Sunday, January 21, 2018

UMEME WAINGIA KIJIJI CHA KONGO BAGAMOYO.


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na viongozi wa kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo Wilayani Bagamoyo wakati alipofika kijijini hapo leo tarehe 21 January 2018, kukagua kazi ya uwekaji nguzo za umeme kwenye mradi wa umeme vijijini REA awamu ya tatu.
  ...............................................
Kijiji cha Kongo kata ya Yombo Halmashauri ya Bagamoyo wilayani Bagamoyo, hatimaye kimepata matumaini ya kupata umeme baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 40 sasa.

Matumaini hayo yamekuja kufuatia ahadi aliyoitoa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu katika Mkutano na wananchi wa kijiji hicho hivi karibuni ambapo aliwaahidi umeme kupatikana kijijini hapo Tarehe kumi February 2018.

Naibu waziri huyo wa Nishati, leo tarehe 21 January 2018 alitembelea kijiji cha Kongo ili kujionea kazi ya uwekaji nguzo inayofanywa na mkandarasi Sengerema ambapo alisema ameridhishwa na kasi ya uwekaji nguzo na kuwataka wananchi wa kijiji cha  Kongo kuwa na subira kwani zimebaki siku chache ili wapate umeme.

Mgalu alisema katika kutekeleza sera ya kuwahudumia wanyonge chini ya Rais Dkt. Magufuli kila kijiji kitapata umeme ili wananchi wote wapate huduma zinazotolewa na serikali kwa nchi nzima bila ya kubagua.

Aidha, amemuagiza meneja wa  TANESCO wilaya ya Bagamoyo kuandaa fomu kwaajili ya kuwapatia wananchi ili wafanye mchakato wa kulipia na kuunganishiwa umeme haraka iwezekanavyo.

Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Naibu waziri, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa alisema anamshukuru Naibu waziri huyo wa Nishati kwa kushughulikia kero ya muda mrefu ya wananchi wa kijiji hicho na hatimae utekelezaji umeanza.

Alisema kufuatia utekelezaji wa kuingiza umeme kijijini hapo ni wazi kuwa wananchi hao wataendelea kujenga imani na serikali yao ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.

 Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu akisaini kitabu cha wageni katika kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo Wilayani Bagamoyo wakati alipofika kijijini hapo leo tarehe 21 January 2018, kukagua kazi ya uwekaji nguzo za umeme kwenye mradi wa umeme vijijini REA awamu ya tatu, kushoto ni Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa.
 
Baadhi ya Viongozi wa Kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo Wilayani Bagamoyo wakimsikiliza Naibu waziri wa Nishati (hayupo pichani) akizungumza wakati alipofika kijijini hapo kukagua kazi ya uwekaji nguzo za umeme.
 Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu akielekea kuangalia nguzo za umeme katika kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo Wilayani Bagamoyo wakati alipofika kijijini hapo leo tarehe 21 January 2018, kukagua kazi ya uwekaji nguzo za umeme kwenye mradi wa umeme vijijini REA awamu ya tatu, kushoto ni Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, na kulia ni Diwani wa kata ya Yombo Mohamedi Usinga.
 Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, Diwani wa kata ya Yombo Mohamedi Usinga pamoja na viongozi wa kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo Wilayani Bagamoyo wakishika moja kati ya nguzo za umeme zilizowekwa kijijini hapo kupitia mradi wa umeme vijijini REA awamu ya tatu.

Thursday, January 18, 2018

WAZIRI MWIGULU AKUTANA NA VIONGOZI KUJADILI MASUALA YA JESHI LA MAGEREZA



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, akizungumza wakati wa kikao cha kujadili masuala mbalimbali ya Jeshi la Magereza baada ya kukutana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Mstaafu Projest Rwegasira (kushoto) na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dk . Juma Malewa.Kikao hicho kimefanyika leo ofisi ya wizara,jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Mstaafu Projest Rwegasira (kushoto) na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dk. Juma Malewa(kulia), wakimsikiliza Waziri wa wizara hiyo, Dk. Mwigulu Nchemba walipokutana kujadili masuala  ya jeshi hilo. Kikao hicho kimefanyika leo ofisi ya wizara,jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Mstaafu Projest Rwegasira, akifafanua jambo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dk. Juma Malewa (kulia), wakati wa kikao cha kujadili masuala mbalimbali ya jeshi hilo.Kikao hicho kimefanyika leo ofisi ya wizara,jijini Dar es Salaam.

Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI-WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI



MARUFUKU KUWACHANGISHA MICHANGO WANAFUNZI- RC PWANI.


Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amesema mwalimu Mkuu yeyote atakayechangisha michango kwa wanafunzi na kupelekea uzito wa kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto shule atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kazi.
Hayo aliyasema jana Tarehe 17 Januari 2018, wilayani Bagamoyo alipofanya ziara katika Halmashauri ya Chalinze ambapo alitembelea shule ya Sekondari Mboga ili kuoana idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza amba wmeripoti shuleni hapo.
Alisema Rais Dkt. John Magufuli ametangaza elimu bure kwa wananchi wote hivyo haipaswi kwa mtu yeyote kukwamisha dhamira ya Rais magufuli ya kutoa elimu bure.
Alisema wapo baadhi ya walimu wakuu wamekuwa kikwazo cha watoto kwendda shule kwa kuwapa orodha kubwa ya mahitaji hali inayopelekea kuondoa dhana nzima ya elimu bure kwa wananchi.
Alisema ni marufuku kwa walimu wakuu wote mkoani Pwani kuweka masharti kwa mwanafunzi kuripoti shule kwa nama yeyote ile.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa wa Pwani alitoa siku saba kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaripoti shule na kwamba kata ambayo itashindwa kutekeleza hilo Mratibu elimu kata atasimamishwa kazi.
Wakitoa taarifa ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2018 mbele ya Mkuu wa Mkoa maafisa elimu wa Halmashauri ya Bagamoyo na Chalinze wamesema mpaka sasa wanafunzi walioripoti shuleni kwa Halmashuri ya Chalinze ni asilimia 50. 63 na Halmashauri ya Bagamoyo ni asilimia 43.48 tu.