Friday, November 2, 2018

VIJIJI VYA CHALINZE VYATAKIWA KUTHAMINI MICHANGO YA WADAU

 Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chalinze,Mheshimiwa Saidi Zikatimu akizungumza wakati wa kufungua ofisi ya serikali ya kijiji cha Tonga kilichopo kata ya Msoga.
.....................................
 
Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, Mheshimiwa Saidi Zikatimu,amevitaka vijiji kutambua michango mbalimbali ya wadau katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya halmashauri ya Chalinze,agizo hilo amelitoa leo katika hafla ya ufunguzi wa ofisi ya Serikali ya kijiji cha Tonga katika kata ya Msoga.

Ofisi ya serikali hiyo ya kijiji imejengwa kwa ushirikiano wa halmashauri ya wilaya,kijiji na wadau mbalimbali wa maendeleo katika halmashauri na kugharimu jumla ya fedha za kitanzania milioni 25.1.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa ofisi hiyo Zikatimu amewapongeza viongozi wa serikali ya kijiji cha Tonga kwa kuwatambua wadau waliochangia katika ujenzi wa ofisi ya kijiji na kuwataka viongozi wa vijiji vingine wilayani humo kuendelea kuwatambua na kuwashukuru kwa jitihada wanazozifanya wadau katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Aidha Zikatimu katika hotuba yake ya ufunguzi wa ofisi ya kijiji aliwataka vijana na wanawake kujiunga katika vikundi na kupata mikopo kutoka mfuko wa vijana na wanawake unaotokana na mapato ya halmashauri."Halmashauri tunazo pesa kwa ajili ya kuwakopesha vijana bila riba tunatekeleza ilani kwa vitendo karibuni tuijenge nchi kwa pamoja."

Aliendelea kuwashukuru wadau mbalimbali wa maendeleo wanaojishughulisha na utatuzi wa kero mbalimbali kwa kuipongeza kampuni ya SAYONA Fruits ambayo imekuwa ikiisaidia halmashauri ya wilaya katika kuboresha huduma za jamii kwa kukamilisha ujenzi wa jengo la maabara na nyumba ya mganga katika kijiji cha Mboga.

Mwenyekiti wa halmashauri aliwataka wananchi kuitumia ardhi na siyo kumiliki ardhi pasipo kuiendeleza na kwa wanaomiliki ardhi bila kuiendeleza serikali itachukua hatua ikiwa ni pamoja kuichukua ardhi hiyo na kuirejesha kwa wananchi ili itumike kwa mujibu wa sheria taratibu na kanuni na si vinginevyo.

Hata hivyo Diwani wa kata hiyo Hassani Mwinyikondo aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Tonga kwa kujitoa kujenga ofisi nzuri na ya kisasa na hii ni namna ya kuboresha miundombinu katika sekta ya utawala bora na kuvitaka vijiji vyote ndani ya kata ya Msoga kuanzisha ujenzi wa ofisi za serikali za vijiji ili utoaji huduma kwa wananchi uwe na tija.
 
 Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, Mheshimiwa Saidi Zikatimu, akifungua ofisi ya serikali ya kijiji cha Tonga kilichopo kata ya Msoga.
   
Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, Mheshimiwa Saidi Zikatimu, akipanda mti katika eneo la ofisi ya serikali ya kijiji cha Tonga mara baada ya kuifungua rasmi ofisi hiyo

RAIS DKT. MAGUFULI AONGOZA KIKAO CHA BARAZA LA MAWAZIRI IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika leo Ijumaa tarehe 2 Novemba  2018 Ikulu jijini Dar es Salaam.

PICHA NA IKULU

MAJALIWA AMAFARIJIKA NA MAENDELEO YA VIWANDA.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema amefarijika na maendeleo ya ujenzi wa viwanda kwenye mkoa wa Tanga kwa sababu vitasaidia katika ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira.

Aliyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Novemba 1, 2018) alipotembelea kiwanda cha saruji cha Rhino na kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh, vyote vya jijini Tanga.

Waziri Mkuu ambaye jana alihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga, aliwapongeza wawekezaji wa viwanda hivyo kwa kuunga mkono mkakati wa Serikali. 

Alisema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kukuza uchumi kutoka wa chini hadi wa kati ifikapo 2025 kwa kupitia sekta ya viwanda.

Akizungumzia kuhusu kiwanda cha Rhino, Waziri Mkuu alisema kiwanda hicho na vingine vya saruji nchini vitasadia kupunguza gharama ya saruji nchini na kurahisisha ujenzi.

“Serikali inaamini kwamba uwepo wa viwanda mbalimbali nchini si tu utawezesha ukuaji wa uchumi wa Taifa, pia utasaidia katika kumaliza changamoto ya ajira hususani kwa vijana.”

Akiwa katika kiwanda cha Tanga Fresh, Waziri Mkuu aliwataka wafugaji mkoani Tanga wabadili mfumo wa ufugaji na wafuge kwa kutumia njia za kisasa ili waongeze uzalishaji.

“Wafugaji lazima wakubali kubadilika watumie fursa ya uwepo wa kiwanda hiki kwa kufuga kisasa ili wapate maziwa mengi kwa sababu wana uhakika wa kuyauza kiwandani hapa”.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka wananchi walioajiriwa kiwandani hapo wafanye kazi kwa bidii, uaminifu na wawe waadilifu na wasijihusishe na vitendo vya wizi kwa kuwa havina tija.

KAMATI YA BAJETI YAKUTANA NA WIZARA YA FEDHA

Waumbe wa Kamati ya Bajeti wakijadili Taarifa za Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/2020 na Mwongozo wa maandalizi ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2019/20 – 2021/22 kataika Kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Ukumbi wa Msekwa Jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti Mheshimiwa George Simbachawene akielezea jambo mbele ya Kamati hiyo ilipokuwa ikijadili Taarifa za Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/2020 na Mwongozo wa maandalizi ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2019/20 – 2021/22 katika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Ukumbi wa Msekwa Jijini Dodoma. Kulia kwake ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip  Mpango.