Friday, October 26, 2018

WAZIRI MKUU APOKEA RIPOTI YA KAMATI YA KUCHUNGUZA AJALI YA KIVUKO CHA MV NYERERE

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea Ripoti ya Kamati iliyoundwa na Serikali Kuchunguza Ajali ya Kivuko cha MV Nyerere kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati  hiyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstafu, Jenerali George Waitara, kwenye Makazi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam, Oktoba 25, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha  Ripoti ya Kamati iiyoundwa na Serikali Kuchunguza Ajali ya Kivuko cha MV Nyerere  baada ya kukabidhiwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu, Jenerali George Waitara (kushoto) kwenye Makazi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam, Oktoba 25, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wajumbe wa Kamati iliyoundwa na Serikali Kuchunguza Ajali ya Kivuko cha MV Nyerere baada ya kupokea Ripoti ya Kamati hiyo kwenye Makazi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam, Oktoba 25, 2018. Kushoto ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera na Uratibu, Profesa Faustin Kamuzora na  wapili kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu, Jenerali George Waitara.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
...............................


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea ripoti ya uchunguzi wa  ajali ya kivuko cha MV Nyerere kutoka kwa kamati iliyoundwa na Serikali kwa ajili ya kuchunguza ajali hiyo.

Amepokea ripoti hiyo leo (Alhamisi, Oktoba 25, 2018) kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati  hiyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstafu, Jenerali George Waitara,kwenye makazi ya Waziri Mkuu, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuishikuru kamati hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kazi kubwa waliyoifanya ambayo imethibitisha umakini wao.

Pia ameipongeza kamati hiyo kwa namna walivyotumia muda wao vizuri kwa kufanya kazi hiyo na kutoa mapendekezo kwa Serikali juu ya mambo waliyoyabaini.

“Nimepokea taarifa kwa niaba ya Serikali, Serikali itafanya mapitio ya taarifa yote na viambatisho vyake na itapitia kwa kina mapendekezo mliyoyatoa ambayo yote yatafanyiwa kazi.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali inaamini mambo yote yaliyosheheni katika taarifa hiyo ni yale ambayo Watanzania wanasubiri kuona yakifanyiwa kazi.

MV Nyerere ilipindika na kuzama Septemba 20, mwaka huu katika ziwa Victoria ambapo Watanzania zaidi 200 walipoteza maisha na wengine Zaidi ya 40 waliokolewa.

Septemba 24 mwaka huu Waziri Mkuu alitangaza kamati ya kuchunguza ajali ya kivuko cha MV Nyerere yenye wajumbe saba ambayo iliyoongozwa na Jenerali mstaafu, Waitara.

Akitangaza majina hayo kwenye kijiji cha Bwisya katika kisiwa cha Ukara, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza, Waziri Mkuu alisema wajumbe hao wanapaswa kuikamilisha kazi hiyo ndani ya mwezi mmoja.

Aliwataja wajumbe wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi, Mhandisi Marcelina Magesa, Wakili Julius Kalolo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bi. Queen Mlozi.

Wengine ni SACP Camillus Wambura na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uratibu Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Bashiru Taratibu Hussein.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati  iliyoundwa na Serikali Kuchunguza Ajali ya Kivuko cha MV Nyerere  baada ya kupokea Ripoti ya Kamati hiyo kwenye Makazi ya Waziri Mkuu, jijini Dar es salaam, Oktoba 25, 2018. Kushoto kwa Waziri Mkuu ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera  na Uratibu) Profesa Faustin Kamuzora na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu, Jenerali George Waitara.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiagana na Mwenyekiti wa Kamati  iliyoundwa na Serikali  Kuchunguza Ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu, Jenerali, George Waitara  baada ya kupokea Ripoti ya Kamati hiyo kwenye Makazi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam, Oktoba 25, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Thursday, October 25, 2018

WANANCHI WA CHALINZE WAHAKIKISHIWA KUPATA MAJI APRIL 2019-SAMIA.


NA MWAMVUA MWINYI, CHALINZE 

SERIKALI imewahakikishia wananchi wa jimbo la Chalinze ,mkoani Pwani kuwa wataondokana na tatizo la maji na kubaki historia ifikapo mwezi april mwakani. 

Tatizo la maji limekuwa likiwapa shida wananchi hao kwa miaka mingi hali iliyokuwa ikiondoa imani na serikali yao. 

Akizungumza na wakazi wa Chalinze, makamu wa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu alisema ,shida ya maji Chalinze imekuwa kubwa ambapo wamekuwa wakikosa huduma hiyo ya maji safi na salama ya uhakika. 

“Tukiahidi tunatekeleza, na serikali mkiiona haitekelezi baadhi ya mambo kwa haraka lazima inasababu na inatolea ufafanuzi wa kusuasua kwa jambo husika “
“Faraja inakuja, naimani ifikapo 2019 kero hii itakuwa historia, “alisisitiza. 
Pamoja na hayo, Samia amewataka akinamama wajawazito wakiwa tayari kujifungua wakimbilie hospital ama vituo vya afya badala ya kuendekeza masuala ya kishirikina suala linalosababisha vifo kwa mama na mtoto. 

Aliwaomba ,watumie vituo vya afya kunusuru vifo vya akinamama na watoto. 

Akizungumzia tatizo la mgogoro wa wakulima na wafugaji aliwaasa waheshimiane. 

Akitolea ufafanuzi juu ya kudhibiti tatizo hilo, naibu waziri wa mifugo na uvuvi, Abdallah Ulega alisema, NARCO inaanzisha maeneo ya wafugaji na imetenga heka 100,010 ambapo ng’ombe watahamishia malisho ndani ya Narco.

“Miezi mitatu ng’ombe mmoja atalipiwa sh. 10,000 na ukiisha muda huo unaanza mkataba upya”alielezea.

Ulega alifafanua, njia hiyo itapunguza ongezeko la mifugo hiyo.
Alieleza itakuwa ni ofa kwa wafugaji kunenepesha ng’ombe wao kwenye shamba hilo la serikali. 

Awali mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete alieleza changamoto ya kero ya maji ni kubwa kwa kipindi kirefu. 

Anasema ,uchelewaji wa hatua za kupata huduma ya maji inaleta sura ya kufanya siasa kwa wananchi ambao bado wanaiamini serikali yao. 

Ridhiwani aliiomba, serikali kuendelea kusukuma na kuusimamia mradi wa CHALIWASA ili uanze kazi haraka na kuondoa kero hiyo.