Tuesday, October 16, 2018

MKUU WA MKOA WA PWANI AKUTANA NA MKURUGENZI NA MTENDAJI MKUU WA BENKI YA CRADB

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mheshimiwa Mhandisi Evarist Ndikilo, akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bibi Theresia Mmbando pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Bibi Jokate Urban Mwegelo alipokutana na Benki ya CRDB katika  mkutano wa pamoja wa kujadili maandalizi ya wiki ya Maonesho ya Viwanda ya Mkoa wa Pwani na Mkurugenzi Mtendaji  na  Mwendeshaji  wa Benki ya CRDB Ndugu Abdulmajid Nsekela

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mheshimiwa Mhandisi Evarist Ndikilo, akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bibi Theresia Mmbando pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Bibi Jokate Urban Mwegelo alipokutana na Benki ya CRDB katika  mkutano wa pamoja wa kujadili maandalizi ya wiki ya Maonesho ya Viwanda ya Mkoa wa Pwani na Mkurugenzi Mtendaji  na  Mwendeshaji  wa Benki ya CRDB Ndugu Abdulmajid Nsekela, wengine ni Wakuu wa idara mbalimbali kutoka benki ya CRDB , Teddy Maganga Mratibu wa Matukio pamoja na Philomena Kasanga ambaye ni katibu wa mkuu wa Mkoa wa Pwani



MAGAZETI YA LEO OKTOBA 16. 2018.

BIDHAA ZA MILIONI 93 ZATEKETEZWA BAGAMOYO.


Bidhaa za vyakula zenye thamani ya shilingi milioni 93,277,368. zimeteketezwa wilayani Bagamoyo baada ya kubainika kuwa hazina ubora kwa matumizi ya binadamu.

Akizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa amesema bidhaa hizo zimeteketezwa kufuatia uchunguzi uliofanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) kanda ya mashariki na kubaini kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu.

Mkuu huyo wa wilaya alisema Bidhaa hizo zimeingia Bagamoyo kwa magendo kupitia njia ya Bahari ambapo zilikamatwa kufuatia doria iliyowekwa na idara ya forodha wilaya kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu huyo wa wilaya ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya, amewaonya watu wenye tabia ya kupitisha bidhaa za magendo Bagamoyo na kusema kuwa kwa sasa wamejipanga kudhibiti hali hiyo.

Alisema kwa sasa Kamati ya ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo imejiwekea mikakati mipya ya kudhibiti bidhaa zinazopitishwa kwa njia za magendo na kusema kuwa Bagamoyo sasa sio salama kwa wapitisha magendo.

Aliongeza kwa kusema kuwa kitendo cha kuingiza Bidhaa kwa njia za magendo ni hatari kwa maisha ya binadamu, usalama wa wilaya yake na inaleta hasara kwa Taifa.

Akifafanua zaidi alisema Bidhaa zinazopiishwa kwa njia za magendo zinakuwa hazikidhi vigezo vya kuingia sokoni kwaajili ya matumizi, hivyo bila ya kudhibitiwa zinaweza kuleta madhara kwa watumiaji ambao ni wananchi wanaotegemewa katika ujenzi wa Taifa.

Alisema licha ya kuleta madhara kwa Afya za watumiaji lakini pia njia za magendo zinaweza kutumika hata kusafirishia wahamiaji haramu ambao wanaweza kuleta machafuko kwa kuwa njia hizo hutumika na watu wenye tamaa ya fedha bila ya kujali maslahi ya Taifa.

Aliendelea kusema kuwa njia za magendo hutumika na wafanya biashara ambao wana lengo la kukwepa kulipa ushuru na kodi ya serikali na hatimae kuzorotesha miradi ya maendeleo ambayo inategemea kodi.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, ametoa wito kwa wafanyabiashara wanaotaka kupitisha bidhaa zao Bagamoyo kutumia Bandari iliyopo kisheria ili bidhaa hizo zilipiwe kodi na ushuru kwaajili ya kuiingizia serikali mapato.

Alisema hatawavumilia wale wote watakaotumia njia ambazo sio rasmi kwa lengo la kukwepa kodi na kuikosesha mapato serikali.

Alisema Bagamoyo ni mji wa kihistoria hivyo unahitaji kuijiimarisha kiuchumi na kwamba uchumi hauwezi kuimarika bila ya kulipa kodi zilizopo kisheria.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaagiza wakurugenzi wa Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze kusimamia mapato ya serikali ili kuongeza ukusanyaji wa mapato ambayo ndiyo yanayotegemewa kuleta maendeleo katika wilaya na Taifa kwa ujumla.

Aliongeza kwa kusema kuwa, vipo vyanzo vingi ndani ya wilaya hiyo ambavyo vikitumika vizuri Bagamoyo inaweza kujiletea maendeleo yenyewe.
Mkaguzi wa chakula kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini, (TFDA) kanda ya Mashariki, Khalifa Sume amethibitisha kuwa bidhaa hizo hazina ubora kwa matumizi ya binadamu na kusema kuwa zinapaswa kuteketezwa ili kuepuka madhara ambayo yangeweza kujitokeza baada ya kutumia bidhaa hizo.

Khalifa alisema bidhaa hizo za vyakula zimeteketezwa kwa mujibu wa sheria ya chakula, Dawa na Vipodozi sura Na 219 ya Mwaka 2003 na kanuni zake za utupaji wa vyakula visivyofaa za Mwaka 2006.

Akizungumzia swala hilo Afisa Mwandamizi wa Forodha Bagamoyo Noeli Makere alisema kukamatwa kwa Bidhaa hizo ni mpango mkakati wa kuhakikisha mianya yote ya kukwepa kodi ya forodha ndani ya wilaya ya Bagamoyo inadhibitiwa ili kuongeza ukusanyaji wa mapato unaotokana na Bidhaa zinazoingia wilayani humo kwa njia ya Bahari.

Alisema Bidhaa yoyote itakayokamatwa nje ya eneo la Bandari muhusika atapaswa kulipa kodi pamoja na faini zake zilizopo kwa mujibu wa sheria.
Aliongeza kwa kuwataka wafanya biashara kutumia Bandari ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza mara tu bidhaa zinapokamatwa.

Bidhaa zilizokamatwa na kuteketezwa kwa kukosa ubore ni pamoja na Mafuta ya kupikia lita 26,840, Sukari kilo 46,300, Mchele kilo 5,400, Maziwa lita 950 na Biskuti kilo 60 ambavyo vyote hivyo vikiwa na thamani ya shilingi milioni 93,277,368.

Wilaya ya Bagamoyo ina jumla ya Bandari bubu (fukwe) zaidi ya 30 ambazo hutumika kupitisha bidhaa za magendo kwa lengo la kukwepa kulipa kodi huku baadhi yao hutumia Bandari bubu hizo (fukwe) kupitisha wahamiaji haramu.
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa (Mwenye miwani katikati) akiwa na watumishi kutoka Idara ya Afya, TFDA, na Idara ya forodha wakiteketeza Bidhaa za Chakula ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu.

Afisa Mwandamizi wa Forodha Bagamoyo Noeli Makere akizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG katika zoezi hilo lililofanyika hvi karibuni.

Vijana wakiendelea na zoezi la kumwaga Mafuta ya kupikia ambayo yamebainika kuwa hayafai kwa matumizi ya binadamu.

Sehemu ya Sukari na Mafuta ya kupikia vilivyoteketezwa baada ya kubainika kuwa havifai kwa matumizi ya binadamu.




BAGAMOYO KWANZA BLOG YAPATA LESENI KUTOKA TCRA.

Blog  ya BAGAMOYO KWANZA yapata usajili na kukabidhiwa leseni itakayowawezesha kuendelea kutoa huduma za kutoa Habari kwa njia ya mtandao.

Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) lililotolewa Tarehe 20 April 2018 limewataka wamiliki wa Blog, Majukwaa ya mtandaoni (Online forums) Radio na Televisheni za mtandaoni kufanya usajili na kupatiwa leseni itakayowaruhusu kutoa huduma kwa njia za mtandao.

Usajili wa Blog, Majukwaa ya mtandaoni, (Online forums) Redio na Televisheni za mtandaoni unafanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 4 ya Maudhui Mtandaoni ya Mwaka 2018 (The Electronic Postal Communications (online content) Regulations, 2018) ambapo TCRA imepewa dhamana ya kuandaa na kutunza Rajisi ya watoa huduma za maudhui kupitia Blogu, Majukwaa mtandaoni (online Forums), Redio na Televisheni mtandaoni, ili kudhibiti na kuchukua hatua panapotokea ukiukwaji wa Kanuni hizo.
 
Hivi ndio vyeti vinavyokuwezesha kumiliki Blog Tanzania.

                                                                                                



Friday, June 8, 2018

TAARIFA KWA UMMA JUMUIA ZA KIDINI NA VYAMA VYA KIJAMII

Ofisi ya Msajili wa Jumuia za Kidini na Vyama vya Kijamii Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, inazikumbusha Taasisi zote za Kidini na Vyama vya Kijamii vilivyosajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kulipa Ada na Madeni waliyonayo kabla ya tarehe 30/6/2018.

Sheria ya Jumuia, Sura ya 337 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002 (The Societies Act) inayozisajili Jumuia za Kidini na Vyama vya Kijamii inawataka wote waliosajiliwa kulipa ada zao za kila mwaka kwani kutokulipa ada ni kukiuka masharti ya Sheria iliyowasajili.

Jumuia za Kidini na Vyama vya Kijamii vinatakiwa kufika kwenye Ofisi za Msajili wa Vyama vya Kijamii na Taasisi za Kidini ili kuhakiki madeni yao hivyo kuwawezesha kulipa madeni stahiki wanayodaiwa pamoja na ada zao za mwaka huu wa fedha.

Uhakiki wa madeni hayo utahusisha nyaraka mbalimbali kama vile risiti ya mwisho ya malipo, nakala ya Cheti cha Usajili na Taarifa ya Utendaji yenye saini za Viongozi wawili.

Malipo yote yawasilishwe kupitia benki ya NMB Akaunti namba 20110013811 yenye jina MOHA REVENUE COLLECTION.