Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Mamkamba.
(MB) akitoa Taarifa kwa Umma kuhusu marufuku ya uzalishaji, uingizaji ,
usambazaji,na matumizi ya vifungashio vya plastiki maarufu kama viroba
vinavyotumika kufungashia pombe kali, alipozungumza na waandishi wa habari
Ofisini kwake Mtaa wa Luthuli Jijini Dare es Salaam Leo.
Mtakumbuka tarehe 20 Februari 2017 Ofisi ya Makamu
wa Rais ilitoa tamko la Serikali la utaratibu utakaotumika kutekeleza agizo la
kusitisha utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali zinazofungashwa kwenye
vifungashio vya plastiki (viroba)kuanzia tarehe 1 Machi 2017.
Utekelezaji wa
katazo hili utazingatia Ibara ya 8(1) (b) na 14, Sheria ya Mazingira ya mwaka
2004 na Kanuni zake zilizotungwa kupitia kifungu 230 (2) (f) cha sheria hiyo,
na Sheria ya Leseni za Vileo Namba 28 ya mwaka 1968 pamoja na marekebisho yake
ya mwaka 2012.
Napenda kusisitiza na kuujulisha umma wa Tanzania
kuwa utekelezaji wa maamuzi haya ya Serikali kuhusu usitishaji uingizaji,
uzalishaji, uuzaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki vya kufungia pombe
kali utaanza rasmi tarehe 01 Machi, 2017, katika Mikoa yote ya Tanzania Bara.
Operesheni ya kukagua utekelezaji wa agizo la serikali la usitishaji
utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zinazofungashwa kwenye vifungashio
vya plastiki itaendeshwa nchini kote kuanzia tarehe 2 Machi 2017 kwa kupitia
Kamati za Ulinzi na Usalama na Kamati za Mazingira katika ngazi ya Mkoa, Wilaya,
Tarafa, Kata, Vijiji na Mtaa.
Kamati hizi zitawajibika kuwasilisha
taarifa za operesheni wakati na baada ya operesheni hiyo Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa na nakala Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mnamo terehe 24 Februari 2017, kiliitishwa kikao cha
Mawaziri na viongozi wa taasisi za Serikali kujadili mpango wa utekelezaji wa
zuio hili. Katika kikao hicho, Wizara na taasisi za Serikali zilipewa majukumu
mbalimbali, kama ifuatavyo:
1.
Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), kwa kuzingatia umuhimu wa ujazo katika utozaji kodi,
imeanzisha mfumo wa stempu za Kielektroniki ili kudhibiti ujazo wakati wa
uzalishaji kwa ajili ya kupata mapato stahiki.
Aidha, Mamlaka itahakikisha
kwamba wazalishaji na waingizaji nchini wa malighafi ya pombe kali (ethanol)
wamesajiliwa na kwamba mfumo wa ufuatiliaji wa usambazaji malighafi hiyo
unawekwa.
Wazalishaji na waingizaji wa malighafi hiyo watawauzia wale tu ambao
wamepewa kibali na pia watatakiwa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu (3)
ya kiasi cha ujazo kilichouzwa na wateja waliouziwa ambao wamesajiliwa.
Uuzaji
wa malighafi kwa watengezaji wa pombe kali ambao hawajasajiliwa itakuwa ni kosa
la jinai kulingana na Sheria.
2.
Mkemia Mkuu
wa Serikali ambaye ndiye msajili wa kemikali za viwandani na majumbani,
atasajili makampuni na taasisi zinazoingiza kemikali za viwandani na majumbani
nchini ikiwa ni pamoja na Ethanol. Msajili atawajibika kutoa taarifa
sahihi za majina ya makampuni na watu binafsi na taasisi zinazohusika, kiasi
kilichoingizwa na kimetumika, pamoja na madhumuni ya matumizi.
3.
Kulingana na
sheria ya Leseni ya Vileo Na 28 ya Mwaka 1968 na marekebisho yake ya mwaka
2012, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika operesheni hii
itaratibu zoezi hili katika mikoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji na mitaa yote
Tanzania bara kwa kuhakikisha kuwa wanaofanya biashara ya pombe ya kawaida na
pombe kali (spirit) na watumiaji kinyume na masharti ya leseni za vileo
wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
4.
Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), katika
operesheni hii watakukagua viwanda vyote vinavyojihusisha na uzalishaji wa
vileo na vifungashio vya aina mbalimbali vya kufungia pombe kali kama vimekidhi
viwango vya kitaifa Ukaguzi katika viwanda vya plastiki utachunguza kama kuna
mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki kwa ajili ya pombe kali.
Mitambo
ya kuzalisha vifungashio vya plastiki kama haitumiki kwa kuzalisha bidhaa
zingine katika kiwanda husika, mwenye kiwanda atalazimika kutoa ufafanuzi wa
hatima ya mitambo hiyo.
Mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki
itakayokutwa inaendelea kuzalisha pombe kali na kufungashia vifungashio vya
plastiki itakamatwa na kutaifishwa na wahusika watashtakiwa.
5.
Wizara ya
Afya Maendeleo ya Jamii, Watoto na Wazee, kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA) na mabwana afya katika operesheni hii watatoa elimu kwa umma na kukagua
maeneo yote yanayotumika kuhifadhia, kuuza na kusambaza vileo vya aina zote, na
kushiriki kukamata vileo ambavyo vipo kinyume cha sheria na kanuni.
6.
Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia Idara ya Habari Maelezo, itasaidia
kutoa elimu kwa umma kuhusu suala hili.
7.
Wizara ya
Mambo ya Ndani, kupitia Jeshi la Polisi, na vyombo vingine vya ulinzi na usalama,
itashiriki katika operesheni, ikiwemo kwenye masuala ya inteligensia.
8.
Ofisi ya
Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira,
wataratibu operesheni.
Kama tangazo letu la tarehe 20/2/2017 lilivyoonesha
muda wa nyongeza unaweza kutolewa kwa wazalishaji halali ambao wataonyesha
ushahidi wa kuelekea kuhamia kwenye teknolojia ya chupa, na kwamba watahitaji
muda mchache kufanya hivyo, na ambao watatimiza masharti kadhaa na kupata
kibali maalum kabla ya tarehe 28/2/2017. Hadi sasa Serikali imepokea maombi ya
wazalishaji.
9. Tutangaza kesho iwapo kuna ambao wamekidhi masharti au la.
Kanuni za upigaji marufuku pombe hizi zipo tayari.
Pia tumepokea malalamiko kwa wazalishaji wengi
kwamba zoezi hili limekuja ghafla na wengine wana malighafi na bidhaa kwenye
maghala. Ukweli ni kwamba Serikali ilitoa taarifa Bungeni, kuanzia mwezi Mei
2016, na mara kadhaa baada ya hapo, na rekodi zipo, kuhusu hatua hizi.
Vilevile, taarifa ya Serikali iliyotangaza kupiga marufuku pombe za viroba
ziliripotiwa kwa ukubwa stahiki kwenye vyombo vya habari, ikiwemo kwenye
ukurasa wa kwanza wa gazeti la Mwananchi, mwezi Agosti 2016.
Katika taarifa
zote za nyuma, Serikali ilitangaza kwamba hatua hiyo itaanza tarehe 1 Januari
2017.
Hatua hizi zimechelewa kwa miezi miwili. Iwapo, baada ya taarifa hizo za
Serikali, kuna mzalishaji ameagiza malighafi au kutengeneza au kuhifadhi pombe
za viroba, au kuchukua mkopo kwa ajili hiyo, atakuwa amefanya hivyo akijua
madhara yake.
Mwisho napenda kutoa wito kwa wananchi wote kutoa
ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi hili la upigaji marufuku matumizi
ya pombe zinazofungashwa katika vifungashio vya plastiki (viroba) kwa kutoa
taarifa kwa vyombo husika ili wale wanaozalisha na kuuza au kuhifadhi waweze
kuchukuliwa hatua stahiki. Zawadi itatolewa kwa watakaotoa taarifa
zitakazowezesha kukamatwa kwa watakaokiuka zuio hili.
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
28/02/2017
28/02/2017