Wednesday, January 16, 2019

BENKI YA KILIMO IHARAKISHE MALIPO YA KOROSHO – WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  wakuu wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma  katika kakao alichokiitisha kwa njia ya video akiwa ofisini kwake jijini Dodoma, Januari 16, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
.......................................

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) ihakikishe inabadilisha mfumo wake ili iweze kuharakisha malipo kwa wakulima wa korosho ambao wameshahakikiwa.


Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, 16 Januari, 2019) wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TADB kwenye kikao alichokiendesha kwa njia ya video (video conferencing) kutokea ofisini kwake Mlimwa, Dodoma.


Wakuu wa mikoa hiyo mitatu walikuwa kwenye mikoa yao na Mkurugenzi Mkuu wa TADB, alikuwa Dar es Salaam.


“Hakikisha mnaharakisha malipo ya wakulima lakini pia suala la uhakiki linabaki palepale ili tuwalipe wakulima wanaostahili,” amemweleza Mkurugenzi Mkuu wa TADB, Bw. Japhet Justine.


Waziri Mkuu amesema Serikali bado inapokea malalamiko kutoka kwa wakulima kuhusu suala la malipo ya korosho kwani kwa kawaida malipo ya mkupuo yote huwa yamekamilishwa ifikapo Januari 10 ya kila mwaka.


“Matarajio yetu yalikuwa ni kuvuna tani 245,000 au zaidi kidogo lakini umesema hadi sasa korosho zilizo kwenye maghala ni tani 206,000 maana yake takriban tani 40,000 ziko AMCOS au majumbani kwa wakulima. Na ambazo mmezilipia hadi sasa ni tani 92,000 na pointi zake. Tuko chini ya nusu.”


“Hili zoezi la uhakiki na malipo, lilianza Novemba 27, 2018 na leo ni tarehe 16 Januari, 2019 na hatujafika hata asilimia 50, maana yake zoezi hili tutalimaliza Aprili mwanzoni. Haiwezekani! Tunapata lawama kutoka kwa wakulima wa korosho kwa sababu hii kasi ni ndogo; na haya siyo malengo ya Mheshimiwa Rais, aliyetaka korosho zinunuliwe na Serikali.”


Waziri Mkuu alihoji ni kwa nini benki hiyo haishirikiani na vyama vikuu (unions) au vyama vya msingi (AMCOS) ili kubaini idadi halisi ya wakulima na idadi kamili ya kiasi walichovuna kwa sababu kila AMCOS ina wanachama wake wanaojulikana.


“Zao la korosho lina mfumo wa ushirika. AMCOS ziko kwenye ngazi ya vijiji na unaweza kukuta AMCOS moja ina wanachama zaidi ya 200, sasa bila kupitia kwenye hizi AMCOS unawezaje kujua kila mkulima amevuna kilo ngapi na anadai kiasi gani kwa kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko pekee?


“Kuna Wilaya zina AMCOS zaidi ya 50. Ni kwa nini msitumie mfumo huo lakini mkawatenga kwenye makundi mawili yaani wakulima wenye chini ya kilo 1,500 au zaidi ya 1,500 ili muweze kufanyia uhakiki kwa urahisi?” aliluliza.


Ameitaka benki hiyo izishirikishe AMCOS na UNIONS pindi malipo yanapofanyika ili nao wajue ni wanachama wao gani ambao wameshalipwa. “Mfumo unaotumika sasa unapeleka malipo moja kwa moja kwenye akaunti ya mtu binafsi, kwa hiyo AMCOS wanakuwa hawana taarifa, na wao pia wanachangia kushiriki kutoa malalamiko.”


Waziri Mkuu pia alitumia fursa hiyo kuwataka wakuu wa mikoa hiyo wahuishe taarifa zao na wamtumie ili aweze kuzitumia kuratibu zoezi zima. “Mniletee taarifa zenu mkionesha ni kiasi cha korosho mlitarajia kuzalisha; mmeshakusanya kilo ngapi hadi sasa ambazo ziko kwenye maghala; kama malipo yameanza, ni wakulima wangapi wameshalipwa; 


na fedha kiasi kila mkoa umeshapokea hadi sasa,” amesisitiza.
“Nimeongea na wakurugenzi wa CRDB na NMB na kuwasisitiza kuwa suala la miamala ya malipo ya korosho lifanywe mchana na usiku ili malipo yakamilike kabla ya Januari mwishoni,” amesema.


Kwa upande wao, wakielezea changamoto wanazokabiliana nazo, wakuu hao wa mikoa walisema kuwa suala kubwa ni ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima, baadhi ya AMCOS na vyama vya msingi kulipwa mara nyingi zaidi ya vyama vingine, miamala ya malipo ya wakulima kukataliwa na Benki na hali ya kutoaminiana baina ya timu ya uhakiki na watendaji wa wilaya na mikoa ambao ni wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama.


Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa TADB, alisema fedha iliyolipwa kwa wakulima wa korosho hadi sasa ni sh. bilioni 306 kwa wakulima zaidi ya 156,000. “Korosho zilizolipwa hadi sasa ni tani elfu 92.7 ambazo ni wastani wa asilimia 44,” alisema.


Hata hivyo, Bw. Justine alisema zaidi sh. bilioni 11 zimekwama kulipwa kwani taarifa za kibenki zinaonyesha kuna matatizo hasa kwenye majina.
“Majina ya waliopeleka mzigo, yanatofautiana na majina ya akaunti za benki. Majina yaliyokataliwa na mfumo wa kibenki yatabandikwa kwenye vyama vya msingi ili wakulima wakarekebishe taarifa zao,” alisema.


Alisema takriban sh. bilioni 15 zimelipwa wa watoa huduma ambao ni wasafirishaji, wapagazi na wenye maghala.

Tuesday, January 15, 2019

BENKI KUU YAHAMISHA MALI NA MADENI YA BANK M KWENDA BENKI YA AZANIA

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Bernard Kibesse akitangaza uamuzi wa Benki Kuu kuhamisha mali na madeni ya Bank M kwenda Azania Bank Limited leo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam
..........................................


Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kuhamisha mali na madeni ya Bank M kwenda Azania Bank Ltd.


Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Bernard Kibesse, amesema katika mkutano na waandishi wa habari BoT jijini Dar es Salaam tarehe 15 Januari 2019 kwamba kwa sasa, Benki Kuu, Azania Bank Ltd na wadau wengine wanaendelea kuandaa taratibu za kisheria za kukamilisha mchakato wa uhamishaji wa mali na madeni ya Bank M kwenda Azania Bank Ltd.


“Wateja wenye amana na wadau wengine wa Bank M watataarifiwa tarehe ya kuanza kupata huduma za kibenki kupitia Azania Bank Ltd,” alisema na kuongeza kuwa “wateja wenye mikopo wanatakiwa kuendelea kulipa mikopo yao kulingana na mikataba yao.”


Katika mkutano ambao pia ulihudhuriwa na Naibu Gavana (AIC), Bw. Julian Banzi Raphael, Dkt. Kibesse alisema, Benki Kuu iliamua kuhamisha mali na madeni ya Bank M kwenda benki nyingine kama njia ya kutatua matatizo ya benki hiyo ambayo imekuwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu tangu mwezi Agosti mwaka 2018.


Katika Naibu Gavana Kibesse amewahakikishia wananchi kwamba Azania Bank Ltd “itakuwa na ukwasi wa kutosha kuweza kuwahudumia wateja wake na wateja wapya kutoka Bank M baada ya kuchukua mali na madeni ya benki hiyo.”


“Mtaji wa Azania Bank Limited unatarajiwa kufikia kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 164 ambacho ni juu zaidi ya mtaji wa shilingi bilioni 15 unaotakiwa kisheria,” alisema.


Naibu Gavana ameuhakikisha umma kwamba Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kulinda maslahi ya wateja wenye amana katika mabenki na kuimarisha uhimilivu katika sekta ya fedha nchini.


Benki Kuu ya Tanzania ilichukua usimamizi wa Bank M Ltd mnamo tarehe 2 Agosti 2018 baada ya Benki Kuu, ambayo inajukumu la kusimamia na kudhibiti mabenki na taasisi za fedha, kubaini kuwa Bank M ilikuwa na upungufu mkubwa wa ukwasi na hivyo kushindwa kulipa madeni yake.


Baada ya kuiweka chini ya usimamizi wake, Benki Kuu ilisitisha shughuli za utoaji wa huduma za kibenki za Bank M kwa muda wa siku 90 ili kuipa nafasi Benki Kuu kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.


Mnamo tarehe 2 Novemba 2018 Benki Kuu iliongeza muda wa usimamizi kwa siku 60 ili kupata muda wa kutosha wa kutathmini hali ya kifedha ya Bank M, ambayo ilikuwa ni hatua muhimu katika utatizo wa matatizo ya Benki hiyo. Hatua hizo ndio zimefikisha hatua ya leo.


Bank M ilipewa leseni na kuanza kufanya shughuli za kibenki hapa nchini mwaka 2008, na kuwa miongoni mwa benki zilizokua kwa haraka na kuwa na mali zenye thamani zaidi ya shilingi za Kitanzania trilioni moja. Bank M ilikuwa na jumla ya matawi matano, matatu yakiwa jijini Dar es Salaam na mengine mawili yakiwa katika majiji ya Arusha na Mwanza.

DC LINDI ATAKA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA YA KUBANGUA KOROSHO.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shahibu Ndemanga akizungumza na wajasiliamali.
................................................

Na Hadija Hassan, Lindi

Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shahibu Ndemanga amewataka wajasiliamali wa Wilaya hiyo kuchangamkia fulsa ya ubanguaji  wa korosho  iliyotolewa na Serikali ili waweze kujikwamua kiuchumi

Ndemanga ameyasema hayo Leo alipokuwa anafunga mafunzo ya ubanguaji bora wa korosho yaliyotolewa na shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo Sido mkoa wa Lindi yaliyofanyika Mjini hapo

Ndemanga alisema Serikali ilipoamua korosho zote zibanguliwe ndani ya Nchi ilikuwa na lengo la kuinua uchumi wa Wananchi wake

Alisema uamuzi wa Sido wa kuwakusanya Wajasiliamali na kuwapa mafunzo ya ubanguaji bora wa korosho ni kitendo cha kizalendo kwani kutawafanya wajasiliamali hao kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya ubanguaji  vitakavyoweza kuwaongezea vipato vyao

Kwa upande wake  Afisa uendelezaji mafunzo kutoka katika shirika hilo la Sido Aizack Daniely  alisema kuwa katika mafunzo hayo ya siku tano yenye  Lengo la kuongeza kasi  ya uongezaji wa thamani  katika zao la korosho ili wananchi waweze kupata kipato kupitia ubanguaji na kutoa ajira kwa jamii, jumla ya wajasiliamali 48 wameshiriki kutoka wilaya za Lindi na  Nachingwea wakiwemo  wanawake 15na wanaume 33

Danieli alisema katika mafuzo hayo washiriki walipata fulsa ya kujifunza hatua  za ubanguaji bora wa korosho , Teknolojia na ubanguaji bora na usalama na Afya kiwandani

Aliyataja mambo mengine kuwa ni ubora , usalama na usafi wa chakula (korosho) katika   uzalishaji, utumiaji  na matengenezo madogo  madogo  katika mashine za ubanguaji ,upangaji  wa madaraja  pamoja na  ufungashaji  na utunzaji  wa madaraja kwa korosho zilizobanguliwa

Nae Meneja wa Sido mkoani hapo Mwita Kasisi alisema kuwa Mafunzo hayo yataendelea kufanyika katika wilaya zingine  kulingana na mahitaji ya wilaya husika

Kasisi aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo washiriki wataweza kupata ajira kutokana na viwanda vya ubanguaji wa korosho vitakavyofunguliwa  na wengine watakwenda kuanzisha viwanda vyao ambavyo vitatengeneza ajira kwa wananchi wengine

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa Chama Cha Wabanguaji Wadogo wadogo Mkoa wa Lindi,  mwalimu mstaafu Mariamu Kaisi alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza kasi ya utendaji kazi tofauti na awali walipokuwa  wanabangua korosho hizo kwa mazoea

Wajasiliamali hao wakiwa katika mafunzo ya ubanguaji bora wa korosho
Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shahibu Ndemangaakikabidhi cheti kwa mmoja wa wajasilimali hao.