme huo uwe chachu ya kufanya vizuri katika mitihani yao ,pamoja na kuhaidi kufuatilia hatua kwa hatua katika matokeo ya mitihani ya majiaribio,moko na hata ile ya kitaifa

Mgalu pia aliwataka wanafunzi wa Shule hiyo  kusoma kwa bidii ili kubadilisha matokeo mabaya ya mwaka uliopita , pamoja na kuwataka wanafunzi wa kike kuepuka vishawishi kwa vijana wa kiume

“Nawaomba musome watoto wangu hasa watoto wa kike, mshika mawili moja umponyoka ni aibu sana tukionekana mikoa ya kusini na ukanda huu kwamba sisi wanafunzi wetu wengi wanafeli kwa sababu ya kupata ujauzito wakati tupo sisi wenzenu wa mfano tumetoka kusini na tulivumilia hizo mimba tulikuja kuzipata baadae baada ya kuanza maisha yetu” alisema Mgalu

Akizungumza mara baada ya kuwashwa umeme huo Mkuu wa shule hiyo  Alidi Namulungu, alisema kuwa moja ya  sababu iliyowafanya wafanye vibaya katika Mtihani wa Mwaka uliopita ni Wanafunzi kukosa Nishati mbadala ya kusomea hasa nyakati za usiku kwani walikuwa wanatumia vibatari ambavyo vilikuwa vinamwanga hafifu

Alisema upatikanaji wa umeme huo utakuwa mkombozi kwa walimu na wanafunzi hasa wakati wa kujiandaa na mitihani yao kwa wanafunzi hao kuweza kusoma nyakati za jioni  pamoja na kuwasaidia katika suala la ulinzi na usalama shuleni hapo

Image may contain: 6 people, including Subira Mgalu, people standing and outdoor
Image may contain: 5 people, including Subira Mgalu, people standing, tree, sky, outdoor and nature

VIJANA TUMIENI FURSA ZILIZOPO NCHINI KUANZISHA VIJIWE VYA KIUCHUMI - WAZIRI MHAGAMA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wanakikundi cha Rasupashoma Group, Bw. Ibrahim Malabela jinsi wanavyotengeneza viatu bora na vyenye kudumu kwa muda mrefu. (Mwenye miwani ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali (Mst.), Nicodemus Mwangela na (Kulia) ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na vijana wanaopata mafunzo ya kilimo bora na ufugaji wa kisasa katika kituo cha Maendeleo ya Vijana – Sasanda kilichopo Kata ya Nyimbili, Mkoani Songwe alipofanya ziara kukagua maendeleo na miradi ya vijana katika kituo hicho.
...........................


Na; OWM (KVAU) – SONGWE

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa zilizopo kwenye maeneo yao kwa kuanzisha vijiwe vya kiuchumi.


Kauli hiyo ameitoa na Waziri Mhagama wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo na miradi ya vijana iliyopo katika Kituo cha Maendeleo ya Vijana, Sasanda kilichopo Kata ya Nyimbili, Mkoani Songwe.


Akiwa katika ziara hiyo Mhe. Mhagama alieleza kuwa, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeendelea kutimiza azima yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, hivyo vijana watumie fursa hiyo kujifunza mambo muhimu na kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo vitawafanya wabadilishe vijiwe wanavyokaa kuwa vya kiuchumi.


“Tunataka kuona vijana watakapo jifunza kilimo bora, ufugaji wa ng’ombe au nyuki wataweza kuboresha thamani mazao na bidhaa kwa kuanzisha viwanda vidogo ndani ya Mkoa wa Songwe, mkakati wetu katika kituo hiki ni kutoa mafunzo yatakayowawezesha vijana kuongeza thamani ya mazao na bidhaa watakazozalisha ambazo zitakuwa ni kichocheo muhimu katika kufikia maendeleo yao” alisema Mhagama


Aliongeza kuwa, Takribani vijana 500 kwenye kituo hicho wamejifunza stadi za maisha, ufundi na elimu mbalimbali zinazotolewa kwenye kituo ambazo zitawawezesha kujipatia kipato.


Sambamba na hilo, Mhe. Mhagama aliwahimiza Viongozi wa Mkoa kushirikiana na Ofisi yake ili waweze kuwasaidia vijana ambao wamekwisha anzisha viwanda vidogo vidogo ndani ya mkoa huo kwa kuwawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuwatafutia soko la uhakika ndani na nje ya nchi.


Aidha, Waziri Mhagama alitoa rai kwa vijana kujiunga kwenye vikundi ambavyo ni endelevu na vyenye muelekeo  wa kuanzisha viwanda  vidogo vitakavyowawezesha kujiajiri na kuajiri wenzao na pelekea kufikia uchumi wa kati kama mpango wa maendeleo wa taifa unavyoelekeza. 


Pia, aliwaelezea juu ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru ambazo zitafanyika katika Mkoa huo na kuwataka vijana na wanawake kutumia fursa hiyo kuutangaza vyema mkoa wa Songwe.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Bw. James Kajugusi alieleza kuwa kituo cha Maendeleo ya Vijana cha Sasanda kimewawezesha vijana kujitambua na kujiwekea malengo ya maisha na kuyatekeleza kwa faida yao, jamii na taifa kwa ujumla.


“Tunatarajia kuanzisha mafunzo na programu zitakazowaelekeza vijana masuala ya kilimo biashara ambacho kitasaidia upatikanaji wa malighafi zitakazokuwa zinahitajika kwenye viwanda vilivyopo nchini,” alisema Kajugusi


Naye Bw. Silia Kibona ambaye ni mnufaika kupitia kituo hicho, aliishukuru Serikali kwa kuwajengea mazingira ya kujifunzia ambayo yamewasaidia kupata mafunzo muhimu na aliwahamasisha vijana wenzie kuhudhuria mafunzo yanayotolewa kwenye kituo hicho.


Kituo cha Maendeleo ya Vijana – Sasanda kilianzishwa mwaka 1979 kwa ushirikiano wa Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni wa Taifa, Vijana na Michezo iliyopo wakati huo pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. 

Uanzishaji wa Kituo hicho ulifuatia kuanzishwa kwa mpango wa kuunda vikundi vya vijana vya uzalishaji mali, uliolenga kuwawezesha vijana wasio na ajira kuweza kujiunga na kufanya kazi za kujitegemea hasa katika sekta ya kilimo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na vijana walionufaika kupitia kituo cha maendelo ya vijana, Sasanda alipotembelea kuona mradi walioanzisha katika Kata ya Nyimbili. (Wenye miwani) ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali (Mst.), Nicodemus Mwangela.