Monday, February 18, 2019

JUMAA :CCM ITASHINDA NAFASI ZOTE SERIKALI ZA MITAA.

MJUMBE wa  mkutano  mkuu wa chama cha  mapinduzi (CCM) kupitia mkoa wa Pwani Haji Jumaa  alisema kuwa kipindi hiki  cha uchaguzi awana wasiwasi  wa aina yeyote yule kuhusu viongozi wao  kuchaguliwa.


Kauli  hiyo  ameitoa jana wakati wa mkutano wa viongozi wote wa chama hicho katika kata ya Nianjema wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ambapo walikuwa wakijadili kile  walichowafanyia wananchi tangu  kuchaguliwa kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.


Aliongeza  kuwa usemi  huo unatokana  na kile kilichoahidiwa kwa wananchi na viongozi wetu  kipindi walipokuwa  wakiomba ridhaa ya kuongozi na jinsi walivyotekeleza ahadi zao.


"Naamini chaguzi zijazo CCM itashinda  kila  kitongoji bila kupoteza  hata  kimoja kutokana na uwepo wa utitili wa maendeleo kwa wananchi kuwa ya uhakika na huduma walizokuwa  wakizihitaji kuwafikia"Alisema Jumaa.


Aliongeza kuwa kutokana na kazi  kubwa  inayofanywa na mwenyekiti wa Ccm taifa  ambaye pia ni Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuwa mstali wa mbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi kazi ya uchaguzi ujao itakuwa  kama tunasukuma mlevi.


Aidha  aliongeza  kuwa kwa mkoa wote Ccm imejipanga kuwa na viongozi imara na watakao kuwa ni chaguo sahihi la wananchi  na watakao  waletea maendeleo wanayoyahitaji.


Kwa upande  wake diwani wa kata hiyo ya Nia njema Abdul Pyalla amempongeza Mnec huyo kwa jinsi alivyoelezea mambo mengi  yaliyofanywa na Rais  wa jamhuri ya muungano wa Tanzania katika kipindi hiki na hivyo  kuwarahisishia wagombea .


Aliongeza kuwa kwa kata ya Nia njema kuna mengi yamefanyika ikiwemo kujenga shule  moja ya msingi, kituo cha Afya na shule ya sekondari  pia wamefanikiwa kuchimba visima  tisa vya maji na ukarabati wa barabara  za mitaa.


Akitoa maelezo shukurani kwa viongozi na wanachama  wa chama hicho katibu wa Ccm wilaya hiyo Salum  Mtelela alisema kuwa pindi watakapo  pata  waraka  wa uchaguzi wanachama wote  watapewa taarifa  kwa lengo la kuwapata  viongozi ambao  ni chaguo sahihi la wananchi.

ZAIDI YA BIL 10 KUTENGWA KWA AJILI YA KILIMO CHA MICHIKICHI – MHE MGUMBA

 Naibu waziri wa kilimo mhe omary mgumba (mb) akipanda mti wa mchikichi ikiwa ni ishara ya kuzindua upanuzi wa
shamba la zao hilo katika kambi ya jeshi la kujenga taifa ya
bulombora wilayani uvinza, februari 17, 2019. Wakati wa ziara ya waziri mkuu mhe kassim majaliwa yenye lengo la kuhamasisha  ufufuaji wa zao
la michikichi. 

Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa akisisitiza jambomara baada ya kukagua shamba la mikungu ya mchikichi iliyochavushwa kitalaam ili kupata mbegu bora wakati alipotembelea Kituo cha Utafiti wa Michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma, Februari 17, 2019
 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mikungu ya mchikichi iliyochavushwa kitalaam ili kupata mbegu bora wakati alipotembelea Kituo cha Utafiti wa Michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma, Februari 17, 2019. 
................................................

Na Mathias Canal, wizara ya Kilimo-Kigoma
Serikali imeeleza dhamira yake ya kukabiliana na uagizaji wa mafuta ya kula nje ya nchi kwa kuanzisha mashamba ya michikichi ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa mafuta na uimarishaji wa sekta ya kilimo cha mazao hayo kwa wananchi.

Tayari Wizara ya Kilimo imetenga zaidi ya Bilioni 10 kwa ajili ya kuendeleza zao hilo katika Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine nchini yenye uwezo wa kuzalisha zao hilo katika mwaka wa fedha ujao.

Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 17 Februari 2019 wakati akieleza namna wizara yake ilivyojipanga kuimarisha zao la Michikichi wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) Mkoani Kigoma.

“Mhe Waziri Mkuu tusingeweza kusubiri hadi mwezi wa saba kwa ajili ya kupitisha bajeti badala yake tayari tumetumia mbinu zingine kwa kutumia fedha za matumizi ya kawaida (OC) kwa ajili ya kuanza kutekeleza adhma ya serikali ya kuendeleza zao la Michikichi na kumaliza zao la mafuta” Alikaririwa Mhe Mgumba.

Alisema kuwa tayari Wizara ya Kilimo imepeleka watumishi wawili Mkoani Kigoma waliobobea katika utafiti wa Michikichi katika Taasisi ya utafiti wa Kilimo TARI-Kihinga huku wengine 10 wakiwa mbioni kuwasili mkoani Kigoma tayari kwa kuanza kazi hiyo.

Pia alisema kuwa Kituo cha Utafiti wa Michikichi TARI-Kihinga sio kituo kidogo tena badala yake kitakuwa kituo kikuu cha Utafiti wa zao hilo nchini huku vituo vingine vyote vya utafiti wa Michikichi vikiwa chini ya Kituo cha TARI-Kihinga.

Mhe Mgumba amezipongeza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Magereza kwa ushirikiano wanaouonyesha katika uimarishaji na uendelezaji wa zao la Michikichi.

“Kama unavyofahamu mchakato wa kuandaa miche ya michikichi unachukua zaidi ya mwaka mmoja na nusu kuanzia kuchavisha mpaka kuwa mche kwa ajili ya kupeleka kwa wakulima, hivyo ushirikiano huo tunaoupata ni utimilifu wa uratibu wa zoezi hili” Alisema

VIJANA ANZISHENI MASHAMBA YA MICHIKICHI-MAJALIWA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka vijana mkoani Kigoma waanzishe mashamba ya michikichi kwa kuwa zao hilo litawapatia kipato cha uhakika.


 Amesema Serikari imedhamiria kufufua zao la michikichi ili kuliwezesha Taifa kujitosheleza kwenye mafuta ya kula na kuokoa fedha za kigeni.


 Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Februari 18, 2019) alipowasalimia wananchi wa kijiji cha Nyakitondo wilayani Kasulu akiwa njiani kwenda Kibondo.


 Waziri Mkuu ambaye yupo mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kufufua kilimo cha michikichi amesema ni vema wananchi wakachangamkia fursa hiyo.


 “Vijana limeni michikichi kwani ukipanda ukiwa darasa la tano baada ya miaka mitatu utaanza kuvuna na kujipatia kipato ambacho kitakuwezesha kujikimu.”


 Amesema kilimo cha zao la michikichi kitawawezesha wananchi hususani vijana kupata mitaji ya uhakika kwa ajili ya shughuli zingine za kiuchumi.


 Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga kuhakikisha Tanzania inaongoza kwa kilimo cha zao la michikichi katika nchi za Afrika Mashariki.


 Kadhalika, Waziri Mkuu amewahamasisha wananchi hao wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili wawe na uhakika wa matibabu kwa yao na familia zao.


 Wakati huohuo Waziri Mkuu ametembelea kambi ya Wakimbizi ya Nduta wilayani Kibondo na kukagua shule ya msingi Kassim Majaliwa na baadae wodi ya wazazi katika Hospitali Nduta.