Friday, December 16, 2016

BANDARI TANGA YAIFUNGA MTWARA MABAO 43-16 MCHEZO WA PETE KATIKA MICHUANO YA BANDARI

mikono
Wachezaji wa timu za Bandari ya Dar es Salaam  na Makao Makuu wakichuana kwenye mchezo wa mpira wa kikapu uliochezwa kwenye uwanja wa Bandari Tanga ambao ulimalizika kwa Bandari Dar kuibuka na ushindi wa vikapu 50 -47.
 
Wachezaji wa timu za Bandari ya Dar es Salaam  na Makao
Makuu wakichuana kwenye mchezo wa mpira wa kikapu uliochezwa kwenye uwanja wa Bandari Tanga ambao ulimalizika kwa Bandari Dar kuibuka na ushindi wa vikapu 50 -47.
 
 Wachezaji wa kuvuta kamba timu ya Bandari ya Tanga wakichuana dhidi ya Makao Makuu mchezo umalizika kwa Tanga kuibuka na ushindi wa seti 2-0 mchezo uliochezwa viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlaly mjini Tanga
 
TIMU ya Mpira wa Pete ya Bandari ya Tanga leo wameweza kuibuka na ushindi wa mabao 43-16 dhidi ya Bandari ya Mtwara kwenye michuano ya Bandari inayoendelea mjini Tanga.

 Mchezo huo ambao ulichezwa kwenye viwanja vya Bandari mjini hapa ambapo mpaka timu zote zinakwenda mapumziko Bandari Tanga ilikuwa ikiongozwa kwa mabao 23 -17 dhidi ya Mtwara.

 Halikadhalika Tanga wakiweza kuibuka pia na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Makao  Makuu kwenye mchezo wa mpira wa miguu
uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari Popatlaly mjini hapa.

Katika mchezo mwengine uliochezwa kwenye uwanja huo timu ya Bandari ya Dar es Salaam iliweza kuibuka na ushindi dhidi ya Makao Makuu kwa mabao 36-13.

Wakati huo huo,Timu ya Bandari ya Dar es Salaam imeweza kuibuka na ushindi wa vikapu 50 -47 dhidi ya Makao Makuu kwenye mchezo wa mpira wa kikapu uliochezwa kwenye dimba hilo la Bandari mjini hapa.

Kwenye mchezo mpira wa miguu uliozikutanisha Bandari Mtwara na Maziwa Makuu ambapo timu hizo mpaka dakika 90 zilijikuta zikigawana pointi moja moja baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1.

 Ili kuonyesha wana umahiri mkubwa kwenye michezo Bandari Tanga wanaume waliweza kuibuka na ushindi wa seti 2-0 dhidi ya Makao Makuu kwenye mchezo wa kuvuta kamba.

Wakati wanaume wakiibuka na ushindi huo wanawake nao waliweza kuwaunga mkono wenzao kwa kuibuka na ushindi wa seti 2-0 dhidi ya Makao makuu kwenye mchezo wa kuvuta kamba uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Popatlaly.

Mashindano hayo ambayo yalifunguliwa jana na Mkurugenzi wa Bandari nchini (TPA) Deusdedit Kakoko ambaye aliwataka wanamichezo hao kuzingatia nidhamu na maarifa kwenye michezo yao ili kupata ushindi.

Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha.

SIMBACHAWENE AFAFANUA AGIZO LA RAIS MAGUFULI KUHUSU ‘WAMACHINGA’

sumba-2
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene akitoa maelezo kwa waandishi wa habari juu ya kutoeleweka vema Agizo la Rais Dkt. John Magufuli kuhusu zoezi la usitishaji wa kuwaondoa Wafanyabiashara ndogo ndogo katikati ya miji na kuwatafutia maeneo rafiki kufanyia biashara zao kushoto kwake ni Naibu Katibu TAMISEMI (Afya) Dk. Zainab Chaula.
 .............................................
Serikali imewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha wanatekeleza agizo la Rais Dk.John Magufuli la kuwatafutia maeneo ya kufanyia biashara Wafanyabiashara ndogo ndogo ‘wamachinga’ na si kuwaacha wafanye biashara zao kiholela.

Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), George Simbachawene alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Amewataka wakuu hao kuwawekea Wamachinga utaratibu wa kupangiwa maeneo ya shughuli zao yenye wateja wa kutosha, miundombinu rafiki na washirikishwe katika michakato yote wakati wa maandalizi ya maeneo hayo.

Amefafanua kuwa Rais Magufuli alisitisha zoezi la kuwaondoa kiholela wamachinga kutoka katika maeneo wanayofanyia biashara zao kwasasa hadi pale mamlaka husika zitakapoandaa maeneo maalum kwa ajili yao.

“Maagizo ya Rais yameonesha namna anavyowapenda na kuwathamini wamachinga na aliweka msisitizo wasiondolewe mpaka pale yatakapotengwa maeneo mbadala,”amesema Simbachawene.

Amebainisha utaratibu wowote wa kuwapangia maeneo mapya uzingatie ushirikishwaji ili kuondoa msuguano wakati wa kuwahamisha na kwamba pale inapowezekana wapangiwe maeneo ya katikati ya mji ikibidi kuteua mitaa mahsusi kwa utaratibu utakaowekwa ili wafanye biashara zao.

Pamoja na maelezo hayo, Simbachawene amesema Rais alisisitiza kwamba maagizo yake juu ya wamachinga hayana maana kuwa kwasasa wamachinga wafanye biashara zao kwenye barabara za kupita magari na watembea kwa miguu au kwenye hifadhi za barabara.

Amewasisitiza wakuu hao kujipanga kutekeleza maagizo ya rais kwa ufasaha, weledi na umakini mkubwa ili kuwasaidia wamachinga kufanya biashara zao na kujipatia kipato na kuzitaka mamlaka za serikali kuheshimu shughuli zao.

Wakati huo huo, Simbachawene amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa ya Rukwa na Arusha watafute shule ndani ya mikoa yao na kuwapanga wanafunzi ambao wameondolewa shule za sekondari Makuyuni na Milundikwa ambazo majengo yake yamerudishwa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT).

Amesema serikali imelazimika kuwaondoa wanafunzi 254 wa shule ya Makuyuni wa kidato cha kwanza hadi cha tatu na katika shule ya Milundikwa wanafunzi 120 wa kidato cha tano na sita.

Pia amesema walimu na watumishi wasio walimu ambao walikuwa wakifundisha katika shule hizo wapangiwe kwenye shule watakazopelekwa wanafunzi hao.

Ametaka utekelezaji huo wa agizo hilo ufanyike kabla shule hazijafunguliwa januari 2017 na lizingatie kutowavuruga wanafunzi wa kidato cha sita ambao tayari wamesajiliwa kufanya mtihani wa Taifa mwezi mei, 2017.
sumbaa-1
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene akitoa Agizo juu ya Shule za Sekondari za Makuyuni (Arusha) na Milundikwa (Rukwa) ambazo majengo yake yalikuwa ni makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na baadae Halmashauri zikapewa kuyatumia majengo hayo kama shule za Bweni na kwa sasa zinarejeshwa tena mikononi mwa Jeshi kutokana na kuongezeka kwa  shughuli za Jeshi.