Saturday, February 23, 2019

MHE. MKUCHIKA AWAKUMBUSHA MAAFISA UTUMISHI KUINGIZA TAARIFA SAHIHI ZA WATUMISHI KWENYE MFUMO WA HCMIS


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb), akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi (hawapo pichani) katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo. Kushoto ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Dkt. Bora Haule.
 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb), akijibu hoja za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo. Kushoto ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Dkt. Bora Haule.

..................................


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika amewakumbusha Maafisa Utumishi kuingiza taarifa sahihi za watumishi kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) ili kutozalisha watumishi hewa na kupunguza kero kwa wastaafu katika kupata haki zao kama inavyostahili.

Mhe. Mkuchika ameyasema hayo wilayani Ruangwa wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, kabla ya kutembelea utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, endapo maafisa utumishi watashindwa kuingiza taarifa sahihi za watumishi kwenye mfumo wa HCMIS itasababisha kupoteza taarifa na ikitokea mtumishi kufariki au kustaafu itapelekea Ofisi ya Rais Utumishi kukosa taarifa sahihi za mtumishi huyo wanapotaka kuandaa stahili zake.

“Niwakumbushe maafisa utumishi nchini kuhakikisha mnatimiza wajibu wenu kwa kuwahudumia ipasavyo watumishi wa umma walio katika maeneo yenu ya kazi na wananchi kwa kutoa huduma bora kwa wakati na bila upendeleo,” Mhe. Mkuchika amesema.

Aidha, Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, endapo maafisa utumishi watatekeleza wajibu wao ipasavyo, watumishi wastaafu watapata haki yao ya kulipwa mafao kwa wakati kama inavyostahili na kuwahimiza maafisa utumishi kufuatilia mafao ya watumishi wastaafu kwa moyo bila kulazimishwa wala kutaka rushwa.

Mhe. Mkuchika amesema kuwa, ili Serikali iweze kufanikisha zoezi la ulipaji mafao kwa mtumishi mstaafu kwa wakati na kwa usahihi, ni wajibu wa Afisa Utumishi kuhakikisha taarifa zilizopo kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) ni sahihi.

“Si jambo zuri kwa mtumishi kusafiri kutoka kituo chake cha kazi kwenda Ofisi ya Rais Utumishi, Dodoma kufuata huduma ambayo Afisa Utumishi anaweza kuitatua,” Mhe. Mkuchika amesisitiza.

Mhe. Mkuchika ameweka bayana kuwa, endapo mtumishi atafuata huduma Ofisi ya Rais Utumishi, atamrudisha mtumishi huyo kwenye kituo chake cha kazi ili jambo lake lifanyiwe kazi na Afisa Utumishi husika.

Ameongeza kuwa, Serikali imetoa mafunzo ya matumizi ya mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) kwa maafisa utumishi lakini mpaka sasa, Ofisi ya Rais Utumishi imekuwa ikipokea malalamiko ya watumishi wanaosafiri kutoka vituo vyao vya kazi kwenda Dodoma kuangalia taarifa zao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) yuko katika ziara ya kikazi mkoani Lindi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.
 

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hashim Mgandilwa akitambulisha makundi ya watumishi waliohudhuria kikao kazi kati ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo mkoani Lindi.

Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Katibu wa Chama cha Walimu wilaya ya Ruangwa, Bi. Suzan Eliamini akiuliza swali wakati wa kikao kazi kati ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) akikagua ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Namkonjela, wilayani Ruangwa mkoani Lindi iliyojengwa kwa fedha za TASAF. Kushoto kwake ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Dkt. Mahela Godfrey na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Dkt. Bora Haule.   

MICHEZO NI MUHIMU KWA USTAWI WA AFYA-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Shule ya Sekondari ya  St. Pamachiwa  Inclusive wilayani Hai, Februari 22, 2019. Kulia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Isaac Amani na wa pili kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
...........................


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema wanafunzi wanatakiwa washiriki katika michezo mbalimbali kwa sababu ina umuhimu mkubwa kwa ustawi wa afya ya binadamu pamoja na maendeleo ya nchi. 

Ameyasema hayo jana (Ijumaa, Februari 22, 2019) wakati akizindua shule ya Sekondari Jumuishi ya Mtakatifu Amachius Inclusive katika wilaya ya Hai, Kilimanjaro. Amezindua shule hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.

“Lakini katika dunia ya leo michezo ni ajira na chanzo kikubwa cha mapato kwa vijana na Taifa kwa ujumla. Kwa kifupi michezo ni moja ya sekta muhimu kwa maendeleo ya Taifa, hivyo wazazi waruhusuni watoto washiriki.” 

Alisema kutokana na umuhimu wa michezo, Serikali imetenga vipindi kwa ajili ya elimu ya michezo katika ratiba za masomo na kuendesha mashindano ya michezo shuleni yaani UMITASHUMTA na UMISSETA. 

Waziri Mkuu alisema kuna wakati baadhi ya shule hususani za binafsi, dini na mashirika zimekuwa hazioni umuhimu wa kuwa na vipindi hivi au kushiriki katika mashindano. 

“Hivyo, taasisi zetu zizingatie kuwashirikisha wanafunzi katika programu za ufundishaji michezo na kushiriki mashindano ili waweze kujenga afya ya mwili na akili, kukuza amani, ushirikiano, upendo na mshikamano kati ya yao.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuutaka uongozi wa shule ya Sekondari Jumuishi ya Mtakatifu Amachius Inclusive kuwa na walimu watakaofundisha vipindi vya michezo pamoja na kuwawezesha wanafunzi wao kushiriki mashindano ya michezo.