Wednesday, August 9, 2023

WAHUDUMU WA AFYA MOI KUIMARISHA ZAIDI HUDUMA KWA WAGONJWA

 


Na Mwandishi wetu-MOI, 9 Agosti, 2023 Dar es salaam.


Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof.Abel Makubi amefanya kikao cha kimkakati na watumishi wa kada za wahudumu wa afya na huduma kwa wateja na viongozi wao kwa lengo la kuboresha huduma kwa wateja wanaofika MOI kupata huduma.


Prof. Makubi amewapongeza wahudumu wa afya wa Taasisi ya MOI kwa kazi kubwa wanayoifanya kwani wao ni jicho la hospitali na ni sehemu kubwa katika uendeshaji wa Taasisi.


“Napenda kuwaomba idara zote tuongeze ufanisi katika kazi ili kuendelea kuboresha huduma na kuongeza mapato ambayo yataimarisha Taasisi kifedha ili kuboresha huduma zetu na uendeshaji wa hospitali" Alisema, Prof.Makubi.


Kwa upande mwingine Prof. Makubi amesema kwa sasa kipaumbele cha Wizara ya Afya chini ya Waziri Ummy Mwalimu (MB) ni ubora wa huduma hivyo lazima tutaboreshe huduma kutoka hapa tulipo kwenda mbele zaidi ikiwa ndio ajenda ya kwanza kuliko zote kwenye sekta ya Afya.


“Inabidi tuzingatie mambo muhimu kama salamu, kukaribisha mgonjwa, kumpa pole mgonjwa na ndugu wa mgonjwa wafikapo MOI, kumuelekeza anapotaka kufika pamoja ,kumuuliza kama anachangamoto au mahangaiko na kuondoa vitu kama chuki vilevile kuwa wepesi katika utoaji huduma ili mgonjwa asikae muda mrefu kusubiria matibabu" Alisema Prof Makubi.


Aidha ,Prof.Makubi amewaomba watumishi wote kubadilisha fikra, kuwa na mtazamo chanya kuwa na 'Sense of ownership' na kuzingatia maadili kama kutokupokea rushwa na kutoa taarifa potofu, kujituma vilevile utunzaji wa mali za Taasisi.


Kikao hichi ni muendelezo wa vikao baina ya Prof. Makubi na makundi mbalimbali ya watumishi kwa lengo la kuboresha huduma. Katika kikao hicho Prof Makubi amewakumbusha watumishi wote wa MOI kuhudhuria mkutano mkuu wa watumishi wote wa MOI siku ya Jumamosi tarehe 12/08/2023 katika ukumbi wa CPL Muhimbili. 






UFAFANUZI WA WASIO RAIA NA DIASPORA KUMILIKI ARDHI NCHINI.







MAGAZETI YA LEO TAREHE 09 AGOSTI 2023.

 


















Tuesday, August 8, 2023

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO AWAASA WAZALISHAJI WA ZAO LA KAHAWA WA NCHI ZA AFRIKA.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa nchi za Afrika wanachama wazalishaji wa zao la kahawa kuwekeza zaidi katika kupata vifaa na mashine za kisasa za uchakataji wa zao hilo ili kuongeza thamani ya kahawa kabla ya kuuzwa nje ya bara hilo.

 

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akihutubia viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya kahawa Barani Afrika wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 25 za Afrika Wanachama Wazalishaji wa Zao la Kahawa unaofanyika Kampala nchini Uganda. Amesema ili kuinua sekta hiyo ni muhimu sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali kuweka msisitizo katika kuongeza thamani ya zao hilo pamoja na kuwekeza katika vifungashio bora.

 

Aidha Makamu wa Rais amewasihi wakulima wa zao hilo kujikita katika kilimo bora na cha kisasa kwa kutumia teknolojia rafiki ili kuhakikisha sekta hiyo inakua na mchango mkubwa kwa wananchi na uhifadhi wa mazingira.

 

Pia Makamu wa Rais ametoa rai kwa Shirika la Kimataifa la Kahawa Afrika (IACO) kuharakisha maendeleo ya kituo cha ubora cha zao la kahawa nchini Tanzania kama ilivyokubaliwa hapo awali na kuahidi kwamba serikali ya Tanzania itatoa ushirikiano wote unaohitajika katika kufanikisha jambo hilo.

 

Makamu wa Rais ameeleza kwamba licha ya bei ya kahawa kuwa na mwenendo mzuri kwa kipindi kirefu bara la Afrika limeendelea kubaki nyuma kwa kuwa na asilimia 12 tu ya uzalishaji duniani huku mwelekeo katika ukanda huo ukiendelea kupungua kwa kasi. Amesema ni muhimu kutatua changamoto zilizopo na kuchukua hatua kuhakikisha fursa ya uzalishaji kahawa inatumika vema kwa kuzingatia kuongezeka kwa bei ya zao hilo duniani na uwepo wa soko la watu bilioni 1.4 lililopo Afrika.

 

Akitaja hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha sekta ya kilimo ikiwemo kilimo cha kahawa, Makamu wa Rais amesema bajeti ya kilimo imeendelea kuongezeka katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo ya kifedha, serikali inatoa ruzuku katika mbolea pamoja na kuongeza usambazaji bure wa mbegu za kiwango cha juu za zao la kahawa. Ameongeza kwamba juhudi zingine ni pamoja na kuiwezesha benki ya maendeleo ya kilimo na kuhakikisha utoaji wa mikopo ya kilimo katika riba isiozidi asilimia tisa.

 

Aidha Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea na jitihada za kuhakikisha wanawake na vijana wanashiriki katika mnyororo wa thamani katika uzalishaji wa zao la kahawa ikiwemo uanzishwaji wa Chama Cha Wakulima Wanawake wa Kahawa (TAWOCA), kuwawezesha vijana kimafunzo ili kuzalisha kahawa bora na kufanya biashara ya zao hilo.

Makamu wa Rais amesema kupitia hatua zilizochukuliwa, mafanikio mbalimbali yamepatikana ikiwemo kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la kahawa kwa asilimia 19 kutoka tani elfu 66.5 mwaka 2018/2019 hadi tani elfu 82.5 mwaka 2022/2023. Pia kuongezeka kwa fedha za kigeni kutokana na uuzwaji wa zao hilo kutoka dola za marekani milioni 123.2 mwaka 2018/2019 hadi dola milioni 235.6 mwaka 2022/2023 huku eneo la uzalishaji likiongezeka kutoka hekta 218,966 mwaka 2018/2019 hadi hekta 265,000 mwaka 2022/2023.

 

Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 25 za Afrika Wanachama Wazalishaji wa Zao la Kahawa umebeba kauli mbiu isemayo “Mageuzi katika sekta ya kahawa kwa kuongeza thamani”. Mkutano huo umelenga kuendelea kusimamia ajenda ya kahawa katika orodha ya bidhaa za kimkakati chini ya umoja wa Afrika kupitia mpango wa Maendeleo ya Afrika (AU Agenda 2063). Pia kuongeza thamani na matumizi ya ndani ya zao hilo, kupanua wigo wa biashara ya kahawa kupitia eneo huru la biashara Barani Afrika (AfCFTA) pamoja na kubadilisha uzoefu kuhusu za mabadiliko ya tabianchi na UVIKO19 katika sekta ya Kahawa.

 

Aidha Mkutano huo ni mwendelezo wa Mkutano wa kwanza uliofanyika Mei mwaka 2022 Jijini Nairobi nchini Kenya huku Mkutano wa Tatu ukitarajiwa kufanyika nchini Tanzania.

 

Kando ya mkutano huo Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Uganda Mheshimiwa Jessica Alupo.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

08 Agosti 2023

Kampala – Uganda.



PROFESA MKENDA ATOA MAELEKEZO KWA TAASISI KUENDELEZA UBUNIFU


 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ametoa maelekezo kwa taasisi mbalimbali nchini kuendeleza bunifu na kuziingiza sokoni ili ziweze kushindana katika soko la dunia.


Akizungumza baada ya kutembelea banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya, Profesa Mkenda amesema maendeleo ya teknolojia yanayofanywa na taasisi za Serikali ni makubwa.


“Tunachohitaji vile vilivyogundulika visiwe tu vya maonesho mwaka huu au mwakani, tunataka tuvione vinaingia sokoni vinaanza kuuzwa,” amesema Profesa Mkenda.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu Veta, Anthony Kasore, amesema wanawafundisha vijana ili kuwaandaa kuingia kwenye soko la ajira katika nyanja mbalimbali za uwekezaji, viwanda, kilimo na ufugaji.

Tumekuja na bunifu kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kufanya shughuli zao za kilimo na ufugaji kwa urahisi,” amesema Kasore.


Kwa mujibu wa Kasore, kupitia mradi wa sumu kuvu vijana 420 kutoka katika wilaya 20 wamepatiwa ujuzi wa kutengeneza vihenge ambapo Serikali itawapatia vifaa bure kuweza kujiajiri.


Kaimu mkurugenzi huyo, amesema pia ujenzi wa vyuo vipya katika wilaya 64 na kimoja katika Mkoa wa Songwe utaongeza wigo wa mafunzo ya ufundi stadi kutolewa kote nchini.