Monday, October 22, 2018

WAZIRI MKUU APONGEZA USHIRIKIANO WA VIONGOZI WA DINI NA SERIKALI.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hasani Bin Mussa Kabeke wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza  Oktoba 22, 2018 akiwa njiani kwenda mkoani Simiyu ambako kesho anatarajia kufungua maonesho ya wajasiriamali.   

Sheikh huyo amechaguliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.
..............................................


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ushirikiano mzuri baina ya taasisi mbalimbali za dini nchini na Serikali ni jambo la muhimu katika kuboresha na kuimarisha amani.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 22, 2018) alipowasili jijini Mwanza akiwa njiani kwenda mkoani Simiyu ambako kesho anatarajia kufungua maonesho ya wajasiriamali.

Alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, Waziri Mkuu amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiwemo wa Serikali na wa dini mbalimbali.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mkakati wa viongozi wa dini wa kuunda kamati za amani nchini ambapo walianzia kwenye ngazi ya mkoa na sasa wamefikia katika kata.

“Viongozi wa dini mnadhamana kubwa katika kulifanya  Taifa liendelee kudumisha amani, utulivu na mshikamano, hivyo ushirikiano wenu na   Serikali ni muhimu.”

Amesema viongozi wa Serikali wakati wote wamekuwa tayari kufanyakazi na viongozi pamoja na taasisi mbalimbali za dini, lengo ni kuimarisha amani na utulivu uliopo nchini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mwanza inawajibu wa kuhakikisha kwamba maeneo ya mkoa huu yanaendelea kuwa salama.

Pia, Waziri Mkuu amempongeza Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hassan Bin Mussa Kabeke kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.

“Nakupongeza kaimu sheikh wa mkoa kwa kuteuliwa na ninakutakia kila la heri katika kazi yako na kwamba dhamana yako kubwa ni kuwaunganisha waislamu na waumini wa dini zote.” 

MJUMBE WA KAMATI KUU CCM TAIFA, MAKAMU WA RAIS AHUDHURIA MKUTANO WA KAMPENI JIMBO LA JANG`OMBE

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na Katiba ya Chama mgombea wa CCM nafasi ya Uwakilishi Jimbo la Jang`ombe Bw. Ramadhan Hamza Chande wakati wa mkutano wa kumnadi mgombea wa Uwakilishi jimbo la Jang`ombe kwenye viwanja vya Baja. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa mkutano wa kumnadi mgombea wa Uwakilishi jimbo la Jang`ombe kwenye viwanja vya Baja.
 ......................................

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo alikuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kampeni jimbo la Jang`ombe ambapo Chama Cha Mapinduzi kimemsimamisha Bw. Ramadhan Hamza Chande kugombea nafasi ya Uwakilishi katika jimbo hilo.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa, Makamu wa Rais amewataka wakazi wa Jang`ombe kufuata nyayo walizoachiwa na Wazazi wao.

Mheshimiwa Samia amewambia wakazi wa jimbo hilo kuwa atatoa ushirikiano wa kutosha kwa kufanya kazi pamoja na Viongozi wa Jimbo hilo katika kuboresha huduma za afya na elimu.

Pamoja na Viongozi wengine Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mbunge mteule wa jimbo la Liwale kutoka mkoani Lindi Bw. Zuberi Kachauka ambaye aliwaambia wakazi wa Jimbo la Jang`ombe kuwa upinzani umekufa kwa kukosa sera na viongozi bora.

Kampeni za Uwakilishi jimbo la Jang`ombe zilianza tarehe 14 Oktoba na zinatazamiwa kukamilika tarehe 25 Oktoba  2018 na tarehe 27 Oktoba wananchi watapiga kura kumchagua Mwakilishi wa jimbo hilo.

WAZIRI MKUU, MAJALIWA AWASILI JIJINI MWANZA.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella  (katikati) wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza akiwa njiani kwenda mkoani Simiyu ambako kesho anatarajia kufungua maonesho ya wajasiriamali. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hasani Bin Mussa Kabeke wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza  Oktoba 22, 2018 akiwa njiani kwenda mkoani Simiyu ambako kesho anatarajia kufungua maonesho ya wajasiriamali.   Sheikh huyo amechaguliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.