Friday, November 2, 2018

WATANZANIA TUSHIRIKIANE KATIKA MAMBO YA MSINGI- RAIS MAGUFULI.

Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewa himiza watanzania kushirikiana na Serikali yake katika masuala makubwa ya msingi ili kuliletea Taifa maendeleo ya haraka.

Akizungumza leo katika ukumbi wa Nkrumah katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam,  wakati wa Kongamano kuhusu hali ya uchumi na Siasa nchini, lenye mada isemayo “Miaka Mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano Tunatoka Wapi, Tuko Wapi na Tunakwenda Wapi?”, Rais Magufuli alisema kuwa anawaomba watanzania kuendelea kushirikiana Serikali yake ili kujiletea maendeleoa.

“Nawaomba watanzania katika mambo makubwa ya msingi ni lazima tusimame kwa pamoja, na si kujali itikadi za vyama vyetu vya siasa”alisema Rais Magufuli.

Aidha, alisisitiza kuwa “ mambo ya chama yatatuchelewesha, watanzania hawataki vyama, wanataka maendeleo”

Katika kongamano hilo ambalo Rais Magufuli alikuwa mgeni maalum, amesisitiza namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwaletea maendeleo watanzania kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kujenga uchumi.

Rais Magufuli amekaribisha sekta binafsi katika kilimo ili kuimarisha sekta hiyo kwa kuwekeza katika kilimo cha kisasa na ikiwa ni pamoja na kupata soko la uhakika la mazao ya wakulima.

“Benki ya kilimo ina shilingi bilioni 300, sekta binafsi wanaweza kuja kushirikiana na Serikali kwa kuanzisha viwanda vitakavyosaidia sekta hiyo ya kilimo” alisema Rais Magufuli.

Kuhusu matumizi ya lugha ya kiswahili, Rais Magufuli alisema aliamua kuzungumza kiswahili kwa sababu kiswahili ni utamaduni wa mtanzania, lakini ni lugha ya kumi kwa kuwa na wazungumzaji wengi duniani, na ni lugha ya pili Afrika.

Hivyo, amewataka watanzania kukithamini zaidi kiswahili, licha ya kuwa wanaweza kujifunza lugha nyingine zozote.

Sambamba na hilo, Rais Magufuli ambaye amezungumza baada ya kusikiliza mada tano zilizotolewa na wanataaluma wakongwe wa uchumi, lugha, siasa na utawala amnbapo Rais aliahidi kufanyia kazi mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa katika kongamano hilo, ambayo anaamini yataleta tija na maendeleo kwa Taifa.

Mada zilizowasilishwa na kujadiliwa ziligusia masuala mbalimbali kama vile viwanda, nishati ambapo ifikapo mwaka 2020 vyanzo vya nishati jadilifu na visivyojadilifu vitazalisha megawati  5,000 na mwaka 2025 megawati 10,000 za umeme.

Aidha, mafanikio mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na ukuaji wa uchumi kwa asilimia saba na jitihada sahihi zinazofanywa kuelekea asilimia nane, na kufanya Tanzania kuongoza katika nchi za Afrika Mashariki, na kuwa  miongoni mwa nchi 5 za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.

Vile vile, katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano, pamoja na mafanikio mengine makubwa ya kufufua miradi ya msingi wezeshi, kama ununuzi wa ndege saba, uboreshaji wa bandari, viwanja vya ndege na barabara ni fursa ya kuwezesha miaradi mingine ya kiuchumi,mfano,viwanda vipya zaidi ya 3,066, vilivyojengwa vitahitaji huduma za maji umeme, barabara, bandari kama mahitaji wezeshi ya msingi.

Huduma kama usafiri wa anga zimeboreshwa, ikiwemo sekta ya utalii ambapo mikakati ya sekta hiyo, matarajio yake mwaka ujao watalii wanaotarajiwa kutembelea Tanzania wataongezeka hadi kufikia milioni 2, kiwango kitakachokuwa karibu mara mbili ya watalii waliokuwa wanatembelea Tanzania miaka ya nyuma.

Katika kongamano hilo, wahudhuriaji walipata fursa ya kujadili  mada zilizotolewa, ambazo kwa ujumla tafiti za mada zimebaini juhudi kubwa alizofikia Rais na Serikali yake kwa muda mfupi na wasomi tafiti zao zimebaini kuwa  miradi mikubwa inayoendelea vema, itawezesha miradi mingine kuanzishwa au kufufuliwa na kuleta maendeleo, mfano ujenzi wa Umeme ni mradi utakaowezesha ujenzi wa viwanda, pia wameeleza changamoto na kutoa maoni.

Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na watendaji mbambali  wa Serikali, wakiwemo viongozi wastaafu, wabunge pamoja na wanafunzi wa vyuo na sekondari.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa Mshiriki Maalum akiwa pamoja na washiriki wengine wakisikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na Watoa Mada katika Kongamano la Hali ya Uchumi na Siasa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano lililofanyika katika ukumbi wa Nkuruma uliopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa Mshiriki Maalum, akizungumza na Wageni mbalimbali wakiwemo Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Viongozi wa Kiserikali, Mabalozi kutoka nchi mbalimbali, pamoja na wananchi   waliohudhuria katika Kongamano la Hali ya Uchumi na Siasa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano lililofanyika katika ukumbi wa Nkuruma uliopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Baadhi ya Washiriki wa Kongamano la Hali ya Uchumi na Siasa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano wakisikiliza kwa makini wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa mshiriki Maalum alipokuwa akizungumza katika ukumbi wa Nkuruma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.



Thursday, November 1, 2018

SERIKALI YAMALIZA MGOGORO WA KIWANDA CHA CHAI MPONDE

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumz jambo na Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba katika mkutano aliouhutubia kwenye kijiji cha Mponde wilayani Lushoto, Novemba 1, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
.........................................................

 SERIKALI imemaliza mgogoro uliodumu kwa miaka mingi kati ya wakulima wa chai wa wilaya za Lushoto na Korogwe na kampuni ya Mponde Tea Estate uliosababisha kufungwa kwa kiwanda cha chai cha Mponde baada ya kuagiza kiwanda hicho kianze kazi.

“Waziri Mwijage na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilomo Prof. Siza Tumbo hakikisheni kazi ya kukagua kiwanda na mitambo inafanyika haraka na kubaini mitambo ipi ni mizima na ipi ina hitilafu ili ukarabati ufanyike na kiwanda kianze kazi mara moja.”

Uamuzi huo wa Serikali umetangazwa leo (Alhamisi, Novemba 1, 2018) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Kweminyasa kata ya Mponde, wilayani Lushoto baada ya kutembelea kiwanda hicho .

Waziri Mkuu amesema mwaka 1999 Serikali iliamua kuwapa wakulima wa chai na kiwanda hicho  kwa ajili kuwawezesha kuwa na sehemu ya kuchakata chai yao lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi. Imeamua kukirudisha Serikali baada ya kuwepo migogoro iliyoathiri uzalishaji kiwandani hapo.

Kuhusu suala la madeni ya watumishi, ameagiza watafutwe na madai yaorodheshwe kwa ajili ya malipo, amewahakikisha wananchi hao kuwa suala la ajira ambazo zilipotea baada ya kiwanda kufungwa zitarudi kwa sababu Serikali inataka kuona kiwanda kikifanya kazi.

“Serikali imeamua kukichukua kiwanda hiki ambacho awali ilikikabidhi wakulima wa chai na kwamba itahakikisha lengo lake la kuboresh kilimo linafanikiwa na  wakulima wanaendelea kulima zao la chai. Hatutaki kusikia masuala ya Utega wala Mponde hapa si mahali pake.”

Amesema wakulima hao walikosea kwa kuunda Umoja wa Wakulima wa Chai (UTEGA) ambapo katika kusajili badala ya kuanzisha ushirika wao walisajili NGO ambayo ilikuwa na wanachama wake, huku kiwanda kikiwa kimeanzishwa kwa ajili ya wakulima wote, jambo ambalo lilisababisha mgogoro baina ya wakulima na viongozi wa UTEGA.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa wakati mgogoro huo ukiendelea kati ya UTEGA na wakulima wa chai wasiokuwa wanachama wa NGO hiyo, uliibuka mgogoro mwingine baina ya wakulima wote pamoja na muwekezaji ambaye ni kampuni ya Mponde Tea Estate baada ya kukabidhiwa kiwanda hicho  na uongozi wa UTEGA bila ya wao kushirikishwa.

Amewasisitiza wakulima wafufue mashamba yao kiwanda ni cha  Serikali  hivyo watakuwa wamepata sehemu ya uhakikika ya kupeleka chai ambayo itachakatwa. Pia ameagiza Mrajisi wa Ushirika aende kwa wakulima na kutambua idadi yao pamoja na kujua ukubwa wa mashamba yao.

Amesema baada ya kubaini idadi ya wakulima na ukubwa wa mashamba yao awasaidie katika kuunda vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) kisha kuunda ushirikia wao ambao watautumia katika kusimamia zao lao la chai na kuhakikisha mkulima ananufaika.

Waziri Mkuu amesema zao la chai ni miongoni mwa mazao makuu sita ya kimkakati, mengine ni korosho, kahawa, tumbaku, pamba na chikichi, hivyo amewataka wafufue mashamba yao na waendelee kuiamini Serikali yao ambayo imejidhatiti kuwahudumia.

Awali,Waziri wa Nchi Ofisi ya Makam wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba alisma Mgogoro huo wa kiwanda cha Mponde ulianza tangu mwaka 1999 na ilipofika mwezi Mei 2013, wananchi walimlalamikia kwa kushindwa kutatua tatizo hilo.

Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli aliwaomba wananchi hao waendelee kuwa na subira wakati suala lao likiwa linaendelea kushughuliwa na Serikali. “Mgogoro huo umesababaisha kudhorota kwa uchumi kwa sababu wananchi wengi waliacha kulima chai baada ya kiwanda hicho kufungwa miaka mitano iliyopita.”

Hivyo Makamba ameiomba Serikali iwasaidie wakulima wa zao la chai kuwapa miche mipya pamoja na pembe jeo kwa ajili ya kufufua zao hilo na kukiwezesha kiwanda cha chai MPonde kupata malighafi kama ilivyokuwa hapo awali.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema kuwa  tayari amekuja na wataalam kwa ajili ya kukagua mashine zote zilizopo kiwandani hapo ili mchakato wa kukiwasha uanze  mara moja.

Mwijage alisema “mimi kama Waziri mwenye dhamana ya viwanda nawaambia wananchi muondoe wasiwasi tayari kiwanda kimeshafunguliwa maana sitaondoka hapa Bumbuli mpaka kieleweke.”
 
Wananchi wakimpungia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati  alipowasili kwenye kijiji cha Mponde wilayani Lushoto kukagua kiwanda cha chai cha Mponde na kuzungumza na wananchi, Novemba 1, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)