Tuesday, November 7, 2023

WAFANYABIASHARA KISARAWE WALIA NA TRA.

 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara (JWT),Hamis Livembe akizungumza na wafanyabiashara wilayani Kisarawe.

.....................................

Wafanyabiashara Kisarawe walia na TRA wasisitiza elimu ya mlipa kodi


Na Mwandishi Wetu, Kisarawe 


WAFANYABISHARA wilayani Kisarawe mkoani Pwani, wameiomba Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwapa elimu ya kutosha kuhusu ulipaji kodi wa hiari na matumizi ya mashine za EFD.


Ombi hilo lilitolewa na baadhi ya wafanyabishara wilayani humo, wakati wa mkutano wao na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabishara (JWT) wakiongozwa na Mwenyekiti wake Hamis Livembe, wakiwa kwenye ziara ya kikazi ya kusikiliza kero mkoani humo.


Mfanyabishara Christina Mulu, amesema TRA wanatakiwa kuwapa elimu ya kutosha kuhusu ulipaji kodi badala ya kukazania kukusanya bila kuwasikiliza wafanyabishara kwanza.


"Wafanyabiashara wengi hatuna elimu ya kodi, matumizi ya EFD hatujui wakati mwingine risiti zinagoma kutoka na mashine kusumbua sasa TRA wakija wao ni kutaka tu kutoza faini badala ya kutupa elimu kwanza," amesema Mulu.


Mfanyabishara John Masine, amewataka TRA kuwasaidia wafanyabishara urahisi wa kupata kodi na kuwalinda kwa kuondoa wamachinga mbele ya fremu za biashara.


"Mfanyabishara amekodi nyumba analipa kodi TRA, lakini anakuja mmachinga anaweka kibanda mbele yake na anauza bidhaa zinazofanana kwa bei ya chini zaidi na wala halipi kodi yoyote TRA zaidi ya ushuru wa serikali ya mtaa na hakuna anayejali zaidi ya kutaka kukamua kodi bila kujua tunauza au laa," amesema Masine.


Naye Mfanyabishara Ester Moshi, ametaka wafanyabishara kutofunga biashara siku ya Jumamosi ya mwisho wa mwezi ambayo ni siku ya usafi kwasababu wanakwamisha shughuli za kiuchumi.


"Siyo kwamba siku hiyo biashara hazifanyiki hapana, zinafanyika lakini kwa kujificha na kukimbizana wakati serikali inaweza kupunguza muda ikawa muda wa kufungua ni saa 2 badala ya 4 asubuhi," amesema Moshi.


Naye Ofisa wa TRA wilayani humo, Mohamed Chifu, ameushukuru uongozi wa JWT, kwa kazi kubwa wanayofanya ya kusikiliza kero za wafanyabishara lakini pia kutoa majibu ya kina kuhusu mambo mbalimbali yanayowahusu.


Amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo TRA wilayani humo ni wafanyabishara wengi kuwa wa hali ya kati ambapo wanalipa kodi ndogo.


"Wengi wao wanalipa kodi ya ndogo kwa sababu ya halihalisi ya biashara, haujawa mji wa biashara kubwa. Kero ambazo zinatuhusu nimezibeba na naahidi nitaziwasilisha na kuzifanyia kazi," amesema.




Baadhi ya wafanyabiashara wilayani Kisarawe 



 

UJENZI WA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA LA HOIMA UNASHIRIKISHA WAZAWA MKOANI KAGERA

 

Wakandarasi na wa watoa huduma 42 wapatiwa kazi


Dodoma


Imeelezwa kuwa ujenzi wa Mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga unashirikisha wakandarasi wazawa kutoka mkoani Kagera.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga, kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu kutoka mkoani Kagera Mhe. Neema Kichiki Lugangira aliyetaka kujua je ni wakandarasi wangapi kutoka mkoani Kagera wamepata kazi katika mnyororo wa ujenzi wa bomba la mafuta la Hoima mkoani Tanga. 


Mhe. Kapinga amesema kuwa wakandarasi wakuu wa Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga wanaendelea kushirikiana na wakandarasi wadogo, wajenzi na na wanna huduma mbalimbali katika mikoa yote inayopitiwa na Mradi. 


Mhe. kapinga aliongeza kuwa jumla ya wakandarasi na watoa huduma 42 wamepata kazi mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa ujenzi wa Mradi huu ikiwemo uuzaji wa vifaa vya ujenzi, huduma za usambazaji wa mafuta, huduma za umeme na hoteli. 

MAGAZETI YA TANZANIA LEO TAREHE 07 NOVEMBA 2023

 

















Monday, November 6, 2023

DKT. BITEKO ASHIRIKI MAZISHI YA KAKA WA WAZIRI MKUU MAJALIWA

 

Asisitiza Watanzania wanaupendo wa dhati kwake


Waziri Mkuu Majaliwa awashukuru Watanzania kwa kumfariji


Ruangwa - Lindi


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameungana na Viongozi mbalimbali wa kitaifa na Watanzania kwa kutoa salamu za pole kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa kufuatia kifo cha Kaka yake, marehemu Issa Juma, aliyezikwa leo.


Akizungumza leo Novemba 6, 2023 wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi wakati akitoa salamu hizo kwa niaba ya waheshimiwa Mawaziri, Dkt. Biteko amesema watanzania wanaupendo wa dhati kwa Waziri Mkuu Majaliwa ambao wameuonesha pia katika kipindi hichi cha kumpoteza marehemu kaka yake.


"Sisi ni kielelezo kuwa Watanzania wanaupendo nawe ndio maana tumekuja kuungana pamoja na wewe, kulia pamoja na wewe lakini kukutia moyo kwamba sisi tuliofika hapa na wengine tunakupa pole kwa msiba wa kumpoteza kaka," ameeleza Dkt. Biteko.


Amesema kuwa, jambo lolote linalotokea ni mipango ya Mwenyezi Mungu hivyo ni muhimu kuombeana heri ili tuwe na mwisho mwema duniani. 


Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewashukuru Watanzania kwa kumfariji katika kipindi hichi cha msiba wa kaka yake. Amesema amepokea salamu za pole kutoka kwa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar, Dkt.Hussein Mwinyi na watanzania wote wanaompa pole na kumfariji.


Naye, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson akiwasilisha salamu kwa niaba ya Wabunge, ametoa pole kwa Waziri Mkuu Majaliwa na familia yote kwa kuondokewa na mpendwa wao na kusisitiza kuendelea kushirikiana na kutenda mazuri yanayompendeza Mungu.


Wengine walioshiriki kumpa pole Mhe. Waziri Mkuu ni Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa ya Lindi na Mtwara, Wakuu wa Wilaya, vyama vya siasa na wananchi wa mkoa huo. 











JWT YAANZA ZIARA PWANI,KUTATUA KERO KWA WAFANYABIASHARA

 

Na Mwandishi Wetu, Pwani.


JUMUIYA ya Wafanyabiasha nchini (JWT) imeanza ziara ya kikazi ya kusikiliza kero za Wafanyabishara katika Wilaya zote za Mkoa wa Pwani.


Lengo la ziara hiyo ni kusikiliza kero za wafanyabishara, wenye viwanda na kampuni ili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu na kuepuka changamoto ikiwamo migomo ya mara kwa mara.


Mwenyekiti wa JWT, Hamis Livembe, akiongozana na viongozi wengine mapema leo, wamewasili ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani na kufanya mazunguzo na Katibu Tawala, Rashid Mchatta kabla ya mikutano yao.


Livembe amesema Rais Samia anawapenda wafanyabishara ndio sababu amewaagiza wasikilize kero zao ili kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.


Amesema wafanyabishara wakiungana wanaweza kujisemea na kumaliza kero zao bila kufunga biashara wala kufanya vurugu hivyo ni muhimu kujitokeza kwenye mikutano hiyo.


Naye Mchatta ameipongeza jumuiya hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuisaidia serikali kusikiliza kero hizo nchi nzima na kuzifikisha kwenye mamlaka husika.


"Niwasihi tu viongozi wa JWT msiache kuwaelimisha wafanyabishara umuhimu wa kulipa kodi pamoja na hayo wazingatie tahadhari za mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini," amesema.





VIJANA 24 KUTOKA TULIA TRUST WAMEHITIMU TaSUBa, BAGAMOYO.

 

Na Athimani Shomari

Vijana 24 kutoka Taasisi ya Tulia Trust ya Mkoani Mbeya wamehitimu mafunzo yao ya mwezi mmoja ya Sanaa na Utamaduni leo Tarehe 06 Novemba 2023, katika chuo cha TaSUBa Wilayani Bagamoyo na kufanikiwa kuongeza elimu yao ya Sanaa na Utamaduni,
ambapo sasa wanaweza kufanya shughuli zao  kwa ufanisi zaidi ukilinganisha na awali.

Mgeni Rasmi katika Mahafali ya kumaliza mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye, ametoa wito kwa vikundi mbalimbali nchini vinavyofanya shughuli za Sanaa na Utamaduni kufika chuoni hapo ili kupata elimu itakayowaongoza katika kazi za Sanaa na Utamaduni.

Dkt. Makoye alisema TaSUBa ni sehemu ya kulea wasanii wa aina mbalimbali ikiwemo wale wa ngoma za asili hivyo watanzania wasione uvivu kujiunga na chuo hicho kwa kukuza Taaluma zao ili waweze kufikisha kwenye jamii ujumbe unaolingana na maadili ya kitanzania kwa weledi uliotukuka.

Wakati huohuo Dkt. Makoye ameishukuru Taasisi ya Tulia Trust ya Mkoani Mbeya kwa kugharamia mafunzo ya vijana hao ili wapate mafunzo sahihi ya Sanaa na utamaduni kwa lengo la kukuza vipaji vyao, kuongeza vipato vyao na kufikisha ujumbe kwa jamii kwa njia ya Sanaa na Utamaduni.

Alisema Tulia Trust, imekuwa msatari wa mbele katika kuwafadhili vijana mbalimbali kuendeleza vipaji vyao vya Sanaa na Utamaduni katika chuo hicho kinachotoa mafunzo ya Sanaa na Utamaduni kilichopo chini ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambpo miongoni mwao
wapo wanaopata kozi fupi, ngazi ya cheti na Astashahada.

Awali wakisoma risala mbele ya mgeni rasmi, wahitimu hao walismea wanaishukuru Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kwa
kuwapokea na kuwapa mafunzo bora yatakayowawezesha kufanya shughuli
zao kwa ufanisi zaidi ukilinganisha na awali kabla ya kupata mafunzo hayo.

Walisema uwepo wa TaSUBa na vijana kupata fursa ya mafunzo chuoni hapo
kumewafanya vijana wengi hapa nchini kuiona thamani ya vipaji walivyonavyo kwani vinaendelezwa na hatimae wananufaika kupitia vipaji hivyo.

Waliongeza kwa kusema kuwa katika mafunzo hayo waliyopata wamefanikiwa
kujifunza ngoma mpya ambazo walikuwa hawazijui, lakini pia wameweza kujifunza namna ya kufanya maboresho ya ngoma zao za asili za mkoa wa Mbeya.

Aidha, sambamba na hayo, vijana hao pia walisema wameweza kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu Sanaa na Utamaduni wa Mwafrika kupitia Tamasha la 42 la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ambalo lilifanyika chuoni hapo (TaSUBa) mwezi Oktoba 2023.

Kupitia risala yao, vijana hao wamemshukuru Mbunge wa Mbeya Mjini na
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, pamoja na Taasisi ya Tulia Trust, kwa kutambua uwepo wa vijana na kuwashika mkono kwa kuwawezesha kutoka kwenye hatua moja kwenda hatua nyingine na kunufaika kupitia vipaji walivyonavyo.

Taasisi ya Tulia Trust ya Mkoani Mbeya imeasisiwa na na Mbunge wa jimbo la Mbeya mjini, ambae pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, lengo likiwa ni kuwasaidia
vijana na wakazi wa mkoa huo kwa ujumla kutatua changamoto mbalimbali
zinazowakabili.











Picha zote Na Herry Pesa

Sunday, November 5, 2023

RAIS, SAMIA AMKABIDHI NYUMBA MAMA JANETH MAGUFULI.


Rais Samia Suluhu Hassan amemkabidhi Nyumba Mjane wa Rais wa awamu ya Tano Dkt John Magufuli, Mama Janeth Magufuli jijini Dar es Salaam, leo Tarehe 05 Nobemba 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi mfano wa ufunguo mjane wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Mama Janeth Magufuli ikiwa ni ishara ya kukabidhi nyumba mpya ya kuishi kwa familia ya Dkt. John Pombe Magufuli iliyopo wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam ambayo amejengewa na Serikali kwa mujibu wa sheria, Jijini Dar es Salaam tarehe 5 Novemba, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa nyumba mpya ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, na kuikabidhi kwa Mama Janeth Magufuli, nyumba hiyo imejengwa na Serikali kwa mujibu wa sheria, Jijini Dar es Salaam tarehe 5 Novemba, 2023.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na mjane wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Mama Janeth Magufuli wakati wa hafla fupi ya kukabidhi nyumba ya kuishi iliyopo wilaya ya Kinondoni ambayo imejengwa na Serikali kwa mujibu wa sheria, Jijini Dar es Salaam tarehe 5 Novemba, 2023.