Wednesday, February 2, 2022

WAWEKEZAJI KUTOKA SAUDI ARABIA KUWEKEZA TANZANIA.

 No description available.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (katikati) akizungumza na ujumbe wa wawekezaji kutoka Kiwanda cha Pioneers Chemical Factory cha nchini Saudi Arabia wanaotembelea Tanzania kuangalia fursa za biashara na uwekezaji.Kikao hicho kilifanyika ofisini kwa Mhe. Waziri Mtumba jijini Dodoma.

....................................................

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa wawekezaji kutoka Kiwanda cha Pioneers Chemical Factory cha nchini Saudi Arabia wanaotembelea Tanzania kuangalia fursa za biashara na uwekezaji.

 

Mhe. Waziri Mulamula amekutana na Ujumbe wa wawekezaji hao ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma leo tarehe 02 February 2022. Ujumbe wa wawekezaji hao umeongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Saudia Arabia Mhe. Ali Mwadini umeelezea utayari wao wa kuja kuwekeza nchini.

Akizungumza katika kikao hicho Balozi Mulamula amewakaribisha wawekezaji hao na kuwahakikishia mazingira rafiki ya uwekezaji nchini na kwamba Tanzania iko tayari kuwapokea.

Amesema Tanzania na Saudia zina uhusiano wa muda mrefu ambao una historia ya aina yake na kwamba uwekezaji kutoka kwa kampuni hiyo ni sehemu ya kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia.

Kampuni hiyo inayomiliki viwanda mbalimbali nchini Saudi Arabia inajishughulisha na uzalishaji wa pembejeo za Killimo hususan, mbolea za kupandia na kukuzia mimea pamoja na dawa (pesticides) aina ya ‘phosphorus, nitrogen, potassium na sulfur’.

Mbali na uzalishaji wa mbolea na dawa, Kampuni hiyo pia inazalisha vifaa vya kilimo vya plastiki ikiwa ni pamoja na khusambaza bidhaa katika nchini za Saudi Arabia, ukanda wa Mashariki ya Kati na duniani kote.

 

Wawekezaji hao waliwasili nchini Januari 28, 2022  wametembelea Mikoa ya Mtwara, Lindi na Dodoma na kukutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Mikoa hiyo, wadau wa sekta binafsi na wakulima wa korosho kuzungumzia biashara na uwekezaji katika nyanja hizo. 

Wawekezaji hao wamemuhakikishia Mhe. Waziri Mulamula juu ya nia yao ya kuja kuwekeza Tanzania na kutaja maeneo ambayo ni kipaumbele chao kuwa ni madini, biashara, kilimo na mifugo.

No description available.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (katikati) akizungumza na ujumbe wa wawekezaji kutoka Kiwanda cha Pioneers Chemical Factory cha nchini Saudi Arabia (walioko kushoto) wanaotembelea Tanzania kuangalia fursa za biashara na uwekezaji.

No description available.

Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Ali Mwadini (katikati) katika kikao na Wawekezaji kutoka nchini Saudi Arabia(hawapo pichani) kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati Balozi Hemedi Mgaza na kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi Balozi Edwin Rutageruka wakati wa kikao na wawkezaji hao.

No description available.

Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Ali Mwadini akiwa nje ya jengo la Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba akizungumza na wawekezaji kutoka Kiwanda cha Pioneers Chemical Factory cha nchini Saudi Arabia aliokuja nao Tanzania kuangalia fursa za biashara na uwekezaji baada ya kumalizika kwa kikao chao na Mhe Waziri Mulamulajijini Dodoma

 

 

MBARONI KWA KUUZA JEZI BANDIA ZA YANGA

 No description available.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam ACP  Muliro Muliro akiwaonyesha waandishi wa habari jezi bandia za timu ya Yanga Afrika 1208 ambazo wamezibaini zinazotengenezwa na kusambazwa na kampuni ya GSM.

……………………

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limewakamata watu 17 kwa tuhuma za kuuza jezi bandia za timu ya Yanga Afrika 1208 zinazotengenezwa na kusambazwa na kampuni ya GSM.

Kazi hiyo ilifanyika katika maeneo mbali mbali ya Jiji Dar es salaam,lakini pia kwa kushirikiana na baadhi ya mikoa nchini kwa kipindi cha kuanzia tarehe 02.01.2022 hadi tarehe 28.01.2022.

Katika Jiji la Dar es salaam Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa watano, akiwemo Zahiri Hassan (17) Mmwera aliyekutwa huko Uwanja Benjamin William Mkapa akiwa na Jezi bandia za Timu ya Yanga 52, Kariakoo mtaa wa Agrey alikamatwa Majiba Ndahya (50) Msukuma akiwa na Jezi 124, Mohamed Ramadhani (26) Mchaga alikutwa na Jezi 86, John Staslaus (19) Mchaga alikamatwa na Jezi 39 Watuhumiwa hao waliwataja wenzao wa Zanzibar, ambapo Uwanja wa Amani watuhumiwa watatu walikutwa na Jezi bandia 36.

Jezi zingine bandia 134 zilipatikana kwa kushirikiana na Polisi Mkoa wa Tanga na Mwanza ambapo watuhumiwa tisa walikutwa na Jezi 811.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam linawatahadharishawananchi wote wanaojihusisha na vitendo vya kutengeneza, kuuza na kusambaza, bidhaa kwa kuiga au kufananisha nembo za biashara au huduma za watu wengine iliyosajiliwa kisheria, kufanya hivyo ni kosa nakinyume na sheria za nchi.

Jeshi la Polisi litashirikiana na mamlaka nyingine za kisheria ili kuona watuhumiwa wamechukuliwa hatua kali za kisheria

MULIRO J. MULIRO– ACP

KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM

DAR ES SALAM.