Friday, March 1, 2019

MIPANGO YA SERIKALI KUHUSU GESI YA KUSINI IKO PALEPALE – MGALU

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza wakati wa hafla ya uwashaji rasmi wa umeme katika kijiji cha Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini, akiwa katika ziara ya kazi, Februari 27, 2019.

Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye akizungumza, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mwenye kilemba cha njano – meza kuu) kijijini Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini, Februari 27, 2019. Naibu Waziri aliwasha rasmi umeme kijijini hapo.
...................................


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka watanzania kuondoa shaka kuhusu mipango ya serikali kufuatia gesi iliyogunduliwa mikoa ya kusini, kwani haijabadilika na inaendelea kutekelezwa.


Aliyasema hayo jana Februari 27, 2019 kijijini Ntauna, Kata ya Rondo, Lindi Vijijini, alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku nne mkoani Lindi ambapo alikagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, kuwasha umeme katika vijiji mbalimbali na kuzungumza na wananchi.


“Nataka niwaaminishe wana-kusini, yale ambayo serikali iliahidi baada ya kugundua gesi, mipango yake iko palepale na inafanyiwa kazi,” alisema.


Akifafanua zaidi, Naibu Waziri Mgalu alisema moja ya mambo ambayo serikali iliahidi ni umeme wa uhakika utakaowezesha uwekezaji.


Alisema hadi sasa, taratibu za kukamilisha ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme wa gesi Mtwara wenye megawati 300 na Somanga Fungu wenye megawati 330 ziko katika hatua za mwisho.


“Mradi utaanza ndani ya mwaka huu wa fedha ambao utawezesha mikoa hii kuzalisha umeme wa kutosha kuweza kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.”


Aidha, aliongeza kuwa, jambo jingine kubwa ni kuviwezesha viwanda vya maeneo husika kupata umeme wa gesi ambapo alisema tayari kiwanda cha saruji cha Dangote kimeshaunganishiwa.


Pia, alisema, serikali inaendelea kuzungumza na viwanda vya mbolea ili vizalishe mbolea inayotokana na gesi ili pamoja na mambo mengine viongeze ajira kwa wananchi.


Vilevile, alisema kwa Mkoa wa Lindi, eneo la Likongo, serikali inatarajia kujenga kiwanda cha kusindika gesi iwe katika hali ya kimiminika ambapo Rais John Magufuli ametoa mwongozo wa kufanya mazungumzo na mbia mmoja mmoja. Alisema mazungumzo yanaendelea vizuri.


Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alizungumzia tathmini ya ziara yake mkoani Lindi, ambapo alisema imekuwa yenye mafanikio.


Alisema, kazi ya kuwaunganishia wananchi umeme vijijini inaendelea na ametoa wito kwa mkandarasi husika kuboresha utendaji wake ili kuhakikisha anafikia malengo ya kukamilisha kazi yote kwa mujibu wa mkataba ifikapo Juni 30, mwaka huu ambapo ndipo mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza utakuwa unahitimishwa.


Naibu Waziri alisema yeyé pamoja na viongozi wengine wa Lindi akiwemo Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya na Wabunge wamekubaliana kumsimamia mkandarasi husika katika kuhakikisha anatimiza wajibu wake ipasavyo.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, ambaye alifuatana na Waziri wakati akihitimisha ziara yake, aliwahakikishia wananchi wa eneo husika kuwa yeyé pamoja na viongozi wenzake watamsimamia mkandarasi husika ili kuhakikisha kazi inatekelezwa kwa ufanisi.


“Tumekabidhiwa hawa tuwasimamie, kwa hiyo nichukue nafasi hii kuwathibitishia kwamba tutawasimamia kwelikweli ili kuhakikisha zoezi hili linakamilika vizuri sana,” alisisitiza.


Naye Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa upande wa nishati ambapo alisema imekuwa ikifanya kazi nzuri sana.


“Tunawashukuru sana Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kama kuna Wizara inafanya vizuri, basi Wizara hii inafanya vizuri.”


Hata hivyo, Nnape alisema anatambua kiu kubwa ya umeme waliyonayo wananchi na kuwasihi kuwa wastahimilivu maana zoezi la kuunganisha umeme ni hatua kwa hatua, awamu kwa awamu. Alisema anayo imani kubwa kwamba vijiji vyote vitafikiwa na huduma hiyo kabla ya mradi kuisha.


Mkurugenzi wa kampuni ya State Grid, ambayo ndiyo inatekeleza uunganishaji wa umeme mkoani Lindi, Charles Mlawa, akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo, aliahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi.


Katika ziara hiyo, viongozi wa ngazi mbalimbali walipongeza utendaji kazi wa Wizara pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuomba jitihada zinazofanyika ziendelee.


Katika Miradi ya Umeme Vijijini, Mzunguko wa Kwanza (REA III – 1), jumla ya vijiji takribani 133 vitaunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi bilioni 31.9. Matarajio ni kuwaunganishia wananchi takribani 5,337.


Akiwa Lindi vijijini, Naibu Waziri aliwasha umeme katika vijiji vya Ntauna, Mvuleni na Tulieni.

DC KAWAWA AKABIDHI HUNDI YA MILIONI 338.3 KWA VIJANA NA WANAWAKE CHALINZE

Image may contain: 8 people, people smiling, people standing
  Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mheshimwa Zainabu Kawawa, akiwa ameshika mfano wa hundi ya milioni 338.3 kwaajili ya vijana na wanawake Halmashauri ya Chalinze.

Image may contain: 7 people, people sitting
 Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mheshimwa Zainabu Kawawa, akizungumza na wana vikundi vilivyopata mikopo hiyo.
.....................................
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mheshimwa Zainabu Kawawa, amekabidhi hundi yenye thamani ya Fedha za kitanzania milioni 338.3 zilizotolewa na Halmashauri ya  Chalinze kwa vikundi 64 vya Vijana na wanawake kwa robo ya pili ya mwaka wa Fedha wa 2018/2019.


Fedha hizo ni asilimia 10 ya Mapato ya ndani yanayo kusanywa na halmashauri hiyo 


Makabidhiano hayo yamefanyika jana katika uwanja wa polisi Chalinze ambapo Mkuu huyo wa Wilaya katika hotuba yake ya kukabidhi hundi aliupongeza uongozi wa halmashauri ya Chalinze kwa kuheshimu na kutii maelekezo ya serikali kwa kutenga asilimia 10 ya Mapato ya ndani na kuwakopesha wanawake, vijana na walemavu.


Hata hivyo Kawawa alihimiza ukusanyaji wa Mapato ya halmashauri kwa kuwataka wananchi na wataalamu kuziba mianya yote inayoweza kusababisha upotevu wa Mapato na kusababisha miradi mbalimbali ya maendeleo kutotekelezeka hivyo kukwamisha utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi. 


"Mikopo hii ya wanawake na Vijana itatekelezeka kwa sababu ya juhudi ya ukusanyaji wa Mapato inayoendelea, ndiyo maana miradi yetu katika maeneo mbalimbali inaendelea kutekelezwa. "Kawawa alisema.


Akitoa ufafanuzi wa taarifa hiyo katika hafla ya ugawaji hundi kwa wanawake na Vijana, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Chalinze Bwana Shabani Millao alieleza kuwa robo ya pili ya mwaka wa Fedha 2018/2019 halmashauri hiyo imetoa kiasi cha shilingi milioni 338.3.


Alisema fedha hizo zimetolewa ili kutekeleza bajeti na maagizo ya serikali ya kuwakwamua vijana na wanawake katika lindi la umasikini wa kipato kwa kuwakopesha asilimia kumi ya makusanyo ya Mapato ya ndani ya halmashauri.


Aidha Millao alieleza kuwa mpaka sasa takribani miaka mitatu tangu ianzishwe halmashauri ya Chalinze imekwisha toa mikopo kwa wanawake na Vijana jumla ya Fedha za kitanzania milioni 967 kwa vikundi 257.


 Aliongeza kuwa, hali hiyo inawawezesha Vijana na wanawake kujiajiri wenyewe kutokana na shughuli za ujasiriamali wanazozifanya kutokana na mikopo hiyo.


"Halmashauri ya Chalinze mpaka sasa haina deni lolote kwa upande wa Asilimia 10 ya Mapato ya ndani yanayo takiwa kupelekwa kwa wanawake na Vijana tunatekeleza kwa kadiri tunavyokusanya na kuisimamia bajeti kwa mujibu wa sheria." Millao alisema.


Kwa upande wake Afisa maendeleo ya Jamii anayeratibu vikundi Bi Wahda Mwishehe aliwataka wanawake na Vijana kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili waweze kukopesheka kwa urahisi na kuwataka warejeshe mikopo kwa wakati ili mikopo hiyo waweze kukopeshwa na wengine.


 “ Akinamama wenzangu tuweni waaminifu kwa kurejesha mikopo mliyochukua kwa wakati kwani mambo yamekuwa rahisi kwa sasa kwani serikali imeondoa riba kwa wanawake na Vijana wanapokopeshwa na halmashauri, Mwishehe alifafanua.


Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze Mhe Saidi Zikatimu alieleza kwa kina mafanikio ya halmashauri yake katika ukopeshaji fedha kwa vikundi vya wanawake na Vijana kwa kusema kuwa kwa halmashauri ya Chalinze kutoa mikopo siyo tatizo bali wanawake na Vijana kutounda vikundi kwa wakati ili kupatiwa mikopo hiyo.


Zikatimu alitoa rai kwa maafisa maendeleo wa halmashauri kuwafikia wanawake na Vijana katika vijiji vyao na kuwapa Elimu ya namna ya kujiunga katika vikundi na kuwaelewesha mchakato mzima wa namna ya kupata mikopo,


"Fedha tunazo tunahitaji Vijana na wanawake wajitokeze kuomba mikopo na mikopo hii haina riba kiasi cha Fedha atakachokopeshwa mlengwa ndicho atakachorudisha“. Zikatimu alieleza.
Image may contain: 19 people, people smiling, outdoor

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mheshimwa Zainabu Kawawa akiwakabidhi wawakilishi wa vikundi katika halmashauri ya Chalinze hundi hundi ya milioni 338.3.

MAGAZETI YA LEO MACHI 1, 2019.