Wednesday, October 31, 2018

WAZIRI MKUU ASEMA SERIKALI INABORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI.



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wa kijiji cha Lukozi wilayani Lushoto wakati alipowasili kijijini hapo akiwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga, Oktoba 31, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
......................................


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya halmashauri ya wilaya ya Lushoto.

Amesema lengo ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya chenye uwezo wa kutoa huduma mbalimbali muhimu zikiwemo za maabara, upasuaji na mama na mtoto.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Oktoba 31, 2018) wakati akizungumza na wakananchi katika kata ya Malindi, baada ya kutembelea jengo la soko mbogamboga la Malindi.

Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga vizuri katika sekta ya afya baada ya bajeti ya kununulia dawa kuongezeka kutoka sh. bilioni 31 kwa mwaka na kufikia bilioni 269.

“Hatutaki tena kusikia mgonjwa anaenda hospitali na kukosa dawa biashara hiyo tumeimaliza, Rais Dkt. John Magufuli ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa.”

Amesema katika wilaya ya Lushoto Serikali imetenga sh. bilioni 1.4 kwa ajili ujenzi na ukarabati wa majengo ya vituo vya afya vya kata za Kangagai. Mnazi na Mlola.

“Halmashauri wekeni mpango thabiti wa kujenga wodi mbili kati yake moja ya wanaume na nyingine ya wanawake, lengo la Serikali ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi.”

Aizungumzia kuhusu mradi wa ujenzi wa soko, Waziri Mkuu amesema mradi huo ni sehemu ya huduma zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii nchini.

Waziri Mkuu ametaja huduma nyingine zinazotolewa na Serikali kwa wananchi ni za afya, elimu, maji, uchumi na ujenzi na uboreshwaji miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara.

Hivyo, amewataka wananchi watumie vizuri soko hilo  ambalo linatoa fursa kwao kufanya biashara katika eneo zuri na kuwawezesha kuuza bidhaa zao zikiwa katika ubora.

Pia amewashauri wakulima hao wajiunge katika vikundi na kuanzisha ushirika wao ili waweze kusaidiwa na Serikali katika kupata mikopo kwa ajili ya kuzalisha kwa ubora zaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto, Bibi Ikupa Mwasyoge amesema kukamilika kwa soko hilo kutainufaisha halmashauri na wananchi.

Bibi. Ikupa amesema ujenzi wa jengo hilo la soko la ghorofa mbili lililojengwa kwa awamu mbili ulianza mwaka 2011 na umekamilika Septemba 2018, umegharimu sh. bilioni 1.1.

Amesema halmashauri itanufaika kwa kupata ushuru na wananchi ambao wengi wao ni wakulima wa mboga na matunda watakuwa na sehemu ya uhakika wa kufanyia biashara.

“Wakulima 35,000 wa kata ya Malindi na kata jirani za Lukozi, Manolo na Shume wanaozalisha wastani wa tani 5,900 za mboga na matunda kwa mwaka watanufaika.”

Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za afya nchini.

Amesema bajeti ya dawa katika halmashauri hiyo imeongezeka kutoka sh milioni 183 za dawa zilizokuwa zinatolewa awani na sasa imefikia sh milioni 565.

Mbunge wa jimbo la Mlalo, Bw. Rashid Shangazi ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuwasaidia wananchi wa halmashauri kuongeza thamani ya mazao yao kabla ya kuuza.

Awali,Waziri Mkuu alizindua jengo la utawala la Halmashauri ya wilaya ya Lushoto lililogharimu sh. bilioni 4.3. Kukamilika kwa jengo hilo kutaboresha huduma kwa wananchi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipozindua Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto  akiwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga Oktoba 31, 2018. Kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na wapili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba. Wapili kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu, watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela. na kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto, Ikupa Harrison Mwasyoge. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Soko la Kisasa la mbogamboga na matunda linalojengwa na Serikali katika kijiji cha Malindi wilayani Lushoto, Oktoba 31, 2018. Alikuwa katika ziara ya Mkoa wa Tanga.  Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



 

WANANCHI WAMETAKIWA KUBADILI MFUMO WA MAISHA NA KUZINGATIA LISHE BORA

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akipokea zawadi ya mbuzi kutoka kwa Diwani wa Kinyambuli Rubeni Charles wakati alipofanya ziara katika kijiji hicho ili kujionea hali ya ujenzi wa kituo pamoja na utoaji huduma za afya kijijini hapo.
..........................................

Na WAMJW-MKALAMA,SINGIDA

Watanzania kote nchini wametakiwa kufuata kanuni na taratibu bora za maisha ikiwemo kubadili mfumo wa maisha ili kuepuka kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na udumavu kwa watoto wachanga.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katika Wilaya ya Mkalama Mkoa wa Singida wakati alipotembelea kituo cha afya na kuongea na wananchi.

“Serikali chini ya uongozi wa Rais Magufuli inataka kila mtanzania awe na afya bora, ndo maana tunajitahidi kutoa elimu kwa umma kuhusiana na kutunza afya zenu ikiwemo kufanya mazoezi na kuepuka vyakula ambavyo si salama kwa afya zetu pamoja na kubadili mfumo mzima wa maisha”. Alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha,Naibu waziri huyo ameendelea kusisitiza kwa upande wa  akina mama walio na watoto wadogo chini ya miaka miwili kuendelea kuwanyonyesha na kuwapa vyakula vyenye lishe bora watoto wao ikiwa ni sehemu ya kumsaidia mtoto kukua kiakili na kuwa  na afya bora huku akisisitiza siku 1000 za mwanzo kwa mtoto ndizo siku muhimu katika kumuwezesha kuwa na afya bora na kukua vizuri.

“Siku 1000 za mwanzo tunaanza kuzihesabu toka mimba inapotungwa, anapozaliwa na kufikisha miaka miwili, hiki ni kipindi muhimu sana cha mama kumnyonyesha mtoto ikiwa ni pamoja na kumpa vyakula vyenye lishe ili mtoto aweze kuwa na afya bora na ubongo unaofanya kazi sawa sawa”. Alisisitiza Dkt. Ndugulile.

Pamoja na hayo, Dkt. Ndugulile amekipongeza kituo cha afya cha Kinyambuli kwa kuzitendea haki fedha zilizotolewa na Serikali Shilingi milioni 400 ili kusaidia kupanua kituo hicho kwa kujenga majengo mapya ya kuhudumia wagonjwa pamoja na nyumba za watumishi.

“Nawapongeza sana wananchi wa Kinyambuli kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa kituo hiki, ninachokiona hapa kipo mara 300 nchi nzima, kwa kweli mnastahili pongezi na fedha za serikali tulizoleta milioni 400 mmezitendea haki”. Alisema Dkt. Ndugulile.

Hata hivyo Dkt.Ndugulile  amesema serikali bado ina nia kubwa ya kuboresha hali ya utoaji huduma za afya nchini, huku ujenzi wa Hospitali kubwa ya wilaya ya Mkalama ukitarajiwa kuanza kabla ya mwisho wa mwaka huu. 

Dkt. Ndugulile amesema mkoa wa Singida umetengewa bajeti ya Bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga Hospitali kubwa ya wilaya ya Mkalama pamoja na Singida DC.

Kwa upande wake diwani wa Kinyambuli, Rubeni Charles ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli kwa kuwakumbuka wananchi wa kijiji hicho kwa kutoa fedha za ujenzi wa kituo kikubwa cha afya.

“Kwakweli naishukuru sana serikali kwa kutukumbuka, wananchi wa kijiji hiki walikua wanapata shida sana kupata huduma za afya hasa wakinamama wajawazito ambao tulipoteza wengi kutokana na kukosa huduma hii muhimu”. Alisema Rubeni. 

 
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akinawa mikono baada ya Uzinduzi wa Mradi Mkubwa wa Maji  wenye uwezo wa kuzalisha lita za ujazo  Elfu 30 kutoka kijiji cha  Rurumakilichopo kata ya Kiomboi wilaya ya Ilamba, ikiwa ni muendelezo wa zaiara yake Mkoani Singida.
 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiangalia chanjo zilizohifadhiwa katika boksi maalum wakati alipotembelea Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi iliyopo wilayani Iramba katika Mkoa wa Singida. Kushoto ni muhudumu wa chanjo Christowelo Palangyo na Dkt. Abbas Sepoko (kulia).

 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiionesha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Iramba (hawapo pichani) dawa za serikali zilizo na alama maalumu ili zisiuzwe katika maduka binafsi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Gwaula.