Wednesday, January 9, 2019

UCHAGUZI WA YANGA KUFANYIKA BWALO LA MAAFISA WA POLISI OYSTERBAY JUMAPILI JANUARI 13,2019

Uchaguzi wa kugombea nafasi za Uongozi ndani ya Klabu ya Young Africans utafanyika kwenye Bwalo la Maafisa wa Polisi Oysterbay Jumapili Januari 13,2019.

Kadi zitakazotumika katika Uchaguzi ni kadi za Kitabu na kadi za Benki zilizohakikiwa.

Kampeni za kuelekea Uchaguzi huo zimefunguliwa rasmi leo.

Akitangaza kufunguliwa kwa kampeni hizo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF Malangwe Mchungahela amewataka wagombea kufanya kampeni kwa amani bila kumchafua mwingine.

Mchungahela ameongeza kuwa kila mgombea anaruhusiwa kujinadi kokote ikiwemo katika tawi lolote la Young Africans.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Young Africans ambaye pia ni Msaidizi wa Kaimu Mwenyekiti Siza Lyimo amewataka Wanachama kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo utakaokuwa wa amani na utulivu.

Amewataka Wanachama kupita mapema kwenye matawi yao kuhakiki kadi zao za Uwanachama ili kupunguza usumbufu siku ya Uchaguzi.

JESHI LA POLISI PWANI LATOA MSAADA KWA WATOTO YATIMA.

 Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, katika kuukaribisha mwaka mpya, limetembelea kituo cha watoto wenye uhitaji maalum cha Fadhila kinacholea watoto yatima eneo la Misugusugu Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto waliopo kwenye kituo hicho. 

Msaada huo umekabidhiwa na Dr. Mkuu wa Polisi Mkoa wa Pwani ASP Festo kwa niaba ya Af Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi Wankyo Nyigesa ni:- Dawa za chooni box 3, Sabuni za kuoshea vyombo box 2, Pampers box 3, Sabuni ya unga ndooo 2, Sukari kilo 50, Kalamu box 6, Sabuni ya miche box 5, Mafuta ya kupaka box 3, Mafuta ya kula lita 20, Madaftari katoni 1, Chumvi katoni 1, Juice katoni 1, Mchele kilo 100, Unga kilo100 na mbuzi wa 2. 

Mbali ya vitu hivyo, watoto hao waliweza kupatiwa flana za usalama barabarani na vipeperushi vya usalama barabarani na vya kupinga vitendo vya ukatili baada ya kuwa wamepatiwa elimu ya usalama barabarani na dawati la elimu kutoka ofisi ya mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Pwani wakishirikiana na mabalozi wa usalama barabarani (RSA) pamoja na ofisi ya dawati la Jinsi Mkoa wa Pwani juu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuripoti vituoni pale wanapofanyiwa vitendo hivyo.

 Aidha, Dr wa Polisi aliweza pia kuonana na watoto wenye matatizo mbalimbali ya kiafya kutoka katika kituo hicho na kuweza kuwapatia tiba, ambapo amefungua milango kwa uongozi wa kituo hicho kuwapeleka kwenye matibabu kwenye zahanati ya Polisi watoto wenye uhitaji maalumu wa kuonana zaidi na Daktari kwajili ya matibabu ya kina. 

Dr. Festo ameongeza ofisi yake itaweka utaratibu wa kupita na kuwajulia hali kila baada ya wiki mbili kituoni hapo ikiwa ni katika kujenga mahusiano bora baina ya Polisi na jamii yenye uhitaji maalum. 

Awali, akizungumza na viongozi wa kituo hicho cha Fadhila pamoja na watoto wanaolelewa hapo, Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Pwani Mosi Ndozero-ASP ameeleza kuwa, Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Pwani limelenga katika mwaka 2019 kutoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi maalum na kufungua klabu za mabalozi wa usalama barabarani kwenye maeneo mbalimbali na kwa kuanzia wameamua kuendesha mafunzo ya usalama barabarani kwenye vituo vya watoto wenye uhitaji maalum kundi ambalo limekuwa likisahaulika kwa muda mrefu. 

Kadhalika, mbali ya utoaji wa elimu katika kituo hicho pamoja na utoaji wa msaada, Mkuu huyo wa usalama barabarani Mkoa wa Pwani alitumia muda wake kula pamoja na watoto wa kitu hicho ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa kituo hicho bi Suleiha amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa msaada wanaoendelea kukipatia kituo chake mara kwa mara. "Tunaomba mtufikishie salam zetu kwa viongozi wote wa Jeshi la Polisi kwa msaada wenu wa mara kwa mara katika kituo chetu, mbali ya kuwa mna majukumu mengi ya kufanya lakini mmekuwa mkisaidia sana jamii kama wazazi kwenye malezi ya watoto wetu hawa".

Vitu mbalimbali vilivyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kituo cha watoto wenye uhitaji maalum cha Fadhila kinacholea watoto yatima eneo la Misugusugu Wilaya ya Kibaha Mkoani humo.
  
 Dr. Mkuu wa Polisi Mkoa wa Pwani, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Festo akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhi msaada huo.
 
 Dr. Mkuu wa Polisi Mkoa wa Pwani, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Festo akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhi msaada huo.
 
 Picha zote Na Jeshi la Polisi Pwani.

Thursday, January 3, 2019

DC MUHEZA: NITASHIRIKIANA NA WANAMICHEZO KUHAKIKISHA TUNAPATA TIMU YA LIGI KUU

Mkuu wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha
Tumbo akizungumza wakati akifunga Mashindano ya Kombe la Kabunda Cup
........................................


Mkuu wa wilaya ya Muheza Mkoani Tanga Mwanasha Tumbo amesema atashirikiana na wanamichezo ili kuhakikisha wanaweza mazingira mazuri yatakayowezesha kupatikana timu ambayo itaweza kushiriki ligi madaraja ya juu ikiwemo Ligi kuu.

Mwanasha aliyasema hayo wakati fainali michuano ya kombe la Kabunda Cup iliyokuwa ikichezwa kwenye viwanja vya Vikonge Mtindiro wilayani Muheza ambapo alisema ili kuweza kuhakikisha wanafanikisha jambo hilo wataendelea kuhamasisha vijana kujikita kwenye michezo.

Alisema licha ya kuhamasisha michezo kutokana na kwamba ni ajira ambayo inaweza kuwainua vijana kuichumi na kupata maendeleo lakini pia aliwahaidi kuwajengea kiwanja cha mpira chenye matofali ili waweze kuonyesha umahiri wao na hatimaye wilaya hiyo iweze kupata mafanikio kwenye soka.

“Leo nimekuja hapa kuhimitisha Ligi hii kwanza nimefurahishwa sana na viwango ambavyo mmekuwa mkivionyesha kwenye mchezo huu nimeongeza na Diwani wenu hapa na niwahaidi kwamba nitawajengea kiwanja chenye matofali ili hari ya kushiriki kwenye michezo muweza kuendelea nayo na tunaamini siku zijazo tutairudisha Muheza kwenye ramani ya soka “Alisema DC Mwanasha.

Alisema kwamba anafanya hivyo ili kuweza kuchochea maendeleo ya mchezo huo ambao vijana wakiweka bidii
na nia wanaweza kufika mbali ikiwemo kuitangaza wilaya hiyo lakini pia kupata manufaa kama walivyokuwa Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Awali akizungumza katika fainali hiyo Katibu Msaidizi wa Kamati ya Mashindano hayo Salehe Mwinjuma alisema lengo la mashindano hayo yalikuwa ni kuweza kuinua vipaji vya wachezaji wachanga kwenye Kata hiyo yaliyoanzishwa na mdau wa michezo Seif Kabunda kwa kushirikisha timu 20 zilizocheza kwa mtindo wa makundi.

Alisema kwamba msimu ujao ligi hiyo itakuwa na mabadiliko makubwa kutokana na mdhamini wa mashindano hayo kuamua kujipanga upya na kuja kinyengine lengo kubwa likiwa kuhakikisha michezo inapata mafanikio.

Katika fainali hiyo timu ya Ushirika FC waliweza kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Kombe la Kabunda Cup baada ya kuibamiza Kwarabuye FC mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Vikonge Mtindiro na kujiny’akulia kombe na kitita cha sh.milioni moja . 

Katika mchezo huo ambao ulikuwa mkali na wenye ushindani mkubwa uliohudhuriwa na Mkuu wa wilaya ya Muheza
Mwanasha Tumbo ambaye ndie alikabidhi zawadi kwa washindi kwenye michuano hiyo.
 

Mkuu wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha
Tumbo kushoto akimkabidhi Kitita cha Milioni moja Nahodha wa timu ya Ushirika Amiri Nko baada ya timu yao kuibuka na ushindi kwenye michuano ya Kombe la Kabunda Cup kushoto ni Afisa Michezo wa wilaya ya Muheza Anania Sama

MKUU wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Tumbo kushoto akimkabidhi Kombe la Ubingwa wa Mashindano ya Kabunda Cup Nahodha wa timu ya Ushirika Amiri Nko kushoto ni Afisa Michezo wa wilaya ya Muheza Anania Sama.

Katibu Msaidizi wa Kamati ya Mashindano hayo akisoma risala.

MKUU wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Tumbo katika akiwa kwenye picha ya pamoja na wachezaji