Thursday, January 17, 2019

MIL. 40 ZAKARABATI MABWENI CHANGARIKWA, CHALINZE.


Mwenyekiti wa Bodi ya shule Sekondari ya Changalikwa Omari Mhando akikagua moja ya mabweni yanayokarabatiwa.
Picha na Omary Mngindo.
...........................................................


Na Omary Mngindo, Chalinze.

KIASI cha shilingi milioni 40 zilizotolewa na Halmashauri ya Chalinze, wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, zinakarabati mabweni manne katika shule ya sekondari ya Changarikwa iliyoko Kata ya Mbwewe wilayani hapa.


Hatua hiyo inalenga kuboreshwa kwa miundombinu shuleni hapo kwenye mabweni ya Benjamen Mkapa, Jakaya Kikwete na Salma Kikwete, ili wanafunzi wawe katika mahali safi na salama wakati wakipata elimu yao.


Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi shuleni hapo Omary Mhando, aliyewahi kuwa diwani kwenye Kata hiyo miaka kadhaa iliyopita, ambapo alisema wamepokea fedha kiasi cha shilingi milioni 40 kwa ajili ya zoezi hilo.


Aliongeza kwamba awali mabweni hayo yalikuwa katika hali mbaya kutokana na uchakavu wa milango na madirisha, ambapo baada ya kupatikana kwa fedha hizo kazi inakwenda vizuri, na kwamba wanategemea kumalizika ifikapo mwishoni mwa mwezi wa pili.


"Shule yetu chini ya Mwalimu Mkuu
Sylivester Omari imekiwa na  changamoto kubwa ya uchakavu wa milango na madirisha, tukaomba fedha halmashauri yetu ya Chalinze, wakatuingizia kiasi cha shilingi milioni 40 ambazo tunaendelea nazo katika ukarabati," alisema Mhando.


Aliongeza kwamba mpaka sasa wakati kazi hiyo ikielekea ukingoni wametumia kiasi cha shilingi milioni 13, na kwamba wanataraji kutengeneza vitanda vya chuma vipatavyo 100 katika fedha hizohizo za shilingi milioni 40.


Kwa upande wake mwalimu Tete Emulike amezungumzia changamoto ya ukosefu wa uzio shuleni hapo, hali inayosababisha ufinyu wa usalama wa mali za shule, na wamafunzi na kwamba kipindi cha mapumziko ya wanafunzi kunakuweo na uvamizi mkubwa wa mifugo.


"Shule yetu ina eneo kubwa ambalo halina uzio, hali hii inahatarisha usalama wa wanafunzi na vifaa, pia kipindi cha likizo za wanafunzi mifugo inakuwa kero kwani inaingia ndani ya eneo hali inayosababisha usumbufu mkubwa," alisema Mwalimu Emulike.


Nae mmoja wa mafundi aliyejitambulisha kwa jina la Juma Semlamba alisema kwamba kazi ya ukarabati wa milango itakamilika ndani ya siku saba kuanzia Jumatano ya Jan 16 na kukabidhi kazi hiyo.


Ukarabati huo mbali ya milango ya mbao katika vyumba vya mabweni hayo, pia imewekwa milango ya vyuma (Mageti) nje ya mabweni hayo hali inayothibitisha kuimarishwa kwa miundombinu hiyo.

MGUMBA AKERWA NA KITALU CHA MIWA KIGONGONI BAGAMOYO.

 Naibu waziri wa Kilimo, Omari Mgumba (kushoto) akiongea kwa uchungu kuhusu shamba la miwa la Kigongoni Bagamoyo, ambalo mpaka sasa halijafanyiwa kazi.
........................................... 

Naibu waziri wa Kilimo, Omari Mgumba amekerwa na kitendo cha kuchelewa kuanza shughuli za upandaji mbegu za  miwa katika kitalu cha Kigongoni ambapo Jeshi la Magereza limeingia mkataba na NSSF.


Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea vitalu hivyo na kukuta pori lililotelekezwa, Naibu waziri huyo alisema serikali inatumia muda, na fedha katika kuanzisha miradi mbalimbali hivyo kila mtu kwenye nafasi yake anapaswa kutimiza wajibu wake ili kutimiza malengo ya serikali.


Alisema katika awamu hii ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli kila mtu anapaswa kuwajibika ipasavyo na kuacha ubabaishaji ili dhamira ya Rais ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi iwezi ionekano kwa vitendo.


Aliongeza kwa kusema kuwa, watendaji wa serikali, na taasisi zake wamekuwa wakifanya kazi kwa kusua sua ukilinganisha na taasisi binafsi jambo ambalo alisema katika awamu hii kila atakaejaribu kukwamisha miradi ya serikali hatovumiliwa.


Katika hatua nyingine Naibu waziri huyo amefurahishwa na shamba la miwa la Bagamoyo Sugar ambapo miwa yake imestawi vizuri kwaajili ya uzalishaji wa sukari katika kiwanda cha Bagamoyo sugar kilichopo kata ya Makurunge wilaya ni Bagamoyo.


Alisema Bagamoyo sugar inastahili pongezi kutokana na uwekezaji wake ambao unaona nia ya dhati ya uanzishwaji wa kiwanda hicho.

Mratibu wa Kiwanda cha Bagamoyo sugar, Sufiani alisema kiwanda hicho kitakapokamilika kinatarijiwa kuzalisha sukari huku mabaki ya miwa kuzalishia umeme.
 Mkuu wa Gereza la Kigongoni, Mrakibu wa Magereza (SP) Muyengi Bulilo akionyesha ramani ya shamba la miwa Kigongoni Bagamoyo.
 
 Naibu waziri wa Kilimo, Omari Mgumba (kushoto) akikagua shamba la miwa la Bagamoyo sugar lililopo kata ya Makurunge wilayania Bagamoyo, Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa anaefuata ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda.
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa (kulia) akimuonyesha Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda shamba la miwa kwaajili ya uzalishaji wa sukari katika kiwanda cha Bagamoyo sugar.