Tuesday, April 2, 2019

MWENGE WA UHURU 2019 WAWASHWA RASMI SONGWE.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasha Mwenge kuashiria kuzinduliwa kwa mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Mlowo mkoani Songwe.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Mwenge kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa kwa mwaka 2019 Ndugu Mzee Mkongea Ali kutoka Mjini Magharibi kuashiria kuanza kwa mbio za Mwenge wa Uhuru 2019.


Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
....................................


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa Wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutumia mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2019 kumkumbuka Baba wa Taifa kwa kupinga vitendo vya dhulma, ufisadi, rushwa, maradhi, chuki, dharau na kuwataka kuenzi umoja na mshikamano wetu kuchapakazi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.


Makamu wa Rais ameyasema hayo leo kwenye sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge Kitaifa zilizofanyika kwenye uwanja wa Mlowo mkoani Songwe na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.


Kaulimbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 ni “Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke  kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”


“Nimependezwa na kaulimbiu hii ambayo inauwiano wa moja kwa moja na jukumu langu la kila siku la kusimamia na kutunza mazingira ya nchini. Sote tunafahamu kuwa bila utunzaji thabiti wa mazingira basi vyanzo vya maji hupotea”alisema Makamu wa Rais


Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama nchini inaendelea kuimarika ambapo huduma ya maji vijijini  imeongezeka kutoka wastani  wa asilimia 58.7 kwa mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 64.8 mwezi februari 2019 na miji mikuu ya mikoa kutoka asilimia 78 mwezi machi 2018 mpaka asilimia februari 2019.


“Niwahakikishie wananchi tutatekeleza kwa vitendo ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inayotutaka kuboresha huduma ya maji vijijini kufikia asilimia 85 na mijini kwa asilimia 95 ifikapo 2020”alisisitiza Makamu wa Rais 

 
Aidha, Makamu wa Rais kupitia hadhara ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019 ametoa wito kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji, ujenzi, ukataji na uchomaji miti kwenye vyanzo vya maji.


Makamu wa Rais pia amewakumbusha wananchi juu ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwezi oktoba 2019 kuhakikisha wanachagua Viongozi wachapakazi na wenye dhamira ya maendeleo kwa jamii.


Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 zitaongozwa na Ndugu Mzee Mkongea Ali kutoka Mjini Magharibi

MGUMBA ATAKA USHIRIKA UCHUKUE MIKOPO KWAAJILI YA WAKULIMA.

Naibu waziri wa Kilimo Mhe. Omari T. Mgumba (Mb)  akiwa ofisi ya mkuu wa mkoa wa arusha alipokutana na wataalamu wa kilimo ,ushirika na umwagiliaji kabla ya kuanza ziara ya kuzungukia  maeneo mbalmbali mkoani hapo.
...............................


Bashiri Salum,Wizara ya Kilimo Arusha


Vyama vya Ushirika vimeshauriwa kukopa fedha kwenye Mabenki kwa ajili ya  wanachama wao kwa kuwa waliowengi hawakopesheki hivyo kufanya shughuli za kilimo kuwa ngumu.


Akizungumza katika kikao kilicho wakutanisha Maafisa Ushirika, umwagiliaji na afisa kilimo  Mkoani Arusha Naibu Waziri Kilimo Mhe. Omari Mgumba amesema miundombinu mingi ya umwagiliaji inahitaji marekebisho makubwa  ili kuweza kutumiwa na wakulima.


Aidha miundombinu hiyo imekosa ukarabati kutokana na wakulima kutokuwa na mitaji ya kutosha na kutoaminiwa na taasisi za fedha kusaidia ukarabati huo.


Ameshauri tume ya Ushirika kuvisimia vyama vya ushirika ili viweze kukopa fedha Benki Kwa ajili ya wanachama lengo likiwa ni kufanya ukarabati Wa miundombinu ya umwagiliaji ambapo kila mwanachama atawajibika kuchangia huduma hiyo.


Hatuwezi kufanya Kilimo cha kibiashara Kwa kutegemea mvua ambazo Nazo zimekuwa haziyabiriki nawashauri tume ya Ushirika na tume umwagiliaji kusimamia vyama hivyo kwenye skimu mbalimbali za umwagiliaji kukopa fedha ambazo zitatumika kurekebisha miundombinu ya umwagiliaji badala ya kutegemea serikali, alisema Mhe. Naibu Waziri.


Naibu Waziri aliwataka maafisa ugani kuwafikia wakulima na kuelimisha namna ya kutumia na kutoa elimu juu ya matumizi bora ya viuatilifu vya mimea ili kupambana na visumbufu vya mazao ambavyo vimekuwa vikimsababishia mkulima hasara kubwa.


Naye afisa Umwagiliaji wa kanda mhandisi Juma Mdete amesema katika ukanda huo eneo ambalo linafaa kwa kilimo cha umwagiliaji ni hekta elfu 40 kati ya hilo linalotumika ni  hekta elifu 24 tu.


Amesisitiza kwamba pamoja na matumizi kidogo ya eneo la umwagiliaji lakini maeneo yanayomwagiliwa yanasaidia upatikanaji wa chakula wakati wa ukame.


Akichangia wakati wa mjadala huo Afisa Kilimo Mkoa wa Arusha Bwana Daniel Loiruck amethibitisha kwamba ukiondoa Magonjwa ya mlipuko na uvamizi wa visumbufu vya mimea  maafisa kilimo wamekuwa wakijitahidi kuwafikia wakulima ili kutatua changamoto zinazowakabili.


Naye mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoani Arusha bwana Loata Erasto Sanare  akamueleza Mhe. Naibu waziri kwamba hali ya ukame mkoani humo ni kubwa hivyo kuishauri serikali kuanza kufikiri njia mbadala ya kupambana na hali hiyo.


Msimu wa kilimo upo katikati lakini mpaka sasa hakuna mvua na tumezunguka sehemu mbalimbali hapa arusha mahindi yamekauka hata mvua ikinyesha  haiwezi kuleta mabadiliko tunaishauri serikali kufikiri mbinu za kukabiliana na hali hiyo’. Alisisitiza bwana Loata  Sanare