Sunday, February 3, 2019

MIAKA 42 YA CCM YAADHIMISHWA KWA KUFANYA USAFI CHALINZE

Image may contain: 2 people, people standing and outdoor
 Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Bagamoyo kimeadhimisha miaka 42 ya siku ya kuzaliwa kwa chama hicho kiwilaya katika kata ya Pera kijiji cha Pingo katika Halmashauri ya wilaya ya Chalinze kwa kufanya usafi katika eneo la Ujenzi wa shule ya sekondari ya Pera inayojengwa kwa nguvu za wananchi na kituo cha afya cha Pingo. 


Maadhimisho hayo yamepambwa na wananchi,vikundi mbalimbali vya sanaa na wanachama wa chama cha Mapinduzi kutoka Halmashauri Zote mbili wilayani Bagamoyo na Vijana wa chama cha Mapinduzi ambao waliandamana kutoka eneo la Ujenzi wa shule ya sekondari ya Pera hadi eneo la mkutano katika viwanja vya kijiji cha Pingo.


Maandamano hayo yaliyoongozwa na Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Bagamoyo Bwana John Francis Masenga na kupokelewa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo Bwana Sheriff Zahoro. 


Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo katika hotuba yake aliyasema mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kitaifa lakini pia katika ngazi ya wilaya kwa kuyasema mafanikio yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Chama cha Mapinduzi katika nyanja mbalimbali za maisha hususan katika sekta za Elimu, Afya na utoaji huduma kwa wananchi Kwani watumishi wa serikali wamekuwa waadilifu na wanatoa huduma kwa wananchi kwa wakati.


Aidha aliwashukuru madiwani, wabunge na Mkuu wa wilaya kwa usimamizi na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Mwisho aliwataka wananchi kuendelea kuiunga Mkono serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Image may contain: 1 person, smiling, sitting and outdoor 
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo Bwana Sheriff Zahoro akizungumza katika maadhimisho hayo.
Image may contain: 4 people, people sitting 

Friday, February 1, 2019

DC KAWAWA ATOA SALAMU ZA SERIKALI CHALINZE

Image may contain: 1 person, sitting and indoor
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Mheshimiwa Zainabu Kawawa akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani Halmashauri ya Chalinze.
................................. 


Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Mheshimiwa Zainabu Kawawa amewataka waheshimiwa madiwani wa Halmashauri  ya Chalinze wilayani humo, kuwaelimisha wafanyabiashara wadogo ili wapate vitambulisho vya ujasiriamali ambavyo vimetolewa na serikali kwa kulipia Tsh 20,000.


Aidha amewaonya wanasiasa kutoingiza siasa katika zoezi la ugawaji vitambulisho bali zoezi hilo lizingatiwe sheria taratibu na miongozo iliyotolewa na serikali katika kuwakwamua wajasiriamali kiuchumi,na akaagiza zoezi hili liwe limekamilika kabla ya mwezi Machi mwaka huu.


Mheshimiwa Kawawa akazungumzia ufaulu wa matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2018 na kuipongeza Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo kwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa na kuitaka Halmashauri  ya Chalinze kuweka mikakati ya ushindi kitaaluma kama ilivyo kwa Halmashauri ya Bagamoyo. 


Hata hivyo Mheshimiwa Kawawa aligusia changamoto ya ukosefu wa maji katika Halmashauri ya chalinze na kulaani kitendo cha mkandarasi aliyeahidi kupatikana kwa maji wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuendelea kulifanyia kazi suala la maji.


Mwisho Mama Kawawa aliwashukuru watendaji wa Halmashauri ya Chalinze kwa kumpa ushirikiano katika utendaji kazi na kuwataka wataalamu wafanye kazi zao kwa kuzingatia taaluma zao na kuwa wakweli kwa utekelezaji wa Majukumu ya serikali "Nataka serikali inapotoa fedha za miradi nione mradi umetekelezeka kwa wakati pasipo ubabaishaji hiyo ndiyo kazi ya mwanasiasa kuona matokeo".Kawawa alisema.


Imeandaliwa na msemaji wa Halmashauri ya Chalinze.
Image may contain: 4 people
Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Chalinze wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa alipokuwa akizungumza katika kikao hicho.


WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUHAMASISHA MATUMIZI YA BIMA YA AFYA.

Meneja Mahusiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, (NHIF)  Anjela Mziray 
 .........................................................

Na Hadija Hassan, MTWARA.

Waandishi wa habari Nchini Tanzania wametakiwa kutumia Taaluma  zao katika kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kutumia Bima ya Afya  ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,(NHIF)

Wito huo umetolewa na  Meneja Mahusiano wa Mfuko huo  Anjela Mziray wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha waandishi wa Habari wa Vyombo mabali mbali wa Mikoa ya Lindi na Mtwara

Kikao hicho chenye lengo la kuimarisha mahusiano , kupeana ufahamu wa mambo mabil mbali yaliyojitokeza na yanayoendelea kujitokeza yanayohusiana na Bima ya Afya na kuweka mikakati ya pamoja  ya jinsi ambavyo Mfuko huo  unaweza kushirikiana na wanahabari  katika kuelimisha Umma

Mziray alisema waandishi wa habari wamekuwa na nafasi kubwa ya kuleta mrejesho  katika Mfuko huo,

“tunajua kama waandishi wa habari mmetumia vyema kalamu zenu katika kuwahabarisha umma juu ya shughuli tunazozifanya, kwa kutambua umuhimu wenu mfuko wa taifa wa Bima ya Afya unakili kwamba bado unauhitaji mkubwa wa kundi hili Muhimu ” Alisema Mziray

Mziray aliongeza kuwa  kama waandishi wa habari ni wajibu wao  kuendelea kuelimisha Umma kuwa Afya ni msingi wa Maendeleo na ni mtaji wa kila Mwananchi kwani unamuwezesha kupanga mipango yake ya kimaendeleo katika ngazi ya kaya pamoja na  kuchangia pato la taifa

“ifike maali wananchi wote hapa nchini waone umuhimu wa kutumia Bima ya Afya kwani mara zote ugonjwa hauna muda wala saa, na wala haupigi hodi unaweza kuugua wakati wowote tena mbaya zaidi ukiwa huna hata fedha ya hakiba mfukoni hivyo kutumia Bima ya Afya ni kama kujiwekea Akiba pale unapougua kwani hutohangaika tena kutafuta fedha kwa ajili ya matibu” aliongeza Mziray

Kwa upande wake Lucy Ogutu mwandishi wa habari wa ITV Mkoa wa Mtwara alisema ili wananchi wengi  waweze kuhamasika zaidi juu ya utumiaji wa Bima za Afya ni muhimu kwa Serikali kupanua Wigo wa upatikanaji wa Vifaa tiba pamoja na Madawa katika Vituo vya Afya na Zahanati hasa za vijijini ambako wanakosa chaguo la pili kama watakosa huduma kutoka katika Zahanati hizo

Akifunga kikao hicho mwnyekiti wa klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Lindi, Christopha Lilai  Aliushukuru uwongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuwakutanisha pamoja  waandishi wa habari wa Mikoa hiyo pamoja na kuwahasa waandishi wa Habari  kujiunga na ufuko huo.

WAINGIZA MAGENDO PWANI KUKIONA.

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI 

JESHI la polisi mkoani Pwani, limeweka bayana kuendelea kukaza uzi, katika kupambana na wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kwa njia za magendo kwa lengo la kukwepa ushuru na kuisababishia serikali kukosa mapato. 


Kutokana na kuchukua hatua hiyo jeshi hilo, limefanikiwa kukamata madumu 86 ya mafuta ya kula ambayo hayajalipiwa ushuru yakiwa yamehifadhiwa ndani ya stoo ya mfanyabiashara Mmas Athumani (35) mkazi wa Kongowe Kibaha mkoani hapo. 


Akieleza juu ya suala hilo, kamanda wa polisi mkoani Pwani, (ACP) Wankyo Nyigesa alisema, madumu hayo yamefikia jumla ya madumu 107  ya mafuta ya kula yaliyokamatwa katika kipindi cha wiki moja.


“Taarifa tumezipata kutoka kwa raia wema, ambapo walieleza mafuta hayo yameingizwa nchini kupitia Bagamoyo na kukwepa ushuru wa serikali kisha kusafirishwa kwa njia za panya hadi kwenye stoo hiyo eneo la Kongowe “alifafanua Wankyo. 


Alitaja mafuta ni dumu moja lita 20 aina ya jenau, madumu 26 ya lita 20 aina ya MTRA pamoja na madumu 59 ya lita 20 aina ya oki. 


Aidha Wankyo alisema, pia limekamata mifuko 18 ya sukari ambayo imeingizwa nchini kutoka nchi jirani kwa kukwepa ushuru. 


Wakati huo huo, wanamsaka mfanyabiashara mmoja ambae kwa sasa jina linahifadhiwa aliyetoroka baada ya kuona maafisa wa polisi wakimfatilia na kutelekeza madumu 21 ya mafuta ya kupikia aina ya Micogold yenye ujazo wa lita 20 kila moja ambayo hayajalipiwa ushuru eneo la Magomeni Bagamoyo. 


Kamanda huyo alitoa wito kwa wafanyabiashara, kuacha kujihusisha na biashara za magendo na ukwepaji wa ushuru katika biashara wanazofanya .


Wankyo aliwapa salamu kwamba, watambue hawapo salama kwani jeshi hilo limejipanga vilivyo kwenye KUTINDUA  mitandao yote ya wafanyabiashara wanaoingiza mali za magendo na ukwepaji ushuru kupitia bandari bubu.