Thursday, April 25, 2024

SERIKALI YASHAURIWA KUVILINDA VIWANDA VYA NDANI KWA KUVIWEKEA MAZINGIRA RAFIKI YA UZALISHAJI ILI VILETE TIJA YA MAENDELEO HAPA NCHINI.

 

Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi, na Nisbati, kutoka Baraza la wawakilishi Zanzibar, wakisikiliza maelezo kutoka kwa wataalam wa kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege cha Coast Concrete Poles Ltd kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani.

................................

Na Athumani Shomari

Bagamoyo

Serikali imeshauriwa kuvilinda viwanda vya ndani kwa kuviwekea mazingira rafiki uzalishaji ili vilete tija ya maendeleo hapa nchini.


Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea Kiwanda cha kutengeneza Nguzo za umeme za zege cha Coast Concrete Poles Ltd kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani, Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi, na Nisbati, kutoka Baraza la wawakilishi Zanzibar, Mh. Yahya Rashid Abdallaa, amesema viwanda vya ndani vina faida kubwa kwakuwa malighafi  wanazotumia ni zile zinazopatikana hapa nchini na hii husaidia kuongeza kipato kwa wananchi wazalishaji wa malighafi hizo.


Amesema miongoni mwa faida hizo ni kuongezeka kwa kipato kwa wananchi wazalishaji malighafi huku serikali ikinufaika kwa kukusanya kodi kwani wazalishaji wa malighafi hao ni walipa kodi.


Aliongeza kwa kusema kuwa, maendeleo katika nchi yoyote duniani huchangiwa na uzalishaji wa viwanda mbalimbali kwakuwa licha ya bidhaa zinazozalishwa kunuisha taifa lakini pia wananchi hupata ajira kupitia viwanda hivyo na kuounguza wimbi la watu wasiokuwa na ajira.


Alisema ili kuwavutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza hapa nchini, Serikali inapaswa kuweka mazingira rafiki ambayo yatawavutia wengi kuja kuwekeza na kukuza soko la ajira kwa wananchi.


Akizungumzia faida waliyopata katika ziara hiyo, Mwenyekiti huyo wa kamati ya Mawasiliano, Ardhi, na Nisbati, kutoka Baraza la wawakilishi Zanzibar, Mh. Yahya Rashid Abdallaa, amesema ni pamoja na kuona utengenezaji wa nguzo za umeme za zege ambazo ni hatua ya maendeleo kwa Taifa.


Alisema nguzo za umeme za miti hazidumu muda mrefu kwani zinaweza kukumbwa na madhara mbalimbali ikiwemo kuungua moto na kuliwa na wadudu hatimae kuanguka hali itakayopelekea mashirika ya umeme ya Tanesco na ZECO kutoa huduma chini ya kiwango kwakuwa kila wakati hulazimika kukata umeme ili kubadili nguzo.


Alisema Kamati hiyo imejionea utengezaji wa nguzo za zege katika kiwanda cha Coast Concrete Poles Ltd kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani, na hivyo itaishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuona nama ya kuanza kuzitumia nguzo hizo za zege kwa Shirika la umeme Zanziba (ZECO).


Kwa upande wake mjumbe wa Kamati hiyo, Mh. Simai Mohamed Said amesema serikali iangalie namna ya kuwapunguza kodi wazalishaji wa viwanda nchini ili kukabiliana na changamoto ya uendeshaji kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.


Alisema uendeshaji wa viwanda una kabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ugumu wa kuoata malighafi, na kodi kubwa ambapo alisema ipo haja ya serikali kuweka kodi Rafiki.


Akitoa ufafanuzi wa ubora wa nguzo za umeme za zege, Mhandisi wa uhakiki ubora wa kiwanda hicho, Fred Jachi alisema utengenezaji wa nguzo hizo unazingatia ubora wa viwango katika kila hatua ya utengenezaji.





Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi, na Nisbati, kutoka Baraza la wawakilishi Zanzibar, wakisikiliza maelezo kutoka kwa wataalam wa kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege cha Coast Concrete Poles Ltd kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani,


No comments:

Post a Comment