Thursday, April 25, 2024

AJALI YA MOTO YAUA WANNE NGARA.

 

Alodia Babara

Ngara.

Watu wanne katika kata ya Rusumo wilaya ya Ngara mkoani Kagera wamepoteza maisha na wengine saba kunusurika kwenye nyumba baada ya chumba walichokuwa wamelala kuwaka moto kutokana na jiko la mkaa ambalo limesababisha madumu ya petroli yaliyokuwa yamehifadhiwa katika chumba hicho kushika moto na kulipuka.


Kamishna msaidizi mwandamizi wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Kagera Zabron Muhumha amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Aprili 25, 2024 saa 04:00 alfajiri na kusababisha vifo vya vijana wanne waliokuwa wamelala kwenye chumba kimoja.


Amesema jeshi la zimamoto na uokoaji kituo cha Rusumo kilipata taarifa ya tukio la moto wa kuunguza nyumba inayomilikiwa na Didas Dominick Kalido yenye vyumba vinne ambapo watu waliolala katika nyumba hiyo walikuwa 11 na miongoni mwa chumba kimoja cha nyumba hiyo walikuwa wamelala vijana wanne na wote walipoteza maisha na saba walitoka wakiwa na majeraha madogomadogo.


“Waliofariki ni Rajabu Paul (16) mnyambo mkazi wa Kahaza Rusumo, George Josephat (18) mkazi wa Mwibumba Rusumo, Eustace amejulikana kwa jina moja ni mkazi wa Muleba na Revocatus Jacob (16) mkazi wa Mwibumba Rusumo alikuwa anauza mayai ya kuchemsha” Amesema Kamanda Muhumha.


Aidha amewataja wengine saba ambao walikuwa kwenye nyumba na walitoka na majeraha madogo kuwa ni Deokres Medard (31) mhaya, Pelis Theofil (20) mkazi wa Rusumo, Elizaberth John (24) Mhaya, Rashid Peter (29) mhangaza,  Safina Theophil (12), Evelin Rashid miaka miwili, Bismas Theores miezi kumi.


Amesema kuwa, baada ya jeshi hilo kufanya uchunguzi wa awali umebaini kuwa chumba walichokuwa wamelala marehemu kilikuwa kinahifadhi madumu ya petrol na aliyekuwa anauza mayai alichemsha mayai kwa kutumia jiko la mkaa na hivyo wakavuta hewa chafu wakawa wamezidiwa na madumu ya petrol yakashika moto na kulipuka na kusababisha vifo vyao.


Amesema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospital ya wilaya ya ngara, Nyamihaga na taratibu nyingine za mazishi zinaendelea kufanyika.


Ametoa wito kwa jamii kuwa makini katika kuhifadhi vitu vya milipuko kama petrol nadisel, kwenye nyumba ambayo wanalala kwani ni hatari sana na kuwa wameishapigia kelele wananchi kuacha tabia hiyo na pamoja na kutoa elimu mara kwa mara bado wananchi wameendelea kuhifadhi petrol kwenye nyumba wanazolala.


Amewataka wauza patrol na disel kutouza katika madumu kwani ni hatari na badala yake wawawekee moja kwa moja kwenye vyombo vyao vya moto na akatolea mfano wale wanaoishi visiwani kuwa na vibari maalum vya kusafirisha petrol na disel, na kuhusu majiko ya mkaa watu waache tabia ya kulala nayo ndani yakiwa yanawaka au watumie nishati mbadala.


CCM MKOA WA PWANI YAWANOA VIONGOZI WAKE.

 







Na Omary Mngindo, Mlandizi.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kupitia Katibu wake wa Siasa na Uenezi,  DAVID MRAMBA kimeanza ziara ya Tarafa kwa Tarafa kikiwapiga msasa viongozi wake wa ngazi za Kata.


Katika ziara hiyo iliyoanzia Tarafa ya Mlandizi Jimbo la Kibaha Vijijini ilihudhuriwa na viongozi wanaotokea Kata sita zinazounda Tarafa hiyo, na kupewa jina la Step by Step inayolenga kuwaweka pamoja viongozi hao.


Kwa upande wake Katibu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya ya Kibaha JOEL KITUU amezungumzia semina nzuri ya Makatibu, Uenezi pamoja na Katibu Uhamasishaji wa Vijana.


PENDO ERNEST Katibu wa Siasa na Uenezi Kata ya Janga amegusia shilingi milioni NANE kutoka mfuko wa Jimbo, zilizolenga kumwaga kifusi eneo la Zahanati ya Fiona, ambapo zimemwagwa trip mbili tu.


HADIJA MAGUTO Katibu CCM Tawi la Mkwajuni Kata ya Mtambani amezungumzia fidia kupisha barabara ya Mzenga mpaka Makofia Bagamoyo, ambapo amesema wanapata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.


DKT. ROSE KUTOA MABATI 100 UJENZI WA OFISI YA CCM KILOMBERO.

 

Na Mwandishi Wetu, Kilombero

MWENYEKITI wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk. Rose Rwakatare, ameahidi kutoa mabati 100 kwaajili ya ujenzi wa ofisi ya chama hicho Wilaya ya Kilombero inayoendelea kujengwa ambayo itagharimu milioni 250 hadi kukamilika.


Alitoa ahadi hiyo jana April 24, 2024 mara baada ya kutembelea ofisi hiyo kuangalia maendeleo ya ujenzi wake alipokuwa kwenye ziara yake ya kukagua athari za mafuriko katika Wilaya hiyo.


Kwenye ziara yake hiyo juzi, Dk. Rose alitoa msaada wa tani tano za mchele kwa waathirika wa mafuriko wa Jimbo la Mlimba mkoani humo.


Akizungumza kwenye eneo la ujenzi wa jengo hilo juzi, Dk. Rose aliwapongeza viongozi wa chama hicho mkoa wa Morogoro kutokana na kasi kubwa ya ujenzi huo.


“Mara ya mwisho kufika hapa ujenzi ulikuwa haujaanza na mimi kama mwenyekiti wa wazazi wa Mkoa nitatoa mabati 100 kwaajili ya kupaua nawaomba wanachama wengine wajitokeze kuchangia jengo hili kwasababu hiki ni chama chetu wote,” alisema Dk. Rose.


Alisema jengo hilo litakuwa na manufaa makubwa kwa chama hicho na kwamba iwapo wanachama wengine watajitokeza kwa wingi kutoa michango yao linaweza kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.


Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Kilombero, Joseph Mwambeleko, alimshukuru Dk. Rose kwa kutembelea maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya chama na msaada wa mabati 100 ambao ameahidi kuutoa.


Aliwaomba wanachama wa chama hicho na wadau wa maendeleo nchini kuchangia ujenzi huo na kwamba misaada hiyo haiku kwaajili ya mtu binafsi bali kwaajili ya chama chao.


“Chama chetu kitajengwa na nguvu ya wanachama kwa hiyo nawaomba wenye nia ya kutaka kusaidia wasiogope kitu chochote kwasababu hawamchangii mtu wanakichangia chama chao,” alisema.


Alisema jengo hilo linajengwa kwa nguvu za wanachama na marafiki wa chama hicho ambao chama kimewaandikia barua ya shukrani kutambua mchango wao.


Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero, Mohamed Msuya, aliwaomba wadau wa maendeleo Wilaya ya Kilombero kuendelea kuchangia ujenzi wa ofisi za chama hicho.


“Wakati wa uchaguzi mwaka juzi niliahidi kwamba kipaumbele changu ni kujenga ofisi za chama na leo nafurahi sana kuona jengo limesimama na bado asilimia ndogo tu likamilike kwa hiyo wanachama waje watusaidia kumalizia ujenzi,” alisema.


“Huu si wakati wa uchaguzi, uchaguzi ni 2025 kwa hiyo watu wasiogope kuja kuchangia ujenzi wa jengo la chama chao, nawahakikishia kuwa wote watakaokuja tutawalinda,” alisema Msuya.




MAGAZETI YA LEO TAREHE 25 APRIL 2024.

 



























SERIKALI YASHAURIWA KUVILINDA VIWANDA VYA NDANI KWA KUVIWEKEA MAZINGIRA RAFIKI YA UZALISHAJI ILI VILETE TIJA YA MAENDELEO HAPA NCHINI.

 

Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi, na Nisbati, kutoka Baraza la wawakilishi Zanzibar, wakisikiliza maelezo kutoka kwa wataalam wa kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege cha Coast Concrete Poles Ltd kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani.

................................

Na Athumani Shomari

Bagamoyo

Serikali imeshauriwa kuvilinda viwanda vya ndani kwa kuviwekea mazingira rafiki uzalishaji ili vilete tija ya maendeleo hapa nchini.


Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea Kiwanda cha kutengeneza Nguzo za umeme za zege cha Coast Concrete Poles Ltd kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani, Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi, na Nisbati, kutoka Baraza la wawakilishi Zanzibar, Mh. Yahya Rashid Abdallaa, amesema viwanda vya ndani vina faida kubwa kwakuwa malighafi  wanazotumia ni zile zinazopatikana hapa nchini na hii husaidia kuongeza kipato kwa wananchi wazalishaji wa malighafi hizo.


Amesema miongoni mwa faida hizo ni kuongezeka kwa kipato kwa wananchi wazalishaji malighafi huku serikali ikinufaika kwa kukusanya kodi kwani wazalishaji wa malighafi hao ni walipa kodi.


Aliongeza kwa kusema kuwa, maendeleo katika nchi yoyote duniani huchangiwa na uzalishaji wa viwanda mbalimbali kwakuwa licha ya bidhaa zinazozalishwa kunuisha taifa lakini pia wananchi hupata ajira kupitia viwanda hivyo na kuounguza wimbi la watu wasiokuwa na ajira.


Alisema ili kuwavutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza hapa nchini, Serikali inapaswa kuweka mazingira rafiki ambayo yatawavutia wengi kuja kuwekeza na kukuza soko la ajira kwa wananchi.


Akizungumzia faida waliyopata katika ziara hiyo, Mwenyekiti huyo wa kamati ya Mawasiliano, Ardhi, na Nisbati, kutoka Baraza la wawakilishi Zanzibar, Mh. Yahya Rashid Abdallaa, amesema ni pamoja na kuona utengenezaji wa nguzo za umeme za zege ambazo ni hatua ya maendeleo kwa Taifa.


Alisema nguzo za umeme za miti hazidumu muda mrefu kwani zinaweza kukumbwa na madhara mbalimbali ikiwemo kuungua moto na kuliwa na wadudu hatimae kuanguka hali itakayopelekea mashirika ya umeme ya Tanesco na ZECO kutoa huduma chini ya kiwango kwakuwa kila wakati hulazimika kukata umeme ili kubadili nguzo.


Alisema Kamati hiyo imejionea utengezaji wa nguzo za zege katika kiwanda cha Coast Concrete Poles Ltd kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani, na hivyo itaishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuona nama ya kuanza kuzitumia nguzo hizo za zege kwa Shirika la umeme Zanziba (ZECO).


Kwa upande wake mjumbe wa Kamati hiyo, Mh. Simai Mohamed Said amesema serikali iangalie namna ya kuwapunguza kodi wazalishaji wa viwanda nchini ili kukabiliana na changamoto ya uendeshaji kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.


Alisema uendeshaji wa viwanda una kabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ugumu wa kuoata malighafi, na kodi kubwa ambapo alisema ipo haja ya serikali kuweka kodi Rafiki.


Akitoa ufafanuzi wa ubora wa nguzo za umeme za zege, Mhandisi wa uhakiki ubora wa kiwanda hicho, Fred Jachi alisema utengenezaji wa nguzo hizo unazingatia ubora wa viwango katika kila hatua ya utengenezaji.





Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi, na Nisbati, kutoka Baraza la wawakilishi Zanzibar, wakisikiliza maelezo kutoka kwa wataalam wa kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege cha Coast Concrete Poles Ltd kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani,