Thursday, November 1, 2018

MTANGAZAJI SAMADU HASSAN WA STAR TV AFARIKI DUNIA.

MTANGAZAJI maarufu wa Habari wa Kituo cha Runinga cha Star Tv na Radio Free Africa, (Sahara Media Group) ambaye pia alikuwa mkongwe kwenye tasnia hiyo, Samadu Hassan amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, nyumbani kwake eneo la Miembe Mitatu, jirani na kituo cha Chakechake wilayani Nyamagana jijini Mwanza.

Mdogo wa Samadu, Latifa Hassan amesema kaka yake alikuwa akisumbuliwa na kifua kwa zaidi ya wiki moja, kabla ya kufikwa na umauti.
“Jana jioni, Samadu alirudi nyumbani kwake akitokea kazini alikuwa mzima wa afya, lakini alikuwa akidai kifua kinamsumbua. 

Tulikula naye pamoja chakula cha jioni, akadai kifua kinamsumbua, tulimwambia twende hospitali ili akatibiwe, lakini alisema atakwenda kesho (leo).”

“Ilipofika saa sita kasoro usiku, ghafla hali yake ikabadilika na kuanguka chini na kuanza kutokwa na mapovu mdomoni. Tulikimbia kwenda kutafuta gari kumuwahisha hospitali, hadi tunapata gari na kurudi ndani, tulikuta tayari ameshaaga dunia,” amesema Latifa.

JWTZ KUWA MWENYEJI WA MAZOEZI YA MAJESHI YA NCHI ZA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI MKOANI TANGA


Mkuu wa Mafunzo na Operesheni  (JWTZ) Meja Jenerali Alfred Fabian Kapinga akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Mkuu ya Jeshi la Wananchi Upanga jijini Dar es salaam wakati alipotangaza kufamyika kwa mazoezi ya pamoja kwa nchi za Afrika Mashariki yatakayofanyika mkoani Tanga mwezi ujao, Kushoto ni Kanali Martin Msumali Naibu Mkurugenzi wa Mafunzo Makao Makuu ya Jeshi.
Mkuu wa Mafunzo na Operesheni  (JWTZ) Meja Jenerali Alfred Fabian Kapinga akifafanua zaidi wakati  akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mazoezi ya kijeshi yatakayofanyika mkoani Tanga na kushirikisha majeshi ya nchi za Afrika Mashariki kushoto ni Kanali Martin Msumari Naibu Mkurugenzi wa Mafunzo Makao Makuu ya Jeshi na kulia ni Meja Gaudence Ilonda Kaimu Mkurugenzi wa habari na Uhusiano (JWTZ)
.................................................
 
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanatarajia kuwa wenyeji wa zoezi la mafunzo yaitwayo Ushirikiano imara 2018 litakaloshirikisha nchi za Afrika Mashariki zikiwemo Burundi, Rwanda, Kenya na Uganda ambapo mafunzo yataendeshwa mkoani Tanga .

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam Mkuu wa Mafunzo na Operesheni  (JWTZ) Meja Jenerali Alfred Fabian Kapinga amesema kuwa, zoezi hilo ni la medani na litafanyika katika wilaya za mijini pamoja na Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Ameeleza kuwa zoezi hilo litaanza rasmi tarehe 05 mpaka 21, sambamba na hilo mafunzo hayo yatalenga kujenga uwezo wa kukabiliana na uhalifu pamoja na majanga.

Pia amesema kuwa dhumuni la zoezi hilo kikanda ni kubadilishana uzoefu wa kiutendaji, kuimarisha mahusiano baina ya nchi, majeshi ya Afrika Mashariki pamoja na taasisi zingine za kiraia ambazo zitashiriki zoezi hilo.

Sanjari na hilo kutakuwa na kazi za kusaidia jamii katika shughuli mbalimbali zikiwemo ujenzi wa madarasa, ofisi za walimu pamoja na vyoo katika Shule ya msingi ya Machemba iliyopo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, pia kutakuwa na utoaji wa huduma za tiba kwa wananchi katika eneo la zoezi.

Hivyo, Meja Fabian ametoa rai kwa wakazi wa Tanga kuonyesha ukarimu pamoja na amani baina ya wageni watakaokua kwa kipindi chote cha mafunzo kama walivoonyesha mwaka jana ambapo mafunzo yalikua yakiendeshwa.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkuu wa Mafunzo na Operesheni (JWTZ) Meja Jenerali Alfred Fabian Kapinga.