Tuesday, February 6, 2024

TAKUKURU KAGERA YABAINI MAPUNGUFU KATIKA MIRADI 16.

 

Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Kagera Pilly Mwakasege akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu  Octoba hadi Desemba 2023

..................................

Na Alodia Babara

Bukoba

TAASISI ya kuzuia na kupamba na Rushwa mkoa wa Kagera kwa kipindi cha Oktoba-Desemba 2023, imefuatilia miradi 19 yenye thamani  zaidi ya shilingi bilioni 6.1 ambapo kati ya hiyo miradi 16 yenye thamani zaidi ya shilingi bil.4.2 imebainika kuwa na mapungufu yaliyohitaji marekebisho.

Kamanda wa taasisi hiyo mkoani humo Pilly Mwakasege amesema kuwa kiasi hicho ni sawa na asilimia 68.50 ya fedha za miradi ambapo kumekuwa na ongezeko la asilimia 18.77 ya miradi hiyo, ukilinganisha na kipindi cha Julai-Septemba mwaka jana.

Mwakasege ameeleza hayo leo Februari 06,2024 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yao kwa kipindi cha robo tatu ya mwisho wa mwaka 2023 ambapo,miradi iliyohusika ni ya ujenzi wa miundombinu ya shule mpya za msingi na sekondari, maji, zahanati pamoja na ujenzi wa madarasa ya msingi na sekondari ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kuendana na thamani ya fedha iliyotumika.

Mwakasege amesema kuwa kwa kipindi hicho walipokea malalamiko 92 kati ya hayo 58 hayahusu rushwa ambapo 34 yanahusu rushwa na majalada yamefunguliwa ambapo 20 uchunguzi wake umekamilika na hatua stahiki zinatarajiwa kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.

“Idara zilizolalamikiwa ni Halmashauri ambapo idara ya fedha kesi moja, Elimu 10, Afya saba, Utawala 12, Biashara moja, Kilimo nane, Ardhi saba, Mazingira tatu na mengine yalihusu sekta binafsi ambayo ni 12, ikiwemo  Maji tatu, Ujenzi tisa, Maliasili saba, Nishati moja, Uhamiaji mbili, Polisi nne, Mahakama tatu, Uchukuzi moja na mamlaka ya mapato Tanzania moja" ameeleza Mwakasege.

 Amesema katika progaramu ya Takukuru rafiki ambayo inatekelezwa kwa kushirikisha wadau katika ngazi ya kata ambapo wananchi hupata fursa ya kuibua kero zinazowakabili katika maeneo yao ambapo kwa kipindi cha Oktoba-Desemba walitembelea kata 11 na kupokea kero kuhusu sekta za Elimu, Afya, Maji, Fedha na Nishati ambapo ufuatiliaji wake unaendelea.

Aidha amevitaja vipaumbele vya Takukuru kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka huu ambavyo ni kuelimisha Umma kupitia njia mbalimbali ili kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika kuzuia vitendo vya rushwa, kutatua kero mbalimbali katika jamii kupitia programu ya Takukuru Rafiki na kuendelea kufuatilia rasilimali za Umma kupitia ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuzuia ufujaji wa fedha za Umma.

 Nyingine ni kufanya chambuzi za mifumo kwa lengo la kuzuia rushwa zinazosababishwa na mapungufu yaliyopo kwenye mifumo ya utendaji wa sekta ya Umma na sekta binafsi ambapo amewahimiza wasimamizi wa miradi ya maendeleo kuwa waadilifu na kuhakikisha fedha zote za miradi zinatumika vizuri.


Monday, February 5, 2024

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA MSD

 



Na. WAF, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI imeitaka Bohari ya Dawa (MSD) kuongeza ufanisi, ubunifu wa hali ya juu kwa kuhakikisha dawa zinanunuliwa, zinahifadhiwa sehemu sahihi, kusambaza dawa hizo kwa wakati katika sehemu zenye uhitaji na kukusanya madeni ili kuweza kuwa imara na taasisi endelevu.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI, Mhe. Stansilaus Nyongo baada ya kupokea taarifa ya hali ya utendaji na majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD).

Mhe. Nyongo amesema kuwa wao kama wawakilishi wa wananchi wataendelea kuishinikiza serikali kuiwezesha MSD kupata mtaji ili kujiendesha kiufanisi katika kusambaza dawa kwa wakati.

“Bohari kuu ina majukumu ya kununua, kutengeneza, kuhifadhi dawa pamoja na kusambaza dawa katika vituo vya  vyote nchini”. Ameeleza  Mhe. Nyongo.

Mhe. Nyongo amesema kwa ujumla kamati imeridhishwa na hali ya utendaji wa Bohari ya Dawa na mipango yake ya utek


Sunday, February 4, 2024

PWANI YAHITIMISHA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 47 YA KUZALIWA KWA CCM

 


Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani leo tarehe 04/02/2024 kimehitimisha sherehe za  Maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM katika Kata ya  FUKAYOSI Wilaya ya  Bagamoyo huku kikiwa na matumaini makubwa ya ushindi kuelekea uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa, Vijijini na Vitongoji 2024.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika kuhitimisha maadhimisho hayo ndg. Mwinshehe Mlao amesema ili CCM iweze kuendelea kudumu lazima Viongozi waondoe ubinafsi.

Mlao amesema unapofika wakati wa uchaguzi Kila mpiga kura ahakikishe anawachagua Viongozi wa Serikali wenye nia njema ya kuongoza na ikitokea  wakawachagua Viongozi kwa ajili ya maslahi yao binafsi basi watakuwa wamepoteza haki za wengine.

Ameendelea kusema kuwa ili kushinda chaguzi zijazo kunahitajika UMOJA huku akisisitiza kuwa kama Kuna mwanachama yeyote mwenye nia ya kugombea na anaonekana kuwa na dosari aambiwe sasa wasisubiri mpaka achukue fomu ndio waseme mabaya yake huko ni kuchafuana.

" Tusikubali kusababisha migogoro isiyo na tija tunapoelekea kwenye chaguzi zijazo na wala tusikubali watu watugawe kwa ajili ya maslahi yao" amesema Mlao

Maadhimisho hayo yameambatana na ukaguzi wa Kituo Cha afya cha Fukayosi kinachojengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 1, Uzinduzi wa ujenzi wa Ofisi ya CCM kata ya Fukayosi, ugawaji wa vifaa vya Shule kwa wanafunzi wanaoishi katika Mazingira magumu, ugawaji wa vyeti vya PONGEZI kwa Kata zilizofanya vizuri katika uingizaji wanachama wapya na usajili kwa mfumo wa kielektroniki sambamba na zoezi la upandaji wa miti.

Taarifa hii imeandaliwa na:

David Mramba
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo CCM
Mkoa wa Pwani.


Friday, February 2, 2024

LIONS CLUB YAKABIDHI MATENKI YA MAJI CHALINZE.

 

MUNTAZIR Bharwan mmoja wa Wanachama wa Taasisi ya Lions Club, akielekeza jambo mbele ya Diwani wa Kata hiyo Mussa Gama mwenye Balaghashia. Picha na Omary Mngindo.

Miriam Kihiyo (Watatu kutoka kwa aliyevaa Balaghashia) akimkanidhi moja ya zawadi mtoto anayetoka kwenye Kituo cha kulelea Watoto wenye Mazingira hatarishi. Picha na Omary Mngindo.


....................................

Na Omary Mngindo, Ruvu.

TAASISI ya Lions Club ya jijini Dar es Salaam imekabidhi matenki 8 ya kuhifadhia maji katika shule za msingi na Sekondari ndani ya Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Mkoani Pwani.

Matanki hayo yanalenga kuwaondolea adha wanafunzi kwenye shule hizo, yamekabidhiwa kwa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Chalinze, Ramadhani Possi, aliyewakilishwa na Miriam Kihiyo Afisa Elimu Msingi.

Muntazir Bharwan alisoma taarifa ya taasisi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Lions Host Kaniz Naghavi, iliyoeleza kuwa kukabidhiwa kwa matenki hayo kumetokana na diwani wa Kata hiyo Mussa Gama kuelezea uwepo wa changamoto kwenye shule hizo.

Hafla hiyo iliyotumika pia kumkaribisha Gavana wa Tanzania District 411C Happiness Nkya, matenki hayo yanakwenda katika shule za Msilale, Chamakweza, Sekibwa, Ruvu, Mnindi, Kitonga na Kwazoka.

"Baada ya kupokea maombi ya diwani Gama tukawasiliana na Kampuni ya Refuelling Solutions (T) Limited na wadau wengine wakiwemo wanachama wa Lions ambao tumefanikisha upatikanaji huu," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Gavana wa taasisi hiyo Nkya alisema kwamba kwa sasa wana wanachama 620 na Club 23, wakati Dar es Salaam zikiwa 14, na kwamba wamekuwa wakisaidia maeneo tofauti wakisaidiana na makampuni mengine.

Kwa upande wake diwani Gama ameishukuru Taasisi hiyo, huku akieleza kuwa imekuwa ikisaidia maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo vifaa katika Zahanati ya Ruvu Darajani, madaftari kwa wanafunzi ikiwemo matenki hayo.

"Club ya Lions imekuwa na msaada mkubwa sana kwetu wanaVigwaza, kwani wanasaidia kutatua matatizo kwenye kata yetu kwa kushirikiana na wadau wengine kutupatia misaada ya fedha na vitu katika sekta mbalimbali," alisema Gama.

Afisa Elimu awali na Msingi wa Halmashauri ya Chalinze, Mariam Kihiyo akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi hiyo,  aliishukuru taasisi hiyo, kwa misaada inayoendelea kuipeleka inayolenga kupunguza vikwazo kwa wanaVigwaza.

"Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze, Alhaj Ramadhani Possi, tunawashukuru sana ndugu zetu wa Lions Club kwa namna mnavyojitoa mkishirikiana na wadau wenu, wanaChalinze tunatambua na kuthamini mchango wenu mkubwa kwetu," alisema Kihiyo.

Samwel Mjema Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Ruvu Darajani alisema matenki hayo yatasaidia kutunza maji pindi yanapokatika, huku akiahidi utunzwaji yaweze kudumu kwa muda mrefu.


Thursday, February 1, 2024

DED BAGAMOYO AZINDUA HUDUMA KITUO CHA AFYA FUKAYOSI.

 

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Bw. Shauri Selenda Leo tarehe 1 Februari, 2024 amezindua rasmi utoaji wa huduma katika kituo Cha Afya Fukayosi.

Akizungumza na watumishi wa Afya pamoja na Kamati ya Maendeleo ya Kata Fukayosi (WARDC) Selenda, alisisitiza kufanya kazi Kwa weledi pamoja na  kunyenyekea wagonjwa kama sehemu ya miiko ya tasnia ya utoaji wa huduma za afya.

" Mgonjwa mpaka anafika hospitali maana yake anahitaji huduma hivyo haina budi kumpokea kwa unyenyekevu na kumsikiliza shida yake na kumpatia matibabu". Alisema Bwana Selenda.           

Kituo Cha Afya Fukayosi kimejengwa kwa kutumia fedha toka Serikali Kuu na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa lengo la kuimarisha huduma za afya ikiwemo Huduma ya Mama na Mtoto, Afya ya dharura na upasuaji wa wajawazito, Maabara, Jengo la Wagonjwa wa nje (OPD), Mionzi, na Jengo la kufulia.

Mkurugenzi Mtendaji alipanda miti kama ishara ya Uzinduzi wa huduma katika kituo hicho Cha Afya Fukayosi. Kituo Cha Afya Fukayosi kilianza Ujenzi Mwaka wa fedha 2021/2022 na kinategemea kuhudumia zaidi ya wakazi 17,000






DC. OKASH ATATUA KERO ZA BODABODA BAGAMOYO.

 

Na Daria Abdul, Hamisi Hamisi, Bagamoyo.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Halima Okash, akishirikiana na  viongozi mbalimbali wa Halmashauri  ya Wilaya hiyo, amefanya kikao na madereva wa pikipiki zinazobeba abiria (BODABODA)  Januari 31,2024 katika ukumbi wa flexible hall Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TASUBA), kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili katika utendaji kazi wao wa kila siku.

 Mhe.Okash, amewasisitiza bodaboda kutii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali, pia wajiepushe na matukio ya uhalifu wa kupora mali za wateja wao.

”Ndugu zangu lazima tutii sheria za usalama barabarani kwani tunawategemea ninyi vijana kuwa ndio Taifa la kesho hizo rizki tunazozipata kuna watu wanatutegemea tusipotii sheria za usalama barabarani, kutakuwa na ajali za mara kwa mara zitakazopelekea kupoteza maisha na kuleta ulemavu.” Amesema Okash

Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Usalama barabarani,  Wilaya ya Bagamoyo (DTO)  Azizi Zubeir, amewataka bodaboda kuhakikisha wanasajili vyombo vyao vya usafiri, leseni pamoja na bima ili wasikamatwe na vyombo vya usalama na kueleza Zaidi kuwa bima itasidia kupunguza gharama ya matengenezo ya vyombo hivyo na matibabu kwa dereva anapopata ajali.

"Ni waambie tu  bodaboda ili ufanye kazi kihalali lazima usajili vyombo vyetu, tuwe na leseni ya udereva pamoja na bima ya chombo husika ili itusaidie kupunguza gharama za matengenezo na matibabu inapotokea ajali.” Amesema Zubeir

Akitoa kero yake katika hafla hiyo Mwenyekit wa Bodaboda kata ya Dunda Ndug, James Mapunda, amesema kuwa wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya usalama barabarani na vyuo mbalimbali vikishirikiana na Jeshi la polisi Wilayani hapo na kuahidiwa kupatiwa leseni za udereva baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo, badala yake hawapewi leseni zao licha ya kulipia fedha kwa ajili ya leseni hizo.

Kwa upande wake Waziri Mohammed (BODABODA), ameeleza kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na kukamatwa na Mgambo  kwa mabavu katika vituo vyao vya kazi (vijiwe) bila ya uwepo wa askari wa Jeshi la polisi kinyume na sheria hali inayopelekea kushindwa kufanya shughuli zao usafirishaji kwa amani.







WALENGWA WA TASAF WATAKIWA KUTUMIA FEDHA ZA TASAF KUJIENDELEZA KIMAISHA.

 

Mkurugenzi wa uratibu  wa shughuli za serikali ofisi ya makamu wa pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Siajabu Suleiman Pandu akizumgumza na wanufaika wa mpango wa TASAF Manispaa ya Bukoba hawako pichani.

..........................................

Alodia Babara,

Bukoba.

WALENGWA wa mpango wa kunusuru kaya maskini nchini, TASAF wametakiwa kuzitumia fedha za mpango huo kama sehemu ya ukombozi, kuimarisha ndoa na familia zao kwa lengo la kuondoa umaskini.

Hayo yamesema Januari 31, mwaka huu 2024, na Mkurugenzi wa uratibu wa shughuli za serikali ofisi ya makamu wa pili wa Rais Zanzibar Siajabu Pandu wakati wadau mbalimbali wa mpango huo walipotembelea walengwa katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kwa lengo la kukusanya maoni na changamoto zinazowakabili walengwa, ambazo baada ya kuzibaini zitawawezesha wadau hao kuboresha mpango unaofuata.

“Serikali tunaamini fedha hii iwe ni sehemu ya ukombozi, kwa hiyo ninawaomba muishi katika ndoa njema, familia nzuri ni sehemu ya ukombozi, fedha ni matokezeo tu sasa tuzitumie hizi fedha kuimarisha ndoa zetu, ndoa si chochote ni subira, tunapaswa kuvumiliana kuhakikisha kwamba tunaishi na watoto wetu kwa pamoja na familia zetu ili kuondoa hali hii ya umaskini” amesema Pandu

Katika ukusanyaji maoni na kusikiliza changamoto za walengwa wadau hao wamegundua kuwa, baadhi ya kaya za walengwa wametelekeza familia zao na kumuacha mzazi mmoja wapo, baba/mama, akiangalia majukumu ya kulea watoto peke yake.

Aidha baadhi ya walengwa wa mpango huo katika mtaa wa Kabale ka Ngaiza manispaa ya Bukoba wakati wakitoa hadithi zao mbele ya wadau hao imeonekana kuwa kuna baadhi ya walengwa ambao ni watoto walishindwa kuendelea katika mpango baada ya wazazi wawili mke na mme kutengana na hivyo watoto kuhamishwa eneo la mtaa husika bila kuwepo mawasiliano na mratibu wa mpango na hivyo kusababisha watoto kuondolewa katika mpango.

Esther Peter mkazi wa mtaa wa Kabale Ka Ngaiza mwenye wategemezi sita, watoto wake wanne na wadogo zake wawili amesema kuwa, yeye anakabiliwa na changamoto mbili mtaji wake kuwa mdogo tofauti na mahitaji yake pamoja na sehemu ya kuishi kwani anaishi kwenye nyumba za kupanga.

Amesema kutokana na changamoto za ndoa watoto waliingizwa kwenye mpango baadaye baba yao akawachukua kuishi nao eneo jingine na hivyo kutokana na kwamba hakuwa na mawasiliano naye watoto waliondolewa kwenye mpango na sasa baada ya kuanza kuishi nao tena anafanya utaratibu wa kuwarudisha kwenye mpango.

“Nashukuru mpango huu wa TASAF na namshukuru Rais wa nchi yetu mama Samia Suluhu Hassan mimi kabla sijaingia  katika mpango huu nilikuwa naishi kwa kuomba omba chakula na nguo kwa watu lakini baada ya kuingia kwenye mpango huu kwa sasa naweza kumudu chakula milo mitatu naweza kuvaa nguo nzuri na kuwanunulia wanangu pia na nimepata mtaji kidogo nafanya biashara ya kuuza samaki” amesema Peter

Amesema, kipindi hicho alikuwa na mdogo wake yuko kidato cha pili lakini kwa sasa amemaliza chuo cha maendeleo ya jamii ingawa bado hajapata ajira na mdogo wake yuko chuo kikuu anasomea sheria.

Aidha walengwa hao wameiomba serikali waendelee kuwa walengwa katika mpango wa kunusuru kaya maskini kwani wapo baadhi yao wamekumbwa na changamoto mbalimbali na hivyo kusababisha kutoinuka kiuchumi na kubaki wakiwa maskini.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kabale ka Ngaiza Longino Goerge ametoa maombi kadhaa kwa wadau hao kuwa, ni pamoja na TASAF kuunda dawati la usuluhishi kwa wanandoa, kuwaingiza wazee kwenye mpango na kutoa ajira kwa vijana waliotokana na mpango.

Akijibu maswali ya mwenyekiti Kaimu mkurugenzi wa mifumo , mawasiliano na ufuatiliaji TASAF makao makuu Peter Lwanda amesema kuwa, wanaendelea kutengeneza mpango mwingine ambao utaendelea.

Kuhusu ajira ameeleza kuwa, TASAF ilikuwa inafuatilia wale wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne  ambao hawaendelei ofisi ya waziri mkuu inawapeleka vyuo vya ufundi na kuwa serikali bado inaangalia matatizo ya ajira na kuyafanyia kazi.

Lwanda akijibia swala la wazee kuingizwa kwenye mpango ameeleza kuwa, watalichukua na kulifanyia kazi mpango ujao.

Ikumbukwe kuwa mkoa wa Kagera una walengwa wa TASAF wapatao 80,563 ambapo tangu mpango ulipoanza mwaka 2015 hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 57.2 zimeishatolewa kwa walengwa hao.





Walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masiki mtaa wa Kabale Ka Ngaiza

Tuesday, January 30, 2024

BARAZA LA MADIWANI LAPITISHA BAJETI YA BILIONI 38.9 KWA MWAKA WA FEDHA 2024/25

 

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo limepokea na kupitisha bajeti ya shilingi Bilioni 38,982,000,000.00 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 huku shilingi Bilioni 6,482,058,127.00 ikitarajiwa kukusanywa katika mapato ya ndani na shilingi 32,496,016,000.00 ruzuku kutoka Serikali kuu.


Bajeti hiyo imepitishwa Tarehe 30 Januari 2024 katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.


Akiwasilisha bajeti hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, ambae pia ni Diwani wa Kata ya Nianjema, Abdul Pyallah amesema ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji isimamie kikamilifu mikakati ya ukusanyaji mapato.


Akizungumza katika Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Mhe. Mohamed Usinga, amemtaka Mkurugemzi kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wakuu wa idara ambao watakamilisha miradi huku ikiwa na madeni.


Usinga alisema ipo tabia ya baadhi ya wakuu wa idara kutekeleza Miradi huku wakiwa wanakopa kwa wazabuni na kuisababishia Halmashauri kuwa na madeni yasiyo ya lazima.


Alisema ni Mkuu wa idara atekeleze Mradi wake kwa mujibu wa bajeti ilivyo na si vinginevyo.


Alisisitiza kwa kisema kuwa, Mkuu wa idara atakasababisha deni kwenye Mradi achukuliwe hatua ikiwa ni pamoja na kuvuliwa madaraka.


Nae Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo amesema atahakikisha anasimamia bajeti hiyo ili kufikia malengo waliyojiwekea katika ukusanyaji pamoja na utekelezaji wa Miradi mbalimbali.



TAKUKURU KAGERA YAWANOA WAANDISHI KUELEKEA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA.

 

Na Alodia Babara

Bukoba

Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU mkoa wa Kagera amewasihi waandishi wa habari mkoani humo kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo katika kuelimisha jamii na kufichua vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.


Mkuu huyo Pilly Mwakasege aliyasema hayo Januari 30, mwaka huu wakati akifungua mafunzo ya siku moja yaliyotolewa na taasisi hiyo kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali mkoani Kagera ambapo amesema kuwa, wanawategemea waandishi wa habari kuwapa ushirikiano katika kuwapatia taarifa mbalimbali zinazohusu vitendo vya rushwa kwa sababu ni watu muhimu katika jamii na wanauwezo wa kufika kokote na wanaaminiwa sana na jamii.



Amesema kuwa, vyombo vya habari vikitumika vizuri vitaleta mabadiliko kwa jamii kwani watapatikana  viongozi bora na si bora viongozi ambao watasimamia vizuri miradi ya maendeleo na kukemea viashiria vya rushwa.


Amewasisitiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao vizuri kwa kuandika mema yaliyofanywa na Serikali kuliko kuitumia tofauti kwani itakuja kuleta athari za rushwa na akaomba kupitia semina hiyo ili wakawe mabalozi na watoe ushirikiano kwa taasisi hiyo.


Aidha amesema  elimu ambayo itatolewa na Takukuru kupitia vyombo vya habari na kuwafikia wananchi itasaidia kujua kwamba  wanapaswa kuchagua kiongozi wa eneo lao ambao wanazitambua changamoto zilizopo kwa undani na watasimamia vizuri maendeleo yao.


Amesema viongozi wanapaswa kutambua kuwa wanapopigiwa kura ile nafasi waliyoipata siyo eneo la kutafuta fursa au mtaji bali ni sehemu ya kwenda kushirikiana na wananchi wao kuwaletea maendeleo. 


“Kiongozi anayetoa rushwa ni yule ambaye hajiamini na hakujiandaa kwa wananchi wake, mkoa wa Kagera tunataka uchaguzi utakapofanyika wachaguliwe viongozi wenye maadili mema watakaosimamia ipasavyo miradi ya maendeleo ya wananchi” amesema Mwakasege.


Kwa upande wake  mkuu wa dawati la elimu kwa Umma TAKUKURU mkoa  Esther Mkokota amesema kuwa, rushwa ni adui wa haki na kuwa inaminya haki za watu kuchagua au kuchaguliwa hivyo akasema waandishi wa habari waelimishe watu juu ya kuacha tamaa ambayo ni kisababishi kikubwa cha rushwa.


Amesema kuwa kuna watu wanapowaona wenzao wana mali wanazitamani mali hizo bila kujiuliza mali hizo walizipata kwa njia ipi na hivyo kusababisha wajihusishe na rushwa jambo ambalo litasababisha mtu kama huyo kuchukuliwa hatua za kisheria.


Mkokota ameeleza kuwa, jamii ijue kuwa rushwa ni njia ya mkato ambayo inatumika kufikia lengo na endapo watachagua viongozi kwa kupewa rushwa wajue watakuwa wamepata viongozi wasiokuwa na sifa, rushwa inazorotesha maendeleo ya nchi na miradi inajengwa chini ya kiwango kutokana na kusimamiwa na kiongozi asiye na maadili mema.


Ameongeza kuwa, wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wachague viongozi bora wenye maadili watakaosimamia miradi ya maendeleo




Sunday, January 28, 2024

KILIMO SHADIDI CHA MPUNGA CHAANZA KUCHANGAMKIWA.


Na Mwandishi wetu- Mbeya.

Wakulima wa zao la mpunga wameeleza kufurahishwa na Mfumo wa Kilimo Shadidi cha Mpunga, chenye kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia mfumo wa kuongeza mpunga (SRI) ambao unapunguza  gharama za uzalishaji huku tija ikiwa inaongezeka  mara dufu ya kilimo cha kawaida.


Hayo yameelezwa  katika kikao Cha mwaka cha Wadau wa Kilimo shadidi kilichofanyika Januari 24-27 Jijini Mbeya katika viunga vya Kituo Cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI Uyole.


Akielezea hili, Mkulima wa Skimu ya Mkula Wilaya ya kilombero Mkoani Morogoro Filbert Kadebe, amesema katika Kilimo cha kawaida alikuwa akipanda mbegu kilogramu 30 kwa hekari moja lakini kwa kutumia  Mfumo wa Kilimo Shadidi cha Mpunga  wenye kanuni ya kutumia kitalu mkeka anapanda mbegu kilogramu 2 hadi 3 kwa hekari moja.


Pia, Kadebe alisema upandaji wa mche mmoja katika kilimo shadidi unatoa machipukizi mengi ambayo hupelekea kuongezeka kwa mavuno ukilinganisha na upandaji wa Kilimo cha kawaida.


Kilimo shadidi cha mpunga  kinachojulikana kitaalamu  (System of rice Intesification- RSI) ni mchanganyiko wa teknolojia za kilimo cha mpunga wa umwagiliaji kwa kubadilisha mfumo wa uratibu wa mimea, udongo, matumizi ya maji na virutubisho kwa lengo la kuongeza tija.


Nchini Tanzania, Kilimo Shadidi Katika zao la mpunga ni matokeo ya utekelezaji wa mradi  wa mifumo ya uzalishaji mpunga inayokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na rasilimali kwa ufanisi.


Mradi huo unatekelezwa na  TARI kwa kushirikiana na taasisi ya Utafiti ya Norway- Norwegian Institute  of Bioeconomy research (NIBIO) na taasisi ya Utafiti ya Swamination (MSSRF) ya nchini India.


Akielezea Mradi huo, Mratibu  wa  mradi ambaye pia ni Mtafiti Mkuu Kituo Cha Utafiti TARI Uyole, Dkt. Atugutonza Bilaro amesema kilimo  hicho kinatekelezwa katika Halmashauri tano ambazo ni Kilombero, Chalinze, Iringa Vijijini, Mbarali na Bunda.


Dkt. Bilaro amesema katika kipindi cha mwaka mmoja tayari wamewafikia Wakulima mia tisa lengo ikiwa ni Katika kipindi Cha miaka mitatu ya utekelezaji wa Mradi wafikie Wakulima 4,500.


Naye kiongozi mwenza wa mradi kutoka taasisi ya (NIBIO) Prof. Udaya Sekhar anaeleza lengo la kukutana ni kujadili maendeleo ya mradi, na kuweka mipango ya kutekeleza katika kipindi cha mwaka wa pili.


kwa upande wake  Mtafiti, taasisi ya MSSRF Dkt. Ramasamy Rajkumar ameeleza kufurahishwa namna ambavyo wakulima na Wadau wengine wameanza kutumia elimu wanayofikishiwa na wataalamu.