Thursday, November 1, 2018

NAIBU WAZIRI MABULA AWATAKA WTAALAMU WA MIPANGO MIJI KUWA NA MIPANGO ENDELEVU KUEPUKA UBMOAJI WA NYUMBA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula akifunga mkutano wa tano wa Bodi ya Usajili Wataalamu wa Mipango Miji jijini Dodoma.
....................................................

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mbaula amewataka wataalamu wa mipango miji kuwa na mipango endelevu  na kabambe katika miji na halmashauri zote nchini ili kuwa na miji iliyopangika na kuepuka ubomoaji nyumba za wananchi unaosababishwa na uelewa mdogo wa sheria na taratibu za mipango miji.

Aliwataka wataalamu wa mipango miji kuwajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao   kuepesha wananchi kuvunja sheria unaosababishwa na wataalamu kutowaeleza ambapo alisema si kila mwananchi anayevunja sheria za ujenzi mjini anafanya makusudi bali wengine hawajui sheria na taratibu na kuhitaji kuelezwa.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano wa tano wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji  jijini Dodoma jana, Dk Mabula alesema maeneo mengi ya miji wataalamu wanahangaika na kazi ya kurasimisha jambo ambalo siyo suluhisho la upangaji miji bali ni kujaribu kuweka viraka katika vazi lililochakavu.

Akigeukia suala la kuwepo maeneo mengi yasiyopangwa, kupimwa na kumilikishwa Dk. Mabula alisema eneo hilo linaibua changamoto mbalimbali kwa jamii ikiwemo ongezeko la  makazi holela maeneo ya mijini, kukua kwa miji isiyo na mpangilio mzuri pamoja na kukithiri kwa migogoro ya ardhi nchini na kuwashauri wataalamu hao wa Mipango mijini nchini kuwafuata wananchi waliko kwa ajili ya kutatua kero zao.

Alizitaka halmashauri ambazo muda wa mipango yake kabambe imeisha kuhakikisha  zinahuisha mipango hiyo ili kuwa endelevu kwa minajili ya kuweka miji salama na ikiwa imeandaliwa miundo mbinu muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya miji na taifa kwa ujumla.

Aidha, Dk. Mabula ametaka maeneo ambayo reli ya SGR inapita ni vyema halmashauri za maeneo husika kuanza kufanya upangaji mapema ili reli itakapoanza maeneo yote yawe yamepangwa, yamepimwa na yamemilikishwa na uendelezaji umefanyika ili kuinua uchumi kwa maeneo husika na kutosubiri wajanja wakaanza kuvamia.

Katika maazimio yake yaliyosomwa na Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu Mipango Miji Hellen Mtutwa, Washiriki walikubaliana Chuo Kikuu cha Ardhi kwa kushirikiana na Bodi ya Usajili Wataalamu Mipango Miji kuandaa muongozo utakaowawezesha Watendaji wa Kata na Vijiji kuwa wasimamizi wa mipango  miji kwenye maeneo yao ili kuepuka ujenzi holela na miji isiyopangwa.

Aidha, Washiriki walikubaliana urasimishaji wa makazi ufanayike katika maeneo yote ya nchi na siyo baadhi ya maeneo na wataalamu mipango miji kuhakikisha wanaandaa andiko la mradi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya upangaji miji badala ya kusubiri serikali pekee.

Mkutano huo wa Bodi ya Usajili Wataalamu Mipango Miji uliokuwa ukijadili matatizo na changamoto zinazowakabili Wataalamu wa taaluma za Mipango Miji katika shughuli  zao na kuweka mikakati ya kukabiliana nazo na kushirikisha wataalamu 260 kutoka Serikali na Sekta Binafsi pamoja na Makampuni yanayojishughulisha na mipango miji.
 
Sehemu wa washiriki wa Mkutano wa tano wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji  uliofanyika jijini Dodoma. (Picha zote na Hassan Mabuye wa Wizara ya Ardhi)

NAIBU SPIKA AKUTANA NA TIMU YA MBEYA CITY FC JIJINI DODOMA

Naibu Spika wa Bunge Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson akizungumza na Wachezaji pamoja na Viongozi wa Timu ya Mbeya City FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara walipotembelea Bungeni kwa ajili Ziara ya Mafunzo hii leo katika Ukumbi wa Pius Msekwa Bungeni Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Mbeya James Kasusura akifafanua jambo mbele ya Naibu Spika wa Bunge Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa katika Ziara ya Wachezaji na Viongozi wa Timu ya Mbeya City FC walipotembelea Bungeni kwa ajili ya Ziara ya Mafunzo hii leo Jijini Dodoma.

Naibu Spika wa Bunge Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson akiwa katika picha ya pamoja na Wachezaji na Viongozi wa Timu ya Mbeya City FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara walipotembelea Bungeni kwa ajili ya kufanya Ziara ya Mafunzo hii leo Jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Bunge)

TRAFIKI WAOMBA RUSHWA WASHTAKIWA KWA WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela orodha ya matrafiki wanaodaiwa kuwaomba rushwa madereva wa noah wilayani Lushoto.

Majina ya trafiki hao wanadaiwa kuomba rushwa kwa madereva wa noah wanaofanya kazi ya kusafirisha abiria ndani ya wilaya hiyo yaliwasilishwa kwa Waziri Mkuu kupitia mabango.

Waziri Mkuu alimkabidhi majina hayo jana jioni (Jumatano, Oktoba 31, 2018) baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Sabasaba, Lushoto mjini.

Baada ya kumkabidhi majina hayo alimuagiza afanye uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazowakabili askari hao na kisha awasilishe taarifa kwake leo Alhamisi Novemba 1, 2018.

Mbali ya wananchi kuwasilisha malalamiko hayo, Pia mbunge wa Lushoto, Shaaban Shekilindi alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kutatua kero hiyo inayowakabili wananchi.

Awali, Waziri Mkuu alizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Lushoto katika ukumbi wa chuo cha Mahakama Lushoto ambapo aliwasisitiza wafanye kazi kwa bidii.

Alisema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haina msamaha na mtumishi wa umma asiyetaka kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia weledi.

Alisema watumishi wa umma wanatakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili ya utumishi ili waweze kutimiza lengo la Serikali la kuwahudumia wananchi kwa kutumia taaluma zao.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Tanga alisema Serikali haina msamaha na mtumishi asietaka kubadilika na kufanya kazi.

Pia, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa umma wahakikishe fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka Wakuu wa Idara kutumia kitabu cha ilani ya uchaguzi cha CCM cha mwaka 2015/2020 kwa sababu kina maelekezo wanayopaswa kuyatekeleza.

“Kitabu kile kina maelezo ya msingi yaliyotolewa na Rais. Dkt. Magufuli ambayo yanatakiwa yapewe kipaumbele cha utekelezwaji, wakuu wa Idara ni muhimu musome na kutekeleza.”

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka wakuu wa wilaya wahakikishe wanasimamia utekelezwaji wa maelekezo yote yaliyoainishwa kwenye kitabu cha Ilani katika maeneo yao.

Kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali nchini, Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua na kwamba suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Sabasaba na kuwapongeza wakazi hao kwa kutunza misitu.

Alisema maeneo mengi nchini wananchi wamekata miti na kusababisha kukauka kwa vyanzo vya maji, ambapo ni tofauti na wilaya ya Lushoto ambayo bado ina misitu minene.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wote wa vijiji na kata waainishe sehemu  zote zenye misitu na vyanzo vya maji katika maeneo yao na wahakikishe wanayalinda.

Alisema mtu yeyote atakayebainika kuharibu mazingira hayo iwe kwa kuchoma au kukata miti achukulie hatua kali. “Ni marufuku mtu yeyote kukata miti bila kibali cha Serikali.”

Nae, Mbunge wa Lushoto Shekilindi alimuomba Waziri Mkuu awasaidie katika kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa katika jimbo hilo ikiwemo ya afya.

Mbunge alisema kwa sasa hospitali ya wilaya hiyo inakabiliwa na ukosefu wa mashine ya x rey, hivyo kusababisha wananchi kusafiri hadi Korogwe au Tanga kufuata huduama hiyo.
 
Waziri Mkuu alisema tayari ameshamuagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kupeleka mashine ya x-rey katika hospitali hiyo.