Sunday, October 6, 2019

BIl. 93.8 ZATUMIKA KUIMARISHA MIUNDOMBINU KATIKA SHULE 588 ZA MSINGI NA SEKONDARI.

Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza wakati alipokuwa akifungua kikao kati ya wizara hiyo na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika katika taasisi ya NACTE Mwenge jijini Dar es salaam.
..............................



Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amewapongeza waandishi wa habari kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuhabarisha Wananchi kuhusu masuala ya sekta ya elimu na Serikali kwa ujumla.


Dkt. Leonard Akwilapo ameyasema hayo wakati wa kikao kati ya wahariri wa vyombo vya mbalimbali vya habari na wizara hiyo ambapo alielezea  kiwango cha elimu nchini na kusema kinaendelea vizuri na hatua mbalimbali zinafanyika kuiboresha sekta ya elimu.
Ameongeza kuwa Dira ya wizara ni kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa.

Dkt. Akwilapo ameongeza kuwa jumla ya shilingi  Bil. 93.8 zimetumika kuimarisha miundombinu katika shule 588 za msingi na sekondari zikiwemo shule kongwe, ambapo serikali imeongeza mikopo ya elimu ya juu kutoka Tzs Bil. 424.7 mwaka 2018/2019 hadi Tzs Bil. 450 mwaka 2019/2020.

Akielezea kuhusu  makusanyo ya madeni ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu amesema yameongezeka kutoka Tzs Bil. 21.1 mwaka 2014/2015 hadi Tzs Bil. 183.2 mwaka 2018/2019 ambapo wizara inafanya mapitio ya sera ya elimu ya mwaka 2014 ili kuifanyia maboresho na kuendana na wakati.

Amewaasa viongozi wa sekta ya elimu kushirikiana na waandishi wa habari kwa uwazi ili wananchi wapate taarifa za sekta ya elimu zenye usahihi na kwa wakati.
 Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Dkt. Leonard Akwilapo katikati akimsikiliza Katibu Mtendaji wa NACTE, Dr. Adolf Rutayuga wakati alipokuwa akitoa salamu zake za ukaribisho  katika taasisi hiyo.

 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi.Sylivia Lupembe akizungumza na kumkaribisha Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Dkt. Leonard Akwilapo ili kuzungumza na wahariri wa vyombo vya habari.

 Ignas Anthony Chonya Mratibu wa Mradi wa TESP Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia akizungumza katika kikao hicho kilichoshirikisha wataalam na wakuu wa vitengo kutoka Wizara hiyo na Wahariri wa vyombo vya habari.
 Mhariri Mkuu wa Clouds Media na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari wanawake TAMWA Bi. Joyce Shebe akitoa shukurani zake kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Dkt. Leonard Akwilapo kufuatia kikao hicho.
 Makuru Petro Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia akiwasilisha mada ya sera na mipango ya wizara hiyo katika kikao hicho.
 Dkt. Lyabwene Mtahabwa Kamishna wa Elimu akiwasilisha mada kuhusu elimu ya Awali wakati wa kikao hicho.

 Baadhi ya wakuu wa vitengo na wahariri wakifuatilia mjadala huo.

 Picha mbalimbali zikionesha wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali wakiwa katika kikao hicho.

Friday, October 4, 2019

WAAJIRI WA AFYA WATAKIWA KUAJIRI WATAALAMU WA MAABARA ZA AFYA WENYE SIFA.

 
Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Bi Theresia  Mmbando, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani,  wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 33 la kisayansi pamoja na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha wanasansi wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT), mjini Bagamoyo, pembeni yake ni Rais MeLSAT, Yahya Mnung'a.
..................................

Waajiri katika sekta ya Afya Mkoani Pwani, wametakiwa kuajiri wataalamu wa Maabara za Afya, waliosomea kazi hiyo ili kupata matokeo mazuri ya vipimo vya magonjwa na tafiti mbalimbali.


Wito huo umetolewa mjini Bagamoyo na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, katika hutuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Bi Theresia  Mmbando wakati wa kufungua Kongamano la 33 la kisayansi pamoja na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha wanasansi wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT).


Amesema matokeo ya wataalamu wa maabara za Afya ndio yanayoweza kuleta mafanikio katika kutatua tatizo iwe ni ugonjwa ama utafiti wa aina mbalimbali.


Aliongeza kwa kusema kuwa, ni vyema sasa waajiri binafsi na serikali kuhakikisha wanaajiri wataalamu wa Maabara za Afya wenye sifa ili kuepuka kupata majibu yasiyo sahihi wakati wa vipimo.


Aidha, amewataka wataalamu hao wa maabara za Afya kutumia vifaa vilivyopo kwa usahihi ili waweze kutoa majibu kwa yaliyo sahihi.


Ametoa wito pia kwa wataalamu hao kujiunga na Chama cha wanasayansi wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT) ili kujadili mambo kwa pamoja na kuweza kuyapatia ufumbuzi wa kitaalamu.


Awali, Rais wa Chama cha wanasayansi wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT) Yahya Mnung'a akisoma hutuba ya chama chao kwa mgeni rasmi, ameiomba serikali kuwepo na kurugenzi ya Maabara ili kuboresha huduma za uchunguzi na utoaji wa huduma za afya.


Alisema katika Mkutano wa Shirika la Afya Duniani, uliofanyika Maputo Msumbiji mwaka 2008, ambapo Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Afya (wakati huo) yapo mambo waliyokubaliana katika mkutano huo.


Alibainisha kuwa, miongoni mwa mambo waliyokubaliana ni pamoja na kila nchi mwanachama ianzishe Kurugenzi ya Maabara ili kuboresha huduma za Uchunguzi na utoaji wa huduma bora za Afya.


Aidha, katika hutua nyingine, Mnung'a  alisema wanaishukuru serikali kwa kuendelea kuimarisha mafunzo ya Maabara za Afya hapa nchini na kuruhusu taasisi binafsi kutoa mafunzo katika ngazi mbalimbali za taaluma hiyo.


Hata hivyo, Rais huyo wa MeLSAT alisema lipo tatizo kubwa katika muundo wa mishahara ya wateknolojia wasaidizi na wanasayansi wa maabara za Afya wa mwaka 2009.


Alisema kuwa, toka kuanzishwa kwa kozi ya stashahada ya juu ya sayansi za maabara za Tiba 1993, hakuna muundo na Daraja la mshahara kwa mtaalamu wa maabara aliyemaliza ngazi hiyo.  


Washiriki wa Kongamano hilo wamesema kukutana kwao kunasaidia kujadili kwa pamoja changamoto zinazowakabili wataalamu wa maabara za Afya na kuona namna ya kuwasilisha mapendekezo yao kwa watunga sera.


 Kongamano la 33 la Kisayansi limeambatana na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa wa Chama cha wanasayansi wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT) ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni "Jukumu la Maabara za Afya katika utoaji wa huduma zilizo bora"
 
Mgeni rasmi katika Kongamano hilo, Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Bi Theresia  Mmbando, (wa tatu kulia) akiwa meza kuu na viongozi waandamizi wa maabara za Afya nchini katika Kongamano la 33 la kisayansi pamoja na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha wanasansi wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT), mjini Bagamoyo.

 Mgeni rasmi katika Kongamano hilo, Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Bi Theresia  Mmbando, (wa tatu kulia)akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Kongamano la 33 la kisayansi pamoja na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha wanasansi wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT), mjini Bagamoyo. 
 Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Bi Theresia  Mmbando, (katikati) akisalimiana na washiriki wa Kongamano la 33 la kisayansi pamoja na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha wanasansi wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT), mjini Bagamoyo.