Wednesday, October 11, 2023

KIKWETE AMPONGEZA BITEKO, KERO ZA UMEME KUSHUGHULIKIWA HARAKA.

 

Chalinze imetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020- 2025 kwa mafanikiopp


Chalinze - Pwani


Serikali imeahidi kushughulikia changamoto ya umeme iliyopo nchini kwa kasi kubwa ili tatizo hilo liweze kuisha katika kipindi kifupi kuanzia sasa.


Hayo yameelezwa leo Oktoba 11, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko katika Mkutano Mkuu Maalum wa Jimbo la Chalinze wa kupokea taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2020-2025) wilaya ya Chalinze mkoa wa Pwani.


Dkt. Biteko amesema kuwa, katika kipindi cha miezi sita inayokuja ukosefu wa umeme nchini utaisha baada ya Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kumaliza tatizo hilo nchini. Amesema Watendaji wanafanya kazi ili watanzania wapate umeme wa kutosha.


Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameiagiza TANESCO kupeleka umeme katika shule ya Sekondari ya Moreto ili shule hiyo iunganishwe na umeme mapema. Aidha amechangia kompyuta 10 kwenye shule hiyo maalum kwa matumizi ya TEHAMA kuwasaidia wanafunzi.


Kuhusu Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Dkt. Biteko ametumia nafasi hiyo kupongeza juhudi zinazofanywa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo ujenzi wa madarasa, zahanati na miundombinu muhimu na pia kufanya vizuri katika makusanyo ya mwaka ambapo wilaya hiyo imekusanya shilingi bilioni 15.


Kwa upande wake, Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa msukumo mkubwa kwenye maendeleo ya nchi yetu na fedha hizo zinaelekezwa katika miradi mbalimbali ili kukuza uchumi wa nchi.


Vile vile, Mhe. Dkt. Kikwete amempongeza Mhe. Dkt. Biteko kwa kuteuliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati hapa nchini na kumsisitiza awe msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali na kufanya kazi kwa bidii.


Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa mkoa wa Pwani unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule, madaraja, vituo vya afya ili mkoa huo ukue kiuchumi na hatimaye kuboresha maisha ya wananchi wake.


Aidha, Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema, katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, halmashauri ya wilaya ya Chalinze imefanikiwa kutekeleza kwa kiwango kikubwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020/25.


"Wananchi wamewezeshwa kiuchumi, hali ya uzalishaji katika Kilimo, uvuvi, umwagiliaji, viwanda na biashara imeongezeka, miundombinu ya shule, zahanati, vituo vya afya na hospitali ya wilaya imekamilika kwa asilimia kubwa na kwenye baadhi ya vijiji na kata ujenzi unaendelea," amesema Mhe. Ridhiwani.


Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okash amesema, katika uongozi wa miaka wa Rais Samia wameshuhudia mabadiliko makubwa kimaendeleo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze. Amesema Mbunge anaonesha ushirikiano 


Wilaya ya Bagamoyo ni miongoni mwa wilaya Saba zinazounda mkoa wa Pwani. Wilaya hiyo ina halmashauri Kuu mbili ambazo ni Halmashauri ya wilaya ya Chalinze na Halmashauri ya Bagamoyo.


Mkutano huo umehudhuriwa na Viongozi Mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wanachama zaidi ya 1000 walioshiriki katika uwasilishwaji wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi CCM 2020/25










Saturday, October 7, 2023

WAWEKEZAJI WAKARIBISHA SOKO LA UTALII NCHINI

 



Na Andrew Chale, Dar es Salaam.


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amesema Serikali ya Tanzania inafanya maboresho makubwa kwenye miundombinu sekta ya utalii na amewakaribisha wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja kuwekeza nchini kwa kuwa Tanzania imejaaliwa kuwa na maliasili za kipekee, vivutio vya kitamaduni na maeneo marefu ya fukwe za Tanzania Bara na Zanzibar.


Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo katika siku ya pili ya Maonesho ya Saba ya Swahili International Tourism Expo – S!TE, 2023 leo Oktoba 7,2023 wakati akifungua Jukwaa la Uwekezaji jijini Dar es Salaam linalojulikana kama “Uwekezaji Endelevu kwa Maendeleo Jumuishi ya Kijamii na Kiuchumi”.


Mhe. Kairuki amesema pamoja na kazi kubwa ya kuboresha miundombinu iliyofanywa na kusaidia kuleta watalii pia amefafanua kuwa ongezeko kubwa la watalii limetokana na kazi nzuri iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya “The Royal Tour”. Filamu hii ilionyeshwa katika vituo vingi vya televisheni vinavyotambulika nchini Marekani na kwingineko duniani ili kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania.


Amesema The Royal Tour na juhudi nyingine za masoko umesababisha kuongezeka kwa idadi ya watalii waliofika kutoka nje ya nchi imeongezeka kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi watalii 1,454,920 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 57.7. Aidha, idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi 2,363,260 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 199.5.


Aidha amesema utalii umeendelea kuwa msingi wa ukuaji wa uchumi wa nchi ambapo amefafanua kuwa sekta, inachangia hadi 17.2% ya jumla ya Pato la Taifa na 25% ya mapato yote ya mauzo ya nje ambapo amesema kuna sekta inaweza kuchangia zaidi kwenye uchumi zaidi pia baada ya kupatikana kwa bidhaa mpya za utalii kama utalii wa mikutano na utalii wa meli ambazo kwa sasa Serikali inafanya kazi.


Akitoa mada kwenye Jukwaa la Uwekezaji Naibu Kamishna wa Uhifadhi kutoka Hifadhi ya Ngorongoro Imani Richard Nkuwi amefafanua kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii na Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imepokea andiko la mradi (project proposal) unaotambulika kama “Development of Water Front and Cruising Ship Terminal” kutoka kwa Mkandarasi tarajiwa. Mradi husika unatarajiwa kugharimu takribani kiasi cha USD 300 milioni na utahusisha ujenzi wa gati la mizigo ya mwambao na ujenzi wa gati la meli za kitalii pamoja na uendelezaji wa ufukwe wa Bahari ya Hindi jirani na gati la meli za kitalii. Ujenzi wa miundombinu husika unategemewa kuanza kabla ya mwaka wa fedha 2023/24.


Mhe. Waziri amezitaja baadhi ya juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha miundombinu kuwa ni pamoja na Reli ya Standard Gauge (SGR) ambayo iko katika hatua za mwisho kukamilika inalenga kuunganisha Jiji la Dar es Salaam kama lango kuu la watalii wanaofika njia ya kati na Kusini, kuimarisha Shirika la Ndege la Taifa kwa kuongeza idadi ya safari za ndege ili kuimarisha utalii kuunganishwa kwa kanda mbalimbali za kitalii za Tanzania.


Pia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal 3 na ukarabati wa Viwanja vya Ndege vya Mikoani.


MAGAZETI YA LEO TATEHE 07 OKTOBA 2023.

 
































SERIKALI ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA KANISA KATOLIKI - DKT. MPANGO.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema serikali itaendelea kufanya kazi na kushirikiana vema na Kanisa Katoliki pamoja na madhehebu mengine ya dini hapa nchini.
 
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa mapokezi ya Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam akitokea Vatican alipopewa hadhi ya Ukardinali. Amempongeza Kardinali Rugambwa kwa kuendelea kuhubiri amani na umoja wa Watanzania na kumsihi kuendelea kuwa chachu ya amani, upendo na umoja. Makamu wa Rais amesema ni baraka kwa Taifa la Tanzania kupata Kardinali wa tatu.
 
Kwa upande wake Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa amewaomba watanzania wa kila dini kuendelea kumuombea ili aweze kufanya vema kazi hiyo kwa uaminifu na kuweza kuleta maendeleo ya mwanadamu kwa ujumla kuanzia hapa nchini kimwili na kiroho na baadaye hata nje ya nchi.
 
Kardinali Rugambwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Kanisa, Serikali na watanzania wote waliomtia moyo na kumtumia jumbe mbalimbali za pongezi zilizompa moyo na kumuimarisha.
 
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
06 Oktoba 2023
Dar es salaam. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimsalimiana na Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa mara baada ya Kardinali Rugambwa kuwasili nchini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam akitokea Vatican alipopewa hadhi ya Ukardinali. (Tarehe 06 Oktoba 2023)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifurahia jambo na Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa mara baada ya kumpokea alivyowasili nchini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam akitokea Vatican. (Tarehe 06 Oktoba 2023).


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa pamoja na viongozi wengine wa Kanisa Katoliki wakati wa Mapokezi ya Kardinali Rugambwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Vatican alipopewa hadhi ya  Ukardinali. (Tarehe 06 Oktoba 2023)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa,Maaskofu pamoja na viongozi wengine wa Kanisa Katoliki wakati wa mapokezi ya Kardinali Rugambwa yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. (Tarehe 06 Oktoba 2023).


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania Askofu Gervas Nyaisonga,Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania Askofu Mkuu Angelo Accattino pamoja na viongozi wengine wa Kanisa Katoliki wakati wa mapokezi ya Kardinali Rugambwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere

Friday, October 6, 2023

REA YATOA MWONGOZO UWEZESHAJI UJENZI VITUO VIDOGO VYA MAFUTA VIJIJINI

 

Mhandisi Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Kelvin Tarimo, akiwaeleza Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Ruvuma, dhamira ya Serikali kuanzisha mpango wa kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta (Dizeli na Petroli) maeneo ya vijijini. Alikuwa akiwasilisha mada katika Baraza hilo Oktoba 5 mwaka huu kwa mwaliko wa Naibu Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Vijana Mkoa wa Ruvuma, Judith Kapinga.

...................................

Veronica Simba na Issa Sabuni – REA

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imedhamiria kuanzisha mpango wa kuwezesha ujenzi wa vituo vipya vidogo vya gharama nafuu vya bidhaa za mafuta (Dizeli na Petroli) maeneo ya vijijini ili kuondosha njia zisizo salama za uhifadhi wa mafuta hayo.

Hayo yamesemwa na Mhandisi Miradi kutoka REA, Kelvin Tarimo wakati akitoa semina kwa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Ruvuma, Oktoba 5 mwaka huu kwa mwaliko wa Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.

Akizungumza na Wajumbe wa Baraza hilo, Mhandisi Tarimo alieleza mambo mbalimbali ikiwemo mwongozo wa ujenzi wa vituo hivyo kwa wale watakaokidhi vigezo na kupata mkopo wa kuvijenga.

Alisema kuwa pamoja na mambo mengine, Mwongozo huo unaainisha bayana vigezo kwa mwombaji wa mkopo ambavyo vimegawanyika katika makundi mawili; kiufundi na kifedha.

Mhandisi Tarimo alivitaja baadhi ya vigezo vya kiufundi kwa mwombaji kuwa ni pamoja na mtu binafsi au kikundi cha wajasiriamali kijijini kilichosajiliwa na Mamlaka husika au Serikali ya kijiji kuwa na kibali cha ujenzi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Kigezo kingine ni mwombaji kuwasilisha kwa REA barua ya maombi ya mkopo wa ujenzi wa kituo au vituo vipya tu na siyo vinavyohitaji ukarabati au vilivyoanza kujengwa.

Aidha, mwombaji atatakiwa kuwa na barua ya uthibitisho kutoka Halmashauri ya kijiji na Wilaya inayomruhusu kuendesha biashara ya kituo cha mafuta katika eneo aliloomba pamoja na kuwa na namba ya mlipa kodi (TIN Namba) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Pia, alieleza kuwa mwombaji anatakiwa kuwa na uthibitisho wa umiliki wa ardhi (Hati Miliki ya ardhi au Hati za kimila au uthibitisho wa umiliki wa ardhi) kutoka kwa Halmashauri ya Kijiji au Wilaya.

Kingine ni kibali cha ujenzi kutoka Mamlaka husika pamoja na kujaza fomu ya kuonesha namna anavyokusudia kufanya biashara ya mafuta.

Akieleza zaidi, Mhandisi Tarimo alisema fedha hizo za Mradi zitakazotolewa kama mkopo, ni sehemu ya juhudi za Serikali zinazolenga kuzuia kuhifadhi mafuta ndani ya nyumba kwa kutumia mapipa na chupa za plastiki katika kuuza mafuta ya petroli na dizeli kwa watumiaji wadogo kama vile waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda katika maeneo ya vijijini.

“Hii ni kutokana na kukua na kuongezeka kwa matumizi ya bidhaa hizi katika shughuli za maendeleo maeneo ya vijijini,” alisema.

Kiasi cha mkopo ni shilingi milioni 75 na riba yake ni asilimia tano ilhali marejesho yake ni hadi kipindi cha miaka saba.

Mhandisi Tarimo ametoa hamasa kwa wananchi wote wenye nia kutembelea tovuti ya Wakala wa Nishati Vijijini ambayo ni www.rea.go.tz ili kusoma Mwongozo kamili wa utoaji na usimamizi wa mkopo wa uwezeshaji wa ujenzi na uendeshaji wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta (petroli na dizeli) vijijini.


WATENDAJI WIZARA YA MADINI WATAKIWA KUPANGA MIKAKATI KUONGEZA BAJETI YA WIZARA

 

Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amewataka Watendaji wa Wizara na Taasisi kujipanga kimkakati kwa kubuni miradi yenye tija kwenye Sekta ya Madini itakayowezesha kuongeza Bajeti ya Wizara na kuhakikisha inakwenda sambamba na Vipaumbele vya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, Dira ya 2030 Madini ni Maisha na Utajiri pamoja na Vipaumbele vya Taifa.


Ametoa rai hiyo leo Oktoba 6, 2023, wakati wa kikao chake na baadhi ya Watendaji hao wa Wizara na Wakuu wa Taasisi za Wizara, ambacho pia kimehusisha watendaji wanaohusika na masuala ya Mipango, Fedha na Rasilimaliwatu kilicholenga kujadili na kujipanga kutekeleza maelekezo, vipaumbele vya Wizara, majukumu, mipango na program mbalimbali ambazo zilijadiliwa wakati wa vikao vya Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde alivyofanya na taasisi zote chini ya Wizara baada ya kuteuliwa na kuapishwa kuwa Waziri wa Madini kwa lengo la kufahamiana, kujengeana uelewa na kuweka mikakati ili kuongeza tija kwenye Sekta ya Madini


Aidha, katika kikao hicho, watendaji hao wamepata wasaa wa kufahamishwa kuhusu namna ya kuandaa mipango na miradi ya kisekta yenye tija kwa taifa kwa kuhakikisha inakwenda sambamba na vipaumbele vilivyopangwa na Wizara na vile vya kitaifa.


Akizungumza katika kikao hicho, Mchumi Mwandamizi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango Khalid Shekimweli amesisitiza kuwa miradi na mipango inayopangwa na sekta ni vema ikazingatia maeneo makuu ya msingi ambayo ni pamoja na kuzingatia masuala yanayohusu huduma muhimu za kijamii, yanayokusudia kuondoa umaskini pamoja na kukuza uchumi.


Awali, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini Bw. Augustino Olal ameeleza kuwa katika Mwaka wa Fedha wizara imepangiwa bajeti ya Shilingi Bilioni 89.3 ambayo imelenga kutekeleza vipaumbele Sita vya Wizara na kuvitaja kuwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli, kuongeza Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa; kuendeleza Madini Muhimu na Madini Mkakati; Kuwaendeleza na kusogezaHuduma za Ugani kwa Wachimbaji wadogo; kuhamasisha shughuli za Uongezaji thamani Madini na kuhamasisha uwekezaji na Biashara katika sekta ya Madini na Uanzishwaji wa Minada na Maoneshi ya Madini ya Vito.


Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri