Meli
mbili za Mv. Ruvuma na Mv Njombe zikiwa katika cherezo katika Bandari ya
Itungi, Wilayani Kyela Mkoani Mbeya, zikiwa katika hatua za mwisho kabla ya
kuanza kufanyiwa majaribio ndani ya Ziwa Nyasa Mwishoni mwa Februari, 2017.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Songoro Marine Transport Ltd, Bw. Saleh Songoro, akionesha mchoro
wa meli mbili za mizigo zenye uwezo wa kubeba tani 1000 kila moja anazoziunda
kwa ajili ya matumizi katika Ziwa Nyasa, katika Bandari ya Itungi, Wilayani
Kyela mkoani Mbeya, baada ya kutembelewa na ujumbe wa Serikali unaofuatilia
masuala ya biashara mipakani mkoani Mbeya.
.................................
UJENZI wa meli mbili za mizigo katika Bandari ya
Itungi wilayani Kyela Mkoani Mbeya, MV Njombe na MV Ruvuma, umekamilika kwa
zaidi ya asilimia 98 na kwamba meli hizo zinatarajiwa kufanyiwa majaribio Ziwa
Nyasa, mwishoni mwa mwezi Februari na kukabidhiwa rasmi Serikalini mwezi Machi,
2017.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro
MarineTransport Ltd ya Jijini Mwanza, inayounda meli hizo, Mhandisi Saleh Songoro,
amesema hayo wakati ujumbe wa Serikali ulioongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa
Wizaya ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, ulipotembelea Bandari
hiyo ukiwa katika zaira ya kukagua hali ya biashara mipakani mkoani Mbeya.
Amesema kuwa kukamilika kwa meli hizo mbili za
mizigo za kisasa zenye uwezo wa kubeba tani elfu moja (1,000) za mizigo kila
moja na kugharimu shilingi bilioni 11, kutaiwezesha Kampuni hiyo kuanza kuunda
meli nyingine ya tatu itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za
mizigo.
Pamoja na meli hizo, Mhandisi Songoro amesema kuwa
mradi huo pia umewezesha kujengwa kwa cherezo cha kwanza na cha pekee kitakacho
iwezesha Mamlaka ya Bandari Tanzania-TPA katika uundaji wa meli na kuzifanyia
matengenezo meli nyingine za ndani na nje ya nchi zikiwemo Malawi na Msumbiji.
Kaimu Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),
Bandari ya Itungi, Bw. Ajuaye Msese, amesema kuwa uamuzi wa Serikali wa
kuunda meli hizo ulikuwa kutatua changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa vyombo
vya baharini vya kusafirisha abiria na mizingo ndani na nje ya nchi kupitia
Ziwa Nyasa.
Pause: Bw. Ajuaye Msese-Kaimu Mkuu wa TPA, Bandari
ya Itungi
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, , pamoja na kupongeza kazi
kubwa iliyofanywa na mkandarasi mzawa, Songoro Marine Transport Ltd, kuunda
meli hizo, wamesema kuwa kukamilika kwa meli hizo kutachochea biashara na
mapato ya serikali kupitia shughuli za usafiri na usafirishaji katika Ziwa
Nyasa.
Prof. Mkenda amesisitiza kuwa Serikali itaangalia
uwezekano namna ya kumtumia Mkandarasi huyo, Bw. Saleh Songoro, kuunda meli
nyingi zaidi za ndani na nje ya nchi ili kukamata soko hilo la utengenezaji wa
meli kitaifa na kimataifa hatua itakayoliletea Taifa sifa, kukuza uwekezaji na
ajira.
Ujenzi wa Meli zote tatu, mbili za mizigo pekee, na
moja ya mizigo na abiria, umekadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 20 na
utakuwa umetekeleza ahadi ya Serikali ya muda mrefu ya kuboresha usafiri wa
abiria na mizigo kupitia Ziwa Nyasa, ambapo unatarajiwa kukuza biashara kati ya
Tanzania, Malawi na Msumbiji, kusisimua uchumi wa wakazi wa wilaya ya Kyela na
ukanda wote wa Kusini.
Aidha kukamilika kwa ujenzi wa meli hizo kutapunguza
matukio ya ajali za mara kwa mara zinazogharimu maisha ya watu wengi wanaotumia
Ziwa Nyasa, linalo tajwa kuwa la pili kwa kuwa na mawimbi makali na la
tano kuwa na kina kirefu cha maji duniani.
Bw.
Juma Nassoro akipaka rangi meli ya mizigo ya Mv Ruvuma, ikiwa ni hatua za
mwisho wa ukamilishaji wa uundaji wa meli hiyo yenye uwezo wakubeba tani 1000
za mizigo itakayokuwa ikifanya safari zake Ziwa Nyasa, wakti Ujumbe wa Serikali
kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ulipofanya ziara katika Bandari ya Itungi,
wilayani Kyela mkoani Mbeya.
Kiongozi
wa Ujumbe wa Serikali unaotembelea kujionea shughuli za biashara mipakani
mkoani Mbeya, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis
Shaaban (Katikati), Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof.
Adolf Mkenda (kulia) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Balozi Hassan Simba Yahya (kushoto), wakisikiliza maelezo ya Kaimu Mkuu wa
Bandari ya Itungi iliyoko Wilayani Kyela Mkoani Mbeya, Bw. Ajuaye Msese (hayupo
pichani) wakati viongozi hao walipotembelea bandari hiyo kujionea ujenzi wa
Meli mbili za mizigo unaoendelea chini ya Mamlaka ya Bandari Tanzania-TPA.
Kaimu
Mkuu wa Bandari ya Itungi, Wilayani Kyela mkoani Mbeya, Bw. Ajuaye Msese
akitoa maelezo mafupi kuhusu Bandari ya Itungi, na majukumu yake kwa ujumla kwa
wageni waliotembelea Bandari hiyo mkoani Mbeya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd,
inayounda meli tatu katika Bandari hiyo, Bw. Saleh Songoro, akielezea historia
fupi ya kampuni yake iliyoingia mkataba na Mamlaka ya Bandari Tanzania-TPA
kuunda meli tatu Ziwa Nyasa, baada ya Ujumbe wa Serikali ukiongozwa na Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, ulipotembelea
Bandari hiyo wilayani Kyela mkoani Mbeya
Mkurugenzi
Mtendaji wa Songoro Marine Transport Ltd, Bw. Saleh Songoro, akionesha moja
kati ya ya meli mbili za mizigo zenye uwezo wa kubeba tani 1000 kila moja
anazoziunda kwa ajili ya matumizi katika Ziwa Nyasa, katika Bandari ya Itungi, Wilayani
Kyela mkoani Mbeya, baada ya kutembelewa na ujumbe wa Serikali unaofuatilia
masuala ya biashara mipakani mkoani Mbeya.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Songoro Marine Transport Ltd, Bw. Saleh Songoro, akionesha mfumo wa
kuongoza meli katika chumba cha nahodha wa meli ya Mv Njombe, huku Katibu Mkuu
wa Wizara ya Viwanda, Biasha na Uwekezaji Prof Adolf. Mkenda, akiangalia kwa
makini mfumo huo wa kisasa namna unavyofanya kazi.
Baadhi ya wajumbe wa Serikali waliofanya ziara katika Bandari ya Itungi
mkoani Mbeya kujionea uundwaji wa meli mbili za mizigo wakishuka kwenye ngazi
baada ya kumaliza kukagua meli ya Mv Njombe inayotengenezwa na Kampuni ya
Songoro Marine Transport Ltd inayoshughulika na kutengeneza vyombo vya usafiri
vya majini katika Bandari ya Itungi, Wilayani Kyela, mkoani Mbeya.
(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)
No comments:
Post a Comment