Wednesday, January 9, 2019

BALOZI WA UHOLANZI NCHINI AIPONGEZA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI)

 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi na  Balozi wa Uholanzi nchini Mhe.  Jeroen Verheul  pamoja na wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya  kumaliza kwa ziara ya Mhe. Balozi  ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa  kwa wananchi. 
....................................


Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepongezwa kwa jitihada zake inazozifanya  za  kuweza kuwafikia wananchi wengi  kwa  kutoa huduma bora za matibabu, elimu na ushauri wa jinsi ya kuepukana na magonjwa ya  moyo.


Pongezi hizo zimetolewa na Balozi wa Uholanzi nchini Mhe.  Jeroen Verheul  alipokuwa  akiongea na wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakati wa ziara yake ya kuangalia huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wagonjwa.


 Mhe. Verheul alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ni moja ya Taasisi zinazofanya kazi vizuri ya kutoa huduma ya matibabu ya moyo  katika nchi zilizopo Kusini mwa Afrika .


Kuhusu Ubalozi wake  kushirikiana na Taasisi hiyo katika utoaji wa huduma kwa wananchi alisema ataangalia ni jinsi gani watashirikiana  katika programu  mbalimbali za afya ambazo zinatolewa  hapa nchini kupitia  Ubalozi wa Uholanzi.


“Wiki tatu zijazo nitaenda nchini Uholanzi ambako tuna mkutano wa mabalozi wote. Kupitia mkutano huo nitaangalia ni Taasisi ipi ambayo itaweza kuja nchini kufanya matibabu ya moyo kama ilivyokuwa kwa nchi zingine ambazo zinatuma wataalamu wake kuja  katika Taasisi hii kutoa huduma za matibabu kwa wananchi”,alisisitiza Mhe. Verheul.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi alimshukuru Mhe. Balozi kwa kuwatembelea na kuona huduma mbalimbali wanazozitoa  na kusema kuwa wanajitahidi kuhakikisha kila mwananchi anayefika katika Taasisi hiyo anapata huduma bora za matibabu ya moyo.


Alisema idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka ukilinganisha na miaka ya nyuma hii inaonyesha kuwa hivi sasa wananchi wenye matatizo ya moyo wanaelewa ni wapi pa kwenda kutibiwa magonjwa hayo.


“Kutokana na wataalamu wetu kuwa na utaalamu wa kutosha na hospitali kuwa na vifaa vya kisasa tumeweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa wengi zaidi kwa mwaka 2018 ukilinganisha na mwaka 2017”.


“Mwaka 2018 tumefanya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa 1053 na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 405 ambapo mwaka 2017 tulifanya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa 225 na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 800”, alisema Prof. Janabi.


Akiwa katika Taasisi hiyo Mhe. Balozi Verheul alitembelea maabara ya uchunguzi wa matatizo na tiba za magonjwa ya moyo (Cath Lab), jengo jipya la watoto ambalo ukarabati wake ukikamilika   litakuwa na vitanda  32 na vitanda tisa katika  chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU), wodi ya watoto na wagonjwa waliofanyiwa na wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua,  chumba cha upasuaji na chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU).
 Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Huduma ya Uuguzi Robert  Mallya akiongea jambo na  Balozi wa Uholanzi nchini Mhe.  Jeroen Verheul  wakati balozi huyo alipotembelea  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo wanazozitoa.  Kushoto ni Mhandisi  wa umeme wa Taasisi hiyo Victor Kaduma.
 Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Sulende Kubhoja akisalimiana na  Balozi wa Uholanzi nchini Mhe.  Jeroen Verheul  wakati balozi huyo alipotembelea  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo wanazozitoa. Katikati ni  Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Huduma ya Uuguzi Robert Mallya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimweleza  Balozi wa Uholanzi nchini Mhe.  Jeroen Verheul  jinsi maendeleo ya ukarabati wa wodi ya watoto unavyoendelea wakati balozi huyo alipotembelea  JKCI kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo wanazozitoa.  Ukarabati wa jengo hilo ukikamilika  litakuwa na vitanda  32 na vitanda tisa katika  chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU).
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiagana na  Balozi wa Uholanzi nchini Mhe.  Jeroen Verheul  mara baada ya balozi huyo kumaliza ziara yake  ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo  kwa wananchi.
Picha na JKCI

RAIS, DKT. MAGUFULI AMTAKA WAZIRI DOTO BITEKO KUANZISHA VITUO VYA MADINI MIKO INAYOFANYA SHUGHULI ZA UCHIMBAJI.

Na Grace Semfuko-MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli  leo Januari 9,2019 amewaapisha viongozi mbalimbali aliowateua Ikulu Jijini Dar Es Salaam na kuwataka kufanya kazi kwa  kuzingatia weledi.


Viongozi walioapishwa ni pamoja na Waziri wa Madini Dotto Biteko, Makatibu Wakuu wa Wizara watatu, Manaibu Makatibu wakuu wa Wizara wawili,Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Balozi pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma na Makamishna sita wa Tume hiyo.


Akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi hao Ikulu Jijini Dar es Salaam Rais Magufuli alimtaka Waziri mpya wa Madini Dotto Biteko kusimamia rasilimali za Madini kwa kuanzisha vituo vya madini kwenye mikoa inayofanya shughuli za uchimbaji.


Rais alisema kumekuwa na changamoto kubwa kwenye sekta ya madini ambapotaarifa zinaonyesha   Tanzania kuongoza katika uchimbaji wa Madini katika Nchi za Afrika Mashariki lakini  imekuwa na kiwango cha chini cha uuzaji wa madini kwenye nchi hizo na kuhoji ni kwa nini kumekuwa na hali hiyo.


Ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Benki kuu ya Tanzania BoT kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa dhahabu kwa wachimbaji hatimaye iweze kuuzwa nje kwa fedha za kigeni ili kuiongezea nchi pato la fedha hizo.


“Ripoti mbalimbali katika nchi za Afrika Mashariki zinaonyesha Tanzania kuwa nyuma katika uuzaji wa dhahabu wakati sisi ndio tunaongoza katika uchimbaji, kwa ripoti hii ni lazima tujiulize tunakwama wapi? Dhahabu tunazochimba zinauzwa wapi? Soko lipo wapi na tunalijua? Tunapouza tunapata fedha kiasi gani? Wizara ipo na wataalamu wake na hapo ndio changamoto inapoonekana” Alisema Rais Magufuli.


“Ndio maana wanasema nabadilisha badilisha viongozi, sitaacha kubadilisha na hata Biteko ukifanya vibaya nitakutoa tu na nitaweka mtu mwingine, nafanya hivi kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania, sisi tumepewa dhamana lazima tuwatumikie Watanzania” alisema Rais Magufuli


Alisema kwa muda mrefu dhahabu imekuwa hainufaishi nchi ingawa sheria zimerekebishwa lakini bado kumekuwa na changamoto kubwa na kuitaka Wizara ya Madini kusimamia bidhaa hiyo na pia kushirikiana na wachimbaji wengine katika kudhibiti madini hayo muhimu kwa Taifa.


Rais pia alitoa pungezi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro kwa kusimamia utoroshwaji wa madini uliofanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu wakishirikiana na baadhi ya viongozi wa juu wa Jeshi hilo wanane wa Mkoa wa Mwanza.


“Nikupongeze IGP kwa kusimamia vyema zoezi lile, na wale askari wafanyiwe uchunguzi na kuchukuliwa hatua ikibainika, naomba vyombo vya habari muandike habari zenu kwa uhakika na sio kupotosha, mfano kuna gazeti moja limeandika habari ya kupotosha kuhusiana na kukamatwa kwa dhahabu ile mkoani Mwanza” alisema Rais Magufuli.


Rais pia aliwataka viongozi aliowateua kushirikiana na kuacha migogoro mahali pa kazi na kwamba anatambua baadhi ya maeneo ambayo viongozi hawaelewani na wakati mwiongine kutoleana maneno yasiyofaa huku akitolea mfano kwenye maeneo ya Nyasa, Gairo na Manispaa ya Dodoma.


Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa aliwataka viongozi walioapishwa kushirikiana katika kuimarisha maendeleo ya wananchi na kwamba ofisi yake itahakikisha wanapata ushirikiano wa kutosha.


Nae Spika wa Bunge Job Ndugai alimwomba Rais Magufuli kuwapa likizi mawaziri angalau kwa muda ili waweze kupumzika ombi ambalo Rais Magufuli alisema iwapo Watanzania hawana likizo katika ujenzi wa Taifa na mawaziri wanatakiwa kufanya kazi  bila kupumzika.


Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma nae alisema Mahakama itashirikiana na viongozi hao katika kuimarisha uhusiano na kufanya kazi kwa kuzingatia weledi.


Viongozi 14 waliapishwa katika hafla hiyo akiwepo Dotto Biteko kuwa Waziri wa Madini ambaye awali alikuwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula ameapishwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya,maendeleo ya jamii,jinsia wazee na watoto, Dorothy Mwaluko ameapishwa na kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na uwekezaji na Elius Mwakalinga kuwa Katibu Mkuu Ujenzi.


Wengine ni Profesa Faustine Kamuzora aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Kagera ambaye awali alikuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dorothy Gwajima kuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI na Dkt Francis Michael kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora.


Aidha Rais pia aliwaapisha Viongozi wa Tume ya Utumishi wa Umma akiwepo Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Steven Bwana pamoja na Makamishna sita wa tume hiyo akiwepo George Yambesi, Yahya Mbila, Daniel Ole Njoolay, John Haule, Hadija Ally Mohamed Mbarak pamoja na Immaculete Ngwale.