Thursday, October 18, 2018

PROFESA MBARAWA AZINDUA KAMPENI YA UTUNZAJI WA VYANZO VYA MAJI

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akipanda mti kwenye chanzo cha Mtawanya, Mtwara Mjini.
.........................


Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa leo amezindua rasmi Kampeni ya Upandaji Miti kandokando ya vyanzo vya maji nchi nzima mkoani Mtwara kwa lengo la kuhakikisha vyanzo hivyo vinatunzwa na kuwa endelevu kwa miaka mingi ijayo.

Profesa Mbarawa amezindua kampeni hiyo kwa kupanda miti nane katika chanzo cha Mtawanya kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mjini na kuzitaka Bodi zote za Mabonde tisa nchini kuweka mkazo na mipango madhubuti ya kusimamia na kutunza rasilimali za maji ziweze kuwa endelevu.

Ametoa agizo hilo kutokana na uvamizi na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji katika maeneo mengi kwa sasa nchini, hali inayohatarisha kiasi kikubwa cha maji kupungua kutokana na vyanzo vingi kukauka, hali inayoweza  kusababisha ukosefu wa maji ya kutosha kwa ajili ya miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali.

Na kutaka vyanzo vyote vya maji vitunzwe na kulindwa kwa kupandwa miti maalumu inayohifadhi maji na kuagiza wale wote wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo waache tabia hiyo na watakao kaidi wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine kwa kuwa sheria inaweka bayana kuhusu jambo hilo.

Ametoa tamko hilo kwa kuzingatia Sheria ya Maji Na, 11 ya Mwaka 2009 inayokataza kufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji, na ikieleza shughuli zote za kibinadamu zifanyike umbali wa mita 6o kutoka chanzo cha maji kilipo na kutaka maeneo yote yawekewe mipaka na vizuizi kuonyesha ukomo wa watu kuingia kwenye vyanzo hivyo.

‘‘Hatutaki kupata hasara kwenye miradi tunayowekeza fedha nyingi, halafu baadae iwe kama magofu kwa kukosa maji. Imefika hatua kuwa ni lazima tuchukue hatua za lazima kuinusuru taifa letu na uhaba wa maji. 

Niwatake wananchi watoe ushirikiano wa karibu na Serikali kuhakikisha vyanzo vyetu vyote vinakuwa endelevu kwa kuzalisha maji ya kutosha na kuwa na uwezo wa kutoa huduma ya uhakika kwa miaka ijayo’’, amezungumza Profesa Mbarawa.

‘‘Kwa kuanza tumepanda miti nane katika chanzo hiki cha Mtawanya, nataka ifikapo Disemba mwaku huu, nikute zaidi ya miti 1,000 kwenye chanzo hiki na zoezi hili lifanyike nchi nzima kwa sababu kama waziri mwenye dhamana ya kusimamia rasilimali za maji nitalisimamia jambo hili ipasavyo’’, ameonya Profesa Mbarawa.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Evod Mmanda amesema ni muhimu zoezi la upandaji miti liwe endelevu lenye kuzingatia upandaji wa miti na kuachana na miti isiyo rafiki na maji kwa lengo la utunzaji wa maeneo yote yenye vyanzo na kutaka wananchi wazingatie sheria iliyopo kwa hiari, pasipo kutumika nguvu na kuonya kuwa hatavumilia uharibifu wa vyanzo vya maji katika wilaya yake.

Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Maji hivi karbuni imetoa Shilingi Bilioni 2.3 kwa ajili ya malipo ya madai kwa wakandarasi mbalimbali wanaotekeleza miradi ya maji katika Mkoa wa Mtwara, ambapo uzalishaji wa maji kwa siku kwa mji wa Mtwara umefikia lita milioni 10, huku mahitaji kwa siku ni lita milioni 13.7.

Fedha hizo zimetolewa kwa lengo la kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma, ambapo hadi sasa miradi 45 ikiwa imeshakamilika na mingine 33 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.



WANAFUNZI WATAKIWA KUWA NA MAADILI MEMA:JAJI MKUU

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wanafunzi  kuwa na maadili mema, kufuata sheria na taratibu za nchi na kuachana na matendo yote yanayokiuka maadili ikiwemo wizi wa mitihani.

Akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Nyampulukano iliyopo wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Jaji Mkuu aliwaambia wanafunzi hao kuwa wizi wa mitihani ni tatizo la kwanza la ukosefu wa maadili katika jamii.

Aliwataka wanafunzi hao kujenge tabia ya kujisomea mambo mbalimbali kwa kuwa karne hii ya ishirini na moja ni karne ya sayansi na teknolojia yenye taarifa nyingi zitakazowasaidia kwa maendeleo yao.

“Karne hii ya ishirini na moja ni tofauti na karne ya ishirini, someni mambo mbalimbali ili mfahamu nchi yenu inakwendaje”, alisema Jaji Mkuu huku akiwasisitiza waisome Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ili wafahamu  Tanzania itakuwa ni nchi ya namna gani.

Aidha, Jaji Mkuu pia aliwashauri wanafunzi watakaopenda kuwa wanasheria hapo baadaye kuhakikisha wanakuwa waadilifu katika jamii kwa kuwa fani ya sheria inahitaji mtu aliye na maadili mema hasa na yule anayechukia na kuvipinga kwa nguvu zote vitendo vya rushwa.

Hata hivyo alisema kutokusoma sheria hakutawazuia kufahamu sheria mbalimbali za nchi na kuwa karne hii ya ishirini na moja inahitaji fani zote kushirikiana ili kuwa na maendeleo.

Akizungumzia rushwa na uchumi wa nchi, Jaji Mkuu alisema ziko nchi duniani zenye rasilimali nyingi na zimeweza kubadili maisha ya raia wake na wakati huo huo zipo nchi zenye rasilimali nyingi lakini hazijaweza kubadili maisha ya watu wake kutokana na rushwa hivyo aliwataka wanafunzi hao kukataa rushwa kwa kuwa ni adui wa maendeleo yao.

Mahakama ya Tanzania imeanzisha mpango wa kuzitembelea shule mbalimbali nchini kwa lengo la kuwaandaa vijana kuwa na maadili mema katika jamii wakiwamo wanasheria wa baadaye.  

Jaji Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Mwanza ambapo anakagua shughuli za mahakama kwenye Mahakama zilizopo mkoani humo.

MAGAZETI YA LEO 18 OKTOBA 2018

Wednesday, October 17, 2018

DC BAGAMOYO ATAKA WANAFUNZI KIDATO CHA NNE KUJIANDAA NA MTIHANI.

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Zaynabu Kawawa. 
...........................

Na Omary Mngindo, Lugoba

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Zaynabu Kawawa, amewataka wanafunzi wa sekondari ya Lugoba kujiandaa vyema na mithihani yao ya kidato cha nne, inayotaraji kufanyika mwanzoni mwa mwezi ujao.

Kawawa ameyasema hayo katika mahafari ya 27 shuleni hapo ambapo alisema maandalizi mazuri kwa ajili ya mitihani ndiyo itayowawezesha kufanya vyema, hatimae kufikia malengo waliyojiwekea, huku akiwataka wazazi kuchangia sekta hiyo ili kukabili changamoto zilizopo. 

Mkuu huyo aliongeza kwamba serikali inaendelea na uboreshaji wa sekta ya elimu sanjali na kuongeza walimu, kukarabati miundombinu hiyo ikiwemo utoaji wa fedha kila mwezi kutoka serikalini.

"Serikali inataka kuboresha zaidi elimu kuanzia ya msingi na sekondari, ili iwe sawa na ya wanafunzi wasio na ulemavu, hatua inayolenga kuwepo elimu jumuishi kwa wanafunzi wote pasipokubagua," alisema Kawawa.

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kuboresha sekta hiyo ikiwemo wanafunzi wenye ulemavu, huku akipongeza wadau waliojenga darasa la wanafunzi wa elimu maalumu hali inayopaswa kuungwa mkono.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Abdalah Sakasa alimwambia Mkuu hiyo kuwa changamoto inayowakabili ni pamoja na gharama ya kununulia kemikali na vifaa vya maabara kipindi cha mitihani ya kitaifa.

Alisema kuwa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1989 ikiwa ni shule za mwanzoni kwa sasa ina idadi ya wanafunzi wapatao 1,388, ambapi kati ya hao wanafunzi waliohitimu wakiwa 73 ambao ndio walioagwa kwenye mahafali hayo.

"Kwanza tunaishukuru serikali iliyoko madarakani chini ya rais Dkt. John Magufuli kwa kuendelea na utoaji wa fedha kwa ajili hiyo, lakini hazikidhi kutokana na gharama kuwa kubwa, tunaiomba kuangalia uwezekano wa kutuongezea ili kuongeza ufanisi wa masomo ya Sayasi", alisema Sakasa.

Aliongeza kwa kusema kwamva changamoto hiyo imekuwa kubwa, hasa ikizingatiwa kwamba shule hiyo ina wanafunzi wengi wanaosoma masomo ya Sayansi.

"Mbali ya changamoto hiyo, pia tunakabiliwa na uchakavu wa sakafu katika baadhi ya madarasa, utatuzi wake ni kuweka marumaru, kuuna madarasa 17 kila darasa moja linagharimu shilingi milioni mbili,"alimalizia Sakasa.
 
Hawa ni baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Lugoba