Thursday, October 25, 2018

KAIMU SHEIKHE WA MKOA WA MWANZA AELEZA MIKAKATI YA KUBORESHA UCHUMI WA VIONGOZI, WALIMU NA MASHEIKHE

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Musa Kabeke akizungumza na wajumbe wa halmashauri ya BAKWATA mkoani Mwanza, masheikhe wa wilaya, Kata na Misikiti ya wilaya zote za Mwanza jana, kwenye ukumbi wa mikutano wa baraza hilo Mbugani katika Wilaya ya Nyamagana jana. Picha na Baltazar Mashaka.
....................................


NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA.

KAIMU Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza Hassan Musa Kabeke amesema moja ya vipaumbele vyake ni kuimarisha uchumi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na elimu ya dini.

Sheikhe Kabeke alitoa kauli hiyo jana kwenye ukumbi wa ofisi za BAKWATA zilizopo Mbugani katika Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, wakati akizungumza na wajumbe wa halmashauri ya mkoa, masheikh wa wilaya na kata mkoani humu.

Alisema miongoni mwa mambo yanayomkera ni hali duni ya maisha na udhalili (unyonge)  hivyo ameweka mikakati na mipango ya kuimarisha uchumi wa BAKWATA ili kubadilisha maisha ya walimu wa madrasa, masheikhe na maimamu wa misikiti ambao ni zao la uislamu (kiwanda) na misingi ya dini hiyo ya Kiislamu.

Kaimu Sheikhe huyo wa mkoa alisema madrasa na msikiti ndio eneo dhaifu kutokana na walimu na masheikhe kushindwa kufundisha elimu ya dini na hata ujira wao ni mdogo wanazidiwa na watumishi wa ndani jambo ambalo linamkera na hivyo ameamua kulitafutia tiba.

Sheikhe Kabeke alieleza kuwa ili kuboresha hali za walimu wa madrasa,masheikhe na maimu na waumini wa kiislamu lazima kuwe na vyanzo vya mapato yatakayosaidia Waislamu na haiwezekani kuendelea kuwa na BAKWATA ombaomba.

“Niwaondoe hofu maana wapo watu wanaosema mimi ni mkali la hasha, mimi nina msimamo kwenye haki.Sote tunachukia ufisadi, wizi na umaskini na hata Mufti wa Tanzania kilio chake ni kutaka kuwatoa waislamu kwenye udhalili (unyonge).Katika hili la kuimarisha uchumi hata mkinilaumu niko radhi na Mwenyezi Mungu atanihukumu,”alisema Sheikhe Kabeke.

Alisema waislamu hawana sababu ya kuwa wanyonge na wasimuone mkali bali atautumia na kuendelea na ukali huo kuwaondoa kwenye unyonge wao kuwataka viongozi dini ya kiislamu na waumini  kutumia neema waliyopewa na Mungu kutafuta pepo na nyumba ya ahera.

Aliongeza kuwa BAKWATA ina hali mbaya kiuchumi na ni taasisi pekee isiyo na wanachama wanaolipa ada wakati chombo hicho kinawapa heshima hivyo kwa Mkoa wa Mwanza dira na mipango yake ya kuleta maendeleo viongozi wa ngazi ya mkoa watachangia sh.8,000 mwezi sawa na sh. 2,000 kwa wiki fedha ambazo zitawekwa kwenye akaunti maalumu.

“Tunataka kujenga uchumi kwa kuangalia rasilimali watu na  kuanzia Oktoba viongozi  watachanga sh. 8,000  kwa ngazi ya mkoa, wilaya sh. 4,000 , kata sh. 500 na tayari akaunti imefunguliwa kwa usalama wa fedha hizo ili ndani ya miaka tujenge jengo la kitega uchumi, kulipa mishahara ya walimu wa madrasa na masheikhe na kutatua kero zao,” alifafanua Sheikhe Kabeke.

Aidha,kuhusu elimu ambayo imegawanyika sehemu tatu, aliwawataka waislamu kuacha kulalamika kuwa taasisi yao inahujumiwa na kuchafuliwa pamoja na kupoteza akidi yao ilhali wenye dhamana ya kufundisha elimu ya dini  shuleni hawatimizi wajibu wao na kusababisha vijana waliolelewa kwa misingi ya dini kiislamu wakosekane.

Alisistiza kuwa kama huo ni ukali basi hana budi kuacha hali iendelee ili uislamu ufe na kutoweka kwa sababu masheikhe na walimu hawaoni umuhimu wa kufundisha elimu ya dini shuleni licha ya kutengwa kwa vipindi vya dini.

Kaimu Sheikh huyo wa mkoa alimshukuru Mufti wa Tanzania Abubakar  Zuberi bin Ali kwa na Baraza la Ulamaa kwa kumteua, kumuona na kumuamini kuwa anafaa kumsaidia kwenye nafasi hiyo kubwa ambayo si ya kukimbiliwa na kuahidi kuwa kwenye uongozi wake hatabadilika na atakubali kushauriwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya BAKWATA Mkoa wa Mwanza Amran Batenga akizungumza na wajumbe wa halmashauri hiyo, masheikhe wa wilaya na kata za mkoani humu jana kwenye ukumbi wa baraza hilo Mbugani katika Wilaya ya Nyamagana.
Kaimu Katibu Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza, sina Mwagalazi akizungumza na wajumbe wa Halmashauri kuu ya baraza hilo, masheikhe wa wilaya na kata wa wilaya za mkoani humu.

SIKU YA PILI MAKAMU WA RAIS AKIWA BAGAMOYO.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa Mhandisi Cyprian Luhemeja (kulia) ya miundo mbinu ya maji itakavyokuwa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa tanki la maji litakalokuwa na uwezo wa kubeba lita milioni 6, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo kwenye ziara ya kuhamasisha shughuli za kimaendeleo mkoani Pwani.
..................................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya awamu ya tano imeendelea kutekeleza ahadi ya kusambaza maji mjini na vijijini ambapo mpaka ifikapo mwaka 2020 inategemea maji yatakuwa yamefika vijijini kwa asilimia 85% na mjini asilimia 90%.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa tanki kubwa la mradi wa maji Bagamoyo lenye uwezo wa kubeba lita milioni 6 ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya siku sita mkoani Pwani.

Makamu wa Rais ameipongeza Dawasa kwa kazi nzuri na amewataka wananchi kupitia kamati mbali mbali za maji kutunza na kuvilinda vyanzo vya maji, miundo mbinu pamoja na mazingira yake.

“Wote tujitahidi kutunza vyanzo vya maji” alisema Makamu wa Rais
Tenki hilo la Bagamoyo linatarajiwa kuhudumia wakazi wote wa mji wa Bagamoyo na vitongoji vyote vinavyozunguka mji huo.

Makamu wa Rais pia alipata nafasi ya kutembelea mradi wa uzalishaji na usambazaji vifaranga wa kampuni ya AKM Glitters na kuzungumza na wananchi waliojitokeza kwenye viwanja vya shule ya msingi Majengo.

Katika ziara hiyo Makamu wa Rais aliongozana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu na vIongozi wengine wa Chama na Serikali.  
 
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa Mhandisi Cyprian Luhemeja (kulia) ya miundo mbinu ya maji itakavyokuwa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa tanki la maji litakalokuwa na uwezo wa kubeba lita milioni 6, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo kwenye ziara ya kuhamasisha shughuli za kimaendeleo mkoani Pwani.
 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa Mhandisi Cyprian Luhemeja (kushoto) na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati wa kukagua Mradi tanki la maji Bagamoyo litakalokuwa na uwezo wa kubeba lita milioni 6, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo kwenye ziara ya kuhamasisha shughuli za kimaendeleo mkoani Pwani.