Monday, October 22, 2018

MAAFISA AFYA WATAKIWA KUSIMAMIA USAFI WA MAZINGIRA ILI KUTOKOMEZA MALARIA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya Wabunge wa kamati ya Huduma za Jamii na Wadau wa Masuala ya Afya (hawapo kwenye picha) katika uzinduzi wa taarifa ya utafiti wa Viashiria vya Malaria nchini.
.......................................

Na WAMJW – Dar Es Salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewaagiza Maafisa Afya nchini kusimamia kwa ukamilifu usafi wa mazingira katika jamii ili kutokomeza ugonjwa wa Malaria.

Waziri Ummy ametoa agizo hilo leo Oktoba 22, 2018 wakati akizindua Taarifa ya Utafiti wa Viashiria vya Ugonjwa wa Malaria wa Mwaka 2017 katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar Es Salaam.

“Nawaagiza Maafisa Afya,  badala ya kupoteza muda mwingi wa kukagua migahawa, bucha za nyama na sehemu ambazo wanajua zinaleta fedha, tunataka pia wajikite katika kusimamia usafi wa mazingira  katika Kata, Vijiji na Mitaa yetu”Alisema Mhe. Ummy.

Katika kuhakikisha hali ya usafi wa mazingira inakuwa endelevu, Waziri Ummy ameagiza Mabalaza yote ya Halmashauri nchini kuweka Sheria na adhabu kali kwa wote ambao wamekuwa wagumu katika kushiriki katika usafi wa mazingira huku Waganga Wakuu wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia vyema utekelezaji wa kanuni na sheria za afya na usafi wa mazingira jambo ambalo litaibua chachu ya ushindi katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Malaria.

“Niyatake Mabalaza ya Hamashauri kuweka hatua kali, sheria kali na adhabu kali kwa wote ambao hawashiriki katika usafi wa mazingira” alisema Waziri Ummy.

Licha ya hivyo Waziri Ummy alisema kuwa Serikali kupitia Wizara inaendelea kutekeleza Mpango endelevu wa ugawaji vya ndarua kupitia wanafunzi wa shule za msingi, kupitia Kliniki za wajawazito na watoto, ambayo hujulikana kama Chandarua Kliniki huku hadi sasa jumla ya vyandarua milioni 31 vimeshagawiwa nchini kote.

Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa Matokeo ya mpango endele u wa ugawaji wa vyandarua yameonesha kuwa asilimia 78 ya kaya nchini Tanzania zinamiliki angalau chandarua kimoja chenye dawa, Katika utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2015-16, ni asilimia 66 tu za kaya zilikuwa zinamiliki angalau chandarua kimoja chenye dawa huku Umiliki wa vyandarua vyenye dawa ni wa kiwango cha juu kwa kaya za mijini (asilimia 81) ikilinganishwa na kaya za vijijini (asilimia 77). 

Kwa upande mwingine Waziri Ummy alitaja Halmashauri zenye maambukizi ya kiwango cha juu ni pamoja na Kakonko 30.8%, Kasulu DC 27.6%, Kibondo DC 25.8%, Uvinza 25.4%, Kigoma DC 25.1%, Buhigwe 24%, Geita DC 22.4%, Nanyamba TC 19.5%, Muleba DC 19.4%, Mtwara DC 19.1%, huku Halmashauri zenye  maambukizi ya kiwango cha chini ya asilimia 0.1 ni Mbulu TC, Mbulu DC, Hanang, Hai, Siha, Moshi MC, Mwanga, Kondoa TC, Meru DC, Arusha CC, Arusha DC,  Munduli, Ngorongoro, Rombo DC
Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akionesha Kitabu cha Taarifa ya utafiti wa Viashiria vya Malaria mbele ya mgeni rasmi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa taarifa ya utafiti wa Viashiria vya Malaria nchini uliofanyika leo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa taarifa ya utafiti wa Viashiria vya Malaria nchini uliofanyika leo jijini Dar es salaam.
 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakioneshana jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya TAKWIMU Dkt. Albina Chuwa (wakatikati).

 
Wabunge wa Kamati ya Huduma za Jamii na Wadau wa Masuala ya Afya wakifuatilia taarifa ya Utafiti ya Viashiria vya ugonjwa wa Malaria nchini iliyokuwa ikisomwa na Mgeni rasmi Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo kwenye Picha) jijini Dar es salaam.

TFDA YATOA ELIMU YA MADHARA YA SUMUKUVU KWA WASINDIKAJI

Meneja wa Mamlaka ya chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya kati DK.Englbert Bilashoboka akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo Pichani) wakati wa Mafunzo ya  wasindikaji wadogo wa bidhaa za unga,unga mchanganyiko ( Composite Flour)na siagi ya karanga yanayofanyika Jijini hapa.
............................

Mamlaka ya chakula na Dawa TFDA kanda ya Kati Dodoma imeanza kutoa elimu kwa wasindikaji wa mazao ya Nafaka baada ya kubaini baadhi ya bidhaa wanazozalisha hususani unga wa mahindi na siagi ya karanga kuwa na vimelea vya ugonjwa wa sumukuvu ambao ni hatari kwa afya ya watumiaji na wakati mwingine husababisha vifo.

Mafunzo hayo yanatokana na ripoti ya ufuatiliaji wa usalama na ubora wa bidhaa zitokanazo na unga mchanganyiko na siagi ya karanga uliofanywa na mamlaka hiyo ya mwaka 2015-2018 na kubaini mazo hayo huzalishwa kwa wingi mkoani humo yana dalili ya uwepo wa fangasi na sumukuvu.

Akizungumza na washiriki Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bw.Maduka Kessy  amesema kuwa wasindikaji wa chakula wanahitajika kuwa wasafi na weledi mkubwa kwa kuwa kinyume na hapo athari yake ya kupata sumukuvu ni hatari kwa walaji.

“Katika ufuatiliji huo ilibainika kuwa bidhaa hizi zilikuwa na dalili ya uwepo wa sumukuvu,hususani katika bidhaa zitokanazo na mahindi na karanga hizi ndizo wajasiliamali wengi wanauza”amesema Bw.Kessy
Kwa upande wake Meneja wa kanda ya kati Dodoma wa Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) Dkt Engelbart Bilashoboka,amewataka wasindikaji kubaini vyanzo vya uchafunzi wa chakula kutokana na sumukuvu ili waweze kuizuia.

Dk.Bilashoboka amesema kuwa wasindikaji wakibaini watakuwa wamewalinda walaji wa bidhaa hizo zinazotengenezwa kwa kuepusha maradhi kama vile ya kuumwa tumbo,kutapika,kuharisha na hali ya umanjano machoni na viganjani na hata kusababisha ba vifo pia.

Aidha amesema kuwa malengo ya  mamlaka hii  kuanzishwa kwake ni kuhakikisha kuwa chakula,dawa,vipodozi,vifaa tiba na votendanishi vitakavyotumika hapa nchini na vinakidhi ubora na usalama kwa watumiaji.

Kwa upande wa baadhi ya Wasindikizaji wamekiri kutokuwa na uelewa juu ya sumukuvu kwani awali walikuwa wakisindika Nafaka Kienyeji bila kuchagua mazao ambayo mengine yana  dalili za uwepo wa vimelea vya ugonjwa huo.
Washiriki wa Mafunzo ya  wasindikaji wadogo wa bidhaa za unga,unga mchanganyiko ( Composite Flour)na siagi ya karanga wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi waliokaa kwenye viti kulia ni Meneja wa Mamlaka ya chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya kati DK.Englbert Bilashoboka na kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw.Maduka Kessy.