Thursday, November 1, 2018

WAWEKEZAJI TOKA CHINA KUWEKEZA TANZANIA.

Mkurugenzi Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Uwekezaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania John Mnali
 ...............................................................

Na Grace Semfuko-MAELEZO

Tanzania imepokea wawekezaji kutoka Jimbo la Guangzhou Nchini China watakaokuja kuwekeza nchini kwenye eneo la ukanda wa uwekezaji la Kilua lililopo Kibaha Mkoani Pwani ambao watawekeza kwenye viwanda vya ngozi kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali.

Akizungumzia ujio huo wa wawekezaji wa China Mkurugenzi Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Uwekezaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania John Mnali amesema kwa awamu ya kwanza wawekezaji hao wametenda Dola milioni mia moja ikiwa ni kiwango cha kuanzia kwa awamu ya kwanza ya uwekezaji huo.

“Tumepokea wawekezaji hawa ambao wanakuja kuwekeza nchini kwa awamu ya kwanza kiwango cha kuanzia ni dola milioni 100, huu sio uwekezaji Mdogo ni uwekezaji Mkubwa sana, hizi ni juhudi za Mohammed Kilua kwa kushirikiana na TIC” alisema John Mnali Mkurugenzi wa Uhamasishaji na uwekezaji wa TIC. 

Mnali alisema wamekuwa wakihamasisha uwekezaji kwenye mataifa mbalimbali Duniani hivyo ujio wa Raia hao wa China ni faraja kubwa kwa Serikali ya Tanzania na hasa katika awamu hii ya Serikali ya Rais Magufuli ya uchumi wa viwanda.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa eneo la uwekezaji la Kilua lililopo Kibaha Mkoani Pwani Bw.Mohammed Kilua amesema pamoja na ujenzi wa viwanda vya ngozi za wanyama kwa ajili ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali lakini pia wawekezaji hao wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya ubanguaji wa korosho pamoja na kilimo cha zao hilo

“ Hawa wawekezaji Kutoka Nchini China pia wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye Korosho, na wiki tatu zijazo tutawapeleka Mtwara kuangalia maeneo ya kuwekeza ili waweze kuangalia namna ya kuwekeza” alisema Mohammed Kilua

TIC -YAJIIMARISHA KUDHIBITI CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WAWEKEZAJI

Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo (kushoto) akizungumza wakati alipotembelea banda la maonyesho ya ,kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) katika maonyesho ya bidhaa za viwandani Pichandege ,Kibaha Pwani.
 Picha na Mwamvua Mwinyi
..................................................


NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA

MENEJA wa kanda ya Mashariki wa kituo cha uwekezaji Tanzania( TIC ),Venance Mashiba ameeleza huduma za uwekezaji ni mtambuka ambapo zinatolewa na taasisi mbalimbali ambazo taratibu zake zikigongana inasababisha changamoto ya ucheleweshaji wa huduma kwa wawekezaji.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ,wakati wa maonyesho ya bidhaa za viwandani yanayoendelea Pichandege Kibaha ,mkoani Pwani , alisema tatizo lipo hasa katika upatikanaji wa ardhi na baadhi ya vibali vinavyochukua muda mrefu kwenye upatikanaji wake .

“Tatizo kubwa lipo kwenye ardhi kwani ardhi zote zipo chini ya halmashauri ,mwekezaji lazima apeleke wazo lake halmashauri na akipatiwa ardhi ndipo aje kwetu kuandikisha mradi wake “
“Sasa mradi wake utakubaliwa endapo atapata ardhi na taratibu za upatikanaji wa ardhi ni nyingi na ni ndefu”alifafanua Mashiba .

Mashiba alieleza ,kutokana na hilo kituo hicho , kimeimarisha huduma zake kwa kuongeza taasisi 11 za serikali ambazo zinatoa huduma mbalimbali, vibali na leseni ili mwekezaji apate huduma mahala pamoja na sio kuzunguka .

Alisema, ikitokea mwekezaji ana changamoto zinazohusiana na huduma zinazotolewa kwenye hizo taasisi basi wakuu wa taasisi hizo hukutana na kuamua kuzitatua .

” Tumeunda kamati maalum ya kitaifa inayojumuisha wakuu wa taasisi za serikali ambazo ni wadau katika kuhudumia uwekezaji ili kuharakisha utatuzi wa changamoto zinawakabili wawekezaji”alielezea Mashiba.

Nae mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo aliipongeza TIC kwa jitihada zake katika kukuza na kuvutia uwekezaji nchini na namna inavyohudumia wawekezaji kupitia huduma za mahala pamoja zinazotolewa na taasisi mbalimbali zilizopo ndani ya ofisi za kituo hicho .

Alielezea kwamba ,Mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayopokea wawekezaji na hivyo nguvu ya kuwahudumia iimarishwe. 
Ndikilo aliitaka TIC kuhakikisha inapata taarifa zinazohusiana na uwekezaji Mkoani humo kwa kuwasiliana na halmashauri za mkoa .

“Kwa kufanya hivyo kutarahisisha uratibu na huduma kwa wawekezaji wa Mkoa na Taifa kijumla ” alisema Ndikilo.

Ndikilo alisisitiza ni vyema wakawa na taarifa za maeneo ya uwekezaji yaliyotengwa pamoja na ,takwimu za miradi ya uwekezaji.

Katika kuhakikisha mkoa wa Pwani unaendelea kuvutia wawekezaji Ndikilo alisema ,atawasilisha TIC maeneo ambayo tayari yametengwa kwa ajili hiyo ili yatafutiwe wawekezaji.

WEMA SEPETU AFIKISHWA MAHAKAMANI KISUTU

Msanii wa Filamu nchini Tanzania, Wema Sepetu,  leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam akisubiri kusomewa mashtaka ya kusambaa mitandaoni kwa video zake za faragha.

Wema amefikishwa mahakamani hapo leo Alhamisi, Novemba 1, 2018,majira ya saa 4 asubuhi akiwa amevaa miwani na kujitanda ushungi huku akisindikizwa na askari wawili ambapo alipelekwa kwenye chumba cha mahabusu cha mahakama hiyo.

Jana taarifa zilisambaa mitandaoni kuwa msanii huyo ambaye ni mshindi wa Taji la Miss Tanzania Mwaka 2006, alikuwa amekamatwa na polisi lakini taarifa hizo hazikuthibitishwa.

Hivi karibuni msanii huyo alisambaza mitandaoni video zake za faragha akiwa na mpenzi wake, anayejulikana kama PCK. 

Licha ya kuomba radhi siku chache baadaye, Bodi ya Filamu nchini ilimfungia msanii huyo kujihusisha na masuala ya sanaa kwa muda usiojulikana huku ikisema adhabu yake halisi inakuja.

Nobemba 31 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliitisha mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia wananchi wa mkoa wake wanaokiuka sheria za mtandao.

Makonda aliunda kamati ya watu 17 watakaofanya operesheni kabambe ya kuwafundisha watu wanaokiuka maadili.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alitoa onyo kwa wananchi wa Dar es Salaam wenye picha za ngono kwenye simu zao kuzifuta kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

SEKONDARI YA LUGOBA YAHITAJI MSAADA WA VIFAA VYA MILIONI 34.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari Lugoba, Alhaj Abdallah Sakasa (kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Saidi Zikatimu (kulia) siku ambayo shule hiyo ilipokea vifaa kutoka kwa wadau wa elimu.
......................................................... 

Na Omary Mngindo, Lugoba Chalinze.

SHULE ya sekondari ya Lugoba iliyoko Kijiji cha Lugoba, Kata Lugoba Halmashauri ya Chalinze, wilayani Bagamoyo Pwani, inahitaji shilingi milioni 34 kuweka marumaru kwenye vyumba 17 vya madarasa shuleni hapo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Alhaj Abdallah Sakasa ameyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, ambapo alisema kwa sasa madarasa 17 sakafu zake zimeharibika kiasi cha kusababisha usumbufu kwa walimu pamoja na wanafunzi.

Alisema kuwa pamoja na kufanyiwa ukarabati kwenye vyumba hivyo, lakini vimekuwa vikiharibika kutokana na matumizi ya viti pamoja na meza zenye miguu ya vyuma hali inayochangia kutokea kwa uharibifu wa sakafu hizo.

Alieleza kuwa kila chumba kimoja cha darasa ili kuwekwa marumaru kinahitaji kiasi cha shilingi milioni mbili kwa ajili ya ukarabati huo, hivyo kufanya kiasi vja sjilingi milioni 34 kujitajika kwa kazi hiyo.

Aidha aliongeza kwa kuishukuru serikali kutokana na juhudi zake za kuboresha elimu, sanjali na kuondoa ada na michango mingine ambayo kwa kiasi fulani kilichangia baaadhi ya wazazi na walezi kushindwa kuwasomesha watoto wao kutokana na michango hiyo.

"Kwaniaba ya walimu wenzangu, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Rais wetu Dkt. John Magufuli kwa kuelekeza nguvu katika sekta ya elimu, sote tu mashahidi, amefuta ada na michango yote, pia kutenga fedha kila mwezi zinazopelekwa kwenye shule," alisema Alhaj Sakasa.

Alhaj Sakasa aliongeza kuwa shule hiyo ilianzishwa mwaka 1989 kama shule za awali za wananchi, ina  wanafunzi wapatao 1,388 wanaendelea na masomo yao huku akitanabaisha kuwa kwa msimu wa elimu kwa mwaka huu wanafunzi 173 wamemaliza elimu yao ya kidato cha nne.

Amewaomba wadau mbalimbali wajitokeze katika kuhakikisha ukarabati huo unafanyika ili kuboresha ufundishaji shuleni hapo.