Wednesday, February 16, 2022

DC MTANDA AWATAKA WAFANYAKAZI KUWA NA TABIA YA KUFANYA MAZOEZI.

 No description available. 

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya chuo Cha Agha Khan kilichopo Kisongo jijini Arusha. ( Picha na Happy Lazaro).

................................................

Mkuu wa Wilaya ya Arusha ,Said Mtanda amewataka wafanyakazi kuwa na tabia ya kufanya mazoezi ili kuwa na utayari wa utendaji kazi kwa ufanisi kulingana na mazingira wanayofanyia kazi.

Aliyasema hayo jana  jijini Arusha wakati akifungua siku ya kuimarisha afya (Wellness day) iliyoandaliwa na benki ya CRDB kwa ajili ya wafanyakazi wake kutoka Kanda ya kaskazini iliyofanyika katika viwanja vya chuo Cha Agha Khan kilichopo Kisongo mjini Arusha.

 

Mtanda alisema kuwa, swala la kufanya mazoezi ni la muhimu Sana kwa ajili ya kuimarisha afya za wafanyakazi na kuongeza ufanisi wa kazi huku wakiepukana na magonjwa yasiyoambukiza.

 

Aliongeza kwa kusema kuwa, endapo mazingira ya kazi yakiwa mazuri hata utendaji kazi wa wafanyakazi unaongezeka  siku hadi siku kwani ni jambo la msingi .

“Unapodili na watu katika Taasisi yoyote lazima uone mahitaji yao, wanahitaji utulivu, mapumziko na kunakuwepo na  mahusiano mazuri kati ya watumishi na Taasisi husika, hivyo lazima waimarishe afya za watumishi ili wasiyumbe kwani kupata watumishi weledi na waaminifu ni changamoto katika nchi yetu, hivyo lazima tulinde afya zao ili kuongeza ufanisi zaidi.”alisema Mtanda.

 

Aidha, alisema kuwa, tusipowekeza kwenye Afya za watumishi wetu kinachofuata ni kuongezeka  kwa umaskini, kwani uwekezaji mzuri  kuliko wote ni kujali afya za watumishi.

 

“kama mnataka msitembee na dozi barabarani na kujiepusha na magonjwa nyemelezi  hakikisheni  mnajijengea tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujiepusha na changamoto hizo zinazoweza kuepukika”aliongeza Mtanda.

Naye Meneja ustawi afya ya wafanyakazi ujumuishaji na uwezeshaji kutoka benki ya CRDB makao makuu, Crescensia Kajiru alisema kuwa, walishafanya programu  hiyo katika kanda mbalimbali huku lengo likiwa ni kuisaidia serikali katika swala zima la kuimarisha afya za wafanyakazi  pamoja na kuwepo kwa  michezo na kupima afya zao  bado wanawajibika kujikita katika kuimarisha afya  za watumishi ambapo programu hiyo itafanyika kwenye matawi yao nchi nzima.

 

Alisema kuwa, wao kama wafanyakazi wa benki  lazima wachukue hatua na tahadhari katika ulaji wa chakula na kufanya mazoezi ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazochangiwa  na magonjwa yasiyoambukiza na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kujali afya za wafanyakazi wao.

 

“Tutakuwa  na mwendelezo  wa siku za afya katika matawi yetu kwani tunaamini afya ya akili ikiwa sawa ndio tutaweza kufanya kazi  kwa ufanisi katika maeneo yetu na kuwa na uwezo mkubwa katika utendaji kazi wetu.” alisema Kajiru.

 

Kwa upande wake Meneja wa benki ya CRDB   Kanda ya kaskazini, Chiku Issa alisema kuwa, wafanyakazi hao wanakaa kwenye viti muda mrefu na  ina madhara yake hivyo mazoezi ni muhimu Sana kwa afya zao na utendaji kazi wao  wa kila siku.

 

Chiku alisema kuwa, programu  hiyo ilianza tangu mwaka jana  kwa lengo la kujenga uelewa kwa wafanyakazi wake katika kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kufanya mazoezi na kujua vyakula vya kutumia ili kuongeza utendaji kazi wao.

No description available.

Meneja wa benki ya CRDB Kanda ya kaskazini,Chiku Issa akizungumza katika hafla hiyo. ( picha na Happy Lazaro).

No description available.

Meneja ustawi afya ya wafanyakazi ujumuishaji na uwezeshaji kutoka benki ya CRDB makao makuu, Crescensia Kajiru akizungumza katika siku ya kuimarisha afya (Wellness day) kwa wafanyakazi wa benki hiyo iliyofanyika katika viwanja vya chuo cha Agha Khan kilichopo Kisongo jijini Arusha. ( Picha na Happy Lazaro).

 

 

Friday, February 4, 2022

RAS PWANI AFUNGUA MAFUNZO YA Uviko -19 KWA WATOA HUDUMA SEKTA YA UTALII.

No description available.

 Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Injinia Mwanaasha Tumbo akifungua mafunzo kwa watoa huduma za utalii kuhusu mwongozo wa kukabiliana na Janga la Uviko-19.

No description available. 

Washiriki wa mafunzo kwa watoa huduma za utalii kuhusu mwongozo wa kukabiliana na Janga la Uviko-19.

......................................

Na Victor Masangu,Kibaha. 

 Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani (RAS), Injinia Mwanaasha Tumbo amefungua  rasmi mafunzo kwa watoa huduma za Utalii kuhusu Mwongozo wa kukabiliana na janga la UVIKO-19 katika Sekta ya Utalii kwenye ukumbi wa mikutano wa  Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

 

Katika ufunguzi huo ambao ulihudhuriwa na watoa huduma kutoka wilaya mbali mbali  za mkoa wa Pwani  wakiwemo  viongozi wa serikali pamoja na wataalamu wa afya.

 

  Mwanaasha alimpongeza Rais wa awamu ya sita Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya dawa za chanjo kwa wananchi lengo ikiwa ni kupambana na maambukizi ya Uviko -19.

   

Pia alisema kuwa  mafunzo hayo yataweza  kuwajengea uwezo watoa huduma za utalii namna ya kukabiliana na UVIKO 19.

 

“Kwa kweli nawapongeza Sana kwa hatua hii ya Kuja katika Mkoa wa Pwani kuwapatia mafunzo haya ambayo nina imani  yatawajengea uwezo kwa  watoa huduma za utalii  juu ya namna bora ya kukabiliana na janga la UVIKO-19 kwa kuzingatia matakwa ya kiafya na usalama.

 

 Aidha aliwataka washiriki wote wa mkoa wa Pwani ambao wameweza kupata fursa ya mafunzo hayo kuyatumia vizuri na kuwataka wawe mabalozi wazuri katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa kupata chanjo.

  

   “Kitu kikubwa ninachowaomba wale wote ambao tumeshiriki katika mafunzo haya inapaswa tumuunge mkono Rais wetu kwa vitendo kwa kuchanja ili wote tuweze kupata Kinga hii ambayo ni muhimu sana kwa afya yetu,”alisema Mwanasha.        

           

Aidha, amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzindua Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

 

Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi msaidizi Idara ya utalii nchini  Richie Wandwi  amebainisha kuwa mafunzo hayo yatafanyika nchi nzima na kwamba  yana umuhimu mkubwa  katika kuendelea kuwajengea imani watalii na ulimwengu kwa ujumla.

 

 Kadhalika alibainisha kuwa   Tanzania imedhamiria kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya kuweka mikakati kabambe ya kupambana na janga la UVIKO 19 kwa kutoa elimu pamoja na mafunzo mbali mbali kwa wananchi.

 

Pia amesema mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha kuwa Watanzania wanaofanya kazi katika Sekta ya Utalii wanakuwa salama.

 

“Kuwepo kwa changamoto ya Uviko- 19 kwa nchi yetu ya Tanzania kumeweza kupunguza idadi kubwa ya kuingia kwa watalii na kupelekea kushuka kwa uchumi na suala zima la kimaendeleo,”alisema Wandwi.

 

 Naye Mganga mkuu wa Mkoa wa Pwani  Gunini Kamba amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika kupata chanjo ili kuweza kujikinga na ugonjwa huo.

 

 Kamba alisema kuwa katika Mkoa wa Pwani bado mwamko ni mdogo hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi ili kuweza kutimiza malengo ya serikali ya kila mwanachi apatiwe chanjo.

  

Mafunzo hayo yamehusisha watoa huduma mbalimbali kutoka Mkoa wa Pwani  katika tasnia ya ukarimu na huduma za malazi na chakula kama vile katika hoteli, loji na kambi za kitalii; aina mbalimbali za waongoza watalii; watoa huduma katika shughuli za utalii wa kupanda mlima, uwindaji wa kitalii na utalii wa utamaduni; wakala wa safari za kitalii pamoja na wakala wa usafiri wa anga.