Tuesday, March 5, 2019

TUMEJIPANGA KUIMARISHA USAMBAZAJI WA PEMBEJEO, MBEGU BORA NA VIUATILIFU – MHE HASUNGA

Mgeni rasmi-Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza umuhimu wa mbegu bora za kilimo wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Mpango wa kuimarisha Mitandao ya Usambazaji wa Mbegu na Viuatilifu, katika ukumbi wa Usungilo Hoteli Jijini Mbeya, Tarehe 5 Machi 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).
..........................

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mbeya

Uimarishaji wa mitandao ya usambazaji mbegu na viuatilifu ni muhimu katika kuhakikisha tija inaongezeka katika Uzalishaji wa mazao yote hususani nafaka, matunda mbogamboga na mbegu za mafuta.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 5 Machi 2019 wakati akizindua Mpango wa kuimarisha Mitandao ya Usambazaji wa Mbegu na Viuatilifu, Mpango unaotekelezwa na Mradi wa NAFAKA na Kampuni ya Kimataifa ya CORTEVA katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini nchini Tanzania.


Katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Usungilo Hoteli Jijini Mbeya Mhe Hasunga alisema kuwa kuimarisha usambazaji mbegu na viuatilifu utamsaidia mkulima kuwa na uhakika wa chakula na kuongeza pato lake hivyo kuchangia katika kuipeleka Tanzania kufikia Uchumi wa Kati kama inavyoeleza sera ya Serikali ya awamu ya tano inayongozwa na Mhe Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Alisema wakulima nchini Tanzania wanategemea Sekta ya kilimo kuchangia katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi, kwa kuwa inatoa ajira kwa asilimia 65 ya wananchi, ina uwezo wa kutoa malighafi ya viwanda kwa asilimia 66 na inachangia asilimia 100 ya chakula kinachopatikana.


Alisema kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya II yaani Agricultural Sector Development Program – ASDP II inaolenga kuleta Mapinduzi katika sekta ya kilimo.


Programu hiyo ya miaka kumi (10) imeanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2018 na inafanyia kazi maeneo ya Usimamizi endelevu wa ardhi na maji, Kuongeza Tija (kuongeza matumizi ya pembejeo), Kuongeza masoko na kuongeza thamani ya mazao, Kuboresha mazingira ya uwekezaji katika kilimo. Hivyo, Uimarishaji wa Mpango wa Kusambaza Pembejeo na Viuatilifu ni moja ya shughuli muhimu katika Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo -ASDP 11 katika kuongeza tija.


“Ni Imani yangu kuwa, kufanikiwa kwa kazi hii ya Mradi wa Nafaka ni kufanikiwa katika utekelezaji wa sehemu ya Programu ya Kuendeleza Kilimo nchini ASDP II. Mradi huu pia utaendelea kuimarisha mahusiano yaliyopo baina na Serikali na Sekta nafsi katika kuendeleza kilimo nchini” Alisema


Kadhalika, Hasunga alisema Serikali inatambua mchango unaotolewa na Shirika la Misaada la Marekani USAID katika miradi mbalimbali husasani katika sekta ya kilimo. Mradi wa NAFAKA ni moja ya michango ya Shirika la USAID katika kuongeza tija kupitia Mashamba darasa, Uendeshaji wa Vikundi na vyama vya wakulima, Kuongeza thamani kwenye usindikaji wa Mahindi kwa njia ya virutubishi kwenye unga, Kuunganisha wakulima na huduma za kifedha Masoko na Bima ya Mazao yaani “Crop Insurance”.


Alisema kuwa Shughuli hizo zinazotekelezwa na Mradi wa NAFAKA kwa kushirikiana na CORTEVA  unaenda sambamba na jitihada za Wizara ya Kilimo katika kuendeleza kilimo. Moja ya maeneo ya kipaumbele yanayotekelezwa na Wizara ni kuongeza tija katika uzalishaji kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, na kuimarisha huduma za ugani.


Maeneo mengine ya Kipaumbele ya Wizara ya Kilimo ni Kutungwa kwa sheria ya kilimo ili kusimamia kilimo, Kuandikisha wakulima wote, Kuongeza uzalishaji wa sukari kuondoa upungufu wa sukari nchini, Kufungamanisha uzalishaji na mahitaji ya viwanda ili kutoa mali ghafi ya viwanda kwa kuongeza uzalishaji, Kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta, Kuanzisha scheme za umwagiliaji ili kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji, Wakulima kuwa na bima ya mazao, na Kuongeza fursa za upatakanaji wa fedha kwa wakulima.


“Ni jambo la faraja kuona sekta binafsi sasa zinatoa mchango katika jitihada za Serikali katika kutoa mafunzo kwa wakulima kwa kuanzisha mashamba darasa, kutoa mafunzo kwa maafisa ugani, kusimamia na kuhimiza matumizi ya mbegu bora na viuatilifu pamoja na kufanya kazi na mawakala wa pembejeo wa daraja la kati na wadogo waliopo vijijini wapatao” Alikariirwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa.


“Ni jambo la kutia moyo kuwa mpango huu utasaidia usambazaji na upatikanaji wa viuatilifu vya kupambana na visumbufu vya mlipuko vikiwemo viwavi jeshi vamizi “Fall Army Worms” katika maeneo yaliyovamiwa kwenye Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini nchini mwetu”


Aidha, alisema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika kilimo ikiwa ni pamoja na kufanya mapitio katika taratibu zilizowekwa katika uzalishaji, usambazaji na uingizaji wa mbegu ili kurahisisha upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima nchini.


Katika suala la soko la mahindi Serikali imesharekebisha suala hil0 na itaendelea kutoa taarifa za hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha taratibu za masoko ya mazao ili wakulima, wafanyabiashara na wadau waweze kunufaika na uwekezaji katika sekta ya kilimo.


Sambamba na hayo pia Waziri Hasunga alisema kuwa serikali itaweka msisitizo katika sekta ndogo ya ardhi ili wakulima kuona umuhimu wake na kuondokana na kilimo kinachotegemea mvua.
 Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Mpango wa kuimarisha Mitandao ya Usambazaji wa Mbegu na Viuatilifu, katika ukumbi wa Usungilo Hoteli Jijini Mbeya, Tarehe 5 Machi 2019.

 Sehemu ya washiriki wa uzinduzi wa Mpango wa kuimarisha Mitandao ya Usambazaji wa Mbegu na Viuatilifu katika ukumbi wa Usungilo Hoteli Jijini Mbeya wakifatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) Tarehe 5 Machi 2019.

 Sehemu ya washiriki wa uzinduzi wa Mpango wa kuimarisha Mitandao ya Usambazaji wa Mbegu na Viuatilifu katika ukumbi wa Usungilo Hoteli Jijini Mbeya wakifatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) Tarehe 5 Machi 2019.

FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY YABADILI NEMBO YAKE, NA HUU NDIO MUONEKANO WA NEMBO YAO MPYA


 Vicent Macha
Dar es salaam
Baada ya zaidi ya muongo mmoja na nusu kufikia Azaki nchi nzima, Sasa Foundation for Civil Society (FCS) inajikita katika kuongeza ufanisi na juhudi za kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wote katika kuleta maendeleo.

Baada ya uzinduzi huu ndio muonekano wa Nembo mpya ya Foundation for Civil Society (FCS).
Hayo yameelezwa mapema jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Bw. Francis Kiwanga wakati wa uzinduzi nembo mpya ya shirika hilo ambayo itaendana na mabadiliko na mfumo wake wa utendaji.

Alisema kuwa hii itahusisha kushirikiana na taasisi zote za Serikali, Bunge, Sekta binafsi, Asasi za kiraia (AZAKI) ili kufikia Maendeleo Endelevu ya Dunia pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa kuboresha maisha ya watanzania ifikapo 2025.

Aidha aliongeza kuwa kwa sasa FCS itatoa ruzuku kwa wastani wa Asasi 150 kwa pande zote mbili za muungano yaani Tanzania Bara na Visiwani kila mwaka, ambapo hapo awali ilikuwa ikitoa kwa Azaki zaidi ya 5500 zilizokuwa zikihudumia wananchi wa mikoa yote hapa nchini.

Alisisitiza kuwa kiasi cha ruzuku kitaongezeka na kwa sasa taasisi hiyo itatoa ruzuku zenye thamani ya billion 11. kwa mwaka na muda wa mkataba pia utakuwa mrefu hadi kufikia miaka miwili ili kupata matokeo mazuri kwa miradi itakayofadhiliwa na FCS.

Akieleza sababu ya kufanya hivyo alisema kuwa wamejikita katika eneo la utawala bora na maendeleo hivyo siyo rahisi kuboresha maeneo hayo kwa mkataba wa mwaka mmoja au miezi sita tu, Hivyo wameona kuna haja ya kuongeza mkataba na kiwango cha ruzuku katika kufanikisha hili.

Na mwisho kabisa alipenda watu wafahamu kuwa FCS ipo kwa ajili ya watanzania hivyo waondoe mila potofu ya kuwa ni chombo ambacho hakina ubia na serikali na kwa sasa watafanya mambo mengi mazuri kwa kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania.


            Mazungumzo ya azaki yanaendelea kupitia hastag hizi.

                                        #AZAKITanzania  / #CivilSocietyTanzania 


Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society Bw. Francis kiwanga akitoa maana ya kitu kimoja baaba ya kimoja katika nembo ya kwanza ya shirika hilo kabla ya kuzinduliwa kwa nembo mpya.


Zoezi la uzinduzi wa nembo mpya ya Foundation for Civil                                        Society likifanyika.
Baadhi ya washiriki kutoka AZAKI mbalimbali hapa nchini wakifuatilia matukio yanayoendelea katika Tafrija hiyo ya Uzinduzi wa nembo mpya ya FCS.

Baada ya Uzinduzi wa nembo mpya ya FCS kulifuatiwa na tukio lingine la uzinduzi wa tovuti mpya (Website) mpya ya shirika hilo kama inavyoonekana pichani.
Washiriki wa semina wakiendelea kusherehekea tafrija.

Picha ya pamoja ya wafanyakazi wa shirika la Foundation For Civil Society. 

Wafanyakazi wa Foundation for Civil Society wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Tafrija hiyo, Ambao pia ni wana AZAKI wanaofanyanao kazi kupitia miladi mbalimbali wanayoiendesha.

RC MTAKA ATOA WITO KWA WANAWAKE KUHIMIZA JAMII KUSOMESHA WATOTO ILI KUONDOKANA NA MILA POTOFU


 Mkuu wa  Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akiimba pamoja na Kwaya ya Upendo kutoka Kanisa la Anglikana Musoma katika Siku ya maombi ya Dunia yaliyofanyika Machi Mosi, 2019 katika Viwanja vya Parokia ya Yohana Mbatizaji Nyamiongo Musoma kwa kujumuisha wanawake wa madhehebu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake WaKatoliki Tanzania(WAWATA)  . 
 Mkuu wa  Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) na Askofu Jimbo Katoliki la Musoma Mhashamu Michael Msongazila wakifurahia jambo katika Siku ya maombi ya Dunia yaliyofanyika katika Viwanja vya Parokia ya Yohana Mbatizaji Nyamiongo Musoma kwa kujumuisha wanawake wa madhehebu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake WaKatoliki Tanzania(WAWATA)  , Machi Mosi, 2019.
Mkuu wa  Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka( wa pili kushoto), viongozi wa Kanisa na baadhi ya viongozi wa wanawake wakiwa  ibada ya siku ya maombi ya Dunia yaliyofanyika Machi Mosi, 2019 katika Viwanja vya Parokia ya Yohana Mbatizaji Nyamiongo Musoma na  kujumuisha wanawake wa madhehebu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA) 
Na Stella Kalinga, Mara
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa wanawake, kuwa mstari wa mbele kuhimiza jamii juu ya umuhimu wa kuwasomesha watoto, ili kuondokana mila potofu  zilizopitwa na wakati, ukiwemo ubaguzi wa kijinsia na mfumo dume.
Mtaka ametoa wito huo, wakati wa siku ya maombi ya Dunia yaliyofanyika Nyamiongo  Manispaa ya Musoma Mkoani Mara ambako alikuwa mgeni rasmi, ambayo yaliwahusisha wanawake kutoka katika madhehebu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA).
Amesema suluhisho la mila potofu zilizopitwa na wakati kama mfumo dume, ubaguzi wa kijinsia na kuona watoto wa kiume ni bora kuliko wa kike ni kuwasomesha watoto wote pasipo kujali kuwa ni wa kike au wa kiume.
“Ukisomesha watoto wako vizuri wakafanikiwa kwenye hiyo nyumba hakuna atakayesema yeye ni bora zaidi ya mwenziye, hakuna atakayesema mimi ndiye mwanaume kwenye hii nyumba na huyu ni  mwanamke, somesheni watoto hayo mambo yote yaliyopitwa na wakati yataisha” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amewaomba wanawake na waumini wote wa ujumla kuendelea kuliombea Taifa, Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wengine, ili nchi iendelee kuwa na amani na viongozi waweze kufanya mazuri yaliyokusudiwa kwa ajili ya Watanzania wote.
Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa viongozi wa madhehebu ya dini pamoja na kusimamia kiroho wawe msaada kwa makundi mbalimbali yaliyomo makanisani hususani vijana na wanawake, ili yaweze kuendesha miradi ya maendeleo itakayowasaidia kubadilisha maisha yao kiuchumi.
Baadhi ya wanawake walioshiriki katika Maombi ya dunia baada ya kusikia hotuba ya Mkuu  wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ambaye alikuwa mgeni rasmi wamesema watahakikisha wanasimamia vema malezi ya watoto wao na kuhakikisha wanasoma huku wakiunga mkono wazo la vikundi kuwa na miradi ya maendeleo.
“ Kama mama nimejifunza mengi; moja ni kuwa tukiwasomesha watoto wetu hakutakuwa na unyanyasaji, mfano kama kuna watu wanafanya ukeketaji kwa watoto wa kike, jamii ikielimika haya hayatakuwepo na tutahakikisha wanasoma mpaka vyuo vikuu; ujasiriamali nao tutafanya ili tujikwamue kwenye umaskini” Devotha Charles mshiriki kutoka Mwisenge
“Baadhi ya wanawake katika makanisa yetu tulikuwa hatua miradi na wengine waliokuwa nayo  ilikuwa  inaenda kwa kusuasua, lakini baada ya ujumbe tulioupokea leo nina hakika utaleta mwamko kwa wanawake wengi kuanzisha miradi ya kuwasaidia kupata kipato” Jackline Cheche mshiriki kutoka Parokia ya Nyamiongo Musoma.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Mhashamu Michael Msongazila amesema maombezi kwa ulimwengu yaendelee kufanyika ili watu waweze kuheshimu uhai wa mwanadamu.
“Ombeeni ulimwengu uheshimu uhai wa mwanadamu tumeumbwa katika sura na mfano wa Mungu, tumekabidhiwa dhamana hiyo ya uumbaji, uhai huu tuulinde tuutetee na tuukuze kwa ajili ya kujenga ulimwengu, maisha yetu yana nafasi ya pekee yanapokuwa na Mungu” alisema Askofu Mlonganzila.
Maombi ya Dunia kwa wanawake wa madhehebu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA) hufanyika kila mwaka Machi Mosi yakiwa na lengo la kuombea familia, Taifa na Dunia kwa ujumla juu ya amani na mahitaji mengine.
MWISHO

MAGAZETI YA LEO MACHI 05, 2019.