Thursday, July 4, 2019

WANNE WAFARIKI AJALI YA GARI LINDI.

Muonekano wa Gari aina ya Haice yenye Namba za usajili T239 DMA, baada ya kupata ajali  katika Mtaa wa Mto Mkavu ,kata ya Mbanja Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mkoani humo ikiwa inatokea Kijiji cha Kiranjeranje wilayani kilwa ikielekea Mjini Lindi. 
................................... 

NA HADIJA HASSAN 04/07/2019 LINDI

Watu Wanne (4) wamefariki Dunia na wengine 10 kujeruiwa baada ya Gari aina ya Haice yenye Namba za usajili T239 DMA kugonga kwa nyuma Tela lenye namba za usajili T747 DKA la Lori lenye Namba za usajili T176 DKA Mali ya Kampuni ya Saruji ya Dangote.


Ajali hiyo imetokea majila ya saa moja na nusu usiku wa Tarehe 02/07/2019 katika Mtaa wa Mto Mkavu ,kata ya Mbanja Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mkoani humo ikiwa inatokea Kijiji cha Kiranjeranje wilayani kilwa ikielekea Mjini Lindi.


Gari hiyo inamilikiwa na mohamedi juma hamisi mkazi wa Manispaa ya Lindi na inafanya safari zake katika Manispaa hiyo na kwenda kiranjeranje wilayani kilwa Mkoani humo.


Nae Abdurahman Shabani Mwenyekiti wa Mtaa wa Mto Mkavu alisema kuwa kabla ya Ajali hiyo kutokea Dereva wa Gali ya Dangote alisimamisha Gari yake pembezoni mwa Barabara ambapo inasadikika alikuwa anafanya marekebisho ya Gari yake ndipo Gari hiyo ya Haice ikaenda kuligonga lori hilo kwa nyuma.


“kabla ya ajali kutokea Yule Dereva wa Dangote alipaki Gari yake kwa ajili ya kufanya marekebisho madogo ndipo Haice ile ikaja kugonga kwa nyuma kwa pembeni baadae ikayumba na kuangukia kichakani ambapo licha ya kugonga lakini pia ilikanyaga miguu ya Dereva wa Dagote ambae alikuwa chini ya Gari yake akifanya marekebisho hayo” alisema Shabani.


BAGAMOYO KWANZA BLOG ilifika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine ambapo ilikutana na Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Jumanne Shija, ambapo alithibitisha kupokea majeruhi kumi(10) na miili ya Marehemu wanne(4) wa ajali ya Gari siku ya jumanne majira ya saa mbili na nusu usiku.


Alisema kati ya majeruhi hao kumi waliowapokea Mmoja akiwa ni mtoto wa kike, wawili waliwatibu na kuwaruhusu kurudi majumbani kwao, sita walibaki hospitalini kwa ajili ya kuendelea na matibabu na wawili kulingana na majeraha waliyonayo walilazimika kuwapa rufaa kwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu zaidi Kuhusu miili ya Marehemu waliowapokea katika Hospitali hiyo.


Shija, alisma Madaktari wameshaifanyia uchunguzi pamoja na kuwatambua Marehemu hao ambapo wanawasubiri Ndugu wa marehemu kwa ajili ya kuwachukuwa.


Nao Baadhi ya majeruhi waliokuwa katika Ajali hiyo akiwemo Robson Moleli na Selemani Sabiini walidai kuwa chazo kikubwa cha kutokea kwa Ajali hiyo ni mwendo mkali wa Gali hiyo ya Haice ambayo ilikuwa inakimbizana na Gari nyingine aina ya costar hali ambayo Dereva wa gali hiyo alishindwa Kuchukuwa tahadhari ya haraka ya kuliweka sawa gari yake mara moja baada ya kuliona Lori lililokuwa limesimama mbele yake.


Sabiini alisema kwa Madereva wa Magari Madogo kwenda mwendo wa kasi na kukimbizana ni kawaida yao , mara nyingi wanadai kuwa wanakimbilia Abiria katika vituo vya Magari vinavyofuata lakini cha ajabu kwa siku hiyo ya jana hakukuwa na shida ya abilia maana magali yote yalipata abiria mpaka wengine waliwaacha kwa kushindwa kuwabebe katika stendi ya Mchinga” alisema.


“Ila kikubwa baadhi ya madereva hawa wanapenda ushindani usio na maana wanakuwa na michezo ya kupima uwezo wa gari kutembea bila kujua kwamba wamebeba dhamana za Roho za watu katika magari yao” aliongeza.


Nae moleri alisema kuwa kutokea kwa ajali hiyo kumeathiri kwa kiasi kikubwa katika shuguli zake za kiuchumi kwani kutokana na kulazwa Hospitalini hapo atashindwa kufanya biashara zake za kila siku.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Pudensiana Protas alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa chanzo cha Ajali hiyo ni Dereva wa Haice kushindwa kuchukuwa Tahadhari baada ya kulikuta roli na baadae kuligonga kwa nyuma hali iliyosababisha vifo na majeruhi kwa abiria waliokuwepo kwenye gali hiyo.


Kamanda Protas pia aliyataja majina ya Marehemu katika Ajali hiyo kuwa ni Hasani Omary (45) Msambaa mkazi wa Dar es salaam, Abdallah Musa Ngalawa (25) Mmakonde Kondakta wa Haice hiyo Mkazi wa Lindi Mjini, Muhibu Abdallah (Kampunda) Mkazi wa Kariakoo Lindi Samweli Warioba Mkazi wa Mpilipili Lindi.


Hata hivyo Kamanda Protas aliwataja Majeruhi wa Ajali hiyo kuwa ni Selemani Saidi ( 67) Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Abdallah Mambo (36) Dereva wa Gari ya Dangote mzigua mkazi wa Dar es salaam, Mwanaidi Hassani (5) Mkazi wa Ng’apa Lindi, Robson Moleri (25) Mmasai Mkazi wa Kariakoo Lindi.


Wengine ni Ally Isumail (41) Mndengeleko Mkazi wa Lindi Majeruhi wengine ni Shufaa Bakari(21) Mwera Mkazi wa Ng’pa Lindi, Angetus Kajuni (20) Mnyakyusa Mkazi wa Manspaa ya Lindi, Saidi Saidi (30) Mkazi wa Manispaa ya Lindi, Yusuph Saidi(36) Mmwela Mkazi wa Lindi, Azizi Tehabu(41)
 
Majeruhiwa ajali hiyo wakipata huduma ya matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi.

 Muonekano wa Gari aina ya Haice yenye Namba za usajili T239 DMA, baada ya kupata ajali  katika Mtaa wa Mto Mkavu ,kata ya Mbanja Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mkoani humo ikiwa inatokea Kijiji cha Kiranjeranje wilayani kilwa ikielekea Mjini Lindi.
 
Wahudumu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, wakitoa matibabu kwa majeruhi.
 
 Askari wa usalama barabarani mkoani Lind, akiwajibika kupima eneo lililotokea ajali


Tuesday, July 2, 2019

VIJIJI 10,278 KUFIKIWA NA UMEME

Image may contain: Subira Mgalu, smiling, standing and closeup
Na Omary Mngindo, Bagamoyo.

SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati imeeleza kuwa, Shirika la Umeme nchini Tanesco mpaka Juni mwaka 2020, vijiji vipatavyo elfu 10,278 vitakuwa vimeshaunganishiwa na huduma ya umeme.

 
Aidha kwenye zoezi hilo la uunganishwaji wa huduma hiyo, katika mpango uliowekwa na serikali unataraji kwamba mpaka ifikapo mwaka 2021 vijiji vyote vilivyobakia 1,990 vitakuwa vimefikiwa na huduma hiyo.


Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, akizungumza na wakazi wa Kitongoji cha Fitina Haina Posho, Kijiji cha Fukayosi wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, ambapo alisema kwa sasa nguvu kubwa imeelekezwa maeneo yaliyopitiwa na umeme mkubwa.


"Usambazaji wa miundombinu ya umeme ina gharama kubwa sana, kilometa moja inagharimu kiasi cha shilingi milioni 50, mpaka kuufikisha hapa sekondari yetu ya Fukayosi mradi huu umegharimu zaidi ya milioni miamoja," alisema Mgalu.


Ameongeza kwamba mwanzoni umeme ulivyofika katika maeneo ya Mwavi, Mkenge, Kidomole na sehemu nyingine, ilitakiwa REA iikabidhi mradi huo Tanesco ili kazi iendelee kwa kuanzia shilingi 170,000, 300,000 mpaka 500,000 kulingana na uhitaji wa nguzo.


Mgalu ametanabaisha kwamba, Tanesco haikuwa na ukiritimba wa kusambaza umeme, isipokuwa changamoto iliyokuwepo wakati huo ni uwezo wa kumudu gharama za uunganishaji wa huduma kwa wananchi.


"Mwaka huu wa fedha 2019/2020 Tanesco wameweka kipaumbele cha kuzalisha umeme wa ziada megawati 300 ukilinganisha na mwaka 2015 ambapo tulikuwa na mapungufu ya megawati 100 kwa siku," alisema Mgalu.


Ally Ally Mwenyekiti wa halmashauri ya Bagamoyo ambae pia ni Diwani wa kata ya Fukayosi, alielezea changamoto zilizokuwepo awali shuleni hapo, zikiwemo umeme, barabara na maji, ambapo CHALIWASA waliweza kupeleka maji, pamoja na wadau wengine wakiwemo taasisi ya Goodneighbour pamoja na halmashauri.


Meneja wa Tanesco wilayani Bagamoyo Kidada Maeda alisema kuwa maeneo mengi hayajafikiwa na umeme na kwamba ofisi yake imelichukua hilo na wataliingiza katika mpango wa ujazilizi, pia wataiingiza katika REA awamu ya 3 sehemu ya 2.


Nae Mwenyekiti wa Kamati ya shule Josefa Lyimo ameshukuru taasisi ya Goodneighbour kwa msaada mkubwa unaopatikana shuleni hapo, huku akiomba umeme usambazwe kukabiliana na changamoto ya wizi, sanjali na kulilia hostel shuleni.

RIPOTI YA CAG, HALMASHAURI YA BAGAMOYO YAPATA HATI SAFI.

Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imefanikiwa kwa mara nyingine tena kupata hati safi (Unqualified Audit Opinion) kwa Mwaka wa fedha 2017/2018, ikiwa ni mara ya tatu mfululizo kwa Halmashauri ya Bagamoyo kupata hati safi.


Hayo yamesemwa jana Julai 01,2019 na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali Mkoa wa Pwani Bi. Mwajuma Mohamedi alipokuwa anawasilisha taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa halmashauri ya Bagamoyo.


Bi. Mwajuma amelieleza baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuwa, kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977 (Rev 2005) ibara ya 143 na sheria ya ukaguzi wa umma namba 11 ya 2918 kifungu cha 10 (1) ni jukumu la la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kufanya ukaguzi wa taarifa za mapato na matumizi ya fedha za umma Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Idara na mashirika ya umma.


Aliongeza kuwa, baada ya ukaguzi huo anatakiwa kutoa matokeo ya ukaguzi na mapendekezo kutokana na ukaguzi huo na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na menejimenti zilizopo kwa mujibu wa sheria.


Zaidi Bi. Mwajuma alisema, "Katika ukaguzi uliofanyika kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imepata hati safi na kufanya halmashauri hiyo kuendelea kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo, kwani kwa Mwaka 2017/2018, mwaka 2016/2017 na mwaka 2015/2016 Bagamoyo imepata hati safi ya Mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG)”.


Nae Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Theresia Mbando akizungumza katika mkutano huo maalum wa baraza la Madiwani amesema, ni jambo la kujivunia kwa Halmashauri na Mkoa wa Pwani kwa Bagamoyo kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo, na kusisitiza kwamba maelekezo na mapendekezo yaliyotolewa na Mkaaguzi na mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) katika ripoti yake iliyowasilishwa katika mkutano huo, yafanyiwe kazi ili kuondoa kasoro ndogondogo zilizoonekana kipindi ukaguzi ulipofanyika, ili Halmashauri iendelee kupata hati safi miaka ijayo.


Bi. Theresia Mmbando pia ametumia nafasi hiyo, kuwaasa Madiwani na Wataalam wa Halamshauri kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na kuongeza ubunifu katika kuanzisha vyanzo vipya vya mapato kwa kutilia mkazo uandishi wa maandiko ya miradi ya kimkakati inayofadhiliwa na Serikali kuu kwa sasa, itakayoisaidia Halmashauri kuongeza mapato yake ya ndani.





Akifunga Mkutano huo wa Baraza la madiwani, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Said Ngatipura amesema, watahakikisha wanasimamia mapendekezo yote yaliyotolewa kwenye ripoti ya Mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa Serikali na kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo inaendelea kufanya vizuri.
 
 Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali Mkoa wa Pwani Bi. Mwajuma Mohamedi akifuatilia Kikao maalum cha Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo kwaajili ya kupokea taarifa ya mkaguzi wa hesabu za serikali.
  Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Theresia Mbando akizungumza katika mkutano huo.
 
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Said Ngatipura akifunga mkutano huo.

MAGAZETI YA LEO JULAI 02, 2019.