Tuesday, October 16, 2018

TAMASHA LA SANAA BAGAMOYO WANANCHI WAKARIBISHWA.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbart Makoye ametoa wito  kwa wakazi wa Bagamoyo na nchi nzima kuhuduria Tamasha la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo linalotarajiwa kuanza Tarehe 20 Oktoba 2018.

Akizungumza na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Chuo hicho Dkt. Makoye alisema kuhudhuria Tamasha hilo ni fursa kwa watanzania na wale wa nje ya Tanzania kujionea taaluma mbalimbali zinazofundishwa chuoni hapo.

Alisema chuo hicho ambacho ni kikongwe hapa nchini kwa kutoa taaluma za sanaa na utamaduni kinawapa fursa vijana kujiajiri katika fani wanazopata chuoni hapo.

Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa, Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo hufanyika kila mwaka na kuandaliwa na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) likiwa na malengo ya

>Kutunza na kuenzi sanaa na utamaduni wa Mtanzania.

>Kutengeneza jukwaa ambalo wanafunzi wa TaSUBa wanalitumia kupima kiwango chao cha umahiri katika sanaa kwa mwaka katika fani za sanaa za maonyesho na zile za ufundi.

>Kukutanisha watu wa tamaduni mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali Duniani ili kuonyesha utajiri wao wa sanaa na utamaduni.

>Kutengeneza jukwaa ambalo ni kiungo cha kujenga mahusiano ya wasanii wa ndani na nje ya nchi kupitia maonyesho ya sanaa na pia kubadilishana uzoefu na mawazo katika kuendeleza tasnia ya  ya sanaa.

Dkt. Makoye alisema mwaka huu Tamasha linafanyika kwa mara ya 37 na litapambwa na mambo mbalimbali ikiwemo Sarakasi, maigizo pamoja na maonyesho ya sanaa za ufundi.

Aidha, alisema katika Tamsha hilo kutakuwa na warsha na semina zitakazohusu mambo mbalimbali ya kijamii.

Jumla ya vikundi vya sanaa 100 vimethibitisha kushiriki na kati ya hivyo vikundi 10 ni kutoka nje ya nchi ambazo ni Kenya, Uganda, Zimbabwe, Ivory Coast, Ufaransa, Zambia,Cameroon, Ujerumani na Finland.

Aliongeza kwa kusema kuwa, ufunguzi rasmi  wa Tamasha hilo utafanyika Tarehe 20 Oktoba 2018 ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Dkt. Harrison Mwakyembe na litafungwa Tarehe 27 Oktoba 2018  ambapo mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Juliana Shonza.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni Sanaa na Utamaduni katika kukuza Uzalendo.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbart Makoye akizungumza na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Chuo hicho Mjini Bagamoyo leo Tarehe 16 Oktoba 2018.
  
Baadhi ya wakufunzi na wageni kutoka nje ya nchi wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa TaSUBa Dkt. Herbert Makoye alipokuwa akizzungumza katika ukumbi wa TaSUBa, Bagamoyo.

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UGAWAJI VIWANJA ‘PANDIKIZI’

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angeline Mabula akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rorya Charles Chacha mara baada ya kumaliza kuzungumza na watendaji wa halmashauri hiyo mwishoni mwa wiki.
.............................................


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumbà na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula amepiga marufuku ugawaji viwanja ambavyo tayari vimemilikishwa huku mmiliki wake wa awali akitafutiwa eneo lingine.

Hatua hiyo inafuatia kushamiri kwa  tabia iliyozoeleka kwa baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri mbalimbali hapa nchini kugawa maeneo ambayo tayari yana wamiliki wake wa awali na kuwapa watu wengine wenye uwezo kifedha huku wamiliki halali kuahidiwa kupatiwa kiwanja kingine.

Mhe. Mabula alitoa kauli hiyo wilayani Musoma mkoa wa Mara mwishoni mwa wiki alipokutana na watendaji wa sekta ya ardhi katika Manispaa ya Musoma pamoja na halmashauri za wilaya za Musoma na Butiama wakati wa ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa wakati wa ziara yake ya februari mwaka 2018.

“Kuanzia sasa ni marufuku kwa watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri kugawa viwanja ‘pandikizi’ katika maeneo ambayo tayari yameshamilikishwa kwa wananchi kwani suala hili limekuwa likileta migogoro mikubwa katika sekta ya ardhi” alisema Mabula.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, suala hilo limekuwa likijitokeza sana hasa maeneo yanayovutia na mara nyingi linachangiwa na maafisa ardhi wasiokuwa waaminifu ambao humpatia mtu mwenye uwezo kiwanja kilichomilikishwa kwa ahadi ya kumpatia mmiliki halali kiwanja kingine.

Alisema,  serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ambayo imekuwa ikiwatetea  watu wa hali ya chini haitavumilia hali hiyo iendelee kushamiri na kusema kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watendaji wote wa sekta ya ardhi watakaoendelea au kubainika kufanya mchezo huo.



MKUU WA MKOA WA PWANI AKUTANA NA MKURUGENZI NA MTENDAJI MKUU WA BENKI YA CRADB

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mheshimiwa Mhandisi Evarist Ndikilo, akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bibi Theresia Mmbando pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Bibi Jokate Urban Mwegelo alipokutana na Benki ya CRDB katika  mkutano wa pamoja wa kujadili maandalizi ya wiki ya Maonesho ya Viwanda ya Mkoa wa Pwani na Mkurugenzi Mtendaji  na  Mwendeshaji  wa Benki ya CRDB Ndugu Abdulmajid Nsekela

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mheshimiwa Mhandisi Evarist Ndikilo, akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bibi Theresia Mmbando pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Bibi Jokate Urban Mwegelo alipokutana na Benki ya CRDB katika  mkutano wa pamoja wa kujadili maandalizi ya wiki ya Maonesho ya Viwanda ya Mkoa wa Pwani na Mkurugenzi Mtendaji  na  Mwendeshaji  wa Benki ya CRDB Ndugu Abdulmajid Nsekela, wengine ni Wakuu wa idara mbalimbali kutoka benki ya CRDB , Teddy Maganga Mratibu wa Matukio pamoja na Philomena Kasanga ambaye ni katibu wa mkuu wa Mkoa wa Pwani



MAGAZETI YA LEO OKTOBA 16. 2018.