Wednesday, August 31, 2016

CHADEMA YASITISHA MAANDAMANO YA UKUTA SEPTEMBA MOSI.

ukuta
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Mh.Freeman Mbowe, amesitisha shughuli za maandamano zilizokuwa zimepewa jina la (UKUTA) kwa Muda wa mwezi mmoja,kwa kile alichodai baada ya kuombwa na viongozi wa Dini na taasisi Mbalimbali, ambapo maandamano hayo yalitarajiwa kufanyika kesho Septemba Mosi nchi nzima.

Mbowe ametoa kauli hiyo ya kuahirisha kwa maandamano hayo mapema leo mchana wakati akizungumza na Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari.Amesema sababu kubwa za kuahirisha maandamano hayo ni busara za viongozi wa dini ambao wameiomba Chadema iwape muda wa kutafuta Suluhu . 

Viongozi mbalimbali wa kidini pamoja na Taasisi mbalimbali za kiraia hatimaye wamesaidia kutokomeza UKUTA kwa kuuomba uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kuahirisha Oparesheni hiyo iliyopangwa kufanyika Septemba mosi nchi nzima. 

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Makao Makuu ya CHADEMA Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa,  Freeman Mbowe amesema  Viongozi hao wakuu wa kidini wamewaomba na kuwasihi katika vikao mbalimbali walivyokaa pamoja nao na kusema tunaheshimu viongozi hao. 

Mbowe amesema wanawapa muda wa wiki mbili au tatu ili waonane na Rais Magufuli kwa lengo la kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huu wa kisiasa na kuliepusha taifa na machafuko ya kisiasa. 

Pia amesema Viongozi wa Taasisi za kiraia kama vile Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC, Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Jukwaa la Wahariri na Jukwaa la Katiba nao wamewasihi kuahirisha UKUTA kwa muda ili kutoa fursa kwa jitihada za mazungumzo na majadiliano kufanyika. 

"Sisi CHADEMA tunatambua na kujali haki zetu za kisiasa kama zilivyofafanuliwa katika Katiba na Sheria za nchi yetu. Hata hivyo tunajali na kuheshimu kwa kiasi kikubwa zaidi haki za Watanzania ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yao" amesema Mbowe

Amesema wanawaomba kuwatangazia viongozi weo wa ngazi zote CHADEMA, pamoja na wanchama,wafuasi na Watanzania wote kuhairisha kwa mwezi mmoja mikutano na maandamano ya amani yaliyopangwa kufanyika nchi nzima kuanzia kesho Septemba Mosi.

GERSON MSIGWA ATEULIWA KUWA MKURUGENZI KAMILI WA MAWASILIANO IKULU.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais, (Director of Presidential Communication - DPC). Bw. Gerson Partinus Msigwa,aliyethibitishwa leo na Rais Dkt John Pombe Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemthibitisha Bw. Gerson Partinus Msigwa kuwa Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais, (Director of Presidential Communication - DPC).

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Agosti 31,2016 na Katibu Mkuu Ikulu Bw. Peter Ilomo imeeleza kuwa Bw. Gerson Partinus Msigwa amethibitishwa kuanzia leo tarehe 31 Agosti, 2016 kushika wadhifa huo.

Kabla ya uthibitisho huo, Bw. Gerson Partinus Msigwa alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais, katika Ofisi ya Rais Ikulu kuanzia tarehe 17 Novemba, 2015.

Jaffar Haniu
Kaimu Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi.
Dar es Salaam
31 Agosti, 2016

Tuesday, August 30, 2016

RC. NDIKILO, ASEMA ULINZI UMEIMARISHWA MKOANI PWANI.

ndi

MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,amesema wanaendelea na mapambano katika eneo la Vikindu na kuimarisha ulinzi wilayani Mkuranga kufuatia kutokea matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea hivi karibuni.

Aidha amevitaka vyama vya  siasa mkoani humo, kuacha kufanya maandamano ikiwemo ya umoja wa kupinga udikteta(UKUTA)na chama kitakachobainika hatua kali zitachukuliwa.

Katika hatua nyingine mhandisi Ndikilo ,amewaomba viongozi wa dini wasichoke kuliombea taifa,kumuombea rais John Magufuli na viongozi wote ili waendelee kuwatumikia wananchi kwa maslahi mapana ya taifa.

Aliyasema hayo, wakati kamati ya amani ya mkoa wa Pwani,ilipokwenda kutoa pole kwa kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo, kutokana na matukio ya kiuhalifu yaliyotokea wiki iliyopita wilayani Mkuranga.

Alisema kuwa serikali hiyo, imejipanga kikamilifu kulinda amani ya wananchi na mali zao sambamba na kuimarisha ulinzi wilayani Mkuranga na maeneo mengine ya mkoa huo.

“Tutahakikisha tunapambana na suala hili kwa kushirikiana na jeshi la polisi Dar es salaam na kwa kupitia uongozi wa amiri Jeshi mkuu litakwisha kwani amedhamiria kwa dhati kupambana na jambo hili ,”

“Na askari hawajakatishwa tamaa ,licha ya kutokea kwa matukio hayo na kwasasa askari wengine bado wanaendelea na mapambano katika maeneo ya wilaya hiyo ili kufichua wahalifu wengine” alisema mhandisi Ndikilo.

Mhandisi Ndikilo,  alielezea kuwa,  kuna kila sababu ya kuimarisha ulinzi na usalama ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.

Alisema dhamana ya kulinda amani ya watanzania ni ya serikali iliyopo madarakani na wakuu wa mikoa ni wasaidizi wa mh. Rais na wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama hivyo atahakikisha anasimamia suala hilo.

Hata hivyo, mhandisi Ndikilo, aliitaka kamati ya amani mkoa, iendelee kushirikiana na serikali ngazi ya wilaya na kuangalia namna ya kuunda kamati hizo wilayani ili zishirikiane kuimarisha utulivu.

Akizunguzmzia kuhusiana na maandamano yanayotarajiwa kufanyika sept mosi mwaka huu,na umoja wa kupinga udikteta(UKUTA),alisema mkoani humo hayataruhusiwa.

Mhandisi Ndikilo,alieleza maandamano hayo hayana tija na mwisho wa siku ni kuleta vurugu na kuhatarisha amani ya mkoa na nchi kijumla hivyo utii wa sheria bila shuruti unahitajika.

Alisema ni vema vyama hivyo vikazingatia taratibu zilizowekwa na serikali ili kuepusha uvunjifu wa amani katika mkoa na endapo kipo chama kitakachokaidi taratibu zilizowekwa, hakitoweza kuvumiliwa.

Mhandisi Ndikilo,aliomba viongozi wa dini wayakataze kwa waumini wao kupitia misikiti na makanisa kwani yamepigwa marufuku.

“Haijakatazwa mikutano ya siasa bali wafanyie kwenye maeneo yao ya kazi kama ni mbunge ama diwani afanye kwenye eneo lake,sio diwani wa mailmoja aende Chalinze hapana,mtusaidie kufikisha salamu kuwa mkoa hautaki kusikia wala kuona maandamano ya UKUTA sijui nini” alisisitiza mkuu huyo.

Kwa upande wake ,kamanda wa polisi mkoani Pwani, kamanda Boniventure Mushongi ,alitoa rai kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano na jeshi la polisi kufichua wahalifu.

Alisema kwasasa wanaendelea na kulinda maeneo mbalimbali ya wilaya ya Mkuranga na kusema matukio mbalimbali yanatokea mara kwa mara wilayani humo, kutokana na maeneo mengi kuwa mapori ambapo baadhi ya watu wahalifu wamegeuza kuwa choo na maficho yao.

Kamanda Mushongi ,alisema jeshi hilo halitosita kuingia kwenye mapori na maficho ambayo wananchi wasamaria wema watatoa taarifa kwa polisi kuyafanyia kazi.

Alisema kuwa ,kikulacho kinguoni mwako hivyo inapaswa jamii itambue hilo kwa manufaa ya mkoa na taifa kijumla.

Kamanda Mushongi,alieleza wananchi wajaribu kuwa macho ambapo aliwaomba watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kutoa mwiba unaosumbua.

Aliasa amani ilindwe na kila mmoja na ni jukumu la kila mmoja kuwa mlinzi wa mwingine na kushirikiana.

Katika kamati ya amani mkoani hapo,ina wenyeviti wenza wawili,alhaj shekhe Hamis Mtupa na padre Beno Kakudo,ambao waliliomba jeshi la polisi lisikatishwe tamaa na yaliyotokea.

Alhaj Mtupa alisema,kweli polisi wengine wamepoteza maisha lakini wasikatishwe tamaa kwani polisi hao wamepotea maisha wakiwa kwenye mapambano na majukumu yao ya kazi.

Alihakikisha kuwa kwa nafasi zao kama viongozi wa kiroho wapo pamoja na wananchi na vyombo vya dola ambavyo vipo kwa ajili ya kulinda jamii na mali zao.

Alhaj Mtupa alisema viongozi wa kisiasa wajaribu kujenga tabia ya kupenda kukaa kwenye meza za mazungumzo ,kupatanisha na kujadili mambo kuliko kwenda katika hatua za maandamano,migogoro ama mapambano hali ambayo inawaweka wananchi katika hali ngumu.

Nae mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama,alichukuwa fursa hiyo,kukemea maandamano hayo na kusema atakaekiuka taratibu zilizowekwa na serikali itageuka kichaka badala ya Ukuta.

Alisema Ukuta wanataka muafaka anashangaa hakuna tatizo ,watu wanafanya fujo halafu hao hao wanasema wanataka muafaka.

Assumpter alisema,wapo watu wanafanya mambo kwa kutaka kuvuruga amani ya nchi wakati nchi siyo ya kuichezea
Aliomba vijana na wananchi wilayani Kibaha,wawe watulivu siku ya sept mosi ili kuondokana na madhara yanayoweza kujitokeza.

Mnamo agost 26 mwaka huu mapigano makali yalitokea baina ya askari polisi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi huko eneo la Vikindu wilayani Mkuranga na kusababisha askari mmoja kufariki dunia na majambazi 14.

Agost 24 majira ya saa 1 /2 usiku ,uvamizi na shambulizi lenye nia ya uovu lililofanywa na kundi la majambazi na kuwauwa askari wanne huko Mbande huko Temeke,ambapo majambazi waliofanya tukio hilo wanadaiwa kuuwawa katika tukio la agost 26 eneo la Vikindu.

AJALI, SANZALE BAGAMOYO, GARI LA PEPSI LAGONGANA NA ROLI KUBWA LA MIZIGO.

Magari mawili ya mizigo yamegongana mchana huu eneo  la Sanzale kichem  chem kati ya Roli kubwa lenye tera namba T.682 DFF la Kampuni ya  PWANI HAULIERS LTD. (PHL) lililokuwalimebeba mzigo, na Canter ya pepsi  yenye namba T. 912 DCC ambalo  lilikuwa limebeba soda.

Kwa mujibu wa dereva Roli lenye Tera, Shomari Shomari aliiambia Bagamoyokwanza kuwa yeye alikuwa anakunja kuingia kiwandani kuingiza mzigo ambapo kutokana na  urefu wa gari alilazimika kuzidi upande wa kulia  ili apate kona ya kukunja kuingia kushoto kwenye Kiwanda.

Shomari aliendelea kusema kuwa, mara baada yeye kuzidi upande wa kulia akiwa ameshaakunja kuingia kusho  kiwandani, mwenye gari ya soda amekuja nyuma yake na kupitia kushoto  ambapo gari ya soda ilikwenda kugonga moja kwa moja kwenye mlango Roli kubwa na kusababisha Ajali iliyopelekea Dereva  wa Gari la Soda kuumia na kukimbizwa Hospitali huku  soda zikiwa zimevunjika.

Wananchi mbalimbali walioongea na bagamoyokwanza, walisematukio limesababishwa na Dereva wa gari la soda kwani yeye hakupaswa kupita  kushoto na badala yake alitakiwa kusubiri  gari ya mbele yake imalize kukata kona ndipo yeye aendelee na safari yake.