Sunday, December 24, 2017

WAZIRI MKUU AUVUNJA MFUKO WA KUENDELEZA PAMBA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa Onyo kwa watumishi wa umma na Madiwani  wa Manispaa ya Songea kwa kuweka mbele maslahi yao binafsi na akawataka wajirekebishe mara moja.Ametoa onyo hilo jana (Jumamosi, Desemba 23, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa manispaa na madiwani kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Songea, mjini Songea Mkoani Ruvuma


PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
..............................................


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuvunja Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Pamba (CDTF) na amegiza wahusika wote wachunguzwe ili kubaini fedha walizokusanya zimetumikaje.

Alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki (Ijumaa, Desemba 22, 2017) wakati akizungumza na wadau wa zao hilo kwenye kikao alichokiitisha mkoani Shinyanga kufanya ufuatiliaji wa maagizo ambayo alikwishakuyatoa. Waziri Mkuu alishafanya vikao vitatu na wadau mbalimbali wa zao hilo.

Alichukua uamuzi huo baada ya kubaini kuwa watendaji wa mfuko huo hawajatekeleza majukumu ya kuundwa kwa mfuko huo lakini pia majukumu yao yanaingiliana na yale ya Bodi ya Pamba Tanzania (TCB).

“Kuna CDTF katika zao la pamba lakini hakuna inachofanya ambacho kinawalenga wakulima moja kwa moja. Tunaiondoa CDTF na kazi zake kuanzia sasa zifanywe na Bodi,” alisema.

“Waziri wa Kilimo peleka timu ya ukaguzi kuona wamefanya nini hadi sasa. Tunataka Bodi ifanye kazi na iulizwe maswali kuhusu zao hili. Endapo kuna jambo halijafanyika, Bodi iwe na uwezo wa kutoa majibu si kusubiri tena mtu wa chombo kingine aje kutoa majibu,” alisema Waziri Mkuu.

“Kwa muundo huu, Mkurugenzi wa Bodi anakaa tu, wakati akisubiri kazi yake ifanywe na CDTF,” aliongeza.

Mfuko wa CDTF unaundwa na wajumbe sita ambao ni wawakilishi wa wakulima wawili, wawakilishi wa wenye viwanda vya kuchambua pamba wawili, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba na Mkurugenzi wa Mazao kutoka Wizara ya Kilimo.

Mfuko huu uliundwa mwaka 1999 na Bodi ya Pamba (TCB) ili uwashirikishe wadau wa zao hilo kuondoa matatizo yaliyojitokeza kwenye sekta hiyo baada ya Serikali kujitoa kwenye uendeshaji wa moja kwa moja wa mazao nchini ikiwemo uzalishaji na biashara kutokana na mfumo wa soko huria.

Desemba mwaka jana, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alifikia uamuzi kama huo na kuamua kusimamisha shughuli zilizokuwa zinafanywa na Mfuko wa Kuendesha Zao la Korosho Nchini (CIDTF) ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha za mfuko huo.

Akitangaza uamuzi huo jijini Dar es Salaam, Waziri Tizeba alisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mfuko huo kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu pamoja na kuwapo kwa malalamiko ya muda mrefu kuhusu utendaji wa mfuko huo.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMAPILI, DESEMBA 24, 2017

Friday, December 22, 2017

WANAWAKE BAGAMOYO WAPEWA SOMO LA UCHUMI.


Mwenyekiti wa UWT wilaya ya kibaha vijijini Leila Hamoud Jumaa watatu kushoto akisikiliza maelezo ya mtaalamu kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini TFDA kanda ya Mashariki, John Mosha wa pili kulia, katika maonesho ya Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo yanayoendelea mjini Bagamoyo katika Viwanja vya shule ya Msingi Mbaruku, wa kwanza ni Katiba wa UWT Bagamoyo Mwatabu Hussein na wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo Teddy Alban Davis.  


 Mwenyekiti wa UWT wilaya ya kibaha vijijini Leila Hamoud Jumaa akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo yanayoendelea katika viwanja vya shule y Msingi Mbaruku.
..............................
Wajasiliamali wanawake Bagamoyo wametakiwa kuacha kukata tamaa katika kujikwamua kiuchumi licha ya changamoto zinazowakabili katika kuzalisha bidhaa, utafutaji wa masoko na ukosefu wa mitaji.

Akizindua maonesho ya siku tano ya Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mjini Bagamoyo, yanayoendelea katika viwanja vya shule ya msingi Mbaruku, Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Kibaha Vijijini, Leila Hamoud Jumaa alisema ili kuweza kujikwamua kiuchumi ni lazima uwepo uthubutu wa utekelezaji wa malengo wanayojiwekea wanawake na kwamba katika kujikwamua changamoto hazikosekani.

Alisema licha ya changamoto hizo bado wanawake wanapaswa kusonga mbele katika kujikwamua kiuchumi.

Awali akitoa taarifa ya jukwaa hilo, Mratibu wa Dawati la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Geofrey Magogwa alisema Jukwaa la uwezeshaji wa wanawake kiuchumi Bagamoyo linakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kukosekana kwa ujuzi wa uhakika, kukosekana kwa mitaji, na taasisi za kifedha kuweka masharti magumu ambayo wajasiliamali wadogo wanashindwa kutimiza.

Kwa upande wake Charles Wambura akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo alisema Halmashauri ya Bagamoyo itashirikiana na vikundi vya ujasiliamali ili kuhakikisha vinapiga hatua kimaendeleo.

Wambura alisema tayari vikundi vingi vimefaidika na asilimia tano inayotolewa na Halmashauri kwenda kwa kinamama na kuongeza kuwa juhudi za kuwasaidia zinafanywa na halmashauri hiyo.

Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mdogo Bagamoyo, Athumani Stili alisema wakazi wa Bagamoyo wakiwemo wanawake wanatakiwa kutumia fursa zinazoingia Bagamoyo katika kujiongezea kipato.

Alisema ujenzi wa Bandari unaotarajiwa kuanza mwezi Januari 2018 ni miongoni mwa fursa za kujiongezea kipato endapo zitatumika vizuri.

Aliongeza kuwa kufuatia ujenzi huo kutakuwa na watu watakaofanya shughuli mbalimbali hivyo kutakuwepo na mahitaji ya aina mbalimbali ambayo waandaaji wa mahitaji hayo ni wakazi wa Bagamoyo.

Akizungumzia lengo la maonesho hayo Mwenyekit wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo, Teddy Alban Davis alisema lengo ni kuwaonesha wanawake fursa za kiuchumi zilizopo Bagamoyo ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuwanyanyua wanawake wa Bagamoyo.

Aliongeza kwa kusema kuwa, Maonesho yatatoa fursa kwa wajasiliamali kufahamiana na kubadilishana mawazo juu ya namna ya kufikia malengo hasa kwa mjasiliami wa chini.

Teddy alisema viongozi wa Jukwaa hilo waliweza kutembelea kata zote za halmashauri ya Bagamoyo na kubaini wajasiliamali ambao wana uwezo wa kuzalisha vitu mbalimbali vyenye ubora lakini hawana masoko na kwamba kupitia maonesho hayo fursa mbali mbali zitapatikana.

Kwa upande wao wajasiliamali waliozungumza na bagamoyokwanza blog walisema wajasiliamali wadogowadogo wanakabiliwa na chnagamoto ya kupata malighafi kwaajili ya kutengenezea bidhaa mbalimbali ambapo hulazimika kununua kwa bei ya juu hali inayopelekea kukosekana kwa faida katika bidhaa wanazozalisha.

Adha, walisema uelewa mdogo miongoni mwa wananchi ni sababu inayopelekea kushindwa kufikia malengo kwakuwa wananchi wengi hawana utamaduni wa kununua bidhaa za ndani hata kama zina ubora unaokubalika.

Nae muwakilishi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA)  kanda ya Mashariki, John Claude Mosha alisema wajasiliamali wanapaswa kufuata taratibu za Mamlaka ya Chakula na Dawa ili kuzifanya bidhaa wanazozalisha kuwa na viwango vinavyokubalika katika jamii.

Alisema kutumia bidha ambazo hazijasajiliwa na mamlaka hiyo ni kunaweza kusababisha madhara kwa watumiajai hivyo ni vyema kumuondoa wasiwasi mtumiajai kwa kuisajili bidhaa kwenye mamlaka ya chakula na dawa.

Maonesho ya Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Bagamoyo yameanza Tarehe 20 Desemba katika viwanja vya shule msingi Mbaruku na yanatarajiwa kufikia kilele chake siku ya Tarehe 25 Desemba 2017 ambapo wajasiliamali wanawake kutoka kata zote 11 za Halmashauri ya Bagamoyo wanaendelea kuonesha bidhaa zao. 



Kikundi cha wajasilimali ambao ni wazee wakishangilia baada ya kukabidhiwa shilingi laki moja na mgeni rasmi 





RAIS WA TFF KUKUTANA NA WAHARIRI WA HABARI ZA MICHEZO.



Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia atakutana na Wahariri wa Habari za Michezo Jumatano Desemba 27,2017.

Pamoja na mambo mengine Rais Karia atazungumzia miezi minne tokea uongozi uliopo umeingia madarakani pamoja na vitu vilivyofanyika katika muda huo.

Aidha Rais Karia ataelezea changamoto mbalimbali zilizopo TFF pamoja na njia gani inatumika/Itatumika kuweza kupiga hatua kwa mpira wa Tanzania.
Taarifa zaidi za mkutano huo wa Rais Karia na Wahariri,mahali utakapofanyika pamoja na mualiko utatolewa kwa vyombo vya habari.
Huu ni mkutano wa kwanza wa Rais Karia na Wahariri wa habari za Michezo tokea ameingia madarakani.

Rais Karia aliingia madarakani August 12, 2017 kwenye uchaguzi uliofanyika mkoani Dodoma baada ya kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi ambao pia uliwaingiza madarakani Michael Wambura kwenye nafasi ya makamu wa Rais.

Wajumbe wa kamati ya utendaji waliongia madarakani kwenye uchaguzi huo ni pamoja na

Kanda namba 13 Dar es Salaam
Lameck Nyambaya

Kanda namba 12 Kilimanjaro na Tanga
Khalid Abdallah

Kanda No 11 Pwani na Morogoro
Francis Ndulane

Kanda Namba 10 Dodoma na Singida 
Mohamed Aden

Kanda Namba 9 Lindi na Mtwara
Dunstan Mkundi

Kanda namba 8 Njombe na Ruvuma
James Mhagama

Kanda namba 7 Mbeya na Iringa
Elias Mwanjala

Kanda Namba 6 Katavi na Rukwa
Kenneth Pesambili

Kanda namba 5 Kigoma na Tabora
Issa Bukuku

Kanda namba 4 Arusha na Manyara
Sarah Chao

Kanda namba 3 Shinyanga, Simiyu
Mbasha Matutu

Kanda namba 2 Mara, Mwanza
Vedastus Lufano

Kanda namba 1 Kagera, Geita
Salum Chama

Imetolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano TFF
Desemba 22,2017